MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeifikisha nchi ya Malawi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kukataa kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir.
Malawi ilikuwa mwenyeji wa Rais Bashir mwezi Oktoba licha ya kufahamu kuwa kuna kibali cha ICC cha kumkamata kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika eneo la Darfur mtuhumiwa huyo.
Taarifa kutoka ICC zinasema Malawi tayari imejitetea kwa madaia kwamba Rais Bashir ana kinga kama rais wa nchi, na wasingeweza kukiuka sera ya Muungano wa Afrika kwa kumkamata kiongozi huyo.
Malalamiko dhidi ya nchi zingine tatu barani Afrika tayari yamewasilishwa mbele ya Baraza hilo. Moja ya nchi hizo ni Kenya, ambayo jaji mmoja mwezi uliopita alitoa kibali cha kumkamata Bashir, jambo lililoleta mtafaruku wa kidiplomasia, ambao baadaye walisuluhisha baada ya Serikali kusema haitamkamata rais wa Sudan.
Viongozi wengi wa Afrika wanashtumu ICC kwa kuchunguza tu madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika na siyo uhalifu katika maeneo mengine duniani. Bashir alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kushutumiwa na ICC, iliyomtuhumu kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur. Amekanusha madai hayo, akisema kuwa yamechochewa kisiasa.
-BBC