IBF/USBA yaongeza Taji jipya kwa Mabondia Afrika

Rais wa IBF/USBA katika bara la Afrika, mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi

Katika mpango wake kabambe wa kupanua wigo wa mabondia wa “Kiafrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi” kujitangaza katika tasnia ya ngumi za kulipwa, Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama Cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA) limezindua taji jipya.

Taji hilo linajulikana kama “Ubingwa wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi” kwa kizungu ni “IBF Africa, Middle East and Persian Gulf Title” au (IBF/AMEPG).

Mpamnano wa kwanza wa ubingwa huo utafanyika katika jiji la Windhoek nchini Namibia Septemba 1, 2012 kati ya “Mtanzania Rajabu Maoja” na bingwa wa Namibia Gottlieb Ndokosho!

Mpambano mwingine unategemewa kufanyika katika jiji la Accra nchini Ghana kati ya bondia Richard Commey wa Ghana ambaye kwa sasa anajifua nchini Uingereza na bondia kutoka nchi ya Qatar ambayo iko katika Ghuba ya Uajemi.

Juhudi hizi za IBF/USBA zinakuja wakati ambapo shirikisho hili limeanzisha programu ya “Utalii wa Michezo” na kuziteua Tanzania na Ghana kama nchi za mfano kwa kipindi cha miaka mitatu

Akizungumzia kuhusu taji hilo jipya Rais wa “IBF/USBA katika bara la Afrika, mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi” Mtanzania Onesmo Ngowi alisema kuwa mabondia wa Kitanzania wanatakiwa kuzichangamkia fursa hizi ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kugombea mataji ya juu zaidi.

Ngowi alibainisha kuwa kwa sasa ni mabondia wachache sana wa Tanzania ambao wana viwango vya juu ukilinganisha na mabondai wa Nchi za Ghana, Namibia, Afrika ya Kusini, Uganda, Nigeria na Misri.

Aliahidi kuwapatia mabondia wa kiatnzania nafasi za kugombea mataji haya kila panapotokea nafasi hizi.