MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera, Rashid Mandawa amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.
Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHI
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika tarehe itakayotangazwa baadaye.
TFF imepokea maombi ya zaidi ya washiriki 40 kwa ajili ya kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi zilizopo, FIFA itafanya mchujo wa washiriki. IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)