Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema huu sio wakati wa kulaumiana wala kushtumiana kutokana na msiba mkubwa uliolipata Taifa kwa kupoteza mamia ya Wananchi kufuatia kuzama kwa Meli ya Mv. Spice Islandars. Badala yake wananchi wanatakiwa kuwa na subira na mshikamano juu ya mtihani huo, huku Serikali ikiendelea na juhudi zake za kutoa msaada na uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo.
Dk. Shein, alieleza hayo huko katika Mkoa wa Kusini Pemba, kwa nyakati tafauti akianzia huko katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu mkoani na Uwanja wa Gombani pamoja na Shule ya Msingi Ziwani wakati alipokuwa akiwafariji wananchi waliofikwa na msiba huo ambao aliufananisha na mtihani kutoka kwa Mungu.
Alisema kuwa msiba huo utabaki kama ni historia kutokea katika Visiwa hivi tokea kuanza kwa Safari za Meli katika Karne zilizopita na kusema kuwa msiba huo sio wa Wazanzibar peke bali ni wa Taifa zima la Tanzania kwa vile kila mmoja umemgusa kwa namna moja ama nyengine.
“Msiba huu haujawahi kutokea katika Historia ya Zanzibar lakini pia, ni msiba wa Taifa kwani nimeambia kuwa hadi ndugu zetu wa Mtwara, Masasi na sehemu nyengine walikuwemo” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein aliwataka Wananchi wa Zanzibar, kuzidi kushirikiana na kusaidiana na kuonesha Utulivu kama waliouonesha katika kipindi kile cha kutokea kwa Mtihani huo kwani yote yaliotokea ni muandiko wa Mwenyeezi Mungu Pekee.
Alifahamisha kuwa Serikali zote mbili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano kwa pamoja zilishirikiana na Wananchi mbali mbali ilikuona wanakabiliana na janga hilo kwa Uokozi wa Watu na kuwazika wale wote walifariki Dunia kila mmoja na Kaburi lake,
“Tulizika maiti zote huko Kama Unguja, kwa vile hatukuwa na namna nyengine kwani Maiti wa maji ya bahari haekeki na Uwezo wa Chumba cha kuhifadhia Maiti katika Hospitali ya Mnazi Mmoja hakina Uwezo mkubwa kwa wakati mmoja na wale maiti walikuwa wengi.” Alieleza Dk, Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk, Ali Moh’d Shein, alieleza kuwa Serikali imejifunza mengi kutokana na Msiba huo, na itajitahidi kuona suala kama hilo halitokei tena.
Aliwahakikishia Wananchi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeazimia kuunda Tume maalumu ilikuchunguza Chanzo cha ajali hiyo, na kuchukuwa ripoti ya uchunguzi huo na hatimae kuchukuwa hatua bila ya upendeleo wala kumuonea mtu.
“Tume tutakayoiunda tutaitangaza haraka sana katika saa zijazo na itafanya kazi bila woga na bila ya kumuonea mtu yoyote” alisema Dk. Shein. Aliendelea kusema kuwa kwa kusaidiana na Wahisani na Wafanyabiashara mbalimbali, Serikali imejiandaa kukabiliana na hali kama hiyo kwa kuwataka Wafanya biashara kuekeza katika usafiri wa Baharini kwa kutafuta Meli kubwa itakayo ondowa shida ya usafiri kati ya Pemba na Unguja.
“ Pale Serikali itakapo kuwa na uwezo itafanya juhudi ya kumiliki Meli yake wenyewe , hapo siku za nyuma srikali ilikuwa ikimiliki meli mbili mbili, kubwa na ndogo..ilikuwa na usafiri wa uhakika kwa Wananchi wa Unguja na Pemba”alisema Dk. Shein.
Alieleza kuwa pamoja na Serikali kufanya wajibu wake mbali mbali , lakini haija sita kufanya hivyo na inaungana na Wananchi wa Pemba , kwa mtihani huo na amewataka kuwa na subra kwani liliandikwa na Allha halina budi kufanyika .
Hivyo aliwashukuru Watendaji wakuu wa Serikali na Taasisi mbali mbali kwa ujumla kwa kazi kubwa waliochukuwa za kukabiliana na Janga hilo kubwa na nchi ikiwa iko katika hali ya Utulivu.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa srikali imejifunza mambo mengi katika tukio hilo na kueleza lengo lake hivi sasa la kujipanga vizuri huku kukiwa na mashirikiano mazuri pamoja na ahadi mbali mbali za kuunga mkono juu ya jambo hilo kutoka kwa washirika wa maendeleo katika kuweka mikakati zaidi. Nao wananchi na viongozi hao walisifu juhudi za serikali chini ya uongozi wa Dk Shein katika kukabiliana na tukio hilo.
Aidha, walieleza kuwa wanaungana na Rais kueleza kuwa huo ni msiba kutoka kwa Allah na kueleza kuwa kama Qur-an na hadithi za Mtume zinavyosisitiza subira basin a wao wamo katika kutekeleza amri hiyo ya Mola wao na Mtume wao Muhammad S.A.W. Kwa mujibu wa uongozi wa Wilaya ya Mkoani ulieleza kuwa watu waliofariki ni 31 na 4 waliokolewa na kwa Wilaya ya mkoani ni 146 walifariki ambapo kwa Shehia ya ziwani peke yake waliofariki ni 56.