JK Kuhutubia Mjini Lindi Siku ya Ukimwi Duniani, Kujumuisha Hotuba ya Novemba

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzie i wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakishuhudia utiwaji saini mkataba wa haja ya kuwepo kwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na nchi za Jumuiya hiyo katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya. Zoezi hili lilifanywa baina ya Mawaziri wa Bishara wa nchi wanachama wa Jumuiya na Kaimu Waziri wa Bishara wa Marekani Bi Rebecca Blank aliyehudhuria kikao hicho.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishuhudia Rais Mwai Kibaki wa Kenya akimkabidhi nyundo Rais Yoweri Muzeveni kama ishara ya kukabidhi Uienyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa nne wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya. (Picha zote na Ikulu)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete hatahutubia taifa Ijumaa, Novemba 30, 2012, kama ilivyo kawaida yake kila mwisho wa mwezi. Badala yake, Rais Kikwete atahutubia Taifa Jumamosi ya Desemba Mosi, 2012 kutoka Uwanja wa Ilulu, mjini Lindi wakati wa Siku ya Ukimwi Duniani ambako atakuwa Mgeni Rasmi.

Wakati huo huo taarifa kutoka Idara ya Mawasiliano Ikulu inasema, Rais Kikwete amerejea nchini jana jioni kutoka Nairobi, Kenya ambapo amehudhuria mkutano wa Viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Africa Mashariki (EAC), mkutano ambao umehitimisha vikao na sherehe mbalimbali za kufungua miradi ya pamoja ya nchi hizi.

Katika mkutano wa leo tarehe 30 Novemba, 2012, Rais Mwai Kibaki wa Kenya amemkabidhi rasmi Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uenyekiti wa Uongozi wa Jumuiya, kikao ambacho kimehudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Tarehe 27 Novemba, 2012 Rais Kikwete amehutubia Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kikao chake cha tatu tangu kuzinduliwa rasmi mwaka huu. Rais Kikwete amesema pamoja na changamoto zilizopo, Jumuiya inazidi kukua na kuimarika.

Tarehe 28 Novemba, 2012 Viongozi wa EAC wamezindua makao ya kudumu ya ofisi za EAC, sherehe ambayo umehudhuriwa na viongozi wa nchi hizi ambapo mara baada ya uzinduzi wa jengo hilo, viongozi wote wakaelekea Athi River na kufungua rasmi barabara ya Arusha – Namanga- Athi River yenye urefu wa kilometa 240. Sherehe ambayo pia umehudhuriwa na Rais Piere Nkurunziza wa Burundi ambapo Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wamewakilishwa na Mawaziri wao Wakuu.

Katika ufunguzi huo, Rais Kikwete amesema Jumuiya hii ni muhimu na yenye manufaa makubwa kwa nchi hizi.

Tarehe 29 Novemba, 2012 viongozi wamekutana katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta na kuzungumzia miradi mbalimbali ya miundombinu ikiwemo, barabara, reli na bandari , miradi ambayo kwa pamoja itahudumia na kunufaisha wananchi wa nchi hizi.