MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeshindwa kusoma hukumu dhidi ya kada wa CCM, Rajabu Maranda na binamu yake Farijala Hussein, kutokana na kutokamilika kwa jopo la mahakimu wanaoisikiliza kesi hiyo.Imeelezwa kuwa mahakimu wawili katika jopo hilo wagonjwa hivyo na kwa hali hiyo hukumu ya kesi hiyo sasa inatarajiwa kusomwa Juni 26 mwaka huu.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba Sh2.2 bilioni, katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), iliyoko katika Benki Kuu ya Tanzania.Jana ndugu na jamaa wa Maranda na Farijala pamoja na waandishi wa habari, walifurika mahakamani, tayari kwa kusikiliza hukumu kuhusu kesi hiyo.
Hakimu Catherine Revocate ,
alisema kesi ilifikishwa mahakamani kwa lengo la kuwasomea washtakiwa hukumu lakini kwa bahati mbaya, mahakimu wawili hawakufika kazini kwa kuwa wanaumwa.
Aliwataja mahakimu hao kuwa ni kiongozi wa jopo, Jaji Fatma Masengi na Projestus Kahyoza. Alisema angeweza kuipanga kesi hiyo wiki ijayo lakini mmoja wa mahakimu hao atakuwa hajiwezi kwa sababu atakuwa na dozi ambayo haimruhusu kufanya kazi.
Alisema kwa msingi huo, anaahirisha hukumu hiyo hadi Juni 26, mwaka huu. Tayari Maranda na Farijala, wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za Epa.
Hukumu hiyo ilitolewa Mei 23, mwaka juzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Hukumu hiyo ilipangwa Aprili 17 mwaka huu na kiongozi wa jopo la mahakimu Jaji Fatma Masengi ambaye kwa sasa anaumwa.
Hatua hiyo iikuja baada ya Maranda na Farijala kumaliza kujitetea na wakili wao Majura Magafu kufunga ushahidi. Maranda akiongozwa na Magafu katika utetezi wake, aliiomba mahakama itupilie mbali ushahidi wote uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwa madai kuwa yeye hakuwahi kuiba wala kughushi.
Alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda kwenye ofisi za Wakala wa Usajili wa Majina ya Biashara na Kampuni (BRELA) kufanya utaratibu wa Kampuni ya Money Planners & Consultant.
Pia alidai kuwa wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa, hakuwahi kupelekwa shahidi yoyote mahakamani kutoka Benki Kuu ya Tanzania, ili kuthibitisha kama iliibiwa.
“Nashangaa kwanini upande wa mashtaka haukuwahi kumwita shahidi kutoka Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani wakati anwuani zao zote walikuwa nazo,” alidai Maranda. Maranda alidai haikuwa kweli kwamba alikuwa anawasiliana na Benki Kuu ya Tanzania kupitia barua ya Septemba 8 mwaka 2005 na kuongeza kuwa yeye alisaini nyaraka baada ya kushawishiwa na Biswalo Mganga Kachele na Mkonyi.
Alidai kuwa hatua hiyo ilikuja baada ya kuelezwa kuwa malipo yaliyofanyika yalikuwa halali na asaini ili mambo yaishe.Alisema yeye ni mmoja kati ya watu waliosaini hundi za kuwalipa watu lakini hakuwahi kwenda BoT na kwamba waliokuwa wakienda ni Paulo Thobias na Fundi Kitunga.
Maranda alisema wakati fedha zinachukuliwa, kampuni ilikuwa chini yao yeye na Farijala lakini fedha zilikuwa si za kwao.
“Niliwapa fedha hizo kwa sababu nilikuwa mfanyabiashara wa mafuta ya jumla na rejareja tangu mwaka 1979, mwaka 2003 ndiyo nilianza kusimamia madeni ya Epa, sikuwa mzoefu wa kufanya hayo,” alidai Maranda. Kwa upande wake, Falijara Hussein (47), alidai uwa kabla ya Mei 23 mwaka juzi, alikuwa mfanyabiashara ya mafuta na nafaka.
Alidai kuwa kwa sasa anaishi katika Gereza la Ukonga, Selo 33 na kwamba anakula bure. Aliiomba mahakama itupilie mbali ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwa madai kuwa hakuna fedha iliyoibwa na yeye hakuwahi kuiba wala kughushi.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis kuwa ni nani aliyepeleka fomu za kubadilisha majina ya umiliki wa Kampuni ya Money Planners & Consultant BRELA?.
Maranda alidai kuwa hajui ila ni kati ya Fundi na Thobias na kwamba kabla ya kufanya mabadiliko hayo wote walienda benki na BRELA kuangalia utaribu kama unawaruhusu au la.
CHANZO: Mwananchi