Hukumu Kesi ya Kikatiba Sheria ya Makosa ya Mtandao ‘Kizungumkuti’

Kutoka kushoto ni Wakili wa Jamii Media, Benedict Ishebakaki Alex, Mmiliki Mwenza wa Jamii Media, Mike Mushi, Mkurugenzi wa Jamii Forum, Maxence Melo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria wakitoka Mahakamani leo walipoitwa kupokea hukumu yao.

 

Wakili wa Jamii Media, Benedict Ishebakaki Alex (kushoto) akiwaongoza baadhi ya viongozi Jamii Media walipokuwa wakitoka Mahakama Kuu leo.

HUKUMU ya kesi ya Kikatiba namba 9 ya mwaka 2016 iliyofunguliwa mwaka jana na Kampuni ya Jamii Media ikipinga baadhi ya vifungu vya sheria ya makosa ya mtandao kwa kile kuingilia uhuru wa maoni na kujieleza wa wananchi imeshindwa kusoma huku kukiwa hakuna sababu zilizotajwa.

Akizungumza leo eneo la Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam Wakili wa Jamii Media, Benedict Ishebakaki Alex alisema awali walipata wito wa mahakama kuwa hukumu ya kesi yao ilikuwa isomwe leo lakini wamefika mahakamani na kutokuta taarifa zozote za kusomwa kwa hukumu hiyo.

“..Kama mnavyojua leo tulikuwa tumekuja kwa ajili ya hukumu ya kesi yetu iliyofunguliwa toka mwaka jana mwezi wa tatu kutokana na rekodi za mahakama tuliambiwa tuje leo saa sita mchana kuja kupokea hukumu kama mnavyojua majaji ambao walikuwa wanasikiliza kesi yetu ni majaji watatu Mh. Jaji Koroso, Mh. Jaji Khalfan na Mh. Jaji Kitusi lakini tumefuatilia leo hapa pamoja na mawakili wa serikali, lakini tulikuwa tunajua jaji Koroso hayupo kuna taarifa kuwa amehamishwa…lakini tulikuwa tunajua labda kuna rekodo yoyote kuwa labda amemwachia faili nani au hukumu itasomwa lini tena…tunaona makarani wanasema hawana taarifa zozote juu ya hukumu hiyo.

Wakili huyo alisema yeye pamoja na mawakili wa Serikali wataendelea kufuatilia kujua hukumu hiyo itasoma lini ili waweze kuipokea.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa haki ya kupata habari nchini, Simon Mkina, akizungumzia kadhia ya hukumu hiyo kutoonekana, amesema inashangaza kuona mahakama hiyohiyo iliyotoa tarehe ya kutolewa hukumu, watendaji wake wanatupiana mpira kuhusu ilipo.

Wamiliki wa mtandao wa Jamii Media na mkuregenzi wa mtandao huo Maxence Melo akizungumza na Maria Sarungi ambaye ni mdau wa masuala ya habari nje ya Mahakama kuu jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Mkina aliongeza katika mazingira ya sasa, mahakama ni mhimili pekee unaobaki kuwa kimbilio ili kupatikana kwa haki, hivyo haipaswi kutiliwa shaka katika utendaji wake.

Kampuni ya Jamii Media, waendeshaji wa mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com mwaka jana walifungua kesi ya kikatiba wakipinga baadhi ya vifungu vya sheria ya makosa ya mtandao kwa kile kuingilia Uhuru wa Maoni na Kujieleza wa wananchi.

Katika kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama Kuu, Kampuni ya Jamii Media ilitaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwa kuwa vinasababisha kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao mitandao ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mtandao wa JamiiForums ni mtandao mkubwa wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki na Duniani ukiwa na wasomaji wasiopungua Milioni 4 kwa mwezi ambapo kwa mwaka 2016, mtandao huu unatimiza rasmi miaka 10 tangu uanzishwe. Mtandao huu unasifika kwa kutoa fursa ya kipekee kwa watumiaji wake kutoa yaliyo mioyoni mwao huku wengine wakijifunza mbinu kadha wa kadha za kijasiriamali, afya, elimu na hata kuibuka wanasiasa wapya waliofundwa na wana JamiiForums.