Na Joachim Mushi, Kibiti
MGANGA Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kibiti, Chagi Jonas Lymo amesema uwepo wa huduma za dharura kwa wajawazito katika kituo hicho cha afya umesaidia kiasi kikubwa katika uokoaji wa maisha ya mamamjamzito pamoja na vifo vya watoto eneo hilo.
Lymo ametoa kauli hiyo leo mjini Kibiti alipokuwa akizungumza na Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance), Rose Mlay pamoja na Mkurugenzi wa World Lung Foundation walipotembelea kituo hicho kuangalia namna kinavyotoa huduma kwa wananchi na changamoto zake.
Akizungumza zaidi, Lymo alisema tangu Kituo cha Afya cha Kibiti kuanza kutoa huduma za dharura kimekuwa msaada mkubwa kwa akinamama wajawazito eneo hilo na kwa sasa idadi ya akinamama wanaojifungulia eneo hilo imeongezeka mara tatu zaidi tofauti na ilivyo kuwa awali jambo ambalo unaonesha wamevutiwa na huduma hiyo muhimu kwa wajawazito.
Alisema kwa sasa kituo hicho kinafanya upasuaji kwa matatizo yote ya uzazi kwa wajawazito, ikiwemo kutoa huduma za kuongezewa damu kwa wajawazito wenye mahitaji jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya mama mjamzito pamoja na mtoto mtarajiwa.
“…Awali tulikuwa hatutoi huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito…tulikuwa hatuna chumba cha upasuaji hivyo tulitoa huduma za uzazi za kawaida, na ilipotokea matatizo kwa mjamzito tulimshauri kwenda ama kwenye hospitali ya Mchukwi (ya kulipia) ambayo ipo umbali wa takribani kilometa 15 au kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya Utete ambayo ni kilometa 84 kutoka hapa,” alisema.
“…Baada ya kuanzisha huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito, akinamama waliokuja kujifungulia hapa waliongezeka…, mwezi wa kwanza tu wa kuanza kutoa huduma hizi wakinamama waliongezeka kutoka idadi ya wagonjwa 35 kwa mwezi waliongezeka hadi kufikia zaidi ya akinamama 100 kwa mwezi,” alisema Lymo.
Alisema kwa mwezi uliopita (Machi) jumla ya wajawazito 135 walifika kupata huduma za uzazi kiasi ambacho kwa sasa ni kikubwa na kinazidi uwezo wa kituo, jambo ambalo alishauri ipo haja ya kituo hicho kuongezewa mahitaji anuai ili kwenda sambamba na ongezeko la wateja wake kwa sasa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe nchini, Bi. Rose Mlay alisema serikali ikiamua kwa kushirikiana na wadau wengine inaweza kumaliza matatizo ya vifo kwa wajawazito pamoja na watoto kwa kusogeza huduma za dharura katika vituo vya afya ambavyo vingi vipo karibu na wananchi.
“…Inawezekana kabisa kupambana na vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto endapo Serikali ikijipanga na kuamua vituo vya afya viwekewe bajeti ya kutosha na hatimaye kuweza kutoa huduma za dharura kwa akinamama wajawazito na watoto,” alisema Bi. Mlay.
World Lung Foundation ndiyo taasisi iliyokiwezesha kituo cha Afya cha Kibiti kuweza kutoa huduma za dharura kwa akinamama wajawazito. Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa World Lung Foundation, Dk. Nguke Mwakatundu alisema taasisi hiyo imevisaidia jumla ya vituo 10 vya afya kutoa huduma za dharura pamoja na kuziwezesha hospitali nyingine tano katika nyanja tofauti kwenye utoaji huduma za afya.