UPATIKANAJI wa huduma za Benki ya NMB umezindi kuboreshwa na sasa umesogezwa zaidi mtaani kwako. Mteja wa NMB na asiyekuwa mteja kupitia huduma ya NMB Wakala sasa anaweza kuweka kutoa fedha na hata kulipia huduma mbalimbali akiwa mtaani kwake bila ya uhitaji wa kufika katika tawi la benki ya NMB.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari alipokuwa akitambulisha huduma hiyo iliyoboreshwa zaidi, Mkuu wa Idara ya Huduma Mbadala za Kibenki wa NMB, George Kivaria alisema kuboreshwa kwa huduma hiyo sasa kunawawezesha wateja kupata huduma za benki hiyo kwa haraka na kwa usalama na uhakika popote walipo.
Alisema huduma hiyo pia inamwezesha mteja wa NMB kuweza kuweka fedha, kutoa, kujua salio lake kwa gharama nafuu zaidi, huku ikitolewa na mawakala zaidi ya 2000 ambao wanapatikana maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo maeneo ya vijijini.
Alisema lengo la NMB ni kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zake tena kwa gharama nafuu. Alisema huduma zingine ambazo wateja wengine hata wasiokuwa na akaynti za NMB wanaweza kufanya kwa mawakala hao ni pamoja na kulipa ada za shule, kulipia tozo za luku, ving’amuzi, malipo ya TRA, leseni na bili za maji.
Alisema huduma hiyo pia imelenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara kujipatia kipato kwa kutoa huduma hizo. Aliongeza kuwa bado benki ya NMB ndiyo inaongoza kwa kuwa na mtandao mkubwa wa huduma nchini, ikiwa na matawi zaidi ya 189 na ATM 700 nchi nzima.