MSICHANA wa kazi ‘House Girl’ amejikuta akiiteketeza kwa moto nyumba ya bosi wake pamoja na vitu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo bila kutegemea baada ya kubandika maharage kwenye jiko la gesi kisha kutoka na kwenda kusuka nyumba moja ya jirani.
Tukio hilo limetokea jana Kigamboni, eneo la Kibada jijini Dar es Salaam ambapo binti huyo wa kazi alikuwa peke yake nyumbani huku mabosi zake wakiwa kazini. Taarifa toka kwa mashuhuda ziliueleza mtandao huu kuwa binti huyo alisababisha maafa hayo baada ya kubandika kwenye jiko la gesi maharage kisha akatoka na kufunga nyumba kwenda jirani kusuka.
Walisema yaelekea mboga hiyo iliungua kabisa kisha moto wa gesi bila uangalizi ulianza kuchoma vitu vingine kabla ya nyumba nzima kuanza kuwaka kisha ikateketeza vitu vyote ndani ya nyumba hiyo pamoja na kuharibika vibaya nyumba yenyewe.