HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAHUSIANO NA URATIBU MHESHIMIWA STEPHEN MASATO WASIRA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2011 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2012/13 DODOMA 14 JUNI, 2012
2
HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAHUSIANO NA URATIBU MHESHIMIWA STEPHEN MASATO WASIRA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2011 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2012/13
3
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likae kama Kamati kwa ajili ya kupokea na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13. Taarifa hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulipitishwa na Bunge hili mwezi Juni 2011. Pamoja na hotuba hii nawasilisha kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipatia fursa hii ya kuwasilisha taarifa hizi. Vilevile, napenda kumpongeza Mhe. Andrew John Chenge kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na Mheshimiwa Dustan Luka Kitandula kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati. Kamati imetupatia maoni na ushauri ambao umesaidia kuboresha taarifa hizi ninazoziwasilisha. Tunaahidi kuipatia Kamati ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake. Aidha, Serikali itaendelea kuzingatia maoni na maelekezo yanayotolewa na Kamati katika hatua mbalimbali za uandaaji na utekelezaji wa mipango ya kitaifa.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wabunge wapya walioteuliwa na Mhe. Rais hivi karibuni. Waheshimiwa hao ni pamoja na: Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb) – Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb) – Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb) -Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) – Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb) – Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb) – Waziri wa Fedha,
4
Mhe. Prof. Sospeter Muhongo – Mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. January Yusuf Makamba (Mb) – Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashid (Mb) – Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb) na Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb) – Naibu Mawaziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Charles Tizeba (Mb) – Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb) – Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Angela Kairuki (Mb) – Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb) – Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Saada Omari Mkuya na Mhe. Janeth Mbene – Wabunge wa Kuteuliwa na Naibu Mawaziri wa Fedha. Aidha, nampongeza Mhe. James Mbatia kwa kuteuliwa kuwa Mbunge. Ninaamini uteuzi wao umezingatia umahiri na umakini katika utendaji kazi ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.
4. Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa kwa ushirikiano aliotoa katika kuandaa Hotuba hii. Aidha, nawashukuru wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango chini ya uongozi wa Ndg. Ramadhani Khijjah, Katibu Mkuu Hazina na Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji Tume ya Mipango. Vilevile napenda niwashukuru wafanyakazi wote wa Taasisi mbili hizi pamoja na Idara na Taasisi zilizo chini yao kwa kufanikisha uandaaji wa Hotuba hii.
5. Mheshimiwa Spika, baada ya maneno ya shukrani naomba sasa nielezee kwa muhtasari taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2011.
5
MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2011
Mapitio ya Mwenendo wa Uchumi wa Dunia
6. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha Duniani, uchumi wa dunia ulikua kwa asilimia 3.9 mwaka 2011 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.3 mwaka 2010. Kiwango kidogo cha ukuaji wa uchumi kilitokana na mtikisiko wa uchumi katika nchi za Ulaya uliosababishwa na miundo tete ya kifedha (financial fragilities), hususan hasara katika sekta ya kibenki, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti kwa nchi nyingi za Ulaya na kukosekana kwa hali ya utulivu katika nchi za kiarabu.
7. Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji wa uchumi katika bara la Afrika kilipungua na kuwa asilimia 2.7 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2010 kutokana na hali mbaya ya kisiasa iliyojitokeza katika nchi za kaskazini mwa Afrika. Kiwango cha ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara nacho kilipungua na kuwa asilimia 5.1 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 5.3 mwaka 2010.
Mapitio ya Mwenendo wa Uchumi wa Taifa
Ukuaji wa Pato la Taifa
8. Mheshimiwa Spika, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 6.4 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010. Kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kulitokana hasa na hali mbaya ya ukame iliyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini ambapo sekta ya kilimo iliathirika zaidi. Aidha, upungufu wa umeme ulichangia kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani na shughuli nyingine zinazohitaji umeme. Pamoja na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, sekta za mawasiliano, huduma
6
za fedha, ujenzi na elimu zilikuwa na ukuaji wa viwango vya juu kati ya asilimia 6 hadi asilimia 19.
9. Mheshimiwa Spika, pamoja na baadhi ya sekta kukua kwa viwango vya juu, ukuaji huu wa uchumi haukupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa kama ilivyotarajiwa kwa sababu sekta zilizokua haraka hazitoi ajira kwa wananchi wengi hasa waliopo vijijini ambao wanategemea kilimo. Kasi ya ukuaji katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri takribani asilimia 75 ya nguvukazi nchini ilipungua, kutoka asilimia 4.2 mwaka 2010 hadi 3.6 mwaka 2011 wakati kasi ya ongezeko la watu imeendelea kuwa juu (asilimia 2.9).
10. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, Pato la Taifa lilikuwa shilingi trilioni 37.5 kwa bei za mwaka 2011. Kutokana na idadi ya watu Tanzania Bara kukadiriwa kuwa watu milioni 43.2 mwaka 2010 na watu milioni 44.5 mwaka 2011, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 869,436.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na shilingi 770,464.3 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 12.8.
Kasi ya Upandaji Bei
11. Mheshimiwa Spika, wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2011 uliongezeka hadi asilimia 12.7 kutoka asilimia 5.5 mwaka 2010. Kuongezeka kwa kasi ya upandaji bei kulichangiwa na: kuendelea kupanda kwa wastani wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia; upungufu wa mvua za vuli katika robo ya nne ya mwaka 2010 ambao ulipunguza mavuno; kupanda kwa bei ya umeme, gesi, mafuta ya kupikia, mchele na sukari; upungufu wa nishati ya umeme; kuporomoka kwa thamani ya shilingi; na upungufu wa chakula katika kanda ya Afrika Mashariki kutokana na hali ya ukame. Mahitaji ya chakula katika nchi za jirani za Kenya, Uganda, Somalia na Sudani ya Kusini yameongeza kasi ya upandaji wa bei za chakula na
7
sukari. Hadi Aprili 2012, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 18.7 ikilinganishwa na asilimia 8.6 Aprili 2011.
12. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati kwa mwaka ulioishia Aprili 2012 uliongezeka hadi asilimia 9.0 kutoka asilimia 5.7 Aprili 2011. Hii ilitokana na kuongezeka kwa bei za mafuta, gharama za usafirishaji na kuongezaka kwa mfumuko wa bei katika nchi zinazofanya biashara na Tanzania hususan China na India (imported inflation). Mfumuko wa bei ya chakula uliongezeka na kufikia asilimia 24.7 Aprili 2012 kutoka asilimia 9.2 Aprili 2011. Mfumuko wa bei ya nishati uliongezeka hadi asilimia 24.9 Aprili 2012 kutoka asilimia 22.1 kwa mwaka ulioishia Aprili 2011.
13. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mfumuko wa bei, Serikali ilichukua hatua zifuatazo: kuhakikisha usambazaji wa chakula katika maeneo yenye uhaba wa chakula; kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula; kuendelea kuimarisha hifadhi ya chakula kwa kuongeza ununuzi wa mazao ya chakula; kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 342 chini ya Mpango wa Dharura; kupandisha kiwango cha riba ya Benki Kuu inayotozwa kwa taasisi za fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58 na kupandisha kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizo zimeweza kupunguza kasi ya upandaji bei kutoka asilimia 19.8 Desemba 2011 hadi asilimia 18.7 Aprili 2012.
Ujazi wa Fedha na Karadha
14. Mheshimiwa Spika, kufikia Desemba 2011, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni 2,008.7 sawa na asilimia 18.2, ikilinganishwa na ongezeko la shilingi bilioni 2,232.4
8
Desemba 2010. Hadi kufikia Machi 2012, ukuaji wa M3 uliongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni 1,767.6 sawa na asilimia 15.7. Ukuaji huu wa M3 ulikuwa chini ya lengo la ukuaji wa asilimia 21.3 Desemba 2011 na asilimia 23.8 Machi 2012. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa asilimia 15.0 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 1,205.8 Desemba 2011 ikilinganishwa na ongezeko la shilingi bilioni 1,438.7 Desemba 2010. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa asilimia 14.8 Machi 2012 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 1,211.8. Kasi ndogo ya ukuaji wa ujazi wa fedha ilitokana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa rasilimali katika fedha za kigeni kwenye benki ikilinganishwa na ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
15. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2012, kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 21.9 ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili lilienda sambamba na kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani (net domestic assets) kwenye benki pamoja na kupungua kwa ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni (net foreign assets) kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa katika: shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9; uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na mawasiliano asilimia 7.9.
Mwenendo wa Viwango vya Riba
16. Mheshimiwa Spika, wastani wa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara ulipungua kidogo hadi asilimia 14.21 Desemba 2011 kutoka asilimia 14.92 Desemba 2010. Vile vile, wastani wa riba za kukopa kwa muda mfupi (hadi mwaka mmoja) ulipungua kutoka asilimia 14.37 Desemba 2010 hadi asilimia 13.73 Desemba 2011.
9
Aidha, wastani wa jumla wa riba za amana za akiba uliongezeka kutoka asilimia 6.09 Desemba 2010 hadi asilimia 7.12 Desemba 2011. Vilevile, wastani wa riba za amana za akiba za muda maalum (miezi 12) uliongezeka hadi asilimia 9.99 Desemba 2011 kutoka asilimia 8.45 Desemba 2010. Kutokana na mwelekeo huo wa riba, tofauti baina ya viwango vya riba za amana na mikopo (mwaka mmoja) ilipungua kutoka asilimia 7.26 Desemba 2010 hadi asilimia 4.59 Desemba 2011. Tofauti hiyo inatokana na kuongezeka kwa ushindani kwa mabenki katika utoaji wa huduma. Aidha, wastani wa riba za amana za akiba uliongezeka na kufikia asilimia 2.90 Desemba 2011 kutoka asilimia 2.43 Desemba 2010.
Thamani ya Shilingi ya Tanzania
17. Mheshimiwa Spika, thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa mwaka 2011 ilishuka kwa asilimia 10.3 hadi wastani wa shilingi 1,579.5 kwa dola moja ya Kimarekani ikilinganishwa na wastani wa shilingi 1,432.3 mwaka 2010. Mwishoni mwa Desemba 2011, bei ya dola ya Kimarekani ilikuwa na thamani ya shilingi 1,587.6 ikilinganishwa na shilingi 1,469.9 mwishoni mwa Desemba 2010. Kushuka kwa thamani ya shilingi kulitokana na: kushuka kwa mauzo nje ikilinganishwa na uagizaji nje; tofauti ya mfumuko wa bei kati Tanzania na nchi inazofanyanazo biashara; ulanguzi au kuotea katika soko la fedha za kigeni (market speculation); na kuimarika kwa dola ya Kimarekani dhidi ya sarafu za mataifa mengine. Hadi Machi, 2012 thamani ya shilingi ilikuwa wastani wa shilingi 1,588 kwa dola moja ya Kimarekani.
10
Sekta ya Nje
18. Mheshimiwa Spika, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje iliongezeka kwa asilimia 17.1 mwaka 2011 na kufikia dola milioni 6,796.3 kutoka dola milioni 5,805.0 mwaka 2010. Ongezeko la mauzo nje lilichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa asilia (kahawa, tumbaku, karafuu na korosho) na bidhaa zisizo asilia hasa madini, na mapato yatokanayo na huduma za utalii na usafirishaji. Uagizaji wa bidhaa na huduma uliongezeka kwa asilimia 33.0 kutoka Dola za Kimarekani milioni 9,017.9 mwaka 2010 hadi dola milioni 11,992.3 mwaka 2011. Ongezeko hilo lilitokana hasa na uagizaji wa mafuta na mitambo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la umeme.
Akiba ya Fedha za Kigeni
19. Mheshimiwa Spika, hadi Desemba 2011, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni 3,761.2 ikilinganishwa na dola milioni 3,948.0 Desemba 2010, sawa na upungufu wa asilimia 4.7. Kiasi hiki cha akiba ya fedha za kigeni kwa mwaka 2011 kilikuwa na uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 3.8 ikilinganishwa na miezi 5.3 iliyofikiwa mwaka 2010.
Uwekezaji Mitaji ya Kigeni ya Moja kwa Moja
20. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, thamani ya mitaji ya kigeni ya moja kwa moja iliongezeka kwa asilimia 97 na kufikia dola za Kimarekani milioni 854.2 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 433.9 mwaka 2010. Ongezeko hili kubwa lilitokana na uwekezaji mkubwa wa utafiti wa gesi katika mikoa ya Mtwara na Pwani ambayo uligharimu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 300. Sekta zilizoongoza katika kupokea idadi kubwa ya miradi kutoka nje ni uzalishaji wa bidhaa viwandani, utalii, majengo ya biashara na usafirishaji.
11
Bajeti y a Serikali
Mapato
21. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012, mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 5,180.6, sawa na asilimia 98 ya makisio ya kukusanya shilingi bilioni 5,217.2. Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 4,765.5, sawa na asilimia 104 ya makadirio ya shilingi bilioni 4,585.5. Ongezeko hili lilitokana na hatua za kiutawala zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
22. Mheshimiwa Spika, mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 272.1, sawa na asilimia 57 ya lengo la shilingi bilioni 473.5. Mapato ya Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 143 sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 237.8. Ukusanyaji huo mdogo wa mapato yasiyo ya kodi ulitokana na kushindwa kwa mashirika na taasisi kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali kama ilivyotarajiwa. Serikali inakusudia kufanya tathmini ya mifumo ya ukusanyaji mapato yasiyo ya kodi kwenye Wizara zenye utaratibu wa kukusanya maduhuli kwa lengo la kuiboresha.
Matumizi
23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/11, matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 9,439.4, sawa na asilimia 87.0 ya makadirio. Matumizi halisi kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012 yalikuwa shilingi bilioni 8,676.8, sawa na asilimia 97.5 ya makadirio ya shilingi bilioni 8,895.8.
12
Misaada na Mikopo
24. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012, Serikali ilipokea misaada na mikopo ya kibajeti ya jumla ya shilingi bilioni 735 ambazo ni asilimia 85 ya makadirio ya shilingi bilioni 869.4 katika kipindi hicho.
Deni la Taifa
25. Mheshimiwa Spika, deni la Taifa limeongezeka kufikia shilingi bilioni 20,276.6 katika kipindi kilichoishia Machi 2012 kutoka shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011, sawa na ongezeko la asilimia 15.4. Kati ya fedha hizo, shilingi 15,306.9 bilioni ni deni la nje ambapo shilingi bilioni 12,342.5 ni deni la umma na kiasi kilichosalia ni deni la sekta binafsi. Hadi Machi 2012, deni la ndani lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,496.5 Machi 2011, sawa na ongezeko la asilimia 10.5.
26. Mheshimiwa Spika, hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali itakayosomwa leo jioni itabainisha kwa kina mwenendo wa mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2011/12 na makadirio ya mwaka 2012/13.
USHIRIKIANO WA KIUCHUMI KIKANDA NA KIMATAIFA
27. Mheshimiwa Spika, ushirikiano wa Tanzania kimataifa na kikanda uliendelea kuimarika na hivyo kuendelea kulijengea Taifa mazingira mazuri ya shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika mwaka 2011, miradi mbalimbali ya maendeleo ya kikanda iliendelea kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90; ujenzi wa barabara ya Arusha-Namanga-Athi-River
13
umefikia asilimi 90: na Tanga-Horohoro asilimia 67.5; na hati ya makubaliano (MoU) ya mradi wa kufua umeme ulioko Murongo/Kikagati umesainiwa kati ya Tanzania na Uganda.
28. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa biashara baina ya Tanzania na nchi za kikanda umezidi kuimarika ambapo mauzo nje yaliongezeka kwa asilimia 75.3 kufikia dola za kimarekani milioni 1,222.4 kwa nchi za SADC na asilimia 12.8 kufikia dola za kimarekani milioni 368.4 kwa nchi za EAC. Uagizaji kutoka nchi za SADC na EAC nao pia uliongezeka kufikia dola za kimarekani milioni 1,199.7 na dola za kimarekani milioni 385.3, sawa na ongezeko la asilimia 36.6 na asilimia 30.3 kwa mtiririko huo. Bidhaa zilizochangia ongezeko hilo ni pamoja na dhahabu, vyandarua, mchele, saruji, chai na vyombo vya majumbani.
MAENDELEO KATIKA SEKTA ZA KIUCHUMI NA KIJAMII
29. Mheshimiwa Spika, napenda nielezee kwa ufupi ukuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali. Mawaziri wa wizara husika wataeleza kwa kina maendeleo katika maeneo yao; hivyo nitatoa tathmini ya kiujumla tu ya maendeleo katika baadhi ya maeneo hayo.
Kilimo, Mifugo, Misitu na Uwindaji
30. Mheshimiwa Spika, shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao; mifugo; na misitu na uwindaji zilikua kwa kiwango cha asilimia 3.6 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2010. Upungufu huu ulitokana na kuchelewa kwa mvua za msimu kwa mwaka 2009/10 ambazo ziliathiri uzalishaji wa mazao. Aidha, mchango wa shughuli za kiuchumi za kilimo ulikuwa
14
asilimia 23.7 ya Pato la Taifa mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 24.1 mwaka 2010.
Uvuvi
31. Mheshimiwa Spika, shughuli za kiuchumi katika uvuvi zilikua kwa kiwango cha asilimia 1.2 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 1.5 mwaka 2010. Kushuka huku kwa ukuaji katika sekta ndogo ya uvuvi kulitokana na matumizi ya zana duni za uvuvi, uharibifu wa mazalia ya samaki na kuongezeka kwa ushindani katika soko la dunia. Mchango wa shughuli za uvuvi katika Pato la Taifa uliendelea kubakia asilimia 1.4 kama ilivyokuwa mwaka 2010.
Viwanda na Ujenzi
32. Mheshimiwa Spika, sekta ya viwanda na ujenzi inajumuisha: uzalishaji bidhaa viwandani; umeme na gesi; usambazaji wa maji; madini; uchimbaji wa mawe na ujenzi. Shughuli za kiuchumi katika sekta ya viwanda na ujenzi zilikua kwa kiwango cha asilimia 6.9 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 8.2 mwaka 2010. Kupungua kwa ukuaji kulitokana na ukuaji mdogo katika shughuli ndogo zote. Mchango wa shughuli za kiuchumi za viwanda na ujenzi katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 22.4 mwaka 2010 hadi asilimia 22.7 mwaka 2011.
33. Mheshimiwa Spika, shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilikua kwa kiwango cha asilimia 7.8 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 7.9 mwaka 2010. Kupungua kwa kasi ya ukuaji kulitokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kutokana na upungufu wa nishati ya umeme na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa malighafi za viwandani, hususan mafuta. Aidha, mchango wa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani katika Pato la
15
Taifa uliongezeka kutoka asilimia 9.0 mwaka 2010 hadi asilimia 9.3 mwaka 2011.
34. Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya umeme na gesi ilikua kwa asilimia 1.5 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 10.2 mwaka 2010. Upungufu huu ulitokana na kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya Mtera na Kihansi; uchakavu wa mitambo ya umeme; na ukarabati wa mitambo ya Songas uliosababisha kusimama kwa uzalishaji wa umeme wa gesi kwa muda. Mchango wa shughuli za kiuchumi katika umeme na gesi ulikuwa asilimia 1.8 katika Pato la Taifa mwaka 2011 kama ilivyokuwa mwaka 2010.
35. Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya ujenzi ilikua kwa kiwango cha asilimia 9.0 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 10.2 mwaka 2010. Ukuaji huo ulichangiwa hasa na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi wa: barabara na madaraja; majengo ya kuishi na yasiyo ya kuishi; na upanuzi wa miundombinu ya maji na barabara. Mchango wa shughuli za ujenzi katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 8.0 mwaka 2011 kama ilivyokuwa mwaka 2010.
36. Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya usambazaji maji ilikua kwa kiwango cha asilimia 4.0 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 6.3 mwaka 2010. Kasi ndogo ya ukuaji ilitokana na ukame uliotokea katika maeneo mengi nchini na uchakavu wa mitambo. Mchango wa shughuli za maji katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 0.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 0.4 mwaka 2010.
Huduma
37. Mheshimiwa Spika, sekta ya utoaji huduma inajumuisha biashara na matengenezo; uchukuzi; mawasiliano; hoteli na migahawa; utawala; elimu; afya; huduma za fedha na bima; na upangishaji wa majengo. Kiwango cha ukuaji
16
wa shughuli za kiuchumi katika utoaji huduma kilikuwa asilimia 7.9 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 8.2 mwaka 2010. Mchango wa shughuli za utoaji huduma katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 44.0 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 43.9 mwaka 2010.
38. Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya mawasiliano katika mwaka 2011 iliendelea kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha ukuaji ikilinganishwa na shughuli nyingine za kiuchumi. Kiwango cha ukuaji katika shughuli za mawasiliano kilikuwa asilimia 19.0 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 22.1 mwaka 2010. Ukuaji huu ulichangiwa na kuongezeka kwa wateja wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi. Mchango wa shughuli za mawasiliano katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 2.2 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 2.1 mwaka 2010.
39. Mheshimiwa Spika, shughuli za biashara na matengenezo zilikua kwa asilimia 8.1 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 8.2 mwaka 2010. Ukuaji huo ulichangiwa na kuimarika kwa biashara ya kikanda. Upungufu wa umeme uliathiri shughuli za biashara na matengenezo na kupunguza kasi ya ukuaji katika sekta. Mchango wa shughuli ndogo za biashara na matengenezo katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 12.2 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 12.1 mwaka 2010.
40. Mheshimiwa Spika, viwango vya ukuaji katika shughuli za utoaji huduma za elimu na afya vilikuwa asilimia 7.4 na 5.4 mwaka 2011, ikilinganishwa na asilimia 7.3 na 6.9 mwaka 2010 kwa mtiririko huo. Ukuaji katika shughuli za utoaji huduma za elimu ulitokana na kuendelea kwa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM II); Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES); na kuongezeka kwa ajira mpya za walimu. Kwa upande wa shughuli za huduma za
17
afya, ukuaji ulichangiwa na utekelezaji wa programu za chanjo, malaria, kifua kikuu na VVU/UKIMWI. Mchango wa shughuli za huduma za afya katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 1.7 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 1.6 mwaka 2010. Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, sekta ndogo ya elimu ilikuwa ikichangia asilimia 1.4 katika Pato la Taifa kila mwaka.
MASUALA MTAMBUKA
Idadi ya Watu
41. Mheshimiwa Spika, kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, inakadiriwa kuwa idadi ya watu Tanzania kwa mwaka 2011 ilikuwa watu milioni 44.5 ikilinganishwa na watu milioni 43.2 mwaka 2010. Kati yao, wanawake walikuwa milioni 22.6, sawa na asilimia 50.7 na wanaume walikuwa milioni 21.9. Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu milioni 43.2 sawa na asilimia 97.0 na Tanzania Zanzibar ilikuwa na watu milioni 1.3. Mgawanyo wa watu unaonesha kuwa asilimia 73.3 wanaishi vijijini na asilimia 26.7 wanaishi mijini.
42. Mheshimiwa Spika, msongamano wa watu kimkoa unaonesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam, una msongamano mkubwa wa watu (2,294) kwa kilometa moja ya mraba, ukifuatiwa na Mwanza watu 186, Kilimanjaro watu 126 na Mara watu 87. Mkoa uliokuwa na kiwango kidogo cha msongamano wa watu ni Lindi yenye watu 14 kwa kilometa ya mraba. Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, mkoa wa Mjini Magharibi ulikuwa na msongamano mkubwa wa watu 2,152 kwa kilometa ya mraba na mkoa wa Kusini Unguja ulikuwa na msongamano mdogo wa watu 135 kwa kilometa ya mraba.
18
UKIMWI
43. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, Serikali iliendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI kwa kutoa huduma za tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI, ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya UKIMWI kwa hiari. Aidha, Serikali iliendelea kuboresha huduma hizi kwa kuhakikisha kuwa dawa za kupunguza makali ya VVU zinapatikana katika vituo vya kutoa huduma. Mwaka 2011, watu milioni 14.9 walipata ushauri nasaha na kupima virusi vya UKIMWI kwa hiari ikilinganishwa na watu milioni 8.9 mwaka 2010. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka kwa watoa mafunzo mbalimbali na ushauri nasaha pamoja na kuongezeka kwa vituo vya kutoa ushauri nasaha na vipimo.
Mazingira
44. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2011, Serikali iliendelea kuwahimiza wawekezaji kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira katika uwekezaji kwa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla na baada ya kutekeleza miradi yao. Katika kipindi hiki, jumla ya miradi ya maendeleo 467 ya uwekezaji ilisajiliwa kwa ajili ya kufanyiwa TAM. Kati ya miradi hiyo, miradi 163 ilipata hati za TAM baada ya kukidhi vigezo ikilinganishwa na miradi 220 mwaka 2010. Aidha, kati ya miradi iliyopewa hati za TAM mwaka 2011, miradi 44 ilikuwa ya mawasiliano; 36 ya viwanda; 28 ya nishati; 17 ya miundombinu; 16 ya ujenzi na uendelezaji kwenye vivutio vya utalii; 12 maji; 7 ya uchimbaji wa madini; na miradi mitatu ilikuwa ya misitu na kilimo.
45. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Mkakati huu wa
19
miaka mitano unaweka mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kusaidia kupunguza gesijoto.
PROGRAMU NA MIKAKATI MBALIMBALI YA MAENDELEO
MKUKUTA NA MALENGO YA MAENDELEO YA MILENIA (MDGS)
46. Mheshimiwa Spika, Tanzania inaendelea kuchukua hatua katika kufikia malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo uwezekano wa kufikia malengo kwa muda uliobaki ni mdogo, hususan katika viashiria vya afya. Vifo vya watoto wachanga na walio na umri wa chini ya miaka mitano viliendelea kupungua japo siyo kwa kasi inayoweza kufikia malengo ya milenia. Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba huduma za afya kwa ujumla wake zinaboreshwa. Kuhusiana na hatua za kudhibiti malaria mwaka 2011, Serikali ilisambaza vyandarua bila malipo katika kaya, katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Jumla ya vyandarua vyenye dawa milioni 17.6 viligawiwa katika kampeni hii. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kuharibu mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kinachojengwa Kibaha katika mkoa wa Pwani. Hatua hizo, pamoja na punguzo la bei za dawa ya mseto ya kutibu malaria ziliimarisha udhibiti wa ugonjwa wa malaria.
47. Mheshimiwa Spika, kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI kilipungua hadi asilimia 2.4 kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 24 ikilinganishwa na lengo la mwaka 2015 la asilimia 1.2. Aidha, kulikuwa na maendeleo mazuri katika viashiria vinavyohusiana
20
na usawa wa jinsia na elimu lakini changamoto iliyopo ni utoaji wa elimu bora hususan, kuimarisha mazingira ya kujifunza na kufundishia. Changamoto nyingine ni kuongeza kasi ya kupunguza umasikini wa wananchi wanaoishi kwa kiwango cha chini ya dola moja kwa siku. Serikali pia inaendelea kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini pamoja na ujenzi wa nyumba bora.
48. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa MKUKUTA-II, matokeo kadhaa yamepatikana kutokana na utekelezaji wa programu mbalimbali. MKUKUTA-II kama ulivyokuwa ule wa kwanza unatekelezwa kupitia programu na michakato ya kitaifa, kisekta na ile iliyo chini ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa pato la wastani la kila mtu kutoka shilingi 770,464.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi 869,436.3 mwaka 2011, kuongezeka kwa uwiano wa kujitosheleza kwa chakula kutoka asilimia 102 mwaka 2010 hadi asilimia 112 mwaka 2011, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma katika ngazi zote, kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na kuboresha sekta za elimu, afya na maji. Kiwango cha ukuaji wa uchumi mwaka 2011 kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010. Ukuaji huu ni chini ya shabaha ya MKUKUTA-II ya kuwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 8 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2015.
49. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mambo yanayohitaji mjadala zaidi na kupewa kipaumbele kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha utekekelezaji wa awamu ya pili ya MKUKUTA, yamechambuliwa kwa kina katika taarifa ya utekelezaji kwa mwaka 2010/11.
21
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
50. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, Serikali iliendelea na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kupitia mifuko yake ya uwezeshaji iliendelea kutoa mikopo yenye mashariti nafuu kwa wananchi. Mifuko hii ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi uliotoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.6 zilizotolewa mwaka 2010, Mfuko wa Rais wa kutoa mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini uliotoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 6.8 kwa walengwa 167,372 na Mfuko wa kuwezesha wakulima ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 49.45 kwa wakulima na wasambazaji wa pembejeo za kilimo. Aidha, Serikali kupitia Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 49.23 kwa wajasiriamali 72,912 ikilinganishwa na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 47.14 iliyotolewa kwa wajasiriamali 72,179 mwaka 2010.
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA MWAKA 2012/13
51. Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea mapitio ya hali ya uchumi kwa mwaka 2011, sasa naomba nielezee kwa muhtasari Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13.
52. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa katika Bunge la mwezi Aprili 2012, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilileta mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13. Hotuba hii ninayoiwasilisha inafafanua kwa muhtasari misingi, malengo na miradi ya maendeleo ambayo Serikali inakusudia kuitekeleza katika mwaka 2012/13 kwa kuzingatia mfumo wa Mpango uliopitishwa na Bunge.
22
MISINGI NA MALENGO YA UCHUMI NA MAENDELEO YA JAMII MWAKA 2012/13
53. Mheshimiwa Spika, malengo ya uchumi jumla na maendeleo ya jamii na mpango wa maendeleo katika mwaka 2012/13 yatakuwa yafuatayo:
i. Pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia 6.8 mwaka 2012, na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 8.5 mwaka 2016;
ii. Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ipungue hadi viwango vya tarakimu moja kutoka asilimia 18.7 Aprili 2012;
iii. Kuongeza mapato ya ndani yafikie asilimia 16.9 ya Pato la Taifa Juni 2012 na asilimia 18.0 mwaka 2012/13;
iv. Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia 18.0 mwishoni mwa Juni 2013, utakaowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi, na kasi ya upandaji bei;
v. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.5;
vi. Kuongeza mauzo ya bidhaa nje kufikia asilimia 23.1 mwaka 2011/12 na asilimia 24.3 mwaka 2012/13;
vii. Kupunguza tofauti ya viwango vya riba za akiba na zile za kukopa;
viii. Mikopo kwa sekta binafsi ikue kwa kiwango cha asilimia 20.0 Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei; na
23
ix. Kuimarisha thamani ya shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
54. Mheshimiwa Spika, malengo tuliyokusudia ya uchumi jumla na Mpango katika kipindi cha mwaka 2012/13 yatafikiwa kwa kuzingatia misingi ifuatayo:-
i. Kuendelea kuimarika kwa amani, utulivu na utengamano;
ii. Viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii vitaendelea kutengamaa na kuimarika;
iii. Mapato ya ndani yataongezeka ili kuweza kugharamia utekelezaji wa maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango;
iv. Maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano yatazingatiwa;
v. Rasilimali zitaelekezwa kwenye maeneo ya miradi ya kimkakati na miradi muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kwa haraka zaidi kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2012/13;
vi. Kuendelea kutekeleza MKUKUTA II;
vii. Kuendelea kuimarisha usimamizi wa fedha za umma;
viii. Kuendelea kuimarisha sera za fedha ili ziendane na sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za amana na za mikopo;
24
ix. Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uchumi, hususan katika ugharamiaji wa miradi ya miundombinu; na
x. Kuendelea kuimarisha mahusiano na Washirika wa Maendeleo na nchi marafiki yataendelea kuimarika.
55. Mheshimiwa Spika, miradi ambayo serikali inakusudia kutekeleza katika mwaka 2012/13 imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Kwanza ni miradi ya kitaifa ya Kimkakati ambayo utekelezaji wake utaleta matokeo ya haraka na kuweka msingi thabiti wa kufika malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Sehemu ya pili ni miradi mingineyo katika maeneo muhimu ya kiuchumi ambayo utekelezwaji wake unatarajiwa kuwezesha ukuaji wa haraka wa uchumi ambao ni shirikishi na kupunguza kiwango cha umaskini.
I. MIRADI YA KITAIFA YA KIMKAKATI
56. Mheshimiwa Spika, katika kuainisha miradi ya kitaifa ya kimkakati, mambo muhimu yaliyozingatiwa ni pamoja na: miradi yenye kuleta matokeo ya haraka, hususan katika kuchochea maendeleo ya maeneo mengine (multiplier effect); uwezo wa mradi husika kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, na hivyo kuongeza ajira; kukabiliana na matatizo ya kiuchumi yaliyopo sasa kama vile mfumuko wa bei; na kuongeza mapato ya Serikali.
25
57. Mheshimiwa Spika, baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Biashara na Uwekezaji Kurasini (Kurasini Logistic/Trade Hub); uimarishaji wa Reli ya Kati: katika maeneo ya Tabora – Kigoma, Isaka–Mwanza; ukarabati wa reli (kilomita 197) katika kiwango cha – 80lb/yards; ununuzi wa vifaa kwa ajili ya ukarabati wa reli (kilomita 197-80lbs/yd; ukarabati na uboreshaji wa njia ya reli katika eneo la Kidete–Gulwe; ujenzi wa daraja la Bahi–Kintinku; na ukarabati wa injini na mabehewa ya treni. Aidha, fedha zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu wa njia ya reli katika maeneo ya kimkakati, reli ya Mtwara – Mbamba Bay/Mchuchuma na Liganga; reli kutoka Dar es Salaam – Isaka – Kigali-Keza/Geita–Msongati, na reli ya Tanga (Mwambani) – Arusha – Musoma.
58. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nishati ya umeme, fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya Ujenzi wa Bomba la Gesi (Mtwara – Dar es Salaam) na mitambo ya kufua Umeme Kinyerezi (MW 150 & MW 240). Aidha, kwa upande wa usambazaji; fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi na uimarishaji wa njia za umeme wa msongo: 220kV North – West Grid; 400 Kv Iringa – Shinyanga; na kV 132 Makambako – Songea. Vile vile, miradi ya upelekaji umeme vijijini imetengewa fedha kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo vijijini.
59. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya barabara, miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa kiuchumi; zinazounganisha Tanzania na nchi jirani; zinazosaidia kupunguza msongamano mijini pamoja na ujenzi wa madaraja na vivuko.
26
60. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya kilimo na viwanda, miradi itakayotekelezwa inajumuisha ile ya kilimo cha miwa na mpunga katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kagera, Kilombero, na Malagalasi; miradi katika Ukanda wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT); ASDP na miradi ya kilimo cha umwagiliaji. Katika eneo la viwanda: miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ile ya chuma na makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, kukamilisha Kiwanda cha Viuadudu Kibaha; Mradi wa Magadi soda-Bonde la Engaruka; na uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZs & SEZs). Aidha, Serikali italipa fidia katika maeneo maalum (EPZ) ya Bagamoyo na Kigoma.
61. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya huduma za kifedha, Serikali itaongeza mtaji katika benki ya wanawake ili kuweza kuhimili ushindani katika soko na kuwa benki ya kibiashara. Aidha, Serikali itawezesha uanzishwaji wa benki ya maendeleo ya kilimo ili kutoa mikopo na huduma za kibenki kwa wakulima na wawekezaji.
62. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ambayo Serikali itatekeleza miradi ya maendeleo ya kimkakati yameelezewa kwa kina katika sura ya tatu ya kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13.
II. MIRADI MINGINE MUHIMU KWA UKUAJI WA UCHUMI
63. Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi ya kimkakati, miradi mingine katika maeneo muhimu ya kiuchumi itaendelezwa ili kuwezesha ukuaji wa haraka wa uchumi ambao ni shirikishi. Miradi hii itagharamiwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi na washirika wa maendeleo. Miradi hii ilichaguliwa kwa kuzingatia miradi inayoendelea, miradi yenye masharti ya kimkataba, na miradi ambayo ina fedha za wahisani.
27
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, miradi itakayotekelezwa katika eneo la elimu na mafunzo ya ufundi itajumuisha: uendelezaji wa ujenzi wa vyumba vya mihadhara, maktaba, mabweni ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya Dar es salaam, Sokoine, Dodoma, Mzumbe, Ardhi, Ushirika Moshi, Ualimu Dar es Salaam na Mkwawa; uendelezaji wa vyuo vya ufundi –VETA; ujenzi wa chuo Kikuu cha Muhimbili sehemu ya Mloganzira; kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES I); ukarabati wa miundombinu katika vyuo vitano vya ualimu; na ujenzi na ukarabati wa Maktaba ya Mkoa, Dodoma. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itaweka nguvu kuandaa watalaam katika fani maalum (urani, gesi na mafuta).
65. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Afya, programu na miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: Mpango wa usimamizi wa sekta ya Afya; kuwezesha programu ya kupunguza vifo vya kinamama wajawazito; kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya magonjwa ya Saratani Ocean Road, Kituo cha Tiba ya Magonjwa ya Moyo kilichopo Hospitali ya Muhimbili na kujenga na kukarabati majengo ya hospitali za mikoa wa Mtwara, Mara na Lindi.
66. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya mifugo na uvuvi, programu na miradi itakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2012/13 ni pamoja na: kuendelea kutekeleza Programu ya ASDP katika sekta ya mifugo; kuwezesha mfumo wa utambuaji na ufuatiliaji wa mifugo; na kutekeleza Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Viumbe wa Bahari katika Ukanda wa Pwani.
28
67. Mheshimiwa Spika, katika eneo la misitu na wanyamapori, miradi itakayotekelezwa ni: kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, wanyamapori na misitu; na kujenga uwezo wa kitaasisi kwa ajili ya usimamizi wa utoaji wa hewa-ukaa.
68. Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati na madini, miradi itakayotekelezwa ni: ujenzi wa ofisi za madini za mikoa ya Mtwara, Dodoma, Geita na Arusha; ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini na Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini; na kuimarisha taasisi zinazoshughulika na tafiti za utafutaji na usimamizi wa madini.
69. Mheshimiwa Spika, katika eneo la ardhi, nyumba na makazi, miradi itakayotekelezwa ni kuanza ujenzi wa mji mpya wa kisasa Kigamboni (satellite city). Aidha, Serikali inatarajia kuanzisha benki-ardhi kwa ajili ya kupata maeneo ya kilimo cha biashara na chakula.
70. Mheshimiwa Spika, katika eneo la usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni: ukarabati viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Mwanza, Kigoma, Tabora, Songwe, Mpanda, Arusha na Bukoba; uendelezaji wa gati nambari nane katika ziwa Tanganyika; na matengenezo ya ndege za Serikali. Aidha, katika eneo la hali ya hewa, shughuli zitakazotekelezwa ni: ununuzi wa vifaa na rada kwa ajili ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania; na kuwezesha vituo vya taarifa ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kuwa na vifaa vya kisasa.
71. Mheshimiwa Spika, katika eneo la maendeleo ya teknolojia na ubunifu, miradi itakayotekelezwa ni: kuendeleza ubunifu katika kuzalisha zana za kilimo zinazoendana na teknolojia ya kisasa kwa kuimarisha Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC); na
29
kuimarisha taasisi za tathmini na ufuatiliaji wa viwango vya bidhaa vinavyohitajika katika soko hususan chakula kwa kuendeleza taasisi ya TIRDO.
72. Mheshimiwa Spika, katika eneo la utawala bora, shughuli zitakazotekelezwa ni: kuimarisha miundombinu na vitendea kazi kwa ajili ya Sekratarieti ya Maadili ya Viongozi na TAKUKURU; kujenga uwezo wa wataalam katika sekta ya sheria na kuongeza vitendea kazi; ununuzi wa vitendea kazi kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia na mali zao na wawekezaji; na ujenzi wa miundombinu muhimu katika sekta ya sheria na utoaji haki.
73. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2012/13, Serikali itaendelea na zoezi la kuandikisha raia ili waweze kupatiwa vitambulisho vya Taifa. Utambulisho wa kitaifa unalenga kuwa na mfumo mzuri wa kuwezesha wananchi na mali zao kutambulika rasmi na kuchangia katika shughuli za kiuchumi na maendeleo. Kukamilika kwa mfumo huu kutaongeza tija na ufanisi katika kuwezesha wananchi kupata mikopo, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
74. Mheshimiwa Spika, katika eneo la kazi na ajira, shughuli zitakazotekelezwa ni: kuwezesha mifuko inayotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana, wanawake na makundi maalum ili kutoa fursa za kupata mitaji ambayo itawawezesha kujiajiri wenyewe. Aidha, Serikali itaimarisha mifumo ya ukaguzi katika sehemu za kazi, usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya kikazi, usimamizi na udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii na ukuzaji wa ajira.
Sensa ya Watu na Makazi 2012
75. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012 ni mwaka wa Sensa ya
30
Watu na Makazi ikiwa ni miaka kumi baada ya sensa ya mwisho kufanyika nchini mwaka 2002. Tarehe 26 Agosti, 2012 ni siku ya Sensa nchini. Kaulimbiu ya mwaka huu ni SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA. Maandalizi ya zoezi hili yanaratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge watakuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha na kuwahimiza wananchi wajiandae na washiriki kikamilifu katika kuhesabiwa.
Maandalizi ya Katiba Mpya
76. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, Serikali ilianza mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya. Katika kutekeleza hilo, Serikali imeunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya. Tume hiyo inaundwa na wajumbe 30 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na inaongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba. Tume ilianza kazi rasmi Mei, 2012 na inatarajiwa kukamilisha kazi hii baada ya miezi 18.
GHARAMA ZA KUTEKELEZA MPANGO
77. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa mwaka 2012/13, shilingi trilioni 4.527 zitetengwa kwa ajili ya kugharamia Mpango. Kati ya fedha hizo shilingi 2.213 trilioni ni fedha za ndani, na shilingi trilioni 2.314 ni fedha za nje. Katika fedha za ndani, shilingi trilioni 1.135 zimetegwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya kimkakati na shilingi trilioni 1.078 zimetengwa kwa ajili ya miradi mingine kwenye maeneo muhimu kwa ukuaji wa uchumi.
31
KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO
78. Mheshimiwa Spika, katika uandaaji wa Mpango tumezingatia changamoto ambazo zinaweza kujitokeza kama vikwazo wakati wa utekelezaji wa Mpango. Vikwazo ambavyo vinaweza kupunguza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka ni pamoja na: upatikanaji na uchelewashaji wa fedha za misaada na mikopo; upatikanaji na ukamilishaji wa mikataba ya wawekezaji na wabia; na mabadiliko ya tabia-nchi.
79. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vikwazo mbalimbali vya utekekelezaji wa Mpango, itailazimu Serikali ichukue hatua zifuatazo: kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato hususan yasiyo ya kodi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kurasimisha sekta isiyo rasmi; kuharakisha zoezi la tathmini ya nchi kuweza kukopa katika masoko ya fedha na mitaji kimataifa; na kuimarisha mifumo ya tahadhari na kujikinga na majanga (disaster preparedness and surveillance).
UFUATILIAJI NA TATHMINI
80. Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji na tathmini utafuata utaratibu wa kawaida wa utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi. Ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya Kitaifa ya kimkakati utafanywa na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango pamoja na taasisi husika. Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI itafanya tathmini na ufuatiliaji wa miradi katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na taarifa zake kuwasilishwa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha.
32
HITIMISHO
81. Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hali ya uchumi wa Taifa, matarajio, misingi na malengo ya mpango na bajeti kwa kipindi cha mwaka 2011/12 ni wazi kwamba hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa zimeweza kuzaa matunda yaliyotarajiwa. Katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2012/13 juhudi zitaendelea kuelekezwa katika kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaimarika zaidi, kupunguza mfumuko wa bei kwa kuongeza uzalishaji wa chakula pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika, na kuzalisha ajira hasa kwa vijana, wanawake na makundi maalum.
82. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.