Hotuba ya Waziri wa Fedha Akiwakilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi 2014/15 (Bajeti-2014/15)

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum (Mb)

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum (Mb)


HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA SAADA MKUYA SALUM (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2014/15
12 JUNI, 2014 DODOMA

1
I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu za Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni makisio ya mapato; Kitabu cha Pili ni makisio ya matumizi ya kawaida kwa wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali; Kitabu cha Tatu ni makisio ya matumizi ya kawaida kwa mikoa na mamlaka za serikali za mitaa; na Kitabu cha Nne ni makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali, mikoa na mamlaka za serikali za
2
mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014 ambao ni sehemu ya bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wakati nikiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Fedha, Wizara ilipata pigo kwa kuondokewa na aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa. Marehemu Dkt. Mgimwa alikuwa ni mtaalamu wa masuala ya fedha, hivyo kwa kipindi kifupi alichokaa Wizarani aliweza kutumia taaluma yake ipasavyo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kusisitiza ukusanyaji wa mapato ya ndani na nidhamu ya matumizi kwa lengo la kupunguza utegemezi. Aidha, marehemu Dkt. Mgimwa alizingatia sheria, taratibu na kanuni katika
3
kutekeleza majukumu yake ambayo ndio msingi mkuu aliotuachia ambao tunautumia na tutaendelea kuutumia. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, amina.
3. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyokuwa nayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kuwa nitatekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini, weledi na uaminifu mkubwa. Aidha, napenda kuwashukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda kwa
4
miongozo yao ya kila wakati katika kufanikisha majukumu ya uandaaji wa bajeti. Vilevile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Adam Kighoma Malima (Mb) na Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri wa Fedha. Kadhalika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano wake mkubwa aliotupa wakati wa matayarisho ya bajeti hii. Kadhalika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa vikao vya Bunge kwa kuongoza majadiliano vizuri bungeni.
5
4. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani kwa wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na wadau mbalimbali kwa kushiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya bajeti hii. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mb) kwa kuchambua kwa kina bajeti za mafungu yote na kutoa mapendekezo na ushauri. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya Bajeti hii.
6
5. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha SMT; Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha SMZ; Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Viongozi Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; wakuu wa idara, vitengo na watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika maandalizi ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014 na nyaraka mbalimbali za kisheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii. Aidha, ninamshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha nyaraka zote za Bajeti kwa usahihi na kwa wakati.
7
6. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2014/15, imezingatia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II). Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
7. Mheshimiwa Spika, Awamu ya pili ya MKUKUTA inafikia tamati Juni 2015, hivyo Bajeti hii ni ya mwisho katika utekelezaji wa MKUKUTA II. Aidha, Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yametumika kama sehemu ya mikakati yetu ya
8
kupunguza umaskini yanafikia tamati mwaka 2015. Hata hivyo, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 utafikia tamati Juni 2016. Hii inamaanisha kwamba MKUKUTA II utafikia ukomo mwaka mmoja kabla ya ukomo wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo. Kazi iliyo mbele yetu ni kutafuta jinsi masuala ya kupunguza umaskini yatakavyooanishwa katika mikakati na mipango yetu baada ya Juni 2015 wakati tunaelekea kuhitimisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano mwaka 2016. Hivyo basi, Serikali inafanya mapitio ya MKUKUTA II na kuandaa mapendekezo ya namna ya kuoanisha masuala muhimu ya kupambana na umaskini katika mipango yetu baada ya Juni 2015.
9
Lengo ni kuwa na Mwongozo mmoja wa kuelekeza shughuli za maendeleo kwa Taifa letu.
8. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imelenga kupunguza gharama za maisha ya wananchi kwa kuendelea na jitihada za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei, kuendelea kuboresha huduma za jamii, kuboresha miundombinu ya barabara, umeme na umwagiliaji, kuongeza mishahara ya watumishi wa umma, kuendelea kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha utawala bora. Aidha, bajeti hii imezingatia pia maandalizi ya Katiba mpya; uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014; na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
10
9. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii vilevile imelenga kupunguza misamaha ya kodi. Serikali imewasilisha kwenye Bunge hili Muswada wa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa. Lengo la Muswada huu ni kupunguza misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kubakiza misamaha yenye tija kwa uchumi na ustawi wa jamii na kuleta usawa na haki katika ulipaji kodi. Aidha, Serikali imewasilisha Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi hapa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa. Katika Muswada wa Sheria ya Fedha 2014 nimependekeza pia mabadiliko kadhaa ya Sheria za Kodi, kama nitakavyoeleza baadae, kwa lengo la kupunguza misamaha ya kodi.
11
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge sote kwa pamoja tuunge mkono jitihada hizi za Serikali ambazo zitasaidia kupunguza misamaha ya kodi na kurahisisha usimamizi wa kodi nchini na hivyo kutoa unafuu kwa walipa kodi, na kuongeza mapato ya Serikali.
10. Mheshimiwa Spika, sambamba na kupunguza misamaha ya kodi na kuongeza haki na usawa katika kutoa misamaha hii, kuanzia mwaka 2014/15, Serikali itachukuwa hatua kuu mbili muhimu. Kwanza, Serikali itakuwa inatoa taarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha. Taarifa hii itajumuisha majina ya watu, taasisi, asasi na makampuni yaliyonufaika na
12
misamaha ya kodi, thamani na sheria iliyotumika kutoa misamaha hiyo. Zoezi hili litahusisha taarifa ya misamaha ya kodi kuanzia mwaka 2010 na kuendelea. Hatua hii itasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji katika suala la misamaha ya kodi na kuwafanya wananchi wajue ni nani anayenufaika na misamaha hiyo. Pili, ni kutoa taarifa ya kina ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa na kuiwasilisha Bungeni kila mwaka ili Waheshimiwa Wabunge mpate nafasi ya kujadili na kutoa maoni yenu.
11. Mheshimiwa Spika, bajeti hii imelenga pia kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Ili kutekeleza azma hii, Serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti na utakamilika
13
kabla ya mwisho wa mwaka 2014/15. Sheria hii inalenga kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau wote wanaotekeleza Bajeti ya Serikali wakiwemo: viongozi na maafisa wa Serikali, Waheshimiwa Wabunge, mashirika ya umma, wakala na taasisi za Serikali, wakandarasi na wazabuni. Katika kuandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti, wadau muhimu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, watashirikishwa kupitia kamati za kudumu za Bunge.
12. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na tatizo la utekelezaji wa miradi chini ya viwango. Katika kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inawiana na uwekezaji katika miradi husika, Serikali imenunua vifaa vya kuhakiki ubora wa miradi ya maendeleo.
14
Vifaa hivi vitatumika katika uhakiki wa miradi inayotekelezwa na wizara, idara, wakala na taasisi za Serikali na mamlaka za serikali za mitaa. Uhakiki huu utasaidia kuhakikisha kuwa, miradi ya maendeleo inayotekelezwa inakuwa ya ubora unaokidhi viwango. Aidha, matumizi ya vifaa hivi yatasaidia kuwabaini wakandarasi dhaifu katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
13. Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti matumizi na kupata thamani ya fedha katika ununuzi wa bidhaa na huduma, Serikali imeamua kuzingatia ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji badala ya wakala kama ilivyo sasa na hatua imeanza
15
kuchukuliwa ili ununuzi wa magari na vyombo vya TEHAMA ufuate utaratibu huo. Aidha, Kutokana na wingi wa mafuta yanayotumika kwenye magari na mitambo, Serikali itaanzisha mfumo mpya wa kielektroniki utakaotumika katika kununua, kutunza na kuuza bidhaa hiyo ili kuwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika ununuzi wa mafuta. Vilevile, inaelekezwa kwamba vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kalenda za kila mwaka, zitachapishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tu. Hii ni kwa wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali, mikoa na mamlaka za Serikali za Mtaa badala ya utaratibu wa sasa ambapo kila taasisi ya Serikali inachapisha kwa utaratibu wake. Pia, ili kupunguza matumizi ya umeme katika ofisi za Serikali, Serikali
16
inakusudia kutumia vifaa vya umeme vyenye matumizi kidogo ya umeme (Enegry saving technology sensors).
14. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ya kudhibiti matumizi ya umma ni kuunganisha matumizi yote ya wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja wa udhibiti wa fedha za Serikali unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Kuanzia sasa, hakuna taasisi yoyote ya umma inayokusanya maduhuli itakayoruhusiwa kutumia fedha walizokusanya kabla ya bajeti yao kupitiwa na kuidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali na fedha zote zinazozidi bajeti
17
iliyoidhinishwa zitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Utaratibu huu unatumiwa na nchi nyingine duniani zikiwemo nchi jirani, na kwa hapa Tanzania utaratibu huu unatumika kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hivyo, Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014 una mapendekezo ya kurekebisha sheria zinazohusika ili kuwezesha utekelezaji wa utaratibu huo na ninaomba Waheshimiwa Wabunge muupitishe kwa kauli moja.
15. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka 2014/2015.
18
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2013/14
16. Mheshimiwa Spika, mipango na Bajeti ya Serikali mwaka 2013/14 iliandaliwa kwa kuzingatia mzunguko mpya wa bajeti na sera za uchumi jumla ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni 18,249 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje na kiasi cha shilingi bilioni 12,604 kilipangwa kutumika kwenye matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5,645 kwenye matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2014, Serikali imekusanya mapato halisi yenye jumla ya shilingi bilioni 12,882 sawa na asilimia 70 ya mapato yote ya mwaka.
19
Sera za Mapato
17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, sera za mapato zililenga kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kugharamia Bajeti ya Serikali. Sera hizo zilijumuisha: marekebisho ya sheria zinazoruhusu misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza; kuanzisha kituo kimoja cha kutoa huduma za forodha katika bandari ya Dar es Salaam, kuendelea kuanzisha vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani (One Stop Border Posts); na kupitia mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo na ardhi.
Mwenendo wa Mapato ya Ndani
18. Mheshimiwa Spika, sera za mapato zililenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya
20
shilingi bilioni 11,154. Tathmini inaonesha kuwa hadi Aprili 2014, mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 7,771.5, sawa na asilimia 75 ya makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 10,395.4. Sababu ya kutokufikia lengo ni kutokufanya vizuri kwa baadhi ya vyanzo vya kodi ambavyo vilitarajiwa kuchangia kiasi kikubwa cha mapato. Kutokana na mwenendo huu wa mapato, inategemewa kuwa hadi tarehe 30 Juni 2014, makusanyo ya mapato yanayotokana na kodi yatafikia asilimia 93 ya lengo la mwaka.
19. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato yasiyotokana na kodi, hadi Aprili 2014, yalifikia shilingi bilioni 425.5 ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 741.1 kwa mwaka.
21
Inakadiriwa kuwa, hadi Juni 2014, mapato yasiyo ya kodi yatafikia asilimia 65 ya lengo la mwaka.
20. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato ya halmashauri shilingi bilioni 252.8 zilikusanywa, sawa na asilimia 66 ya makadirio kwa mwaka ya shilingi bilioni 383.5. Sababu ya kutofikiwa kwa malengo hayo ni pamoja na kuchelewa kuanza ukusanyaji wa ada ya leseni za biashara na kuchelewa kwa zoezi la kuthamanisha majengo kwa mkupuo (mass valuation).
22
Misaada na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali ilitarajia kupata shilingi bilioni 3,855.2 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2014, misaada na mikopo ya kibajeti iliyopokelewa ni shilingi bilioni 734 sawa na asilimia 63 ya makadirio ya mwaka. Kwa upande wa Mifuko ya Kisekta, shilingi bilioni 368.6 zilikuwa zimepokelewa sawa na asilimia 74 ya makadirio ya mwaka. Aidha, kwa upande wa mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo, shilingi bilioni 1,200 zilipokelewa sawa na asilimia 55 ya makadirio ya mwaka.
23
Mikopo ya Kibiashara ya Ndani
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali ilipanga kukopa shilingi bilioni 1,699.9 kutoka soko la ndani kwa utaratibu wa kuuza hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi kwa ajili ya kugharamia bajeti yake. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 552.3 ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 1,147.6 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva. Katika kipindi cha Julai 2013 – Aprili, 2014, Serikali ilikopa jumla ya shilingi bilioni 1,803.9. Kati ya hizo, shilingi bilioni 1,113.3 zilitumika kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zilizoiva (rollover) na shilingi bilioni 690.6 zilitumika kugharamia miradi ya maendeleo.
24
Mikopo ya Kibiashara kutoka Nje
23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali ilipanga kukopa shilingi bilioni 1,156.4 sawa na Dola za Marekani milioni 700 kutoka kwenye masoko ya fedha ya nje ili kugharamia miradi ya maendeleo. Hadi sasa Serikali imepata jumla ya Dola za Marekani milioni 407.9 sawa na asilimia 58 ya makadirio. Dola za Marekani milioni 176.9 zimepatikana kutoka Benki ya Credit Suisse kwa ajili ya kugharamia miradi ya barabara, maji na reli na Dola za Marekani milioni 83 zimepatikana kutoka Benki ya Citi kwa ajili ya kugharamia miradi ya ufuaji umeme inayosimamiwa na TANESCO. Aidha, Serikali itapata Dola za Marekani milioni 148 kutoka Benki ya
25
HSBC kwa utaratibu wa Export Credit Arrangement kugharamia upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Majadiliano ya kupata kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 292 kwa utaratibu huo huo yanaendelea na yako katika hatua za mwisho yakihusisha benki za Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) na Japan Bank for International Cooperation (JBIC), kwa ajili ya mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi II wa Megawati 240.
Sera za Matumizi
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali ilipanga kutekeleza sera za matumizi zifuatazo: kuwianisha matumizi na mapato yaliyotarajiwa; kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti
26
haizidi asilimia 5 ya Pato la Taifa; mafungu kuzingatia viwango vya matumizi vilivyoidhinishwa na Bunge; kutenga fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya vipaumbele; na kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011.
Mwenendo wa Matumizi
25. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili, 2014, Serikali imetoa ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 13,034.7 sawa na asilimia 71 ya makadirio ya mwaka. Serikali iliendelea kulipa mishahara ya watumishi wa umma, ambapo hadi Aprili 2014, shilingi bilioni 3,760 zililipwa sawa na asilimia 79 ya bajeti ya mishahara ya mwaka ya shilingi bilioni 4,763. Shilingi bilioni 1,098 zililipwa kwa
27
watumishi wa Serikali Kuu, jumla ya shilingi bilioni 92 zilitolewa kwa ajili ya watumishi wa sekretarieti za mikoa na shilingi bilioni 2,097 kwa ajili ya halmashauri 161 za majiji, manispaa, miji na wilaya. Vilevile, Serikali ililipa mishahara ya Taasisi na Mashirika ya Umma jumla ya shilingi bilioni 473.
26. Mheshimiwa Spika, Serikali ilipanga kutumia shilingi bilioni 3,319.2 kulipa Deni la Taifa na madeni mengine. Hadi kufikia Aprili 2014, malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 782.7, sawa na asilimia 78 ya makadirio ya shilingi bilioni 998 kwa mwaka. Malipo ya deni halisi la mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 139, sawa na asilimia 36 ya makadirio ya mwaka. Malipo kwa
28
madeni mengine (CFS others) yalikuwa shilingi bilioni 750 ikiwa ni asilimia 96 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 783. Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 1,113.3 kililipia hatifungani na dhamana za Serikali zilizoiva (rollover) sawa na asilimia 97 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 1,148. Matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 3,374.7 ikiwa ni asilimia 69 ya makadirio ya shilingi bilioni 4,912 kwa mwaka.
27. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2014, jumla ya shilingi bilioni 3,115 ziliidhinishwa na kutolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 5,645. Kiasi
29
hicho ni sawa na asilimia 55 ya makadirio ya mwaka. Kati ya fedha zilizoidhinishwa na kutolewa, fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 1,546 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 2,953, sawa na asilimia 52. Aidha, fedha za nje zilikuwa shilingi bilioni 1,569 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 2,692 sawa na asilimia 58 ya makadirio ya mwaka.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
28. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kuhakikisha kwamba Hesabu za Majumuisho za Serikali (Consolidated Financial Statements) zinaandaliwa kwa kuzingatia mfumo wa Viwango vya Kimataifa Vya Uhasibu (IPSAS Accrual Basis), hatua
30
hizo zinalenga kuunganisha hesabu za Serikali Kuu, mamlaka za serikali za mitaa, mifuko ya hifadhi ya jamii, taasisi mbalimbali na mashirika ya umma.
29. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hii ya Serikali ya kuandaa hesabu za majumuisho, Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2013 kwa Serikali kuu zimeandaliwa kwa kuzingatia mfumo wa IPSAS Accrual Basis kwa mara ya kwanza na kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa Sheria. Lengo la kutumia mfumo huu ni kuboresha uwazi na uwajibikaji wa Serikali katika matumizi na usimamizi wa rasilimali zake. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za umma
31
kwa kupanua mtandao wa malipo ya moja kwa moja kwenye benki – TISS katika mikoa 20 ya Tanzania Bara hadi kufikia Mei, 2014 na zoezi linaendelea kwenye mikoa iliyosalia ambapo hadi mwishoni mwa Juni 2014 mikoa yote itakuwa imeunganishwa kwenye Mfumo huu.
30. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza nidhamu na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, Serikali imeanza kufanya ukaguzi wa ndani kwa kuzingatia mwongozo wa ukaguzi wa ndani wenye viwango vya kimataifa ambao ulianza kutumika Julai 2013. Serikali pia imeandaa Mwongozo wa Kamati za Ukaguzi katika Sekta ya Umma kwa lengo la kuboresha utendaji wa Kamati za Ukaguzi na hivyo
32
kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mapato na matumizi ya Serikali. Aidha, Serikali imeendelea kuhakiki madai ya wakandarasi, wazabuni na watumishi, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 58 kimeokolewa katika zoezi hilo.
Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
31. Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini umeainisha mikakati katika nguzo kuu tatu, ambazo ni Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato, Kuboresha Maisha na Ustawi wa Jamii na Kuimarisha Utawala Bora na Uwajibikaji. Mwaka 2013/14 ulikuwa mwaka wa tatu wa utekelezaji wa MKUKUTA II.
33
Mwenendo wa viashiria vya kupima matokeo ya utekelezaji wa MKUKUTA II katika nguzo kuu tatu nilizozitaja unaonesha mafanikio na changamoto. Nitaeleza matokeo kwa baadhi ya viashiria.
32. Mheshimiwa Spika, katika nguzo ya kwanza ya Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato, uchumi umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Ukuaji huu umeongeza pato halisi la wastani la kila Mtanzania hadi kufikia shilingi 1,186,200 mwaka 2013 kutoka shilingi 1,025,038 mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 14. Aidha, umaskini wa kipato umeendelea kupungua ambapo kwa mujibu wa takwimu mpya za Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya Binafsi uliofanyika Mwaka
34
2012, umeonesha kuwa umaskini wa kipato umepungua kwa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asilimia 34.4 hadi asilimia 28.2. Vilevile, umaskini wa chakula umepungua kwa asilimia 2.1 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asimilimia 11.8 hadi asilimia 9.7.
33. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa utekelezaji katika eneo la kuboresha hali ya maisha na ustawi wa jamii, unaridhisha. Aidha, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi elimu ya msingi umeimarishwa kutoka 1:47 mwaka 2012 na kufikia 1:43 mwaka 2013 ikilinganishwa na lengo la uwiano wa 1:40. Katika elimu ya sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ulifikia lengo la MKUKUTA II
35
la 1:28 mwaka 2013. Jitihada za kuboresha huduma za afya, lishe na upatikanaji wa maji safi na salama zimeendelea kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii. Kwa mujibu wa takwimu mpya za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, vifo vya watoto wachanga vimeendelea kupungua kutoka vifo 51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2010 hadi vifo 45 mwaka 2012. Umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka wastani wa miaka 51 mwaka 2002 hadi miaka 61 mwaka 2012.
34. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali imeendelea kutekeleza programu za maboresho. Kupitia programu hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika
36
kuboresha mfumo wa usimamizi wa mali na fedha za umma, mfumo wa sheria na usimamizi wa haki, demokrasia, na utoaji huduma za umma kwa jamii. Hatua hizi zimeboresha upatikanaji wa huduma kwa umma, kupanua demokrasia na kuongeza kasi ya utoaji maamuzi ya mashauri katika mahakama za mwanzo na wilaya.
Tathmini ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)
35. Mheshimiwa Spika, kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia, nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania ziliahidi kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia na shabaha ziliwekwa kwa viashiria mbalimbali kwamba
37
ifikapo mwaka 2015, malengo hayo yawe yamefikiwa. Mapitio ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia yanaonesha kuwa, Tanzania imefanya vizuri na inaweza kufikia malengo yafuatayo: Elimu ya Msingi kwa Wote; Usawa wa Kijinsia na Fursa Sawa kwa Wanawake; Kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga na kupunguza maambukizi ya UKIMWI. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea na jitihada za kuhakikisha malengo yaliyobakia yanafikiwa.
Sekta ya Fedha
36. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza progamu ya maboresho ya sekta ya fedha ili kuhakikisha inachangia kikamilifu katika shughuli za
38
kiuchumi na hivyo kukuza Pato la Taifa. Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (National Financial Inclusion Framework) ulizinduliwa na Serikali Desemba, 2013 kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanafikiwa na huduma za kifedha zilizo rasmi. Aidha, Serikali ilikamilisha mwongozo wa uwakala wa huduma za kibenki ambao umeiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kutoa leseni za uwakala kwa benki za CRDB, Posta, Equity na DCB. Utaratibu huu wa uwakala umepanua wigo wa huduma za kibenki na hivyo kuwafikia walengwa wengi zaidi na kwa gharama nafuu.
37. Mheshimiwa Spika, katika kuangalia vikwazo vya upatikanaji wa huduma za fedha nchini,
39
Serikali ilifanya utafiti mwaka 2013. Matokeo ya utafiti huo yalionesha mafanikio yafuatayo: asilimia 13.9 ya wananchi wanatumia huduma za kibenki ikilinganishwa na asilimia 9.2 mwaka 2009. Aidha, asilimia 43.5 ya wananchi wanatumia huduma zisizo za kibenki (Bima, SACCOS na taasisi ndogo za huduma za kifedha, malipo kwa njia ya simu) ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2009. Asilimia 15.8 ya wananchi wanatumia huduma za kifedha za sekta isiyo rasmi mfano VICOBA, ROSCA (Rotating Saving and Credit Association), VSLA (Village Saving and Lending Association) ikiwa imepungua ikilinganishwa na asilimia 28.9 mwaka 2009. Kwa ujumla utafiti huu unaonesha kuwa asilimia 57.4 ya wananchi wanapata huduma rasmi za kifedha.
40
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
38. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi. Ili kutimiza azma hiyo, Serikali imewasilisha Bungeni muswada wa kurekebisha Sheria ya Ubia Na. 18 ya mwaka 2010 ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa miradi ya PPP. Aidha, Serikali inaazimia kuanzisha Mfuko maalumu wa miradi ya ubia (PPP Facilitation Fund) na kuunda Kamati ya Kitaifa ya PPP (PPP Technical Commitee) pamoja na Kituo cha Miradi ya Ubia (PPP Centre).
41
Deni la Taifa
39. Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa linasimamiwa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004 na Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Madeni. Hadi kufikia Machi 2014, Deni la Taifa linalojumuisha deni la Serikali na deni la nje la sekta binafsi lilifikia shilingi bilioni 30,563 ikilinganishwa na shilingi bilioni 23,673.5 la Machi 2013. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi bilioni 26,832.4 na deni la sekta binafsi la nje ni shilingi bilioni 3,730.6. Deni la Serikali la nje linajumuisha mikopo ya nje kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa, nchi wahisani na mabenki ya kibiashara ambapo hadi kufikia Machi 2014 lilikuwa shilingi
42
bilioni 18,997.6 wakati deni la ndani ni shilingi bilioni 7,834.8. Ongezeko la Deni la Taifa linatokana na kupatikana kwa mikopo mipya, kupokelewa kwa fedha za mikopo ya nyuma kwa kipindi husika pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Uhimilivu wa Deni la Taifa
40. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Deni la Taifa linaendelea kuhimilika Serikali imekuwa ikikopa na kuwekeza katika miradi ya kuchochea ukuaji wa uchumi ili kuwa na uwezo wa kuyalipa madeni hayo pindi yanapoiva. Aidha, Serikali imejiwekea utaratibu wa kufanya tathmini ya uhimilivu wa deni kila mwaka kwa mujibu wa sheria ili kubainisha hali halisi ya deni na uwezo wa nchi kulipa madeni hayo katika kipindi
43
cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Kufuatia utaratibu huo mwezi Septemba, 2013 Serikali ilifanya tathmini ya uhimilivu wa deni kwa kutumia viashiria vilivyokubalika kimataifa. Matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa Deni la Taifa ilibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu.
41. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tathmini hiyo, viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni viko katika wigo unaokubalika kimataifa (debt sustainability thresholds). Baadhi ya viashiria hivyo ni uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa la nje (Present Value of External Debt) kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 24.8 ikilinganishwa na ukomo wa wa asilimia 50. Uwiano wa thamani ya sasa ya deni la
44
nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 121.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 300, Uwiano wa thamani ya ulipaji wa deni la nje kwa thamani ya mapato ya mauzo nje ya nchi ni asilimia 3.34 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 25, Uwiano kati ya ulipaji wa deni kwa mapato ya ndani ni asilimia 4.32 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 22 na uwiano wa deni la Serikali likijumuisha dhamana za serikali kwa taasisi mbalimbali kwa Pato la Taifa ni asilimia 35.58 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 74.
42. Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu kwa kuendelea kutekeleza mikakati
45
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukopa mikopo yenye masharti nafuu na kuhakikisha kuwa fedha zitokanazo na mikopo hiyo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Serikali pia inaweka ukomo wa mikopo yenye masharti ya kibiashara bila kuathiri uhimilivu wa deni. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa dhamana kwa taasisi, mashirika, idara na wakala wa Serikali zinazopata ruzuku kutoka Serikalini.
Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali ilianzisha utaratibu madhubuti wa kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa
46
miradi iliyo katika mpango wa maendeleo ujulikanao kama Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN). Lengo la kuanzisha utaratibu huu ni kuongeza kasi katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambapo Tanzania inatarajia kuwa nchi ya kipato cha kati. Ili kuleta tija na ufanisi utekelezaji wa BRN unahusisha maeneo sita ya kipaumbele ambayo ni:-Kilimo, Elimu, Maji, Nishati, Miundombinu na Utafutaji wa Rasilimali Fedha.
44. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maamuzi yaliyofanyika kwenye maabara ya utafutaji wa rasilimali fedha, Wizara ya Fedha ilipewa lengo la kuongeza mapato mapya kwa jumla ya shilingi bilioni 1,160 kwa mwaka 2013/14; kupunguza nakisi ya
47
bajeti kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa; kudhibiti matumizi; na kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya BRN katika sekta nyingine. Katika mwaka 2013/14, jumla ya shilingi bilioni 1,700 zilitengwa kwenye bajeti kupitia miradi mbalimbali ya sekta zinazotekeleza miradi ya BRN.
45. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2014, mafungu yanayotekeleza miradi ya BRN yamepatiwa jumla ya shilingi bilioni 1,566.7 sawa na asilimia 92 ya bajeti ya miradi ya BRN kwa mwaka 2013/14. Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya maji viijijini shilingi bilioni 226.1; Elimu shilingi bilioni 48.4; Nishati shilingi bilioni 577.5; Uchukuzi ikijumuisha
48
miundombinu ya barabara na reli shilingi bilioni 663.6; na Kilimo shilingi bilioni 51.1.
Mafanikio na Changamoto katika Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2013/14
46. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali imefanikiwa kutekeleza shughuli muhimu za bajeti licha ya kukabiliwa na changamoto kama ilivyoelezwa katika hotuba za mipango na bajeti za wizara, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa husika ambazo Bunge lako tukufu limejadili kwa kina na kuzipitisha. Aidha, Hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu imeelezea mafanikio na
49
changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa kuzingatia hatua hiyo, nitaeleza kwa kifupi baadhi ya mafanikio na changamoto kama ifuatavyo:-
Mafanikio
Ukuaji wa Uchumi
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013 Pato halisi la Taifa limekua kwa asilimia 7.0 ambayo ni sawa na lengo lililowekwa. Aidha, kwa mwaka 2012 ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 6.9 na asilimia 6.4 mwaka 2011. Mafanikio haya yanatokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha uchumi tulivu na utawala bora ambazo ni nguzo muhimu katika kuvutia uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la
50
Fedha la Kimataifa ya mwezi Aprili 2014, Tanzania ni nchi ya 8 katika ukuaji wa uchumi katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, na ya kwanza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ukuzaji wa ajira
48. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2014, jumla ya ajira mpya 630,616 zilikuwa zimezalishwa nchini katika sekta ya umma na sekta binafsi. Kati ya ajira hizo zilizozalishwa, sekta ya elimu ilizalisha ajira 36,073; Afya ajira 11,221; Kilimo ajira 130,974; Ujenzi wa miundombinu ajira 32,132; Nishati na Madini ajira 453; na Mawasiliano ajira 13,619. Aidha, kati ya ajira hizo, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliajiri
51
watu 3,055. Nafasi hizi ni nje ya nafasi zinazohusu sekta ya afya na elimu. Ajira zilizozalishwa katika sekta binafsi zilikuwa 211,970.
Mfumuko wa Bei
49. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini umeendelea kushuka kutoka asilimia 9.4 Aprili 2013 hadi kufikia asilimia 6.3 Aprili 2014. Lengo lililowekwa la mfumuko wa bei hadi Juni 2014 ni asilimia 6.0, ambalo kuna uwezekano wa kulifikia. Kupungua kwa kasi ya upandaji bei kulitokana hasa na sera madhubuti za fedha, hali nzuri ya hewa; jitihada za Serikali kuongeza ruzuku ya pembejeo za kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao; kuimarika kwa
52
upatikanaji wa chakula katika nchi jirani; pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme.
Akiba ya Fedha za Kigeni
50. Mheshimiwa Spika, hali ya akiba ya fedha za kigeni mpaka mwisho wa mwezi Aprili 2014 iliendelea kuwa ya kuridhisha. Katika kipindi kilichoishia Aprili 2014, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Kimarekani milioni 4,647.5 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 4,380.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2013. Kiasi hiki cha akiba ya fedha za kigeni kwa mwaka 2014 kinatosheleza uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.6 ikilinganishwa la lengo la kutosheleza
53
uagizaji wa bidhaa na huduma la miezi 4.0 hadi Juni, 2014.
51. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni pamoja na Serikali kugharamia shughuli za Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba; kulipa mishahara ya watumishi kwa wakati; Ujenzi na utandazaji wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umeendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa; ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali unaendelea kufanyika; fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilitolewa kwa wakati; kugharamia ununuzi wa chakula cha hifadhi ya Taifa; kuendelea kugharamia huduma za jamii; na ununuzi wa pembejeo za kilimo.
54
Changamoto
52. Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio hayo, changamoto mbalimbali zimejitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/14. Changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji kwa wakati wa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara; kuwepo kwa mahitaji makubwa ya fedha ikilinganishwa na upatikanaji wa mapato; ukusanyaji usioridhisha wa mapato yasiyo ya kodi; gharama kubwa za uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme wa dharura; kuongezeka kwa madai ya wakandarasi, wazabuni na watumishi; na kutokamilika kwa urasimishaji wa sekta isiyo rasmi na hivyo kusababisha ugumu wa kutoza kodi.
55
53. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto nilizozieleza, Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki na kusimamia ulipaji kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya mfumo wa Mashine za Kielektroniki za Kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices) ulioboreshwa zaidi; na kuboresha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa kutumia TEHAMA.
54. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa bajeti, Serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti. Kuhusu madai ya Wakandarasi na Wazabuni, Serikali inakamilisha utaratibu wa kusimamia na kuyalipa madai
56
yaliyohakikiwa kupitia Hazina kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zinazohusika. Aidha, Serikali inaendelea kuhimiza Wizara na Taasisi kuzingatia mfumo wa malipo (IFMS) ambao unamtaka kila Afisa Masuuli kutoingia mikataba bila kuwa na LPO inayotokana na mfumo wa IFMS.
55. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misaada na mikopo ya nje, Serikali itaendelea kufanya majadiliano mapema na wahisani pamoja na mabenki ili kuhakikisha kwamba fedha za misaada na mikopo zinapatikana kama ilivyopangwa na kwa wakati. Aidha, Serikali itahakikisha inazingatia na kutekeleza kwa haraka masharti ya fedha za wahisani kulingana na makubaliano.
57
III. BAJETI YA MWAKA 2014/15
56. Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2014/15 itaendelea kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye: Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2014/15 na Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN); Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Programu za Maboresho katika Sekta ya Umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
58
SHABAHA NA MISINGI YA BAJETI KWA MWAKA 2014/15
57. Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2014/15 ni kama ifuatavyo:-
(i) Pato halisi la Taifa linatarajia kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2014 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 7.7 kwa mwaka katika kipindi cha muda wa kati;
(ii) Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja, ambapo maoteo kwa kipindi kinachoishia
59
Juni 2014 ni asilimia 6.0 na asilimia 5.0 Juni 2015;
(iii) Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa asilimia 18.9 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2014/15;
(iv) Kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia 4.9 ya Pato la Taifa mwaka 2014/15;
(v) Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia 15.5 kwa mwaka unaoishia Juni
60
2015 utakaowiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei;
(vi) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne kwa mwaka unaoishia Juni 2015; na
(vii) Kuimarisha thamani ya shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
61
58. Mheshimiwa Spika, ili kufikia shabaha na malengo yaliyoainishwa, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2014/15 ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, utulivu na utengamano nchini, kikanda na Duniani;
(ii) Kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, biashara ya nje na huduma za kifedha;
(iii) Mapato ya ndani yataongezeka kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kubuni
62
vyanzo vipya vya mapato na kupunguza misamaha ya kodi na kuongeza usimamizi;
(iv) Kuimarisha mfumo wa usimamizi na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma;
(v) Mfumo wa IFMS utaimarishwa na kuhakikisha unatumika kuweka mihadi ya huduma na bidhaa kabla ya malipo kuzingatia vipaumbele vilivyopo katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, MKUKUTA II pamoja na miradi itakayokuwepo katika “Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa”;
63
(vi) Sera za fedha zitaendelea kuimarishwa ili ziendane na sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za amana na za mikopo;
(vii) Mtengamano wa kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC utaendelezwa na kutumia vizuri fursa zilizopo; na
(viii) Mazingira ya biashara na uwekezaji yataendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya utekelezaji wa sheria ya PPP ili kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.
64
Sera za Mapato
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala kwa kupanua wigo wa kodi, kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha usimamizi wa kodi, kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kupitia sheria mbalimbali za kodi ikiwemo sheria ya VAT. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge, kikosi cha wataalam (Lab) cha kubuni vyanzo vya mapato katika mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa.
65
60. Mheshimiwa Spika, hatua za kisera za kuongeza mapato zitakazozingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka 2014/15 ni pamoja na:-
(i) Kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi kwa kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
(ii) Kuongeza usajili wa walipa kodi wapya na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato;
66
(iii) Mamlaka ya Mapato Tanzania itaongeza siku za kufanya kazi ili kutoa muda wa ziada wa kuwahudumia walipa kodi bandarini na baadhi ya vituo vya mpakani ;
(iv) Kukamilisha utungwaji na kuanza kutekeleza Sheria Mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT);
(v) Kukamilisha utungwaji wa Sheria ya Usimamizi wa kodi (Tax Administration Act);
67
(vi) Kuendelea kuimarisha na kusisitiza matumizi ya mashine za elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal Devices-EFDs) na kutoa elimu zaidi kwa walipa kodi na wafanya biashara kuhusu matumizi ya mashine hizo;
(vii) Kufuatia kukamilika kwa utafiti wa kuwianisha mifumo ya ukuanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali itaandaa mfumo wa usimamizi na utaratibu wa kukusanya;
(viii) Kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi;
68
(ix) Taasisi, wakala na mamlaka za serikali kuwasilisha maduhuli yote kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia mfumo wa retention;
(x) Ili kukabiliana na ukwepaji kodi, Wizara ya Fedha itatoa namba maalum ya simu na anwani ya barua pepe ili kuwawezesha raia wema kutoa taarifa mbalimbali kuhusu ukwepaji kodi; na
(xi) Wizara, idara zinazojitegemea, mikoa, manispaa, majiji, halmashauri, wakala na taasisi, mamlaka zinazokusanya maduhuli
69
na malipo mengine zinaagizwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kurahisisha ukusanyaji na kupunguza upotevu wa mapato.
61. Mheshimiwa Spika, Sera za mapato katika mwaka 2014/15, zinalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 12,178.0 sawa na asilimia 19.2 ya Pato la Taifa. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi ni shilingi bilioni 11,318.2 na mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 859.8. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 458.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
70
Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu
62. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Kwa mwaka 2014/15, Serikali inatarajia kupokea misaada na mikopo ya masharti nafuu ya kiasi cha shilingi bilioni 2,941.5. Kati ya fedha hizo misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 922.1, Mifuko ya Kisekta shilingi bilioni 274.1 na miradi ya maendeleo shilingi bilioni 1,745.3
63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha na kuanza kutumia mwongozo mpya wa Ushirikiano katika Maendeleo.
71
Mwongozo huu unalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya MPAMITA na uwekaji wa misingi mipya hususan ufanisi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii (Development Effectiveness). Aidha, mwongozo huu unaainisha misingi ya majadiliano baina ya Serikali na wadau wa maendeleo ili misaada na mikopo inayotolewa iweze kuleta tija na matokeo yanayokusudiwa.
64. Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi zao za kuchangia maendeleo yetu, naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wa Maendeleo kama ifuatavyo: Nchi za Canada, China, Denmark, Finland, Hispania, India, Ireland, Italia, Japani, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa,
72
Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi, pia taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, BADEA, Global Fund, OPEC Fund, Saudi Fund, Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mbali na michango yao ya kifedha, Serikali pia inanufaika kutokana na ushauri na mawazo yao katika kutekeleza programu mbalimbali. Tunawashukuru na kuthamini mchango wao.
Mikopo ya Kibiashara ya Ndani na Nje
65. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi
73
kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo. Katika mwaka 2014/15, Serikali inategemea kukopa katika soko la ndani jumla ya shilingi bilioni 2,955.2. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 689.56 sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 2,265.7 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva kwa utaratibu wa rollover.
66. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 1,320.0 kutoka masoko ya fedha ya nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Uamuzi wa kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara umezingatia tathmini ya uhimilivu wa deni
74
la Taifa na umuhimu wa kuendeleza miradi ya kipaumbele hususan miundombinu ambayo itafungua fursa za kiuchumi na kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi.
Sera za Matumizi
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali imekadiria kutumia jumla ya shilingi bilioni 19,853.3 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Katika kipindi hiki mgawanyo wa matumizi ya Serikali utakuwa kama ifuatavyo: Matumizi ya kawaida shilingi bilioni 13,408.2 na matumizi ya maendeleo jumla ya shilingi bilioni 6,445.1.
75
68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itatekeleza sera za matumizi zifuatazo:-
(i) Utoaji wa fedha kwa Mafungu utazingatia maombi na uwasilishwaji wa taarifa za matumizi (performance based disbursement) katika matumzi ya kawaida na maendeleo kwa kila robo ya mwaka;
(ii) Kuwianisha matumizi na mapato yanayotarajiwa;
76
(iii) Kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, ikiwa ni pamoja na kuandaa Sheria ya Bajeti;
(iv) Taasisi zitumie wakala wa Serikali mtandao katika kuweka mifumo ya TEHAMA kwenye Taasisi zao ili kupunguza gharama za washauri kutoka nje;
(v) Wizara, idara zinazojitegemea, mikoa, halmashauri, wakala na Taasisi za Serikali zitafanya manunuzi yote kupitia Mfumo wa EFDs hivyo kuambatisha risiti zinazotokana na mashine za kielektroniki (EFDs);
77
(vi) Malipo yote ya Serikali yatalipwa kupitia akaunti moja ya Serikali iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (Single Treasury Account);
(vii) Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haitazidi asilimia 4.9 ya Pato la Taifa;
(viii) Mafungu yatazingatia matumizi yaliyokusudiwa pamoja na viwango vilivyoidhinishwa na Bunge;
(ix) Kutenga fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya vipaumbele
78
vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo;
(x) Bajeti za Taasisi, wakala na mamlaka za Serikali zitawasilishwa na kuidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali;
(xi) Madai ya wakandarasi, wazabuni na watumishi yatahakikiwa na kulipwa na Wizara ya Fedha kwa kuzingatia bajeti za mafungu husika;
(xii) Serikali itazingatia ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji badala ya wakala; na
79
(xiii) Matumizi yatazingatia Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2004 na manunuzi yatazingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na kanuni zake.
Mgawanyo wa fedha katika Sekta
69. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 mgawanyo wa bajeti kwa sekta ni kama ifuatavyo:-
(i) Nishati na Madini: jumla ya shilingi bilioni 1,090.6 zimetengwa. Shilingi bilioni 290.2 zimetengwa kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini; shilingi bilioni
80
151 kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam; na shilingi bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia Gesi wa Kinyerezi I. Hatua hii inalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kupunguza gharama zake na hivyo kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira.
(ii) Miundombinu ya usafirishaji: jumla ya shilingi bilioni 2,109.0 zimetengwa, ambapo shilingi bilioni 179.0 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa reli ya kati na shilingi bilioni 1,414.8 kwa
81
ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja. Azma hii inalenga kupunguza msongamano wa magari mijini, gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, na hivyo kupunguza mfumuko wa bei.
(iii) Kilimo: jumla ya shilingi bilioni 1,084.7 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya SAGCOT; ujenzi wa maghala na masoko; na upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Serikali itaendelea kuwekeza
82
kwenye ugani kwa kuimarisha vyuo vya utafiti katika kilimo na kuhakikisha kunakuwa na maofisa ugani wa kutosha na mbegu bora. Hatua hii itaimarisha uzalishaji wa mazao, usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika;
(iv) Elimu: jumla ya shilingi bilioni 3,465.1 zimetengwa, ambapo shilingi bilioni 307.3 zimetengwa kugharamia mikopo ya elimu ya juu. Aidha Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha miundombinu ya elimu. Hatua hii itasaidia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na
83
kufundishia, kuimarisha na kujenga madarasa na maabara. Ili kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa za ajira, juhudi zitawekwa pia kwenye kuimarisha vyuo vya ufundi stadi – VETA;
(v) Maji: jumla ya shilingi bilioni 665.1 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa visima katika vijiji 10 kwa kila Halmashauri na kukamilisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam. Hatua hii itawaondolea wananchi kero ya kufuata maji mbali na
84
makazi yao na hivyo kupata muda wa shughuli nyingine za uzalishaji, na kuwaondolea hatari ya kupata magonjwa kwa kutumia maji yasiyo salama;
(vi) Afya: jumla ya shilingi bilioni 1,588.2 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa madawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti UKIMWI na Malaria;
(vii) Utawala Bora: jumla ya shilingi bilioni 579.4 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha utawala bora ikijumuisha kugharamia Bunge Maalum la Katiba; vitambulisho
85
vya Taifa; uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014; kuhuisha daftari la wapiga kura; maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015; mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa haki kwa wakati.
70. Mheshimiwa Spika, mgawanyo huu wa kisekta haujumuishi madeni ya kisekta yanayolipwa kupitia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS).
Masuala yanayohusu Mamlaka ya Serikali za Mitaa
71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, mikoa na halmashauri zimetengewa shilingi bilioni 4,499 ikiwa ni nyongeza ya shilingi bilioni 685.87
86
ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2013/14 ya shilingi bilioni 3,813. Nyongeza hii ni sawa na asilimia 18. Aidha, mapato ya ndani ya Halmashauri yanakadiriwa kuongezeka kwa shilingi bilioni 85.9 kutoka shilingi bilioni 372.6 mwaka 2013/14 hadi shilingi bilioni 458.5 katika mwaka 2014/15. Ongezeko hili la mapato ya ndani ni sawa na asilimia 23.
72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, shilingi bilioni 46.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri mpya ambapo kila Halmashauri imetengewa shilingi bilioni 1.5. Aidha, shilingi bilioni 9.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za wakuu wa wilaya katika maeneo hayo. Serikali itaendelea kuziwezesha Halmashauri hizo kupata
87
nyenzo muhimu za utendaji kazi katika kutekeleza majukumu yao. Aidha, mwaka 2014/15, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa Halmashauri zenye mazingira magumu katika ujenzi wa nyumba za watumishi, ofisi, hospitali, hosteli, madaraja, barabara pamoja na miradi mingine maalum yenye kulenga kutoa huduma za haraka kwa wananchi ikiwamo maji, elimu na afya. Shilingi bilioni 53.99 zimetengwa katika mwaka ujao wa fedha kwa Halmashauri hizo.
73. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, shilingi bilioni 8.7 zimetengwa kwa ajili ya kazi za ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Mikoa 9 nchini. Mikoa hiyo ni Katavi, Simiyu, Njombe, Geita, Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Singida na Tabora. Ni matumaini
88
yangu kuwa kukamilika kwa kazi hizi kutaimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Matumizi kwa Makundi Maalum
74. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kero mbalimbali zinazowakabili walimu hususan walimu wa shule za msingi. Ili kukabiliana na kero hizo, Serikali imejipanga kuziondoa kero hizo kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
(i) Ujenzi wa nyumba za Walimu: Serikali inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa nyumba za walimu kwa awamu. Katika mwaka 2013/14, Halmashauri 40 zilipewa kila moja shilingi milioni 500 ili zianze
89
ujenzi wa nyumba za walimu na kiasi kama hicho kitatolewa kwa Halmashauri hizo kwa mwaka 2014/15. Aidha, shilingi milioni 500 zitatolewa kwa Halmashauri 80 zaidi, hivyo kufanya jumla ya Halmashauri 120 kunufaika na utaratibu huo, lengo likiwa ni kuzifikia Halmashauri zote mwaka 2015/16. Viongozi wa Serikali katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Kata wanahimizwa kusimamia kikamilifu fedha hizo ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa; na
(ii) Malipo ya madai ya walimu: Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa madai
90
ya walimu yaliyohakikiwa, ambapo katika mwaka 2013/14, kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kimelipwa. Aidha, kwa mwaka 2014/15, madai ya walimu ambayo yatakuwa yamehakikiwa yataendelea kulipwa.
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanafunzi katika shule na vyuo mbalimbali ili kuhakikisha vijana wetu wanasoma katika mazingira tulivu na bora. Ili kutekeleza hili, Serikali imepanga yafuatayo:-
(i) Kujenga maabara katika shule na vyuo na kuzipatia vifaa muhimu ikiwa ni
91
pamoja na kutumia maabara zinazotembea ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi;
(ii) Kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi waliopo vyuoni na watakaojiunga na vyuo vya elimu ya juu; na
(iii) Kujenga maktaba mpya, kukarabati na kuimarisha zilizopo kwa kuzipatia vitabu zaidi vya kiada na ziada.
76. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazovikabili
92
vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na makazi na mahitaji mengine. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imepanga kutekeleza yafuatayo katika mwaka 2014/15:
(i) kuendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za askari katika maeneo mbalimbali nchini ambapo jumla ya shilingi bilioni 27.13 zimetengwa kwa ajili hiyo;
(ii) Kuendelea kuwapatia vitendea kazi; na
(iii) Kuendelea kuongeza mishahara ya askari na stahili nyingine kwa awamu kulingana
93
na uwezo wa kibajeti katika kipindi husika.
77. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara. Katika kuendelea na jitihada hizo, katika mwaka 2014/15, Serikali imepanga yafuatayo:-
(i) Kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma; na
(ii) Kufanya marekebisho katika mfumo wa kodi ya mishahara (PAYE) kwa kupunguza
94
kiwango cha kodi hadi kufikia kima cha chini cha kodi cha asilimia 12, kutoka asilimia 13 ambapo kiwango hicho kilikuwa asilimia 18.5 mwaka 2005/06 na kupunguzwa hadi asilimia 13 mwaka 2013/14.
78. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa wastaafu ambao walitoa mchango mkubwa kwa Taifa hili. Kwa sasa wastaafu hawa wapo katika makundi mawili ambayo ni wastaafu wa Serikali ambao hawakuchangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanaolipwa shilingi 50,000 kwa mwezi na aina ya pili ni wastaafu ambao pensheni zao zinategemea michango yao katika mfuko husika.
95
79. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa viwango vinavyolipwa kwa sasa haviendani na uhalisia. Katika kutatua changamoto hii Serikali inapitia viwango hivyo ili kuongeza viwango kutegemeana na mapato ya Serikali na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendelea kuhuisha kanuni za ukokotoaji wa mafao ili kuweka ulinganifu wa mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Ununuzi wa Umma
80. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini, itaendelea kusimamia
96
utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya Mwaka, 2011 ambayo imeanza kutumika Desemba, 2013 baada ya kanuni kukamilika. Sheria hiyo itaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 zikiwemo bei kubwa ya bidhaa ikilinganishwa na bei halisi ya soko pamoja na mchakato mrefu wa zabuni. Hivyo, nitoe wito kwa wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali na halmashauri zote na wadau wote kwa ujumla kuitumia Sheria hii kikamilifu. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuondokana na kasoro na malalamiko yaliyokuwepo hapo awali.
97
Sekta ya Fedha
81. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itakamilisha Sera na Mkakati wa Sekta ya Bima ili kutoa mwongozo wa kufidia hasara zinazotokana na majanga mbalimbali. Aidha, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Taasisi Ndogo za Huduma za Kifedha na kutunga Sheria ya Taasisi hizo. Vilevile, Serikali inaandaa mapendekezo ya kutunga sheria ya mifumo ya malipo ili kuboresha matumizi ya kieletroniki kufanya malipo kwa kutumia simu za mkononi, huduma za benki kwa njia ya mtandao, vituo vya mauzo na mashine za kutolea fedha.
82. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua athari za riba kubwa zinazotozwa na benki na taasisi
98
za fedha kwa mikopo itolewayo ambazo zinasababisha asilimia kubwa ya Watanzania kushindwa kufaidika na huduma za kifedha. Serikali imeanza kuchukua hatua za kutatua changamoto hizo kama ifuatavyo: kutekeleza programu ya kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge, kuanzisha taasisi inayotoa mikopo ya nyumba, kuendelea na zoezi la kutoa vitambulisho vya Taifa na anwani za makazi, kuchochea utumiaji wa Taasisi ya Kuhakiki Ukweli wa Taarifa za Waombaji Mikopo (Credit Reference Bureau), na kuimarisha mifuko ya dhamana ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu pamoja na wadau wengine itafanya tathmini ya viwango vya riba ili
99
kuweza kubainisha sababu za viwango kuendelea kuwa juu na kuchukua hatua zinazostahili.
Ushirikiano wa Kikanda
83. Mheshimiwa Spika, Ushiriki wa nchi yetu katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika unazidi kuimarika, hasa baada ya kusainiwa, kuridhiwa na kutekelezwa kwa itifaki muhimu za biashara na uchumi. Hatua hizi zitaongeza fursa za uwekezaji na hivyo kukuza uchumi na kuongeza upatikanaji wa ajira. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, naomba kutoa taarifa kwamba mtangamano umefikia hatua ya kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha ambapo Itifaki ya kuanzisha Umoja
100
huo ilisainiwa na Wakuu wa nchi za Jumuiya mnamo tarehe 30 Novemba 2013. Ili kuimarisha ushirikiano katika hatua zilizofikiwa, Benki Kuu za nchi wanachama zimekubaliana kurahisisha taratibu za kufanya malipo kati ya nchi zetu (cross border payments), hivyo kuwezesha malipo kati ya nchi zetu kuwa rahisi na hivyo kuhamasisha utumaji wa fedha na biashara.
84. Mheshimiwa Spika, kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha, naomba kutoa taarifa kwamba Serikali inakamilisha maandalizi ambapo kuanzia tarehe 1 Julai, 2014 mizigo inayokwenda nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakaguliwa mara moja katika bandari ya Dar es
101
Salaam na kuruhusiwa baada ya nchi husika kuthibitisha kwa Mamlaka ya Mapato kwamba kodi imelipwa. Hatua hii itapunguza muda wa mizigo hiyo kukaa bandarini, hivyo kupunguza gharama kwa wafanyabiashara na kuhamasisha ukusanyaji wa mapato na ukuaji wa uchumi wa nchi zetu. Kwa upande wa Itifaki ya Soko la Pamoja, naomba kutoa taarifa kwamba utekelezaji unaendelea na Serikali imetoa tangazo la kupunguza masharti ya uwekezaji wa mitaji baina ya nchi wanachama. Kuhusu kuwianisha kodi za ndani, majadiliano ya kupata mfumo bora wa kuwianisha kodi hizo yanaendelea na yatakapokamilika Bunge lako Tukufu litajulishwa. Lengo ni kuhamasisha biashara sawia baina ya nchi wanachama kwa kuwa na taratibu za kodi na viwango
102
vya kodi za ndani visivyotofautiana sana. Kwa upande wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), naomba kutoa taarifa kwamba Serikali inaendelea kutekeleza Itifaki ya Biashara. Aidha, napenda kulishukuru Bunge lako tukufu kwa kuridhia Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya nchi za SADC.
Uhusiano Kati ya Tanzania na Shirika la Fedha la Kimataifa kupitia Mpango wa Ushauri wa Kisera (Policy Support Instrument-PSI)
85. Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa na uhusiano mzuri na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia mpango wa Ushauri wa Kisera ujulikanao kama Policy Support Instrument-PSI.
103
Tanzania ilifanikiwa kujiunga na Mpango huu kutokana na juhudi zinazofanyika za kuimarisha uchumi tulivu na utawala bora. Mpango wa kwanza wa PSI ulianza kutekelezwa Februari 2007 hadi Juni 2010, na mpango wa pili ulianza Julai 2010 na kuishia Juni 2013. Mpango huu umekuwa chanzo kikuu cha kutoa ishara kwa wawekezaji na washirika wa maendeleo duniani juu ya ubora wa sera na mikakati, mipango na uwezo wa serikali katika kusimamia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ukuzaji uchumi, na upunguzaji umaskini nchini. Kutokana na mpango huu, nchi yetu imeendelea kupokea misaada na mikopo mbalimbali ikiwemo ya kibajeti, miradi ya maendeleo pamoja na mifuko ya kisekta. Aidha, IMF imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na
104
misukosuko ya urari wa malipo ya nje kwa kuziba nakisi ya mapato ya fedha za kigeni.
86. Mheshimiwa Spika, Kutokana na mafanikio hayo, Serikali imeridhia kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa PSI ambapo utekelezaji wake utaanza Julai 2014 kwa kipindi cha miaka mitatu. Awamu hii itaendelea kuijengea nchi yetu uwezo wa kuandaa, kutekeleza na kusimamia sera kwa lengo la kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu mbili zilizotangulia pamoja na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na uchumi tulivu na endelevu na hivyo kuvutia zaidi uwekezaji na kuongeza fursa za ajira nchini.
105
Tathmini ya Uwezo wa nchi Kukopa na Kulipa Madeni
87. Mheshimiwa Spika, hatua ambazo zimefikiwa hadi sasa ni kwa kupatikana kwa mshauri mwelekezi wa kuishauri Serikali ambapo Mkataba ulishasainiwa, Serikali pia imekamilisha hatua ya kumpata Mshauri wa Sheria wa Kimataifa (International Legal Adviser). Aidha, Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kupata Kampuni za kufanya tathmini (Rating Agencies). Zoezi hili lilichelewa kutokana na kampuni za tathmini kutokubaliana na aina ya fomu za mikataba zinazoandaliwa na Serikali pamoja na kuleta nyongeza ya gharama nje ya makubaliano yaliosainiwa awali ambapo imeilazimu Serikali kuanza zoezi hilo upya.
106
Kukamilika kwa zoezi hilo siyo tu kutawezesha Serikali kupata mikopo nafuu ya kibiashara kuliko ilivyo sasa, bali kutawezesha makampuni na taasisi binafsi za Tanzania kupata mitaji kwa urahisi kutoka soko la mitaji la kimataifa na kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi ambao ni muhimili wa uchumi. Aidha, zoezi hili ni muhimu katika kuiweka nchi kwenye ramani ya dunia hususan kiuchumi na kutambulika zaidi kwa wawekezaji.
IV. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO
88. Mheshimiwa Spika, Ili kuongeza mapato ya Serikali na kufikia malengo ya kiuchumi katika mwaka 2014/15, napendekeza kufanya marekebisho ya
107
mfumo wa kodi na tozo, ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi na tozo nyingine zisizo za kodi chini ya sheria mbali mbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali. Marekebisho hayo yanahusu sheria zifuatazo;-
a. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
b. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
c. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA 220;
d. Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA 124,
108
e. Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
f. Sheria ya Uwekezaji Tanzania, SURA 38;
g. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82;
h. Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya Mwaka 1972;
i. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
j. Marekebisho ya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na wizara, mikoa na idara zinazojitegemea;
109
k. Usimamizi wa kodi zinazotozwa kwenye mafuta ya petroli yanapoingizwa nchini.
l. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya sheria za kodi na sheria nyingine mbali mbali;
m. Kurekebisha Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348, Sheria ya Msajili wa Hazina SURA 418 na Sheria ya Wakala wa Serikali SURA 245 kwa minajili ya kuelekea kwenye kuunganisha fedha zote za umma chini ya Mfuko Mkuu unaodhibitiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali.
110
(a) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
89. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: –
(i) Kutoa msamaha wa kodi kwenye mapato yanayotokana na mauzo ya hatifungani zitakazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank) katika Soko la Mitaji la Tanzania. Hatua hii itawezesha Benki hiyo kuongeza uwezo wa kutoa mikopo nafuu ya uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile kuendeleza miundo mbinu n.k.
111
(ii) Kutoza Kodi ya Zuio ya asilimia 15 kwenye ada wanayolipwa wakurugenzi wa bodi kila mwisho wa mwaka;
(iii) Kufuta msamaha wa kodi ya makampuni kwenye mapato ya michezo ya kubahatisha;
(iv) Kufuta msamaha wa Kodi ya Zuio kwenye ukodishaji wa ndege kwa walipa kodi wasio wakazi (non-resident). Hatua hii inalenga katika kupunguza misamaha ya kodi na kuongeza mapato ya Serikali;
112
(v) Kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha ya kutoa misamaha ya kodi kwa miradi inayohusu upanuzi na ukarabati (expansion and rehabilitation) inayofanywa na wawekezaji. Msamaha huo hivi sasa unatolewa kwa utaratibu ambapo wawekezaji hupewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji (TIC Certificates);
(vi) Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 13 hadi asilimia 12. Hatua hii inalenga katika kutoa unafuu wa kodi kwa wafanyakazi. Aidha, Serikali itaendelea kuangalia uwezekano wa kupunguza kiwango hiki
113
hatua kwa hatua ili kuwapa nafuu wafanyakazi;
(vii) Kuongeza kiwango cha kutozwa kodi kwenye mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo yanayozidi shilingi 4,000,000 kwa mwaka na yasiyozidi shilingi 7,500,000 kwa mwaka, kutoka asilimia 2 hadi asilimia 4 kwa mauzo, kwa wanaoweka kumbukumbu za mauzo na kuongeza kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 200,000 kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo;
114
Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 31,504
(b) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
90. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
(i) Kufuta Ushuru wa Bidhaa wa asilima 0.15 unaotozwa kwenye uhawilishaji wa fedha (money transfer) ili kuwapa unafuu watu wanaotuma fedha kwa kutumia mabenki na kwa kutumia njia za simu. Badala yake napendekeza kuweka ushuru wa asilimia kumi kwa mabenki na mawakala kwenye mapato wanayopata
115
kwenye tozo na ada wanazokusanya kwenye shughuli za uhawilishaji wa fedha;
(ii) Kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha ya kutoa msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli isipokuwa tu misamaha inayotolewa kwenye mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo (Development Partners) ili kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji nk. Lengo la hatua hii ni kupunguza matumizi mabaya ya msamaha huu na kuelekeza misamaha ya aina hii kwenye miradi ya maendeleo na yenye manufaa kwa umma. Aidha, hatua hii ina lengo la kuifanya Sheria ya
116
Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 iwe sanjari na Sheria ya TIC SURA 38 na Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 ambazo zilifanyiwa marekebisho ili kuondoa msamaha wa kodi kwenye mafuta ya petroli;
(iii) Kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo ya uzalishaji (non-utility vehicles) yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilimia 25 hivi sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka minane na zaidi. Lengo la hatua hii ni kulinda mazingira na kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu ambayo yanasababisha ajali, vifo na kuongeza gharama kwa kutumia fedha za kigeni kuagiza vipuri mara kwa mara;
117
(iv) Kubadilisha ukomo wa umri wa magari ya uzalishaji na yasiyobeba abiria (non-passenger utility vehicles) yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilima 5 hivi sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka minane na zaidi. Aidha, kubadilisha ukomo wa umri wa magari ya kubeba abiria (passenger carrying vehicle) yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilimia 5 sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka mitano na zaidi. Lengo la hatua hii pia ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu yanayoharibu mazingira, kusababisha ajali na vifo na kuongeza mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagizia vipuri mara kwa mara. Hata
118
hivyo hatua hii haitahusisha matrekta ambayo yote yataendelea kuingizwa nchini bila kutozwa ushuru wowote;
(v) Kutoza Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 15 kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambulika katika HS CODE 94.01. Aidha mwaka 2013/14 Serikali ilianza kutoza Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 15 kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambulika katika HS CODE 94.03. Lengo la hatua hizi ni kuhamasisha matumizi ya samani zinazotengenezwa kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira na
119
teknolojia katika kuzalisha bidhaa hii hapa nchini na kuongeza mapato ya Serikali;
(vi) Kurekebisha viwango maalum (specific rates) vya Ushuru wa Bidhaa zisizokuwa za mafuta (Non-petroleum products) kwa asilimia 10. Bidhaa hizo ni pamoja na vinywaji baridi, mvinyo, pombe, vinywaji vikali, n.k. Aidha, bidhaa za sigara zitatozwa Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 25 ili kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku (Framework Convention on Tobacco Control) wa Shirika la Afya Duniani. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba huu kwa kuwa unalingana na azma ya Serikali ya kulinda afya
120
za wananchi wetu. Mabadiliko ninayopendekeza ni kama ifuatavyo:-
a. Ushuru wa vinywaji baridi, kutoka shilingi 91 kwa lita hadi shilingi 100 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 9 tu kwa lita;
b. Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka shilingi 9 kwa lita hadi shilingi 10 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1 tu kwa lita;
c. Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo
121
hayazalishwi hapa nchini kutoka shilingi 110 kwa lita hadi shilingi 121 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 11 tu kwa lita;
d. Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (unmalted), mfano kibuku, kutoka shilingi 341 kwa lita hadi shilingi 375 Kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 34 tu kwa lita;
e. Ushuru wa bia nyingine zote kutoka shilingi 578 kwa lita hadi shilingi 635 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 57 tu kwa lita;
122
f. Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 160 kwa lita hadi shilingi 176 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 16 tu kwa lita;
g. Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka shilingi 1,775 kwa lita hadi shilingi 1,953 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 178 kwa lita;
h. Ushuru wa vinywaji vikali kutoka shilingi 2,631 kwa lita hadi shilingi 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 263 kwa lita;
123
i. Ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka.
Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: –
j. Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 9,031 hadi shilingi 11,289 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na ongezeko la shilingi 2,258 kwa sigara elfu moja au shilingi 2.25 kwa sigara moja;
124
k. Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 21,351 hadi shilingi 26,689 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 5,338 au shilingi 5.30 kwa sigara moja;
l. Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 38,628 hadi shilingi 48,285 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 9,657 sawa na shilingi 9.65 kwa sigara moja;
125
m. Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi 19,510 hadi shilingi 24,388 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 4,878 kwa kilo; na,
n. Ushuru wa “cigar” unabaki kuwa asilimia 30.
Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 124,292.0
(c) Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA 220;
91. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA 220, ili kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha
126
kutoa msamaha wa Ushuru wa Mafuta kupitia Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA 220, isipokuwa misamaha inayotolewa kwenye mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, maji, n.k.
(d) Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA 124,
92. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari SURA 124 kwa nia ya kutofautisha mfumo wa usajili wa magari na ule wa pikipiki kwa kuweka namba zinazoanzia na TZ kwa pikipiki badala ya T.
127
Lengo la hatua hii ni kudhibiti uhalifu unaofanyika kwa kubadilisha namba za magari na kuweka kwenye pikipiki. Hatua hii haitaongeza mapato ya Serikali
(e) Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
93. Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza kiwango cha Ushuru wa Mauzo ya Nje (Export Levy) unaotozwa kwenye ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo moja hadi asilimia 60 au Shilingi 600 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo la hatua hii ni kuzuia biashara ya magendo ya ngozi ghafi. Uchambuzi unaonyesha kuwa hivi sasa hakuna ngozi ghafi zinazosafirishwa
128
nje kupitia vituo vya forodha na badala yake hupelekwa nje ya nchi kwa magendo. Aidha, lengo la kuongeza usindikaji wa ngozi hapa nchini ili kuongeza thamani na ajira bado halijafanikiwa. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 5,778.7
(f) Sheria ya Uwekezaji Tanzania, SURA 38
94. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko yafuatayo kuhusu kodi na uwezekaji:-
i. Napendekeza kuondoa saruji katika orodha ya bidhaa zinazofikiriwa kuwa za mtaji (deemed capital goods) ambazo hupata msamaha wa kodi hivi sasa kupitia TIC. Lengo la hatua hii ni
129
kuhamasisha uzalishaji wa saruji hapa nchini na kulinda viwanda vya saruji kutokana na ushindani wa saruji inayoagizwa nje;
ii. Napendekeza kufuta misamaha ya kodi iliyokuwa inatolewa kwa makampuni ya simu (telecommunication operators) pale wanapoingiza nchini au kununua bidhaa za mtaji (deemed capital goods). Misamaha hii ni ile inayotolewa kwenye vifaa kama; minara ya mawasiliano, jenereta, uzio wa minara, magari, base station, vifaa vya kujikinga na radi na kadhalika.
130
iii. Napendekeza kutoa tafsiri mpya ya wawekezaji mahiri (strategic investors) kwa kufanya marekebisho ya kiwango cha chini cha mtaji kinachotumika katika kuwatambua wawekezaji mahiri. Napendekeza kiwango cha chini cha mtaji wa wawekezaji mahiri wanaotoka nje ya nchi kiongezeke kutoka Dola za Kimarekani milioni ishirini kufikia Dola za Kimarekani milioni hamsini. Lengo la hatua hii ni kuelekeza vivutio vya misamaha ya kodi kwa wawekezaji ambao wanaleta mitaji mikubwa. Hata hivyo, napendekeza kiwango cha mtaji kinachomtambulisha mwekezaji wa Kitanzania kuwa mahiri kibakie pale pale, cha Dola za Kimarekani milioni 20, ili
131
kuwanufaisha wawekezaji wazalendo. Serikali inakusudia kuendelea na uchambuzi wa kubaini namna bora zaidi ya kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye miradi mikubwa na ya kimkakati ambayo itakuwa na msukumo mkubwa na wa haraka wa ukuaji wa uchumi, upanuaji ajira na uongezaji mapato ya wananchi.
Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 43,703.4
132
(g) Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
95. Mheshimiwa Spika, katika marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Elimu na Mafunzo Stadi SURA 82 kupitia Mswada wa Sheria ya Fedha 2013 yaliingizwa maudhui mapya katika sheria hiyo ambapo taasisi zinazonufaika na msamaha wa tozo ya ufundi stadi zilipunguzwa na kubaki Idara za Serikali au Taasisi za Umma tu na ambazo zinapata fedha kwa asilimia 100 kutoka Serikalini.
96. Mheshimiwa Spika, kwa uzoefu wa utekelezaji wa mabadiliko haya tumeona kuwa baadhi ya taasisi ziliachwa katika msamaha huu kimakosa. Kwa mfano, mashirika ya umoja wa mataifa na ofisi
133
za kibalozi hazitozwi kodi wala tozo kama hizi kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa. Hivyo basi, napendekeza kufanya marekebisho ili kuongeza taasisi zifuatazo katika msamaha wa tozo hii: (i) Ofisi za Kidiplomasia, (ii) Mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi za nje zinazotoa misaada ambazo hazijihusishi na biashara kwa namna yoyote ile, (iii) Taasisi za kidini kwa waajiriwa wake ambao ni mahsusi kwa kuendesha ibada tu, (iv) Mashirika yanayotoa misaada ya hiari yasiyojihusisha na biashara kwa namna yoyote ile, (v) Serikali za mitaa, na (vi) Taasisi za elimu na mafunzo zinazotoa huduma bure na hazijihusishi na biashara katika kutoa huduma ya elimu na mafunzo kwa namna yoyote ile.
134
(h) Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya Mwaka 1972
97. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara wamewasilisha mapendekezo ya kutoza viwango mbalimbali vya ada za leseni za Biashara kwa kutumia Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya mwaka 1972. Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Leseni za Biashara Na. 25 ya mwaka 1972, ili kuipa Serikali mamlaka ya kutoza ada za leseni za biashara kwa viwango vilivyopendekezwa.
135
(i) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
98. Mheshimiwa Spika, kikao cha maandalizi ya Bajeti cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) kilichofanyika tarehe 3 Mei 2014 jijini Nairobi, Kenya, kilipendekeza marekebisho ya viwango vya ushuru wa pamoja wa forodha (EAC Common External Tariff “CET”) kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 Kama ifuatavyo: –
(i) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 25 mabasi ya kubeba abiria yanayotambuliwa katika HS CODE 8702.10.99 ambayo yana uwezo wa kubeba
136
abiria 25 na zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuboresha huduma ya usafirishaji wa abiria na kupunguza ajali;
(ii) Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambuliwa katika HS CODE 1001.99.10 na HS CODE 1001.99.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda na wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano. Aidha, itaimarisha utulivu wa bei ya bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia ngano hiyo;
137
(iii) Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri badala ya asilimia 10 kwenye malighafi inayotumika katika kutengeneza sabuni (LABSA) inayotambuliwa katika HS CODE 3402.11.00; HS CODE 3402.12.00 na HS CODE 3402.19.00, kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuendelea kutoa unafuu kwa viwanda vidogo na vya kati vya kutengeneza sabuni, hivyo kuweza kuongeza uzalishaji na ajira;
(iv) Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwenye kemikali za kuua wadudu zinazotengenezwa kwa kutumia petroli zinazotambuliwa katika HS CODE
138
3808.91.39. Hatua hii inalenga katika kuwianisha kiwango cha ushuru unaotumika kwenye kemikali za kuulia wadudu zinazotengezwa kwa kutumia pareto ambazo nazo zinatozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25. Aidha, hatua hii itahamasisha wazalishaji wa dawa za kuua wadudu kutumia pareto inayozalishwa hapa nchini na kuwezesha wakulima wa zao la pareto kuwa na soko la uhakika;
(v) Kupunguza Ushuru wa Forodha unaotozwa kwenye karatasi zinazotambuliwa katika HS CODE 4805.11.00; HS CODE 4805.12.00 na HS CODE 4805.30.00; kutoka asilimia 25 hadi
139
asilimia 10. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za karatasi kwa kuwa karatasi hizo hazizalishwi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hata hivyo karatasi zinazotambuliwa katika HS CODE 4804.11.00. HS CODE 4804.21.00. HS CODE 4804.31.00 na HS CODE 4804.41.00 zitaendelea kutozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25. Karatasi za aina hii ni zile zinazozalishwa na kiwanda cha Mufindi na lengo la kufanya hivyo ni kukilinda kiwanda hicho ambacho ndicho pekee kinachozalisha karatasi za aina hiyo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
140
99. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo: –
(vi) Tanzania kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye mashine za kielektroniki za kukokotoa kodi (EFD) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii itapunguza gharama za kununua mashine hizi na hivyo kuhamasisha matumizi yake na kuboresha usimamizi wa kodi.
141
(vii) Kurekebisha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ili kufuta msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vijiti vinavyotumika katika kutengeneza njiti za viberiti. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha matumizi ya vijiti vinavyotokana na malighafi zinazopatikana hapa nchini.
(viii) Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya majeshi kwa kipindi cha mwaka mmoja. Katika kipindi hicho Serikali ya Tanzania imetakiwa kuangalia njia mbadala hususan za kibajeti
142
katika kutoa unafuu wa gharama za maisha kwa majeshi ya ulinzi.
(ix) Kurekebisha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi za kutengenezea mitungi ya gesi. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji kwenye utengenezaji wa mitungi ya gesi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(x) Kurekebisha Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya
143
mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vifaa vya kuzalisha umeme unaotokana na nguvu za upepo na jua. Hatua hii inalenga katika kutoa unafuu wa gharama za uwekezaji katika kuzalisha na kuendeleza umeme unaotokana na nguvu ya upepo na jua na hivyo kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,456.1
144
(j) Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
100. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na wizara, mikoa na idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.
(k) Usimamizi wa Kodi za Mafuta ya Petroli yanayoingizwa nchini
101. Mheshimiwa Spika, utaratibu wa utozaji wa kodi za mafuta ya Petroli unaotumika hivi sasa ni wa kuchelewesha malipo ambapo kodi inakadiriwa na
145
baada ya kukadiria malipo hufanyika katika siku 45. Tanzania ni nchi pekee inayotumia utaratibu huu katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika Nchi hizo kodi zikishakadiriwa hukusanywa mara moja.
102. Mheshimiwa Spika, kwa kodi ambazo zinachangia mapato mengi kama vile kodi za mafuta ya petroli utaratibu huu unaathiri utekelezaji wa bajeti. Aidha, ucheleweshaji wa malipo hayo hutoa mwanya wa ukwepaji kodi. Ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yake kwa wakati na kuziba mianya ya ukwepaji kodi, napendekeza kodi inapokadiriwa, malipo yafanyike mara moja.
146
(l) Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria nyingine mbalimbali
103. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo katika sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Mapendekezo haya yanaonekana katika muswada wa Sheria ya Fedha ya 2014.
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
104. Mheshimiwa Spika, Hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2014, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
147
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2014/15
105. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na shabaha ya bajeti, sura ya bajeti itakuwa kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 19,853.3 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Mapato ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 12,178.0 sawa na asilimia 19.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 458.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya shilingi
148
bilioni 2,941.6. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 922.2 ni misaada na mikopo ya kibajeti, shilingi bilioni 1,745.3 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 274.1 ni Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.
107. Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya bajeti, Serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni 4,275.2. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 2,265.7 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na mkopo wa ndani shilingi bilioni 689.6 ambao ni asilimia 1.1 ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,320 ambazo ni mikopo yenye masharti ya kibiashara zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
149
108. Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi, jumla ya shilingi bilioni 19,853.3 zimekadiriwa kutumika katika mwaka 2014/15, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 13,408.2 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 5,317.6 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Wakala na Taasisi za Serikali; Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi bilioni 4,354.7, na Matumizi Mengineyo shilingi bilioni 3,735.9.
109. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/15, jumla ya shilingi bilioni 6,445.1 sawa na asilimia 33 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya
150
maendeleo. Aidha, asilimia 69 ya fedha za maendeleo zitagharamiwa na fedha za ndani ambayo ni shilingi bilioni 4,425.7. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 689.6 zinatokana na mkopo kutoka vyanzo vya ndani, shilingi bilioni 1,320 ni mikopo ya masharti ya kibiashara, shilingi bilioni 375.5 ni mikopo ya kibajeti, na shilingi bilioni 2,040.6 inatokana na mapato ya ndani. Kiasi cha shilingi bilioni 2,019.4 kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha Mifuko ya Kisekta sawa na asilimia 31 ya bajeti ya maendeleo.
110. Mheshimiwa Spika, kiwango cha mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo kimeendelea kuongezeka ambapo kwa mwaka 2014/15, fedha za
151
ndani katika bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 4,425.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 2,952.9 zilizotengwa mwaka 2013/14 sawa na ongezeko la asilimia 50.
111. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2014/15, inazingatia pia mahitaji muhimu ya kitaifa ambayo hayawezi kuepukwa ikijumuisha gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Bunge Maalum la Katiba, upigaji kura ya maoni na uboreshaji wa daftari la wapiga kura.
152
112. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, mfumo wa bajeti kwa mwaka 2014/15 unakuwa kama ifuatavyo:-
153
Mapato Shilingi Milioni
A.
Mapato ya Ndani
12,178,034
(i) Mapato ya Kodi (TRA)
11,318,222
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi
859,812
B.
Mapato ya Halmashauri
458,471
C.
Mikopo na Misaada ya Kibajeti
922,168
D.
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo
2,019,431
E.
Mikopo ya Ndani
2,955,227
F.
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara
1,320,000
JUMLA YA MAPATO YOTE
19,853,331
Matumizi
G.
Matumizi ya Kawaida
13,408,218
(i) Deni la Taifa
4,354,731
(ii) Mishahara
5,317,550
(iii) Matumizi Mengineyo
3,735,937
Wizara 3,087,680
Mikoa 84,805
Halmashauri 563,452
H.
Matumizi ya Maendeleo
6,445,113
(i) Fedha za Ndani
4,425,682
(ii) Fedha za Nje
2,019,431
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 19,853,331
154
HITIMISHO
113. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, Bajeti ya mwaka 2014/15 imelenga kuongeza makusanyo ya mapato, hasa ya ndani kwa kuanzisha vyanzo vipya, kuboresha vilivyopo na kupunguza misamaha ya kodi. Aidha, Bajeti hii imelenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika, kuboresha elimu, kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miuondombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege. Hii itasaidia pia kutumia vyema fursa za kijiografia.
114. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, Serikali imepanga kushughulikia kwa nguvu zaidi kero mbalimbali zinazowakabili wananchi zikiwemo kero ya
155
upatikanaji wa maji, nishati ya uhakika, elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki na kusimamia ulipaji kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya mfumo wa Mashine za Kielektroniki za Kutoa risiti (Electronic Fiscal Devices) ulioboreshwa zaidi; kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kwa kutumia TEHAMA.
115. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa bajeti, Serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti. Kuhusu madai ya Wakandarasi na Wazabuni, Serikali inakamilisha utaratibu wa kusimamia na kuyalipa madai yaliyohakikiwa kupitia Hazina kwa kushirikiana na
156
wizara na taasisi zinazohusika. Aidha, Serikali inaendelea kuhimiza wizara na taasisi kuzingatia mfumo wa malipo (IFMS) ambao unamtaka kila Afisa Masuuli kutoingia mikataba bila kuwa na LPO inayotokana na mfumo wa malipo wa IFMS.
116. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misaada na mikopo ya nje, Serikali itaendelea kufanya majadiliano mapema na wahisani pamoja na mabenki ili kuhakikisha kwamba fedha za misaada na mikopo zinapatikana kama ilivyopangwa na kwa wakati. Hata hivyo, upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo kwa wakati inategemea umakini na usahihi wa kutekeleza miradi iliyokusudiwa kulingana na malengo
157
na makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.
117. Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti hii kunahitaji nidhamu ya hali ya juu ya wadau wote ikiwemo Serikali na taasisi zake, Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla. Ili kufikia azma hii juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Natoa rai kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ili Bajeti hii iweze kutekelezwa kama ilivyopangwa. Inawezekana, tutimize wajibu wetu.
118. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.