Hotuba ya Waziri Pinda Akijibu Hoja za Wabunge Kuhusu Bajeti ya Ofisi Yake

Nembo ya Taifa la Tanzania

Nembo ya Taifa la Tanzania

MAELEZO YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU, WAKATI AKIJIBU HOJA ZA WABUNGE KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
• Niruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Rehema kwa kunipa Afya njema hadi leo ninapohitimisha Majadiliano ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.

Mheshimiwa Spika,
• Katika mjadala huu, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 155 Walichangia. Waheshimiwa Wabunge 92 waliochangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 63 wamechangia kwa njia ya maandishi.

• Kama ilivyo miaka yote idadi ya Wachangiaji ni kubwa na muda wetu umekuwa mfupi sana. Hii inaonesha dhahiri jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge mnatambua umuhimu wa majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake.

• Tumejitahidi kujibu hoja hizo kupitia Mawaziri na Naibu Mawaziri, lakini bado zimebaki nyingi. Kama ilivyo ada tutajitahidi kujibu hoja zilizosalia kwa njia ya maandishi.

MAJIBU YA HOJA

Mheshimiwa Spika,
• Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Kanuni ya 99(9) inayohusu kujadili Bajeti ya Wizara, nichukue nafasi hii sasa kujibu na kufafanua baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:

UFISADI KATIKA IPTL ESCROW ACCOUNT

HOJA: Iko hoja kwamba kuna ufisadi katika IPTL, Escrow Account, iliyopo BOT kwa madai kwamba fedha hizo zimetolewa katika mazingira ya Ufisadi, kwa Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Aidha, kuna shinikizo la Ofisi kubwa. (Taarifa zilizotolewa ktika Gazeti la Mtanzania na CITIZEN).

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Ni kweli ziko taarifa zilizotolewa kwenye Magazeti ya Mtanzania na CITIZEN.

• Suala hili ni la muda mrefu tangia miaka ya 1995. Ni suala lililoanzia katika makubaliano yaliyotokana na Capacity Charge na Energy Charge. Kulitokea mgogoro ambao ulianzisha kesi kuhusu tariff hizo. Mgogoro ulihitaji usuluhishi Mahakamani. Aidha, Mgogoro mwingine ulihusisha Wabia wawili VIp Engineering na MECMAR. Wakati mgogoro huo ukiendelea ilikubalika kufungua Escrow Account – BOT ya kuweka fedha hizo ambazo zingelipwa IPTL hadi mgogoro umalizike.

• Yapo masuali ya msingi ya kujiuliza kama wakati mgogoro unaendelea, VAT ililipwa au ilisitishwa. Aidha, ni kujiuliza kama tangu mwaka 2009 Capacity Charge zililipwa.

• MECMAR na VIP waliuza hisa zote (100 Percent) kwa PAP, hata hivyo haijulikani kama pesa hizo ziliwekwa katika Escrow Account. Aidha, matokeo ya kuuza Hisa zote inamaanisha suala la Ufilisi linakufa.

• Uamuzi wa Mahakama ni kupeleka fedha zote za TANESCO IPTL.

• Mambo muhimu ya kujiridhisha ni kuangalia kama Mgogoro huu uliojitokeza majibu yake yanaweza kupatikana bila kutuhumiana. Aidha, kuna haja ya kujua kama katika hatua zote zilizochukuliwa, Kodi halali ililipwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

• Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipoliona kwenye Magazeti alizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO ili kupata ukweli.

• Baadaye akapata barua kutoka kwa Katibu Mkuu, Nishati na Madini yenye Hadidu za Rejea kufanya uchunguzi kujua ukweli. Wakati anaendelea na hilo akapata barua nyingine kutoka kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya kumtaka kufanya uchunguzi, lakini barua hiyo iliandikwa baada ya PAC kumuuliza/kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini juu ya suala hilo.

• CAG anazo barua mbili; ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na kutoka PAC pamoja na Hadidu za Rejea anazofanyia kazi. Mimi nimemwagiza CAG aendelee na uchunguzi huo ili tuweze kujua ukweli wa jambo hili. Hili siyo Siri, naamini ufumbuzi utapatikana. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuvute subira wakati CAG anafanya utaratibu wa kufuatilia na kukagua jambo hili. Aidha, TAKUKURU itahusishwa ili kujua kama pia kulikuwa na harufu ya Rushwa.

HATUA ILIYOFIKIWA KATIKA KUSHUGHULIKIA MGOGORO ULIOPO KATIKA HALMASHAURI YA MANISPAA YA BUKOBA

Mheshimiwa Spika,
• Halmashauri ya Manispaa ya Bukoka imeingia katika mgogoro wa Kiutawala na Kimenejimenti baada ya Baraza la Madiwani kutofautiana kimisimamo na kusababisha kuwepo kwa makundi mawili. Kundi moja linampinga Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo na Kundi la pili linalomuunga mkono. Chimbuko la mgogoro huu ni Uamuzi wa kukasimisha Madaraka kwa Kamati ya Fedha ambapo baadhi ya Wajumbe walikubali na wengine walikataa na kutaka liondolewe kwenye kumbukumbu za Halmashauri. Kutofautiana huko ndiko kulikozaa makundi mawili, moja linalounga mkono wazo la kukasimu na kundi lingine likikataa wazo la kukasimu madaraka ya Baraza la Madiwani kwa Kamati ya Fedha na Uongozi.

Mheshimiwa Spika,
• Baada ya kuwepo kwa makundi hayo, uendeshaji wa shughuli za Halmashauri ulishindikana kutokana na kutofanyika kwa vikao na mikutano ya kisheria ya Halmashauri (Council Statutory Meetings) ambayo ina jukumu la kuidhinisha masuala mbalimbali ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika,
• Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI iliunda Timu iliyoongozwa na Mheshimiwa Abbas Kandoro – Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Taarifa ya Timu na jitihada za Mkuu wa Mkoa zote hazikuweza kutoa suluhu kwa mgogoro huu.

• Kufuatia kutopatikana kwa suluhisho la mgogoro, Waziri mwenye Dhamana na Serikali za Mitaa kwa madaraka aliyonayo chini ya Kifungu cha 37(a) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 na kwa kuzingatia kifungu cha 29(2) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Namba 11 ya mwaka 2008 alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya Ukaguzi Maalum katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Timu ya Ukaguzi Maalum ilitekeleza jukumu iliyopewa la kukagua Hesabu za Halmashauri katika kipindi cha miaka mitatu ya 2010/2011, 2011/2012 na 2012/2013.

• Katika kutekeleza jukumu hilo Timu ilipitia nyaraka mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, pamoja na kuwahoji Waheshimiwa Wabunge, Madiwani, Watendaji na Wananchi pamoja na kutembelea miradi mbalimbali iliyoainishwa katika Hadidu za Rejea ambapo Timu imebaini kasoro, hitilafu na changamoto mbalimbali na kutoa ushauri na mapendekezo katika hoja walizofanyia kazi.

• Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha kuwa Mstahiki Meya, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa na baadhi ya Wakuu wa Idara walishiriki katika kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma.

• Kutokana na ukiukwaji huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitoa ushauri na mapendekezo mbalimbali ya namna bora ya kushughulikia kasoro hizo na hatua stahiki za kuchukua dhidi ya waliohusika.

• Aidha, kutokana na shutuma hizo, Meya wa Jiji la Bukoba alitangaza hadharani kujiuzulu. Tulimshukuru kwa kuandika barua ya kukubali kujiuzulu kwake.

• Hata hivyo, wakati Serikali ilipoanza kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya CAG na baada ya Meya kujiuzulu, baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Bukoba walifungua Shauri la maombi Namba 01/2014 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba. Mahakama imeagiza Halmashauri isikutane na kufanya Kikao chochote hadi kesi hiyo iatakapomalizika.

• Ni kweli kwamba, Meya wa Bukoba siyo Meya tangu alipotoa tamko la kujiuzulu hadharani.

• Nimemuomba Mkuu wa Mkoa asimamie kuwaomba Madiwani waliofungua Kesi Mahakamani kukubali kufuta Kesi hiyo kwa sababu wanaoumia kutokana na mgogoro huu ni Wananchi. Aidha, ni vizuri Vikao vya Mabaraza viendelee chini ya Naibu Meya ili kazi za Maendeleo za Wananchi ziendelee.

Mheshimiwa Spika,
• Katika mazingira haya, Serikali inalazimika kutii amri hiyo ya Mahakama hadi hapo Hukumu kuhusu Shauri hilo itakapotolewa. Nawasihi Wananchi wa Halmashauri ya Bukoba wawe watulivu na wavumilivu hadi hapo suala hili litakapohitimishwa na Mahakama.

MGOGORO WA MSITU WA KITETO

HOJA: Kuzingatia kuwa Hukumu ndio ilikuwa msingi wa kutatua Mgogoro.

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Mgogoro wa Ardhi katika Wilaya ya Kiteto upo katika eneo linalojulikana kama Hifadhi ya Jamii ya Emborley Murtangos iliyopata Usajili mwaka 2013. Eneo hili lenye ukubwa wa Hekta 133,333 lilianzishwa mwaka 2002 na Vijiji Saba vya Nameloc, Kimana, Loltepes, Ndigirish, Nhati, Emarti na Engusero, kwa kila Kijiji kuchangia eneo katika Hifadhi hiyo. Madhumuni ya awali ya Wananchi hao kutenga eneo hilo ilikuwa ni kuhifadhi mazingira pamoja na kulitumia kwa ajili ya malisho ya Mifugo.

• Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwake Wananchi mbalimbali wamekuwa wakiingia katika Hifadhi hiyo kufanya shughuli za Kilimo, licha ya kuzuiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, ambayo imekuwa ikifanya operesheni za mara kwa mara kuwaondoa Wananchi hao. Hali hiyo ilisababisha Wakulima wapatao 50 kufungua Kesi ya Madai dhidi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto. Katika Shauri hilo Wananchi waliofungua kesi walishinda. Hata hivyo, Halmashauri nayo ilikata Rufaa katika Mahakama ya Rufaa dhidi ya Wananchi hao.

Kwa mujibu wa Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa ilitamka kwamba, Eneo la Emborley Murtangos ni Hifadhi na hivyo kuamuru watu wote walioingia ndani ya hifadhi hiyo waondoke.

Mheshimiwa Spika,
• Ni muhimu kuzingatia kuwa Hukumu ya Mahakama ya Rufaa hii ndio ilikuwa msingi wa kutatua mgogoro huu. Katika kutekeleza hukumu hii ndipo yalitokea mapigano baina ya Wakulima na Wafugaji tarehe 12 Januari, 2014 ambayo yalisababisha Vifo vya Watu 10. Kubomolewa kwa Nyumba 10 na kuharibiwa kwa Pikipiki Sita na Baiskeli 53.

Mheshimiwa Spika,
• Kutokana na Taarifa za mapigano hayo, nilifanya Ziara ya Wilaya ya Kiteto tarehe 16 Januari, 2014 na kukagua uharibifu uliotokea kwa kutumia Helikopta ya Jeshi la Polisi na kuzungumza na Wananchi katika maeneo yaliyoathirika.

Mheshimiwa Spika,
• Ni dhahiri kwamba, jitihada za busara zinahitajika katika kutatua mgogoro huu. aidha, tunahitaji kuweka Kipaumbele katika kupanga matumizi ya ardhi.

• Zoezi la kuwaondoa wote walio ndani ya hifadhi linaendelea. Wengi tayari wameshaondoka, waliobaki ni wachache ambao nao wanaondolewa.

• Watuhumiwa 19 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kutokana na vurugu zilizotokea. Aidha, ulinzi katika eneo la Hifadhi ya Emborley Murtangos umeimarishwa.

• Maombi rasmi ya fedha kwa ajili ya kupima na kuhakiki mipaka ya hifadhi yameshaletwa Ofisi ya Waziri Mkuu na suala hilo linashughulikiwa.

• Elimu kuhusu umuhimu wa kuheshimu Hifadhi ya Jamii imetolewa na inaendelea kutolewa kwa Wananchi wa Vijiji vinavyozunguka Hifadhi. Aidha, Vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi hiyo vina Kamati ya Mazingira ili kusimamia suala la mazingira ya Hifadhi.

Mheshimiwa Spika,
• Pamoja na kuwepo kwa hali ya utulivu tangu nilipofanya Ziara hiyo, nasikitika kusema kuwa, hali katika eneo hilo la Hifadhi iliyopo Wilayani Kiteto imekumbwa tena na vurugu.

• Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, kuanzia tarehe 05 hadi 08 Mei, 2014 jumla ya miili ya Watu Wanne imeokotwa katika eneo la Hifadhi la Emborley Murtangos katika Kijiji cha Poropori.

• Tayari Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Mkoa wa Manyara vipo eneo la tukio kulinda Usalama wa Wananchi kuhakikisha mauaji hayatokei tena. Vipo Vikosi viwili vya Jeshi la Polisi katika Vitongoji vya Kimana na Kitongoji cha Poropori.

Mheshimiwa Spika,
• Ninapenda kutumia fursa hii kuwapa pole wafiwa wote na wale walioathirika na matukio hayo. Aidha, natoa wito kwa Wananchi katika eneo la Emborley Murtangos kuheshimu Amri ya Mahakama na kuondoka ndani ya Hifadhi kwa hiari yao.

• Nawasihi Wananchi wa Kiteto kuheshimu uamuzi wa Mahakama. Aidha, kila Kijiji tukae tuzungumze kwa kuzingatia maelekezo ya Mahakama.

• Nawaomba Viongozi wote tuwe na Staha, tuvute subira na tuwasaidie Wananchi kuepuka migogoro zaidi.

VIASHIRIA VYA UCHUMI JUMLA

Mheshimiwa Spika,
• Viashiria vingi vya Uchumi Mkuu vinaendelea kuimarika, vikiwemo ukuaji wa Pato halisi la Taifa, ukusanyaji mapato, kupungua kwa Mfumuko wa Bei na ongezeko la mauzo nje.

• Kwa mfano, katika mwaka 2013 uchumi wetu ulikua kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na Asilimia 6.9 mwaka 2012.

• Makusanyo ya Kodi yameongezeka kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni 117 kwa mwezi mwaka 2005/2006 hadi Wastani wa Shilingi Bilioni 800 kwa mwezi mwaka 2013.

• Mfumuko wa bei umepungua hadi kufikia Asilimia 6.1 mwezi Machi, 2014 ikilinganishwa na Asilimia 9.8 mwezi Machi, 2013.

• Bajeti ya Serikali imeendelea kuongezeka kutoka Shilingi Trilioni 4.2 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Trilioni 19.65.

• Wastani wa Pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 1,025,038 mwaka 2012 hadi Shilingi 1,186,424 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 15.7.

• Naomba nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu viashiria vya Benki ya Dunia juu ya Umaskini ikilinganishwa na hali ilivyo kwa Tanzania, mwaka 2012

Wastani wa Pato la Mtanzania kwa
mwaka 2012 ni = Sh. 1,025,038
Kwa mwezi ni = Sh. 85,419.8
Kwa siku ni = Sh. 2,847.3
Sawa na Dola za Marekani (US $) = 1.78.

Mwaka 2013 Wastani wa Pato la Mtanzania
Kwa mwaka 2013 = Sh. 1,186,424
Kwa Mwezi = Sh. 98,868.67
Kwa siku = Sh. 3,285.62
Sawa na Dola za Marekani (US $) 2.06.

• Kigezo cha Benki ya Dunia juu ya Umaskini ni kwamba Mwananchi anapopata chini ya Dola ya Marekani Moja (1) = Shilingi 1,600/=, basi hiyo anahesabiwa kuwa ni maskini.

• Lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2015 ni kuongeza kipato cha Mwananchi hadi kufikia Dola za Marekani (US $) 3,000 kwa mwaka.

• Kama tutaweza kukuza Uchumi kufikia Asilimia 8.0 kutoka Asilimia 7.0 kwa mfululizo wa miaka 10, tutaweza kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuwa ni Nchi yenye Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025.

• Kutokana na mafanikio tuliyoyapata, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutengemaza (Sustain) viashiria vya uchumi tulivyofikia ili kuongeza kasi ya kupunguza umaskini.

HATUA AMBAZO SERIKALI IMEKUWA IKICHUKUA KUPUNGUZA UMASKINI NCHINI KATIKA KIPINDI CHA 2006 – 2013

1.0 Kilimo

• Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuimarisha Sekta ya Kilimo na kuleta Mapinduzi ya Kijani hapa Nchini. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), azma ya KILIMO KWANZA, Mipango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo na Mifugo, Kuanzishwa kwa mpango wa kukopesha wakulima Matrekta, Uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, kuanzisha Mpango wa Kuendeleza Kanda za Kilimo (SAGCOT) na kadhalika.

• Serikali inatoa ruzuku ya mbolea, mbegu na viatilifu kwa Wakulima kupitia utaratibu wa Vocha. Utaratibu wa utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo umewezesha jumla ya Kaya takriban Milioni 2 kunufaika na Mpango huo.

• Kutokana na juhudi hizi za Serikali matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka Tani 73,000 mwaka 2006/2007 hadi kufikia Tani 240,350 mwaka 2012/2013, na matumizi ya Mbegu bora yameongezeka kutoka Tani 11,056 mwaka 2006/2007 hadi Tani 30,443 mwaka 2012/2013.

• Aidha, ni mara ya kwanza Tanzania inakuwa na chakula cha kutosha katika Maghala yake. Kwa sababu hiyo, kibali kimetolewa cha kuuza Tani 150,000 ili kutoa nafasi ya kuhifadhi mavuno mapya ya mwaka huu.

• Kwa ujumla Kilimo kimeanza kupanuka na kama tutapata maeneo mengine ya uchumi tutaweza kuendelea.

NISHATI

Mpango wa Kuongeza Uzalishaji wa Umeme Nchini

Mheshimiwa Spika,
• Kwa sasa (2014) uwezo wa kuzalisha umeme MW 1,583. Lengo ni kuzalisha MW 2,780 hadi MW 3,000 ifikapo mwaka 2015. Ipo miradi mingi inayotekelezwa na Serikali ili kufikia lengo hilo. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ifuatayo:
(i) Ujenzi wa Mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la kusafirisha Gesi Asili kutoka Mnazi Bay hadi Mtwara na Songosongo Kisiwani (Lindi) kupitia Somanga Fungu hadi Dar es Salaam. Gharama za Mradi huu ni Dola za Marekani Milioni 1,225.3, sawa na Shilingi Trilioni 1.96. Kati ya fedha hizo Asilimia 95 ni Mkopo Nafuu kutoka Benk ya Exim ya China na Asilimia 5 itachangiwa na Serikali.

(ii) Serikali inatekeleza mradi wa kujenga Mtambo wa Kufua Umeme wa Kinyerezi I utakaozalisha MW 150 na Kinyerezi II wa MW 240.

(iii) Serikali imekamilisha Mradi wa Ujenzi wa Mtambo wa kufua umeme wa MW 105 wa Ubungo II, Dar es Salaam. Vilevile, Serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa Mtambo wa kufua umeme wa MW 60 Nyakato, Mwanza.
(iv) Miradi mingine ni Mradi wa Somanga Fungu unaotekelezwa na Kampuni ya Kilwa Energy unaotarajiwa kuzalisha MW 320.

(v) Mradi mwingine ni ule wa kufua umeme wa Mchuchuma wa kuzalisha MW 600 na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka utakaozalisha MW 40.

• Miradi hii ikikamilika itaongeza uwezo wa uzalishaji umeme Nchini na kuondoa tatizo lililopo kwa kiwango kikubwa.

Mafanikio mengine katika Sekta ya Nishati (Umeme Vijijini)
• Serikali imefanikiwa kusambaza Umeme katika Wilaya zaidi ya 117 (sawa na Asilimia 89) kati ya Wilaya 133 zilizopo Nchini.

• Idadi ya Watanzania wanaopata umeme imeongezeka kutoka Asilimia 10 mwaka 2005 hadi zaidi ya Asilimia 30 mwaka 2013/2014.
• Kutokana na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Nishati, Makampuni makubwa yamefanya utafiti na Kugundua Gesi Asilia kiasi cha Fiti za Ujazo zaidi ya Trilioni 35 kwenye kina kirefu cha bahari.

• Serikali inatekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambao ukikamilika utatuwezesha kuwa na uhakika wa Umeme Nchini na wa bei nafuu. Hatua hii itasaidia kuokoa Dola za Kimarekani Milioni 850 kwa mwaka kwa kutumia Gesi Asilia badala ya Mafuta kuzalisha Umeme.

• Gesi nyingi imegunduliwa katika Bahari ya Hindi takriban Kilomita 4 – 5 kwenda chini ya Bahari. Tunasubiri tujue ni kiasi gani cha gesi kimepatikana.

• Serikali inatekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini ambapo wateja 15,305 kati ya wateja 22,000 wameunganishiwa umeme.

RELI/BARABARA

Mheshimiwa Spika,
• Hadi kufikia mwaka 2000, kulikuwa na barabara kuu za lami zenye urefu wa Kilometa 3,904 tu Nchini. Serikali ya Awamu ya Tatu, ilianzisha Miradi 14 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,226. Kati ya Miradi hiyo, Miradi saba (7) ya barabara zenye urefu wa Kilomita 403 ilikamilika katika kipindi cha Awamu ya Tatu kufikia mwezi Desemba 2005. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani ilirithi Miradi saba (7) iliyokuwa bado kukamilika yenye urefu wa jumla ya Kilometa 823 na kuikamilisha.

• Pia Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi mipya 26 ya ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilometa 1759.6. Kati ya Miradi hiyo, jumla ya Kilometa 1270.8 sawa na Asilimia 72 zimekamilika kwa kiwango cha lami kufikia mwezi Machi 2013. Kwa Miradi ya barabara zenye urefu Kilometa 488.8 zilizobaki, inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne (4) imejenga barabara kuu mpya zenye urefu wa Kilometa 2093.8 katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

• Sambamba na ujenzi wa barabara mpya, Serikali pia imeendelea kufanya ukarabati mkubwa wa barabara kuu za lami. Kati ya mwaka 2006 na 2013, Serikali ya Awamu ya Nne imetekeleza Miradi 10 ya ukarabati mkubwa wa barabara kuu za lami zenye urefu wa jumla ya Kilometa 841.2. Kati ya hizo jumla ya Kilometa 650, sawa na Asilimia 77 zimekamilika. Serikali inaendelea kukamilisha Miradi ya barabara zenye urefu wa Kilometa 191.2 zilizobakia kabla ya mwisho wa mwaka huu.

• Vilevile, pamoja na ujenzi unaoendelea katika Miradi hiyo, kuna Miradi mingine 43 iliyobuniwa katika Awamu ya Nne yenye urefu wa jumla ya Kilometa 5,739 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 16 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 3,817, ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa Usanifu, na Miradi 27 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,921 usanifu wake umekamilika na inatafutiwa Makandarasi. Lengo ni kuunganisha kwa awamu Miji Mikuu ya Mikoa yote Nchini kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika,
• Maendeleo ya ujenzi wa barabara yamepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo ya usafiri wa Barabara Nchini. Sambamba na hatua hizo za ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami, Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha mtandao wa barabara zote Nchini kwa kufanya matengenezo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuongeza Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Mfuko wa Barabara.

HOJA ZA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

UANDIKISHAJI WA WAPIGA KURA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA BIOMETRIC

HOJA: Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb.), Kiongozi wa Kambi ya Upinzani anataka kujua ni Sheria gani iliyotungwa na Bunge inayoruhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mfumo wa Biometric. Aidha, anasema:

“kuna mchakato wa maandalizi ya siri unaoendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kuandaa utambuzi wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa “biometric” kwa maana ya kumtambua mpiga kura kwa alama za mwili kama alama za vidole na au mboni ya jicho kama sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015”.

Kwa mujibu wa taarifa tulizokuwa nazo wakati ule, ni kwamba tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilishaanza maandalizi mengi ya msingi bila kushirikisha wadau, hasa vyama vya Siasa, isipokuwa CCM…………. Nilieleza pia kuwa teknolojia hii kwa siku za karibuni imetumika katika chaguzi nchini Ghana na Kenya. Kote huko, ilifeli, na chupuchupu iingize mataifa hayo katika vurugu kubwa za uchaguzi. Mataifa haya yalilazimika kurudia mfumo wa upigaji na kuhesabu kura kwa mkono, hali iliyosababisha hofu kubwa.…………… Niliweka bayana pia kwamba, si kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani haiafiki matumizi ya teknolojia mpya kurahisisha na kuboresha mfumo mzima wa uchaguzi katika nchi yetu, bali inatambua athari kubwa zinazoweza kutokea siku za usoni kama suala lililo “sensitive” namna hii halitafanywa katika misingi ya uwazi na ushirikishwaji wadau muhimu kama vyama vya siasa katika hatua zote la tangu awali kabisa……….”

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Nadhani Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb.), hakunielewa vizuri. Kwenye Hotuba yangu nilieleza kwamba Mfumo wa uandikishaji wa Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia ya Biometric ni Mfumo wa kisasa unaowezesha kuandikisha Wapiga kura wenye sifa kwa muda mfupi. Aidha, Mfumo huo huchukua alama za vidole kwa haraka na kuwapatia Vitambulisho vya Kupiga kura Wapiga kura mara baada ya uandikishaji.

• Kwa kawaida mifumo hii inafanya mambo mengi. Kuna mifumo ya kisasa inayoandikisha, mingine inaweza kutumika kupiga kura, kutoa matokeo kwa mtandao na kadhalika. Tunachodhamiria sisi ni kununua vifaa na Mfumo wa Kielektroniki wa kuandikisha wapiga kura tu.

Mheshimiwa Spika,
• Mfumo wa uandikishaji kwa njia ya Biometric umefanya kazi nzuri katika Nchi zote uliotumika kwa uhakika na kwa muda mfupi sana. Kilichotokea Ghana na Kenya siyo tatizo la uandikishaji wa Wapiga kura bali ni Mfumo wa utoaji matokeo kwa njia ya mtandao. Nchi ya Kenya iliweza kuandikisha Wapiga kura wengi sana katika kipindi cha muda mfupi.

• Napenda kuwahakikishia Wananchi wote kwamba Mfumo wa Biometric utakaotumika Nchini ni wa kuandikisha Wapiga kura tu. Hautatumika kupiga kura wala kutoa majibu kwa njia ya mtandao kutokana na mazingira halisi ya Nchi yetu. Kitakachofanyika siku ya kupiga kura ni kuhakiki alama za vidole ambazo zilichukuliwa wakati wa uandikishaji katika Daftari la Wapiga kura. Mfumo wa Kupiga Kura na kutoa matokeo ya kura utaendelea kutumia utaratibu wa sasa na siyo wa Kielektroniki.

• Ni vyema ikaeleweka kwamba, mchakato wa ununuzi wa vifaa unafanyika kwa kutumia Sheria ya Ununuzi wa Umma. Mchakato unafanyika kwa uwazi na pale ambao baadhi ya Wazabuni hawaridhiki wanashauriwa kukata rufaa. Napenda kuwahakikishia kwamba, hakuna usiri wowote katika mchakato huo.

UCHAGUZI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

HOJA: Maandalizi ya Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa yanaendelea chini kwa chini kwa ajili ya uchaguzi huo kufanyika Oktoba mwaka 2014.

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Serikali tayari imekwishaanza maandalizi ya Uchaguzi katika ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa.

• Kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) sura 288, muda wa Viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kukaa madarakani ni miaka 5. Kwa Viongozi wa Serikali za Mitaa walioko madarakani kwa sasa, muda wao unaishia Novemba 2014. Hivyo uchaguzi wa Viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji utafanywa mwezi Octoba 2014, kama sheria za Serikali za Mitaa inavyoelekeza kwenye kifungu cha 57(1) hadi 57(3).

“ As soon as may be practicable after the registration of a village, the village assembly of the village shall meet for the purpose of electing a village council for the village.

The meeting convened under subsection (1) shall be presided over by a chairman elected by the village assembly from among its members for the purpose of holding elections.

After the expiry of five years from the date when the village council was elected by the village assembly, the executive director of the village district council in which the village is situated, or any other person appointed by the director to be the assistant returning officer, shall in the manner prescribed by the Minister in the regulations convene a meeting of village assembly for election of new members of the council.

• Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 57 (4) cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287, Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa anaweza kuairisha uchaguzi huo hadi tarehe nyingine atakayoona inafaa.

“57(4)Notwithstanding the provisions of subsection (3) and of section 59, where for a reasonable cause or upon the occurrence of an event preventing the holding of elections of village councils, the Minister considers it necessary to postpone the elections to some later date, he may, by notice published in the Gazette, extend the term of office of the members, and the notice shall become effective only upon its approval by resolution of the National Assembly at its meeting immediately following upon the making of the notice by the Minister.”

• Aidha, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi huu Wasimamizi wa Uchaguzi ni Wakurugenzi wa Halmashauri na jukumu la OWM-TAMISEMI ni uratibu tu.

• Ni kweli kwamba, nilipokutana na Vyombo vya Habari tarehe 26 Machi, 2014 nilitoa mwelekeo wa kuongea na Mheshimiwa Rais kuhusu suala hili. Bado nina imani kuwa kwa vile maandalizi yanaendelea, Serikali italitolea uamuzi mapema.

KUZUIA MIKUTANO YA VYAMA VYA SIASA MTWARA NA LINDI

HOJA: Kwa muda unaozidi mwaka mmoja sasa, kumekuwa na zuio la Vyama vya Upinzani kufanya shughuli zake katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kisingizio cha vurugu zilizotokea mwaka jana wakati Wananchi wakikataa Bomba la Gesi kujengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Waziri Mkuu atoe Kauli Bungeni kuwa ni nani aliyetangaza kuzuia shughuli za siasa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, na ni Sheria ipi imetumika kukandamiza haki ya Demokrasia kwa kipindi kirefu hivyo wakati vurugu zilizotokea Mtwara na Lindi zilishakwisha.

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Limejitokeza suala la shutuma la kuwa Vyama vya Upinzani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi vimekatazwa kufanya shughuli zao kwa kisingizio cha vurugu zilizotokea mwaka jana wakati Wananchi wakikataa bomba la gesi kujengwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Aidha, kuna hisia kuwa Serikali imefanya jambo hili bila ya kufikiria. Pia kuna kauli kuwa CCM inaendelea na mikutano yake kama kawaida kwa upendeleo tofauti na Vyama vya Upinzani.

Mheshimiwa Spika,
• Katika kujibu suala hili, ningependa kwanza turudi nyuma kidogo kuangalia chimbuko la suala hili. Kutokana na kuwepo kwa mpango wa Serikali wa kusafirisha Gesi Asilia kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar-es-Salaam, kulitokea makundi ya baadhi ya Wananchi katika Mikoa ya Mtwara na Lindi wakipinga mpango huo. Aidha, baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Siasa walihusika kushinikiza wafuasi wao kukataa mpango huo kupitia Mikutano ya hadhara, Mikutano ya ndani ya Vyama pamoja na kusambaza vipeperushi mbalimbali. Hali kadhalika baadhi ya Viongozi wa Dini kupitia mahubiri yao nao walihusika katika kushinikiza waumini wao kupinga mpango huo wa Serikali.

• Katika Mkoa wa Mtwara kulijitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani uliokuwa ukifanywa na makundi ya Vijana kwa kulenga kuharibu majengo ya Serikali, nyumba za watu binafsi, nyumba za Wanasiasa, kuharibu magari ya watu binafsi na ya Serikali n.k.

• Vurugu hizo zilijitokeza kuanzia tarehe 25.01.2013 katika Wilaya ya Mtwara Mikindani na 26.01.2013 katika wilaya ya Masasi. Aidha wahalifu hao waliendeleza uhalifu kwa kushambulia nyumba za askari wanaoishi uraiani kwa lengo kuiba na kuharibu mali zao pamoja na kuwadhuru askari wanaoishi nje ya kambi. Katika vurugu hizo, jumla ya watu wanne walipoteza maisha. Hata hivyo, baada ya juhudi kubwa ya Serikali, hali ya amani na utulivu ilirejea.

• Pamoja na juhudi hizo, tarehe 22 na 23 Mei 2013, kulitokea tena vurugu nyingine kubwa katika Mji wa Mtwara ambapo kulitokea uharibifu mkubwa wa mali na Raia kujeruhiwa. Aidha, watu watatu walipoteza maisha katika vurugu hizo. Uharibifu huo ulihisisha uchomwaji moto wa nyumba binafsi za askari zipatazo 15, Ofisi za Kata 9, Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo na Ofisi 3 za CCM.

• Kwa kiasi kikubwa, vurugu hizi zilichochewa na Viongozi wa Vyama vya Siasa kwa kutoa lugha za uchochezi. Baada ya matukio hayo, Serikali kupitia Vyombo vyake vilifanya Operesheni maalum ya kiusalama na kuwashika wahusika.

Mheshimiwa Spika,
• Hivi katika hali kama hii, ilitegemewa Serikali ifanye nini? Haiwezekani kusema kuwa Serikali ilikurupuka na kufanya makosa katika kusitisha mikutano ya Vyama vya Siasa ambayo ilikuwa inahamasisha vurugu na uvunjifu wa amani. Uamuzi wa kusitisha mikutano ya aina hiyo ulikuwa ni wa lazima na busara.

• Kilichokatazwa katika Mikoa hiyo ni mikusanyiko ya hadhara inayoweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani. Jeshi la polisi linalo mamlaka ya Kisheria kuzuia au kuvunja mikusanyiko kama hiyo. Mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa ya aina hiii imesababisha vurugu, hasara na maafa makubwa kwa Wananachi na Serikali. Hata hivyo, mikutano ya Kisiasa inayoratibiwa kisheria na Tume ya Uchaguzi inafanyika bila ya kizuizi chochote. Chini ya utaratibu huo, chaguzi ndogo mbili zimefanyika bila ya tatizo lolote. Kimsingi, jukumu hili la Ulinzi na Usalama linahusu Mikoa husika. Na sisi kama Serikali tunategemea tathmini na ushauri kutoka kwao.

Mheshimiwa Spika,
• Baada ya vurugu hizo, kwa sasa hali ya amani na usalama katika Mikoa ya Mtwara na Lindi imeendelea kuimarika. Aidha, misako na doria imeendelea kufanyika ili kudhibiti vikundi mbalimbali vinavyoweza kuhamasisha na kuchochea vurugu kama vile vijiwe vya wavuta bhangi na wanywa gongo. Aidha juhudi za kujenga na kuimarisha miundombinu ya amani zinaendelea.

• Ni kutokana na juhudi hizo za Serikali za kurudisha hali ya utulivu katika Mikoa hiyo, hususan katika Mkoa wa Mtwara, uwekezaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ujenzi wa Bomba la Gesi, Kiwanda cha Saruji cha Dangote, n.k. unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika,
• Baada ya neema hii ya gesi Mkoani Mtwara, wakazi wa Mtwara mbali ya kufaidika kwa gesi asilia ambayo itakuwa ni chanzo cha uhakika cha umeme na matumizi ya gesi moja kwa moja watafaidika pia na kuwepo kwa Wawekezaji wengi walioonyesha nia ya kuwekeza Mkoani Mtwara kutokana na fursa hii. Mpaka sasa kuna Makampuni yapatayo 51 ambayo yameonyesha nia ya uwekezaji katika viwanda vya Saruji, Mbolea, Sekta ya Usafirishaji, Kilimo na Usindikaji, na kuwekeza katika Utalii. Aidha, mabaki ya gesi baada ya kusafishwa ni malighafi muhimu kwa baadhi ya viwanda vikiwemo vya mbolea, kemikali petrol, bidhaa za plastiki, n.k.

• Kutokana na kujengwa kwa viwanda hivyo na uwekezaji unaotarajiwa Mkoani Mtwara, tatizo la ajira Mkoani humo litapungua kwa kiasi kikubwa. Nimeelezwa kuwa, moja ya viwanda vikubwa vitakavyojengwa, kitahitaji Watumishi wa kawaida takriban 50,000 na Wataalam 2,000. Hakika huu utakuwa ni ukombozi mkubwa wa ajira kwa Wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla. Kampuni ya Dangote inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha Saruji Mkoani Mtwara ambacho kimeelezwa kuwa moja ya Viwanda vikubwa vya Saruji Barani Afrika, nacho kitatoa ajira nyingi na za uhakika kwa Wana Mtwara. Niseme tu kuwa, Wananchi wa Mtwara wawe na subira katika mipango hii kwani ni ya uhakika.

Mheshimiwa Spika,
• Ili kuhakikisha kuwa Wananchi wetu wakiwemo wa Mtwara na hususan Vijana wananufaika na ajira za maana katika miradi ya gesi na viwanda vitokananvyo na fursa za gesi, Serikali imejipanga katika kuelimisha watu wetu kama ifuatavyo:

• Mpango wa mafunzo umeandaliwa kwenye Taasisi za Elimu hapa Nchini na nje ya nchi katika eneo la Mafuta na Gesi Asilia. Hapa nchini Vyuo vinavyosomesha Wataalam wetu ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma, Dar es Salaam, VETA-Mtwara, na Madini Dodoma. Kwa Vyuo vya nje ya Nchi, Serikali imepeleka Wanafunzi katika Vyuo vya Trondheim – Norway, na Vyuo vya Aberdeen, Dundee, na Coventry vya Uingereza.

• Vilevile Serikali inagharamia mafunzo ya Wanafunzi 100 kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi kusoma mafunzo ya muda mfupi, VETA Mtwara.

• Katika hatua nyingine, Serikali imeanzisha mpango wa mafunzo wa ushirikiano kati ya Vyuo Vikuu vya Nchi za Angola, Norway na Tanzania (Angola, Norway, Tanzania Higher Education Initiative – ANTHEI) kwa nia ya kutoa mafunzo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika eneo la Petroli na Gesi. Mpango huo umeanza kwa vijana 10 kuanza mafunzo katika Vyuo hivyo Vikuu tangu muhula wa Oktoba 2012.

Mheshimiwa Spika,
• Suala muhimu kwa sasa ni kwa Wana-Mtwara na Lindi kuanza kujipanga na kutambua fursa zilizopo baada ya kupatikana kwa Gesi na kufanya mambo ya msingi yafuatayo:

• Kuongeza ujenzi wa nyumba bora kwa sababu kutakuwa na ongezeko la watu Mkoani watakaokuja kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi;

• Kujenga hoteli na nyumba za wageni zitakazotumiwa na Watu wa hadhi zote;

• Kwa upande wa Vyombo vya Fedha kama vile mabenki ya biashara, wajipanue zaidi katika kupokea biashara zaidi na kutoa mikopo kwa Wananchi.

• Serikali kwa upande wake itaendelea na juhudi za kuimarisha miundombinu ya Barabara, Bandari, Reli na kuboresha kiwanja cha Ndege.

• Katika hatua nyingine, Wana-Mtwara wajiandae kutoa vijana wao kwa kuwapeleka Vyuoni VETA ikiwemo kupata elimu ya Gesi ili waweze kuja kupata ajira za uhakika katika Miradi ya Gesi.

Mheshimiwa Sipka,
• Ninawapongeza Wananchi wote wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa utulivu wao. Aidha, nawapongeza Wakuu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kazi nzuri ya kusimamia ulinzi na usalama katika Mikoa yao. Ni dhahiri kwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuweza kuwaelewesha Wananchi katika Mikoa hiyo faida zitokanazo na rasilimali walizojaliwa kuwa nazo.

Ninawasihi wasitumike na kuhadaiwa kama ilivyokuwa awali na kufanya vurugu zisizokuwa na tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.

MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA TAIFA

Mheshimiwa Spika,
• Kabla ya kujibu Hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kutoa maelezo machache ya awali.

Mheshimiwa Spika,
• Nimeisikia na kuisoma kwa kina Hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb.) ikiwasilisha Bungeni Maoni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Katika Hotuba yake, ameeleza kwa kirefu sababu zilizofanya Umoja wao unaojulikana kwa jina la UKAWA kutoka nje ya Bunge la Katiba na kususia vikao vyake.

Mheshimiwa Spika,
• Kwa ujumla Kauli za Mheshimiwa Mbowe zilikuwa kali na za kutisha. Madai ya kuwepo kwa matusi siyo sababu inayotosha kuwa chanzo cha kususia Bunge na wala kutoka nje siyo suluhisho.

• Kibaya zaidi ni pale alipomhusisha Mheshimiwa Rais kuwa sababu ya kusababisha yote hayo.

Mheshimiwa Spika,
• Bunge Maalum la Katiba lina Wajumbe wa aina tatu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili, Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201 wanaotoka katika Makundi mbalimbali. Ni kwa sababu hiyo, Bunge hili likiwa ni sehemu tu ya Bunge Maalum vilevile halina mamlaka ya kujibu suala lolote linalohusika na Bunge Maalum la Katiba bila ya kujumuisha Uongozi wa Bunge Maalum na Wajumbe wote wa Bunge Maalum.

• Ninapenda kutumia fursa hii kuwashauri “Wana UKAWA” kutafakari matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum la Katiba kwa kupata majibu ya hoja zao. Malalamiko yao yatapata ufumbuzi wakiwa ndani ya Bunge Maalum na si vinginevyo. Sisi wote tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi hii muhimu tuliyopewa kisheria ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Katiba Mpya.

• Hivyo, natoa wito kwa Wajumbe wanaounda kundi la UKAWA ambao wamesusia Vikao vya Bunge Maalum la Katiba na kutoka nje ya Bunge hilo, warejee kwenye Bunge Maalum la Katiba kuendelea na Mjadala wa Rasimu ya Katiba na hapo ndipo mahala pake ambapo hoja za Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb.) zingefaa sana kuwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba na wakati huo huo kutumia utaratibu mzuri wa maridhiano uliowekwa Kikanuni ili kutatua tofauti zilizopo.

• Napenda nitumie pia fursa hii kusisitiza kuwa, siyo kweli kuwa Hotuba ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa kulihutubia Bunge Maalum la Katiba tarehe 21 Machi, 2014 Mjini Dodoma ilikuwa na maneno ya kutukana, dharau au kubeza kama alivyodai Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Hotuba yake hapa Bungeni. Hotuba ya Rais ilikuwa na Lugha ya Staha, yenye hekima na busara na ililenga kutoa mchango wa mawazo katika kutunga Katiba Mpya itakayoweka mbele maslahi mapana ya Taifa letu.

KAULI ZA UCHOCHEZI ZA UPINZANI

HOJA: Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeeleza kwamba kwa niaba ya wanachama wa UKAWA, itaendeleza harakati, nje ya Bunge Maalumu, zitakazowezesha kubadilishwa kwa muundo wa Muungano kwa kuivua Tanganyika koti la Muungano, kuipatia Zanzibar mamlaka kamili ndani ya Muungano na kujenga mahusiano ya hadhi na haki sawa baina ya Tanganyika na Zanzibar. Aidha, wamesema kama tutakwenda katika Uchaguzi Mkuu wa Mwakani bila Katiba Mpya tutaliingiza Taifa katika mgogoro mkubwa wa Kikatiba yaani “Constitutional crisis” ambao utakuwa rahisi kuzaa machafuko haswa kipindi cha uchaguzi.

JIBU:

Mheshimiwa Spika,
• Inasikitisha kuona kauli ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alizozitoa katika Bunge hili la Muungano. Kwamba Wajumbe wanaounda UKAWA katika Bunge Maalum la Katiba wamekataa kuwa sehemu ya usaliti kati ya Bunge hilo na hawatarudi Bungeni hadi usaliti huo kwa Watanzania utakapopatiwa ufumbuzi. Aidha, eti Bunge hilo limejaa kauli za kibaguzi, kashfa, vijembe na matusi dhidi ya “Wana UKAWA”. Kauli hizi zinapotokea kwa Viongozi wakubwa kama hawa lazima tuzipime kwa makini kuona kama hivi kweli Kauli hizi zinataka kuendelea na amani na utulivu tuliyonayo. Nataka kumsihi sana Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb.) kuwa hoja za kukejeliwa na matusi yote haya zilianzia mahali fulani katika Bunge Maalum la Katiba. Kilichofanyika ni kujibizana, hali ambayo siyo nzuri na haioneshi hekima na busara za Waheshimiwa Wabunge na zinazotarajiwa na Wananchi tunaowawakilisha.

• Nawasihi sana tuepuke kutotoa Kauli za aina hii zitakazosababisha mfarakano ndani ya Jamii. Hotuba ya Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe maneno yake yametulazimisha kujibu hoja hizi.

• Aidha, Kauli kwamba wingi wetu kupitia Chama Cha Mapinduzi unatumika kuburuza wachache, si sahihi kwa mtu kujaribu kujenga hisia kwamba yanayosemwa na walio wengi siku zote hayana maana na kwamba hayawawakilishi Watanzania na badala yake yanayosemwa na wachache ndiyo yanayowakilisha Watanzania. Naomba ieleweke kwamba, wingi wetu unatokana na imani ya Wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi kinachoweza kuongoza Nchi. Ni kweli tutaheshimu mawazo ya wachache kwa msingi wa hoja na nimewaomba sana nanyi Mheshimu ya wengi kwa msingi wa hoja.

• Siyo sahihi kwamba unaposhindwa hoja unasusa kikao au unatoka nje ya Vikao vya Bunge. Napenda kuwakumbusha kuwa “Asiyekubali Kushindwa Si Mshindani”.

Mheshimiwa Spika,
• Nimalizie kwa kusema nimesikitishwa sana na Kauli ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni juu ya Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

• Kwa maoni yangu Hotuba ile ilikuwa nzuri sana. Ilikuwa balanced. Katika kila eneo alilogusia alisema maneno yafuatayo kwamba, “Haya ni maoni yangu lakini, ni jukumu la kwenu Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuamua”.

• Kuhusu pale Mheshimiwa Rais alipozungumzia Jeshi, alizungumza kama mfano tu. Kimsingi alikuwa anazungumzia suala la umuhimu wa kuwa na Serikali ya Muungano yenye nguvu. Kama Nchi washiriki zitaachiwa madaraka yote, Serikali ya Shirikisho itakuwa haina nguvu. Ni wazi kwamba Mheshimiwa Rais hakumaanisha Jeshi la Wananchi, kwa sababu Jeshi letu tunajua lina nidhamu ya hali ya juu.

Mheshimiwa Spika,
• Serikali inasikitika na kauli hizo za uchochezi na zinazolenga kuvuruga amani ya Nchi yetu ambazo zinatolewa na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni. Inashangaza kuona kwamba Wanachama wa UKAWA wanaochelewesha mchakato wa Katiba Mpya kwa kutoka nje ya Bunge Maalum la Katiba halafu wanasingizia kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwakani utafanyika bila Katiba Mpya. Kauli kama hizi hazitatusaidia hata kidogo kupata Katiba Mpya ambayo Wananchi wanaisubiri kwa hamu kubwa. Siyo jambo jema sana kwa Kiongozi wa Kitaifa kubashiri machafuko kwa Nchi ambayo Wananchi wake wamejenga utamaduni wa amani kwa muda mrefu. Amani hii tuliyonayo ni Tunu kubwa. Ikitoweka, hakuna atakayebaki salama kamwe.

Mheshimiwa Spika,
• Nitumie fursa hii kuwaomba Viongozi wa UKAWA wafikirie tena uamuzi wao. Aidha, ni vizuri kujua kuwa kama ni matusi tuambizane kuamua tukae pamoja tuelezane kuwa tunaenda mbele na hakuna matusi tena.

• Hebu tutafute njia ya kukaa pamoja tuyamalize. Ni kweli kwamba, CCM tuko wengi, lakini uwingi huu usiwe sababu. Jambo la msingi ni kuangalia namna ya kusonga mbele kwa kujenga hoja.

• Sikubaliani kwamba, wachache tu ndiyo siku zote wako sahihi. Wengi huwa wanakosea.

FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika,
• Lugha za wizi si nzuri kama wangeweza kuuliza wangepata majibu.

• Si sahihi kuwatuhumu Mheshimiwa Aboud na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa wamezitafuna.

• Yawezekana ni hasira, hamjaziona fedha kwa Waziri Mkuu.

• Serikali ilipeleka fedha hizo HAZINA Zanzibar. Ni jambo la kufuatilia tu.

HOJA KWAMBA SERIKALI IMECHOKA

Mheshimiwa Spika,
• Leo sisi ni mkondo tu lakini sote tuko hapa na tumeshirikiana kufikisha Nchi hapa ilipo. Ni vizuri badala ya kulaumiana, tushirikiane kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri. Serikali ni sisi sote. Chama Cha Mapinduzi kinaiongoza tu kwa wakati huu.

• Serikali ina Mihimili Mitatu; Mahakama,Utawala na Bunge. Aidha, kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali. Hiki ndicho tunachokifanya hapa sisi sote.

• You are also part of this Government, na kama tumechoka na nyie pia mmechoka.

MENGINEYO

MASUALA YA JUMLA

Mheshimiwa Spika,
• Yapo maeneo ambayo kutokana na muda sitaweza kuyaongelea kwa sasa, nayo ni Migogoro ya kule Kiru – Babati, Biharamulo na yale aliyosema Mheshimiwa Kafulila, ya kule Jimboni kwake. Yote haya naamini yatakwisha.

MAKANISA KUVAMIWA NA MILIPUKO

Mheshimiwa Spika,
• Jambo linguine ambalo linanipa hofu na hali iliyojitokeza ya kuchoma Makanisa. Tumeshuhudia katika kipindi cha muda mfupi Makanisa yakichomwa kwa tarehe zifuatazo:
i) Tarehe 06/02/2014 – Bukoba
ii) Tarehe 19/02/2014 – Zanzibar
iii) Tarehe 03/03/2014 – Kihonda, Morogoro
iv) Tarehe 03/05/2014 – Mafia
v) Tarehe 05/05/2014 – KKKT Mwanza.

• Hali hii si nzuri – Tanzania haijazoea hali ya milipuko. Ni vizuri Vyombo vya Dola kuchukua hatua za makusudi kudhibiti hali hii.

Mheshimiwa Spika,
• Baada ya maelezo haya, naomba kutoa hoja.