HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. SHEIN KATIKA SHEREHE YA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI SEKONDARI YA UZINI KWA NIABA YA SEKONDARI SABA ZINAZOJENGWA KWA UFADHILI WA BENKI YA DUNIA, JANUARI 3, 2012

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Assalam Alaykum
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (SW) kwa kutujaalia uzima na afya tukaweza kukutana asubuhi ya leo katika hafla hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu hususan katika sekta ya elimu.

Aidha, nachukua fursa hii kuushukuru uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mara nyengine tena kunialika katika hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi ya skuli maalum za Sekondari nane (8) za Unguja. Hafla kama hii tuliifanya siku ya tarehe 20 Disemba, 2011 kwa skuli nane za Pemba pale Mchangamdogo sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi jengo la Chuo cha Ualimu cha Benjamin William Mkapa.

Kitendo cha uwekaji wa jiwe la msingi katika skuli hii ya Uzini ni uwakilishi wa skuli nyingine saba za Unguja. Skuli zinazowakilishwa ni Matemwe, Mwanda, Chaani, Paje Mtule, Tunguu, Dimani na Dole. Huu ni uendelezaji wa jitihada za Serikali katika kuimarisha ubora wa fursa ya elimu ya Sekondari kwa watoto wetu hapa nchini. Hatua hii vile vile ni utekelezaji wa misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964, yanayotimiza miaka 48 mwezi huu, ya kuwapatia fursa ya elimu watoto wote wa Zanzibar bila ya malipo wala ubaguzi wa aina yoyote.

Ndugu Wananchi,
Nimefarijika sana kualikwa na kushiriki katika shughuli hii kwani suala la ujenzi wa skuli hizi za Sekondari ni moja ya ahadi nilizokuwa nikizinadi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Aidha ni jumla ya utekelezaji wa Mpango wa Dunia wa Elimu kwa Wote (Education for All) ambao nchi yetu imeuridhia. Kwa mujibu wa mpango huu, kila nchi ina wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wote waliofikia umri wa kwenda skuli wanapatiwa fursa hiyo.

Kukamilika kwa ujenzi wa skuli hizi kutapanua fursa zaidi kwa watoto kupata elimu ya sekondari kwenye skuli zenye mazingira bora zaidi ya kujifunzia. Skuli hizi zitakuwa na maabara za kisasa kwa ajili ya masomo ya Sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia, Baiolojia na Kompyuta . Aidha, zitakuwa na maktaba za kisasa na huduma za dakhalia, mikahawa na nyumba za walimu.

Natoa wito kwa wazazi na walezi tuwashajihishe watoto wetu waongeze bidii katika masomo yao ili waweze kunufaika na fursa ya kuzitumia skuli hizi zinazojengwa katika kila Wilaya. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ya Awamu ya Saba, itahakikisha kuwa inatoa ushirikiano kwa Wajenzi wa skuli hizi ili kuhakikisha kuwa ujenzi wake unakamilika kama ulivyokusudiwa. Pia, nakuhakikishieni wananchi kuwa pamoja na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kila mwaka, hakuna mtoto atakaekosa fursa ya kujiunga na skuli kwa sababu ya uchache wa nafasi. Nimefarijika kusikia kuwa skuli hii itakapomalizika itatoa fursa kwa wanafunzi zaidi ya 480 wa kidato cha kwanza hadi kidato cha sita. Hili ni jambo la kutia moyo kuwa kumalizika kwa skuli hizi mpya kutatoa fursa kubwa zaidi kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari nchini.

Ndugu Wananchi,
Serikali inathamini sana umuhimu wa elimu katika ustawi wa maendeleo ya nchi yetu. Kwa hivyo, tunalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika uimarishaji wa sekta hii. Katika mwaka huu wa fedha 2011/2012 Serikali imetenga bajeti ya zaidi ya T.Shs. 102.6 bilioni kwa ajili ya kugharamia shughuli mbali mbali za elimu hapa Zanzibar. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 17 ya Bajeti yote ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka 2011/12. Aidha, nimearifiwa kuwa ujenzi wa skuli hii hadi kukamilika kwake umegharimu T.Shs. 1,287,099,957 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima Zanzibar (ZABEIP). Tumeamua kubeba mzigo huu kwa sababu umuhimu wa elimu hauna mbadala.

Nawasihi wazazi wenzangu kwa mara nyengine tena kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa kuwekeza katika kuwapa elimu watoto wetu. Suala la kuwekeza kwenye elimu ya watoto wetu kwa sasa haliwezi kuepukika na elimu haina ughali. Kuna msanii mmoja alisema “Kama elimu ni ghali, jaribu Ujinga”. Kwa hakika, hatuna haja wala sababu ya kujaribu ujinga kwani faida na umuhimu wa elimu kwa maisha yetu sote tunaujua na matatizo yanayoambatana na ujinga yanafahamika; ndio maana tunapambana nao tuuondoshe, kwa sababu ni adui wetu.

Ndugu Wananchi,
Wahenga walisema “Kitunze Kidumu.” Jukumu moja muhimu kwa wanafunzi watakaotumia skuli hizi na wananchi wanaoishi karibu nazo ni kuzitunza. Hatua hii itakuwa ni namna ya kuthamini fursa hii mliyoipata kwa niaba ya wananchi wengine. Aidha, tunategemea mtoe matokeo yanayoonesha ushindani wa kimasomo dhidi ya wengine ambao wanasoma kwenye Sekondari zetu za kawaida. Bila ya shaka huu utakuwa ni ushindani wa kimaendeleo na siyo kuwaona waliokosa fursa hii wamepitwa na wakati. Nia ya Serikali yenu ni kuwapa fursa ya elimu watoto wote wa Unguja na Pemba kwa misingi ya usawa kwa kadri ya uwezo wao.

Kwa mara nyingine tena napenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali na watendaji wake kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa majukumu ya Wizara yake sambamba na usimamizi wa ujenzi wa skuli hizi mpya za sekondari. Nina imani kubwa kuwa ujenzi wa skuli hizi utaendelea kusimamiwa vizuri na kukamilika kama iliyvokusudiwa. Aidha, natoa shukurani kwa wananchi wa maeneo yenye skuli hizi kwa ushirikiano wao kwa Wizara ya Elimu. Narudia kauli yangu niliyoitoa Pemba kuwa nitafuatilia kwa karibu sana maendeleo ya skuli hizi.

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa wenzetu wa Benki ya Dunia kwa kufanya uamuzi wa busara kwa kutupa mkopo huu uliotuwezesha kujenga skuli hizi. Hatua hiyo imetusaidia sana kuelekea lengo letu la kuimarisha fursa kwenye upatikanaji wa elimu ya sekondari hapa Zanzibar.

Kadhalika natoa shukurani kwa Wakandarasi wetu wa ujenzi huu wakiwemo China Railway Jianchang Engineering Co. (T) LTD ya Dar es Salaam, Electrics International Co. Ltd ya Dar es Salaam na China Henan International Corporation Group Co. Ltd ya Dar es Salaam. Vile vile, nawashukuru Washauri wanaosimamia ujenzi huu, ambao ni Hydro Plan Ingenieur ya Ujerumani pamoja na Metroconsult ya Dar es Salaam kwa jitihada zenu na ushirikiano mnaotupa; hali inayoashiria kuwa kwa pamoja tutafanikiwa kukamilisha ujenzi wa skuli hizi za sekondari kwa wakati.

Kwa kumalizia natoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja na wenyeji wetu wananchi wa Uzini kwa mapokezi yenu na ushirikiano mliotupa katika kufanikisha hafla hii ya leo. Narudia ombi langu kwenu kuwa muwe walinzi wa majengo yetu haya na muitumie vizuri fursa hii ili iweze kuwanufaisha vijana wetu wakati huu na siku zijazo.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa skuli zote nane za sekondari za Unguja tunaziwekea Mawe ya Msingi ikiwemo skuli hii ya Sekondari ya Uzini leo tarehe 3 Januari, 2012.

Ahsanteni sana.