HOTUBA YA RAIS WA TANZANIA, JAKAYA KIKWETE, KATIKA SHEREHE YA UZINDUZI WA UJENZI WA BARABARA ZA USAFIRI WA HARAKA WA MABASI JIJINI DAR ES SALAAM SEPTEMBA19, 2012

Mfano wa Kituo Kikubwa cha Mabasi ya Mradi wa Usafiri wa Haraka Dar es Salaam (DART)

HOTUBA YA RAIS WA TANZANIA, JAKAYA KIKWETE, KATIKA SHEREHE YA UZINDUZI WA UJENZI WA BARABARA ZA USAFIRI WA HARAKA WA MABASI JIJINI DAR ES SALAAM SEPTEMBA19, 2012

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (MB), Waziri wa Ujenzi;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mheshimiwa Meck Sadiq, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Serikali mliopo hapa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:

Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kunialika nije kujumuika nanyi katika uzinduzi rasmi wa ujenzi wa awamu ya kwanza wa barabara za Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dar Rapid Transit -DART) zenye urefu wa kilometa 20.9. Kama mtakumbuka, tarehe 10 Agosti, 2010 nilizindua ujenzi wa awamu wa kwanza wa miundombinu ya Mradi wa DART. Leo nazindua ujenzi wa barabara za Mabasi ambao unaanzia Kimara hadi Kivukoni, Magomeni hadi Morocco na Fire hadi Kariakoo. Ujenzi huu unagharimiwa na Serikali kwa kushirikiana na mshirika wetu mkubwa wa maendeleo-Benki ya Dunia.
Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru rafiki zetu hao, Benki ya Dunia, kwa kukubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 225.62 kwa ajili ya mradi huu. Aidha, nafurahi kumwona Mkurugenzi Mkazi wa Benki hiyo akiwa hapa pamoja nasi katika hafla hii. Kuwapo kwake hapa ni ishara tosha kuwa Benki hii ipo tayari kushirikiana nasi kuukamilisha mradi huu na mingine mingi wanayoifadhili ili wananchi wafaidi matunda yake mapema iwezekanavyo.
Ndugu wananchi;
Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana kuhusu tatizo la msongamano wa magari Dar es Salaam. Wote mtakubaliana nami kuwa Jiji la Dar es Salaam linakuwa kwa kasi sana, watu ni wengi na wanaongezeka kila siku. Muda sio mrefu tutapata takwimu sahihi ya idadi ya wakazi wa Jiji hili. Huenda ikawa zaidi ya milioni tano. Watu hawa wanahitaji usafiri wa uhakika na wa haraka ili wawahi kufika kwenye shughuli zao, wafanyakazi wawahi maofisini na wanafunzi wawahi kufika shuleni na vyuoni.
Daladala ni nyingi sana lakini hazijatatua tatizo lililopo na upo ukomo wa kuendelea kusajili daladala. Hatuwezi kuongeza tu idadi yake bila kuzingatia uwezo wa barabara zetu na vituo vya kuziegesha. Vilevile kadri hali ya uchumi inavyozidi kuwa nzuri watu wengi zaidi wanapata uwezo wa kununua magari, hivyo msongamano wa magari unazidi kuongezeka. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020, magari yatakuwa zaidi ya 500,000 Jijini Dar es Salaam, hivyo basi tusipotafuta suluhisho stahiki, upo uwezekano wa tatizo hili kuendelea kuwepo. Msongamano wa magari unaleta adha kubwa kwa wakazi wa Jiji mpaka kufikia baadhi yao wanaamua kuhama makazi yao na kurejea maisha ya kupanga nyumba maeneo yaliyopo karibu na wanapofanyia shughuli zao.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2007 Serikali iliandaa Mpango Kabambe wa Uboreshaji wa Mfumo wa Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam kwa msaada wa Serikali ya Japan. Lengo kuu la Mpango huo ni kutafuta majawabu endelevu ya msongamano wa magari Jijini. Ulipokamilika mwaka 2008 ukaainisha mikakati kadhaa na kutoa mapendekezo ya kupunguza msongamano wa magari barabarani. Mradi huu tunaouzindua leo wa ujenzi wa barabara za Kimara-Kivukoni, Fire-Kariakoo na Magomeni-Morocco pamoja na ujenzi wa Karakana na Vituo vya Mabasi yaendayo haraka ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango huo wa Serikali wa kupunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam.
Kama nilivyoeleza awali, mradi huu utagharimu fedha nyingi hasa ukizingatia kuwa tuna mahitaji mengi mengine katika maeneo ya afya, elimu, maji na kadhalika. Lakini hasara inalopata taifa kutokana na msongamano wa magari ni kubwa zaidi. Hatuwezi kuendelea kusubiri. Hivyo hatuna budi kujifunga mkanda na kutekeleza miradi itakayotatua tatizo hili mapema iwezekanavyo. Kuna mikakati mingine ya kupunguza msongamano wa magari ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hiyo imeelezwa na Mheshimiwa Waziri na dhamira yetu ni kuikamilisha ili kutimiza ahadi iliyotolewa na Chama cha Mapinduzi kwa wakazi wa Dar es Salaam wakati wa Kampeni za Uchaguzi mwaka 2010.
Ndugu wananchi;
Kwa upande wa Serikali, tunaamini kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi huu na mingine iliyoelezwa, kero ya msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam itapungua sana na ufanisi wa kazi maofisini na viwandani utaongezeka na hivyo kuchangia kukua kwa uchumi. Lakini ili mradi uweze kufikia malengo yaliyokusudiwa, ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu sana. Wao ndio waendeshaji wa shughuli za usafiri. Kazi yetu sisi Serikalini ni kujenga miundombinu na kusimamia sera ya sekta nzima ya usafiri na usafirishaji.
Bahati nzuri Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART Agency) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, imeanza kuwaelimisha wafanyabiashara ya usafirishaji nchini namna watakavyoweza kujipanga ili kuendesha biashara hiyo kwa mtindo mpya. Ni matarajio yangu kuwa juhudi hizi zitazaa matunda na wenzetu hawa watabadilika. Nawashauri wafikirie kuunganisha nguvu zao na kuanzisha makampuni makubwa ya usafiri ambayo yataweza kukopeshwa na mabenki ya ndani na nje ya nchi ili yaweze kuendesha biashara hii ya usafiri Jijini Dar es Salaam. Kuendeleza ubinafsi hakutawasaidia, tena huenda kukatoa mwanya kwa makampuni ya kigeni kuichukua biashara hii kwa urahisi.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha usafiri na mtandao wa barabara zetu, wapo wananchi wachache ambao wanajihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu hiyo. Vitendo hivi vinailetea taifa hasara kubwa kwani vinachangia sana kuharibika mapema kwa barabara na madaraja. Baadhi ya vitendo hivi ni kuzidisha uzito wa mizigo kwenye magari, kumwaga mafuta barabarani, kuziba mifereji ya maji na kulima kandokando ya barabara.
Aidha, utupaji wa takataka kwenye madaraja na uchimbaji mchanga kwenye mito husababisha mmomonyoko wa udongo na hatimaye kuanguka kwa madaraja. Wapo pia wezi wa vifaa na alama mbalimbali za barabarani na madarajani. Utakuta mtu anang’oa kingo ya daraja au alama ya kuongoza watumiaji wa barabara na kisha kuuza kama chuma chakavu. Hivi tamaa ya mtu mmoja au wawili ndio isababishe hasara kubwa hivyo kwa jamii nzima? Tusikubali watu wa namna hiyo waendelee kuvuruga mipango yetu ya maendeleo. Anayen’goa au kuharibu vifaa hivyo kwa makusudi na anayenunua wote ni wahalifu. Wafichueni watu hawa ili sheria ichukue mkondo wake.
Ndugu Wananchi,
Nawaomba pia mradi utakapokamilika mzingatie na kuzifuata taratibu na kanuni zitakazowekwa za kutumia huduma hii ya Mabasi yaendayo Haraka. Kutakuwa na barabara maalum za mabasi hayo, madaraja ya watembea kwa miguu, vituo vya kushusha na kupakia abiria. Abiria watatakiwa kuzingatia kanuni na tahadhari za usalama zitakazowekwa ili kuepusha ajali kwa watumaji wa huduma hiyo. Katika hili naomba tuwe makini maana isije ikageuka kuwa tatizo lingine pale watu watakapopuuza tahadhari na kusababisha ajali za mara kwa mara. Itakuwa haina maana kupunguza msongamano wa magari na kisha kuongeza vifo kwa watumiaji wa mabasi yaendayo haraka.
Isije kuwa kama inavyotokea kwenye barabara. Kila tunapoweka barabara kiwango cha lami, ajali zinaongezeka sana. Na, sababu kubwa ya ajali hizi ni mwendo kasi, ulevi wa madereva, uzembe na kutokuzingatia alama za barabarani. Jeshi la Polisi na Mamlaka zinazohusika wahakikishe hili halitokei.
Mheshimiwa Waziri;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi;
Kwa kumalizia naomba nisisitize kuwa miundombinu hii inaigharimu Serikali yetu fedha nyingi. Hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa fedha hizo tunazitumia kujenga barabara imara na zenye ubora wa hali ya juu. Napenda kutoa wito kwa Wakala wa DART, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI, pamoja na Wizara ya Ujenzi ikishirikiana na Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa karibu mradi huu ili ujenzi wake uzingatie viwango vilivyokusudiwa.
Aidha, naiomba Wakala aendelee kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wote ili mfumo huu mpya wa usafiri uweze kueleweka na kutumika kwa ufanisi kama unavyotarajiwa. Hii itawezesha sio tu kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi bali kuinua hali ya maisha ya Watanzania hususan wale waishio Dar es Salaam.
Mwisho, nawashukuru sana wote kwa ushiriki wenu katika hafla hii ya uzinduzi wa mradi huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kufanya kazi iliyonileta – ya kuzindua rasmi ujenzi wa Awamu ya Kwanza wa Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam.
Asanteni kwa kunisikiliza