Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Chuo, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela;
Mheshimiwa Prof. Makame M. Mbarawa (Mb), Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Prof. Idrissa Mshoro, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela;
Profesa Burton Mwamila, Makamu Mkuu wa Chuo – Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela;
Dr. Frannie Lautier, Katibu Mtendaji wa African Capacity
Building Foundation;
Viongozi wa Siasa na Watendaji wa Serikali ;
Wanajumuiya ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mkuu wa Chuo kwa kunialika kuja kujumuika nanyi siku ya leo kwenye uzinduzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Mfuko wa Dhamana wa Taasisi. Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki cha aina yake hapa nchini. Kwangu mimi hii ni ndoto yangu nyingine katika kuendeleza elimu nchini ambayo leo inatimia.
Aliponitembelea Ikulu Dar es Salaam 6 Machi 2007 dada yetu Frannie Lautier wakati ule akiwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, aliniambia kuwa Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini Mheshimiwa Nelson Mandela aliwahi kumuomba Bwana James Wolfenson akiwa Rais wa Benki ya Dunia asaidie Afrika kuendeleza sayansi na teknolojia. Kwa mujibu wa Rais Nelson Mandela hiyo ndiyo njia bora ya kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na msingi madhubuti ya maendeleo endelevu. Bwana James Wolfenson aliliafiki wazo hilo na kuwaagiza wafanyakazi wa Benki ya Dunia wa kutoka Afrika kulifanyia kazi.
Yeye na wenzake wakafanya hivyo na ndipo wazo la kuwa na Nelson Mandela African Institutes of Science and Technology lilipozaliwa. Wazo hilo lilipokelewa kwa furaha na Wakuu wa nchi Januari 2005 katika Mkutano wa Abuja, Nigeria. Iliamuliwa kuwepo na vyuo vinne na kwa kuanzia viwepo vya Abuja na Arusha.
Baada ya kupokea maelezo hayo kutoka kwa Dr. Frannie Lautier sikusita kukubali kuwa Chuo hicho kijengwe hapa nchini. Nikamuagiza Prof. Peter Msola aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kutekeleza uamuzi wangu huo. Mchakato wa kujenga Chuo hiki ulianza wakati huo na leo tunashuhudia matunda yake. Chuo kimekamilika na ninakizindua rasmi.
Mchakato wa kujenga Chuo hiki ulijumuisha mambo mengi na watu wengi. Jambo moja kubwa ni kule kuundwa kwa Kikosi Kazi chini ya uongozi wa Prof. Burton Mwamila kutayarisha mawazo ya msingi, kujenga dhana ya Chuo na kufikiria mambo yote yanayohitajika ya kuwezesha Chuo hicho kuwapo na uendeshaji wake. Baada ya mapendekezo kutolewa ilifuatia kazi kubwa ya kutafuta raslimali za kujenga Chuo.
Lazima nikiri kuwa pale mwanzoni nilidhani kuwa Benki ya Dunia ingetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo hicho. Nilipoulizia nikajibiwa kuwa hapana. Benki hiyo haitafanya hivyo ni jukumu letu. Hali kadhalika Umoja wa Afrika nao wakajibu hivyo na kusisitiza kuwa ni mzigo wa kubebwa na nchi mwenyeji. Niliwaandikia marafiki zangu wawili watatu duniani ambao nao pia hawakunipa majibu ya matumaini.
Tukaamua tuchune bongo zetu kuwezesha Chuo kiwepo. Tulisaidiwa sana na uzoefu wetu wa ujenzi wa UDOM. Hivyo tukaanza kuzungumza na mifuko ya Pensheni ili ikopeshe Serikali kujenga Chuo hiki kama walivyofanya kwa Chuo Kikuu cha Dodoma. Bahati nzuri walikubali maombi yetu pesa ikatolewa na ndiyo maana leo hii tunacho Chuo hiki kizuri na cha aina yake. Sina budi kumpongeza Dr. Frannie Lautier ambaye sasa ni Katibu Mtendaji wa Taasisi ya African Capacity Building Foundation kwa moyo wake wa kizalendo na kwa kufikisha wazo hilo zuri kwangu.
Napenda pia, kutumia fursa hii kutoa shukrani maalum kwa wenzetu wa mifuko yetu ya Pensheni ya NSSF, PPF, PSPF na LAPF kwa kuunga mkono na kusaidia jitihada za Serikali katika ujenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Uamuzi wao wa kukubali maombi ya Serikali kukopa fedha za ujenzi ndio umewezesha Taasisi hii kuwepo. Wakati nikiwashukuru napenda kutoa rai kwa mifuko hii iendelee kuisaidia Taasisi ikamilishe ujenzi katika maeneo yaliyobaki. Nawapongeza pia Mkandarasi na Mshauri Mwelekezi kwa kufanya kazi nzuri na kukamilisha sehemu kubwa ya ujenzi katika kipindi kifupi.
Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru Task Force ya Prof. Benson Mwamila na Kamati ya Katibu Mkuu Fanuel Mbonde pamoja na Wizara, taasisi na idara zote za Serikali ambazo zimefanya kazi kubwa na nzuri na kushiriki katika hatua mbalimbali za ujenzi na ukarabati wa Taasisi hii. Sina budi kuwataja Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Fedha; Wizara ya Afrika ya Mashariki; Wizara ya Maji; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Wizara ya Katiba na Sheria; Wizara ya Nishati na Madini; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na nyinginezo. Aidha, Taasisi ambazo zimehusika kwa karibu pia katika uendelezaji huu ni pamoja na TCU, TANROADS, TANESCO, TTCL, UHAMIAJI, COSTECH na Shirika la Posta Tanzania. Kwa pamoja ninawashukuru sana na kuomba kuwa yale maeneo machache ambayo bado yanaendelea kufanyiwa kazi yakamilishwe haraka.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Nachukua fursa hii kukupongeza wewe kwanza kwa kunikubalia ombi langu la kuwa Mkuu wa Chuo hiki licha ya kuwa unalo jukumu lingine zito la kunisaidia kuongoza nchi yetu. Lakini pia kwa uongozi wako mzuri wa Taasisi hii. Kwa kweli Taasisi imepata bahati kubwa ya kuanza na wewe kama Mkuu wa Chuo. Namshukuru na kumpongeza Prof. David Mwakyusa, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hii, Wajumbe wa Baraza, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Burton Mwamila kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya katika ujenzi na uanzishaji wa hii Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Kwa namna ya pekee natoa shukrani zangu za dhati kwa Mzee Nelson Mandela kwa kukubali Tanzania kutumia jina lake kuiita Taasisi hii. Angekataa, taasisi hii ingekuwepo lakini ikiwa na jina lingine.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Nilieleza kuwa sikusita kukubali pendekezo la kuanzishwa kwa Chuo hiki hapa nchini kwa sababu na mimi natambua nafasi na umuhimu wa sayansi na teknolojia kwa maendeleo ya Afrika. Ni ukweli ulio wazi kuwa maendeleo popote pale yamechochewa na kuletwa na matumizi ya sayansi na teknolojia. Hivyo, jamii ambayo ina maendeleo madogo na matumizi kidogo ya sayansi na teknolojia itakuwa nyuma katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Huo ndiyo ukweli kuhusu kuwa nyuma kwa Bara la Afrika ukilinganisha na Mabara mengine duniani.
Ndiyo maana hata pale tulipokosa msaada na Benki ya Dunia, Umoja wa Afrika na kutoka kwa marafiki niliamua kuwa sisi wenyewe tutafute namna ya kujenga Chuo hiki. Hatukukubali nchi nyingine katika ukanda wetu ipewe nafasi hii badala yetu. Nina kila sababu ya kufurahi kwamba hilo limewezekana kama tunavyoshuhudia sote siku ya leo. Penye nia pana njia.
Kama ilivyoelezwa Chuo hiki kinatoa mafunzo ya shahada za Uzamili na Uzamivu katika taaluma mbalimbali za sayansi na teknolojia. Pia kitakuwa kitovu kikuu cha utafiti katika kuendeleza utambuzi na matumizi ya sayansi na teknolojia hapa nchini na katika Kanda ya Mashariki mwa Afrika. Matokeo ya ubunifu na ugunduzi yatatumika kuongeza kasi ya kusukuma maendeleo ya viwanda na uchumi kwa jumla nchini na kwingineko Afrika na duniani. Taasisi hii itakuwa chachu ya kuendeleza viwanda na uchumi kwa jumla katika nchi zetu.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Mabibi na Mabwana;
Katika kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imetoa msukumo mkubwa katika kuendeleza elimu nchini tangu ya Awali hadi elimu ya juu. Matokeo yake ni kuwa hivi sasa tunao watoto wengi wanaopata elimu ya Awali, Msingi na elimu ya Juu kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. Tumeweza kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 42,000 mwaka 2005 hadi wanafunzi 135,367 mwaka 2011. Lengo letu ni kuona kuwa watu wengi wanaomaliza shahada ya kwanza na ya pili wanapata nafasi ya kuendelea zaidi na masomo ya juu.
Nimekuwa nahimiza vyuo vikuu vyetu nchini viongeze udahili wa wanafunzi wanaosomea shahada ya Uzamili na Uzamivu. Kuanzisha taasisi yetu siyo tu inasisitiza dhamira yetu hiyo bali pia ile ya kutoa msukumo mkubwa katika kuendeleza sayansi na teknolojia nchini. Mtakumbuka pia kwamba kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu ni sera ya Serikali kuwapa kipambele cha kwanza wanafunzi wanaosomea shahada za Sayansi. Kwa sababu hiyo hivi sasa tunao wanafunzi wengi wanaopata shahada ya kwanza katika fani na taaluma mbalimbali za mawanda ya sayansi na teknolojia.
Ndugu Chancellor;
Kuwepo kwa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inaongeza fursa zaidi kwa watu hao kujiendeleza zaidi kitaaluma. Hakika taasisi hii inaiongezea nchi yetu uwezo wa kujiletea maendeleo na kulitoa taifa letu katika lindi la umaskini. Ni tafsiri sahihi na ya vitendo ya kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa “mkitaka kumkomboa maskini, mpeni elimu mtoto wake.”
Kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana pamoja na uhaba wa rasilimali fedha na changamoto nyingi za maendeleo zinazotukabili, tulihakikisha kuwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inajengwa na tutahakikisha kuwa inakua, inastawi na kutambulika kimataifa kuwa kituo kilichotukuka kwa kufikia upeo wa juu kitaaluma na kwa kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Tunataka hapa kiwe kitovu cha elimu bora, utafiti na ubunifu utakaochochea kasi ya maendeleo nchini. Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa hapa na utafiti unaofanyika vinalenga kutatua matatizo halisi yanayoikabili jamii yetu ya uchumi na maendeleo pamoja na viwanda kama inavyosema kauli mbiu yake “Taaluma kwa Manufaa ya Jamii na Viwanda”.
Mkuu wa Chuo;
Kama nilivyokwisha sema awali sisi katika Serikali tutaendelea kuiwezesha taasisi hii kifedha na kwa mahitaji mengineyo muhimu. Pamoja na hayo na ninyi muwe wabunifu kutafuta vyanzo vingine vitakavyowapatia fedha zaidi za kufanya tafiti na kufundishia. Taasisi inaweza kushirikiana na viwanda, vyuo vingine vya utafiti na taasisi mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa kwa ajili hiyo.
Pamoja na kuendelea kuchangia kupitia fedha za utafiti tunazotenga kila mwaka katika bajeti, Serikali itakuwa tayari kushirikiana na taasisi hii kufanya tafiti maalum na kuzigharamia. Aghalabu tafiti hizo itakuwa ni zile zenye manufaa ya moja kwa moja kwa maendeleo ya nchi yetu hususan katika nyanja za kilimo, afya, nishati na mazingira. Nawaomba muwe wabunifu na hodari wa kubaini maeneo ya utafiti na maendeleo ambayo Serikali inaweza kuvutika na kudhamini. Mnaweza kufanya hivyo hata kwa makampuni mbalimbali kwa mambo ambayo watavutika nayo.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Ndugu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo;
Makamu Mkuu wa Chuo;
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana kwa uamuzi wenu wa busara wa kuanzisha mfuko wa dhamana wa taasisi hii yaani the Nelson Mandela African Institute of Science and Technology Endownment Fund. Ni wazo zuri na ni mpango mzuri ambao ukifanikiwa utaisaidia sana taasisi yetu hii muhimu kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa ufanisi. Naliunga mkono wazo hili na naahidi kuwa Serikali na hata mimi binafsi niko tayari kushirikiana nanyi kufikisha jambo hili adhimu.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Chuo hiki au Taasisi hii ni changa sana na ndiyo kwanza inazaliwa hivyo kuna kazi kubwa ya kuilea na kuikuza. Serikali imeonesha kwa vitendo nia yake ya kutaka chuo hiki kiwepo na kiendelee kuwepo kwa miaka mingi ijayo. Ndiyo maana tunaendelea na tutaendelea kukigharamia. Lakini sisi ni Serikali ya nchi maskini hivyo uwezo wetu si mkubwa sana. Wakati mwingine tunaweza kushindwa kutimiza mahitaji kwa wakati si kwa sababu ya kupuuza bali uwezo umepwelea.
Hivyo basi napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa nchi za ukanda wetu kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa Chuo hiki kinakuwa na uwezo wa hali ya juu wa kujiendesha. Isitoshe, taasisi hii si kwa ajili ya Tanzania pekee bali ni kwa manufaa ya nchi zote za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Afrika Kusini mwa Sahara. Natoa wito huo huo kwa wenye viwanda, wafanya biashara na watu binafsi wenye mapenzi mema na nchi yetu na Afrika nao wajitokeze kushirikiana nasi. Yote nyie mtanufaika na wataalamu na utafiti utakapofanyika.
Michango yenu itaboresha mazingira ya Chuo na kuwezesha kupatikana wataalamu wa hadhi ya kimataifa kuwepo hapa chuoni (staff retention). Itawezesha tafiti za hadhi ya kimataifa kufanyika, kuwepo kwa maabara zenye hadhi ya kimataifa. Misaada yenu pia itakiwezesha Chuo kutoa “scholarships” kwa wanafunzi na watafiti.
Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo; na
Wafanyakazi wote wa Chuo cha Nelson Mandela;
Ninyi ndio mlio “jikoni” mnafanya kazi ya kupika chakula. Tulio nje tutajua ubora wa chakula mnachokipika kikitoka jikoni na kuja mezani kuliwa. Ubora wa Taasisi hii utategemea sana kile mnachokifanya katika shughuli zenu za kila siku. Mimi sina wasiwasi hata chembe kwamba mtaweza kufanya kile tunachowatarajia sote. Kwa mfano mtazalisha wataalamu wa hali ya juu watakaohitajika na kila mmoja nchini na hadi duniani kutokana na ubora wao. Taasisi hii itafanya tafiti ambazo matokeo yake yatagombaniwa na viwanda na waendelezaji wengineo kwa ubora wake na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii.
Peperusheni bendera ya Tanzania juu kabisa na tembeeni kifua mbele. Kujengwa kwa taasisi hii kwa nguvu zetu wenyewe tunaithibitishia dunia kuwa Watanzania tukiamua tunawe. Nami ninaamini kwa dhati kuwa mnaweza kuzalisha watalaam na tafiti zenye ubora na kuhimili ushindani kimataifa.
Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Nelson Mandela;
Wanafunzi mnaosoma katika Taasisi hii, ni vyema mtambue kuwa ninyi ni kundi maalum na sehemu muhimu katika historia ya Chuo hiki. Ndiyo wa kwanza hivyo hamtasahaulika. Ninyi ndiyo kielelezo cha kama tunafanikiwa katika dhamira yetu ya kujiletea maendeleo nchini kwa kutumia sayansi na teknolojia. Nawaomba mjitume kwa kadri ya uwezo wenu. Jifunzeni sana, muwe wadadisi wa mambo na wabunifu. Nilipoyaona na kuyasikia kwenye maonesho kabla ya kuja hapa yamenipa faraja kubwa sana. Hakika tumefanya uamuzi sahihi kuanzisha Chuo hiki. Pia tumefanya uteuzi sahihi wa Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Wahadhiri. Hakika shabaha yetu itatimia na Chuo hiki kitakuwa chachu ya kuongeza kasi ya kuleta maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na uzinduzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, nimeombwa pia kuzindua mfuko maalumu wa dhamana wa chuo hiki, yaani, The NM-AIST Endowment Fund for Excellence. Mfuko huu ni njia mojawapo iliyobuniwa ili kuiwezesha Taasisi hii kuwa endelevu, na iweze kujiendesha kwa ubora uliolengwa. Baada ya kuzindua Mfuko huu ninawaomba wadau mbalimbali wachangie kwenye mfuko huu, ikiwa ni pamoja na sekta binafsi hapa nchini ili mfuko uwe kielelezo kingine cha ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi (Public-Private-Partneship) katika utoaji wa elimu ya chuo kikuu. Aidha, naomba mashirika na taasisi za kimataifa, nchi marafiki wa Tanzania, na makampuni ya kimataifa yanayoshiriki katika shughuli mbalimbali hapa nchini, kuchangia kwenye mfuko huu. Kwa hiyo nauagiza uongozi wa chuo hiki kuandaa harambee Dar es Salaam na Arusha mapema iwezekanavyo ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kuchangia kwenye mfuko huu.
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa kumalizia nakushukuru tena Mkuu wa Chuo kwa kunialika. Sasa natangaza rasmi kuwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imezinduliwa pamoja na Mfuko wa Dhamana wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Nakuomba Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais na Mkuu wa Chuo upokee Hati ya kumiliki ardhi ya eneo la Taasisi lenye ekari 3,285, na Cheti cha Usajili wa Mfuko wa Dhamana wa Taasisi.
Asanteni sana