Ndugu Ludovick Utouh, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
Mheshimiwa Dr. John Pombe Magufuli, Waziri wa Ujenzi;
Mheshimiwa Leonidas Gama, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;
Waheshimiwa Wabunge, Mhe. Augustine Mrema, Iddi Azan,
Zainavu Vullu, Joseph Selasini;
Mwenyekiti wa Mkoa;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Mstahiki Naibu Meya;
Madiwani;
Mkurugenzi wa Manispaa;
Viongozi mbalimbali wa Mkoa mliopo hapa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Ndugu Ludovick Utouh kwa kunialika kuja kushiriki nanyi ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali hapa Mkoani Kilimanjaro. Hii ni mara yangu ya tatu katika kipindi kifupi kufungua majengo ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Mwaka 2009 nimefungua jengo la Singida. Mwezi Januari mwaka huu nilifungua jengo la Morogoro na sasa nipo hapa Kilimanjaro kufanya kazi hiyo hiyo. Nimefurahi kuna majengo mengine mawili katika Mikoa ya Lindi na Shinyanga ambayo nayo yamekamilika na yanasubiri kufunguliwa.
Napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza sana wewe Ndugu Utouh na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kufanikisha ujenzi wa majengo haya. Hongereni sana kwa kupiga hatua hii nzuri ya maendeleo. Endeleeni na kasi hii mpaka mtimize ndoto yenu ya kuwa na ofisi zenu wenyewe kwenye kila Mkoa. Nakuahidi ushirikiano wangu na msaada wa Serikali katika kila hatua mtakayopiga.
Mabibi na Mabwana;
Sote tuliopo hapa tunaridhika na jengo hili. Ni zuri, linapendeza na linapendezesha mandhari ya Manispaa yetu ya Moshi. Limejengwa vizuri kwa ustadi mkubwa na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Natoa pongezi kwa wale wote walioshiriki katika kufanikisha ujenzi wa jengo hili. Ninafurahi kusikia kuwa ujenzi wake umefanywa na kampuni za kizalendo za J. S. Khambhaita Ltd ya hapa mjini Moshi, ikiwa mjenzi mkuu. Nawapongeza washauri wasimamizi yaani ya Kampuni ya Space Link ikishirikiana na Digital Space Consultancy, UNDI Consulting Group Ltd., na JB Costcare Consultant Ltd. Nawapongeza wote hao kwa kazi nzuri ya kukamilisha ujenzi wa jengo hili kwa ustadi mkubwa.
Ndugu Wafanyakazi wa Ofisi ya
Taifa ya Ukaguzi;
Naamini kukamilika kwa jengo hili kunawapa faraja kubwa watumishi wa Ofisi ya Ukaguzi ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa mazingira yenu ya kufanyia kazi sasa yamekuwa mazuri. Lile tatizo la ninyi kufanya kazi katika ofisi za kuazima sasa limekwisha. Kupatikana kwa jengo hili sasa kunawaondolea mtihani wa kufanya kazi zenu kwenye ofisi za kupanga au za wale mnaotakiwa kuwakagua. Sasa tunategemea kuwa mtatimiza ipasavyo wajibu wenu. Mtachapa kazi zaidi na kwa uhuru zaidi.
Mabibi na Mabwana;
Kwa ujumla, Serikali inatambua, kuthamini na kuridhishwa na kazi ifanywayo na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha na rasilimali za umma. Kazi yenu ni nzuri na taifa linafaidi matunda yake. Uwajibikaji unazidi kuimarika katika Wizara na Idara za serikali na umakini katika utunzaji na usimamizi wa rasilimali za umma unaongezeka. Utendaji kazi ulio makini wa Ofisi hii umechangia katika kuleta mabadiliko hayo.
Kwa kweli sina budi kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa manufaa ya nchi yetu na maendeleo ya watu wake. Mnatoa mchango muhimu sana. Lakini, pamoja na mafanikio hayo ya kutia moyo, bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Bado kuna wizi, ubadhirifu na matumizi yasiyoridhisha ya fedha na rasilimali za Serikali. Lazima muongeze juhudi zenu maradufu kupambana na changamoto hizo.
Mimi na wenzangu Serikalini tunayo imani kubwa kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi itaendelea na kazi yake nzuri ya kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinatumika vizuri kwa maslahi ya taifa. Tuna imani kuwa mtazishinda changamoto zilizo mbele yenu. Naomba mfanye kazi hiyo kwa umakini na weledi mkubwa. Kama mtu ni mwizi, hata awe kiongozi, anachezea mali ya umma au ni mbadhirifu wa rasilimali za umma, basi achukuliwe hatua zinazostahili. Hakika hii ndio njia pekee itakayowapa wananchi wote wa Tanzania fursa ya kufaidi matunda ya uhuru na kuwapa maisha bora.
Ili kutimiza malengo haya maridhawa hamna budi mfanye kazi kwa ushirikiano wa karibu sana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU); Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) pamoja na taasisi nyingine za Umma zinazofanya kazi katika eneo hili.
Mabibi na Mabwana;
Kwa upande wetu Serikalini tutakuwa bega kwa bega na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kwenye hili hatutawaangusha. Serikali yetu inafuata na kuheshimu utawala wa sheria. Hivyo hatutawaingilia katika utendaji wa kazi yenu. Mtaendelea kuwa huru kama Katiba na Sheria inavyotaka muwe. Kazi kwenu, mshindwe wenyewe! Pale mtapohitaji msaada tuambieni tutaangalia namna ya kuwasaidia.
Aidha, Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi zenu na maslahi ya wafanyakazi kila hali ya fedha itakavyoruhusu. Mahitaji ya Serikali ni mengi na fedha tulizonazo hazitoshi lakini ninyi pia tutawapa umuhimu unaostahili. Nawaomba muendelee kuongeza elimu na ujuzi wa wakaguzi wenu ili muweze kupambana na changamoto za nyakati zinapojitokeza kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kwa ajili hiyo nimefurahi kusikia mnao mpango wa kujenga kituo cha mafunzo pale Gezaulole. Jijini Dar es Salaam hilo ni wazo zuri sana na nawaomba mlitekeleze haraka. Jitahidini kituo kiwe na hadhi ya kimataifa ili angalau kiweze kutoa mafunzo kwa maofisa wetu na wenzetu wa nchi za jirani. Jambo hili linawezekana kabisa.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
Wafanyakazi wa Ofisi ya Ukaguzi;
Kabla sijamaliza napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana kwa taasisi yenu kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa na Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa. Hii ni nafasi adimu na adhimu kwenu na pia ni heshima kwa taifa letu. Kwa kuwa mmekwishaanza ukaguzi wa kimataifa, mkatuwakilishe vizuri huko UN ili taifa letu liendelee kujizolea sifa kama ilivyo kawaida yetu. Nendeni mkatimize wajibu wenu kwa mataifa yaliyotuamini, lakini pia tumieni nafasi hiyo kujenga uwezo wa taasisi yetu na weledi wa wakaguzi wake. Ujuzi mtakaoupata huko utajenga uwezo zaidi wa ukaguzi hapa nyumbani. Miaka sita sio michache, hivyo ninaamini wakaguzi wengi watapata fursa ya kunufaika na fursa hiyo.
Mwisho naipongeza tena Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kupiga hatua hii kubwa ya kukamilisha jengo zuri la Ofisi ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika mkoa wa Kilimanjaro. Kazi iliyobaki mbele yenu ni kulitunza jengo lenu ili libaki kama linavyoonekana sasa kwa miaka mingi ijayo na kufanya kazi kwa bidii zaidi, ufanisi zaidi na uhuru zaidi.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Baada ya kusema hayo sasa nipo tayari kufanya kazi iliyonileta hapa, kazi ya kufungua rasmi jengo jipya la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mkoa wa Kilimanjaro. Nawatakia kila la heri katika mwaka huu wa 2012.
Asanteni kwa kunisikiliza.