HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UZINDUZI WA MABANGO YA KAMPENI YA KUPINGA MAUAJI YA TEMBO NA FARU UTAKAOFANYIKA KATIKA UWANJA WA KIMATAIFA WA MWALIMU JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM,
TAREHE 11 FEBRUARI, 2014
Mhe. Mahmoud Hassan Mgimwa, Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Mhe. Said Meck Sadick, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam;
Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Mama Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Wakurugenzi na Watumishi Mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi Zake;
Viongozi wa Taasisi Zisizo za Kiserikali na wawakilishi wa jamii zinazojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Naibu Waziri kwa kunishirikisha kwenye tukio hili kubwa na la kihistoria la kuhamasisha wananchi kupinga mauaji ya tembo na faru kupitia ujumbe kwenye mabango. Nawapongeza sana kwa ubunifu huu wa aina yake.
Dunia hivi sasa inakabiliwa na wimbi kubwa la ujangili wa wanyama pori hususan ndovu na faru. Nchi nyingi zenye wanyama hao zimekuwa zinakabiliwa na tatizo hilo. Nchi yetu ni moja ya nchi zinazokabiliwa na tatizo hili.
Ndugu wananchi;
Takwimu za hivi karibuni zilizotokana na Sensa iliyofanywa na serikali kwa msaada wa Shirika linalojishughulisha na Uhifadhi la Ujerumani (Frankfurt Zoological Society) katika mfumo wa ikolojia wa Selous-Mikumi pekee zimeonesha kuwa mwaka 2009, katika mfumo wa ikolojia hiyo kulikuwa na tembo wapatao 38,975 na kwa sasa idadi hiyo imeporomoka na kubaki tembo wapatao 13,084.
Takwimu hizi zinamaanisha kuwa idadi ya tembo katika mfumo huo imepungua kwa asilimia 66, hali inayoashiria kuwa kuna kila dalili za mnyama huyu kutoweka katika kipindi kifupi kijacho kama jitihada za makusudi za kuwalinda hazitafanyika.
Katika jitihada za kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutunga sheria kali za uhifadhi wa wanyama pori; kuimarisha doria katika hifadhi za wanyama pori na kuendesha opersheni maalum kutokomeza ujangili. Tuliwahi kufanya Operesheni Uhai mwaka 1987 baada ya hali ya ujangili kuwa mbaya sana. Operesheni hiyo ilihusisha jeshi na ilifanikiwa sana kumaliza tatizo la ujangili. Na kwa kweli na idadi ya tembo ikaongezeka kutoka 55,000 mwaka 1989 mpaka 110,000 mwaka 2009.
Mabibi na Mabwana;
Mwaka jana Serikali iliamua kuendesha Operesheni maalum iliyojulikana kama Operesheni Tokomeza baada ya kuona hali ya ujangili inazidi kuwa mbaya. Hata hivyo, kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake, Serikali iliamua kuisitisha kwa muda operesheni hiyo ili kufanya marekebisho. Sasa tunajipanga kuanza awamu ya pili ya operesheni hiyo. Hatuwezi kuacha, ama sivyo tembo na faru wataisha wote.
Pamoja na kwamba Serikali ina nia thabiti na inafanya kila linalowezekana kutokomeza ujangili, bado tunakabiliwa na changamoto kubwa na ndogo zinazofanya tusifikie hapo tunapopataka. Kwanza ni ule ukweli kwamba eneo linalotakiwa kufanyiwa doria ni kubwa mno. Lina ukubwa wa kilometa za mraba 232,535 pungufu kidogo ya eneo lote la Uingereza. Kwa bahati mbaya hatuna askari wa wanyamapori wa kutosha na vitendea kazi kama vile magari ya doria, vifaa vya kuonea usiku au teknolojia ya kisasa ya kusaidia kufanya doria. Tutafanya kila tuwezalo kupunguza uhaba huo.
Changamoto kubwa kuliko zote ni kuwepo kwa soko kubwa la pembe za ndovu na faru duniani. Ni makusudio yetu kuomba dunia kupiga marufuku biashara ya pembe hizo. Biashara hiyo ikikomeshwa hakuna tembo atakayeuawa. Kichocheo cha ujangili hakitakuwepo.
Ufumbuzi wake unahitaji nguvu ya Jumuiya ya Kimataifa. Hatuwezi peke yetu. Wapo marafiki zetu wanaosaidia jitihada zetu, lakini bado tunahitaji zaidi. Tunahitaji msaada wa kiufundi, fedha na teknolojia ili watu wetu wapate mafunzo bora, ili tuajiri askari wa wanyama pori wengi zaidi na tuwe na teknolojia ya kisasa kukabiliana na ujangili.
Suala la soko pia linahitaji msukumo mpya kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa. Inatakiwa tukubaliane wote kupiga marufuku biashara ya ndovu na pembe za faru au bidhaa zinazotokana nazo. Bahati nzuri usiku huu naenda Uingereza kushiriki kwenye mkutano utaozungumzia masuala ya ujangili na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori. Kwa kutambua jitihada zetu na changamoto zinazotukabili, nimepewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo.
Itakuwa nafasi nzuri kuwaeleza washirika wetu namna tunavyoweza kushirikiana. Nadhani na wao watakuwa tayari kufanya hivyo kwa sababu magenge yanayofanya biashara hii ni hatari kwa usalama wa dunia. Imethibitika baadhi yao wanasaidia vikundi vya kigaidi.
Navyosema hivyo sina maana kuwa wananchi hususan wanaozunguka maeneo ya hifadhi hawana nafasi. Wanayo nafasi na naomba nikiri kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori kwa wakati huu ni wa muhimu sana. Wao ndiyo wanafahamu majangili na wasafirishaji wa ndovu na pembe za faru. Hivyo wananchi wakielimishwa vizuri na kushirikishwa kwenye vita hii naamini tutashinda. Hivyo, naomba wananchi wote tukubaliane kwa kauli moja kuwa tukishirikiana tunaweza kushinda. Tunakubaliana na kauli mbiu yetu ya “ACHA KUUA TEMBO NA FARU – BUNDUKI NA ASKARI PEKEYAO HAWAWEZI KUOKOA MAISHA YA TEMBO NA FARU. TUUNGANE NA SERIKALI KATIKA MAPAMBANO YA KUOKOA WANYAMA HAWA”
Mabadiliko ni mimi na wewe. Naomba tushirikiane kifichua majangili na kulinda wanyamapori kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo. Tanzania bila ujangili inawezekana
Ahsanteni sana na nawashukuru sana kwa kunisikiliza.