Hotuba ya Rais Kikwete Akizungumza na Wazee Mkoa wa Dodoma

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, WAKATI WA MAJUMUISHO YA MKOA WA DODOMA, DODOMA TAREHE 04 SEPTEMBA, 2014

Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji;
Waheshimwa Madiwani;
Wazee Wangu;
Ndugu wananchi;

Kuna methali ya Kiswahili isemayo hakuna refu lisilokuwa na ncha. Hatimaye ziara yangu ya Mkoa wa Dodoma imefikia mwisho. Ziara hii niliyoianza tarehe 28 Agosti, 2014 imenifikisha kwenye wilaya zote za Mkoa wa Dodoma. Madhumuni ya ziara yangu yalikuwa kuona shughuli za maendeleo. Kuona tulipofanikiwa na pale ambapo pana matatizo tupatafutie ufumbuzi. Nimefarijika sana na hatua kubwa za maendeleo ambazo kila wilaya imezifikia. Nimejionea maendeleo makubwa katika sekta na nyanja mbalimbali za maisha ya wananchi wa mkoa huu. Hongereni sana. Aidha, nimeona au kusimuliwa kuhusu changamoto kubwa na ndogo zinazowakabili, ambazo zikiweza kupatiwa ufumbuzi ufanisi utaongezeka na kasi ya kujiletea maendeleo itakuwa kubwa zaidi.
Elimu
Natoa pongezi nyingi kwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa juhudi kubwa mnazofanya na mafanikio mliyopata au mnayoendelea kupata katika kuendeleza elimu Mkoani kwenu. Kwa ajili hiyo basi idadi ya wanafunzi katika ngazi za awali, msingi na sekondari imekuwa kubwa kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa Mkoani Dodoma kuna wanafunzi wa Awali 47,427, wa Shule za Msingi 391,475 na wa Sekondari 59,035 ukilinganisha na wanafunzi wa Awali 55,524, wa Shule za Msingi 152,366 na wa Sekondari 24,288 mwaka 2007. Jukumu lililoko mbele yenu na mbele yetu pia ni kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu mkoani. Pamoja na kupanda kuliko ilivyokuwa mwaka 2012, kiwango cha ufaulu cha asilimia 38.2 kwa shule za msingi na asilimia 55.4 kwa shule za sekondari kwa mwaka 2013 ni chini ya wastani wa taifa wa asilimia 50.61 kwa shule za msingi na asilimia 58.25 kwa shule za sekondari. Hivyo mnayo kazi kubwa ya kufanya ili kufikia kiwango cha ufaulu cha asilimia 60 mwaka huu na asilimia 80 mwakani. Ongezeni bidii.
Napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali kuu tutaendelea kutimiza wajibu wetu kuhusu elimu. Tutaendelea kuleta walimu, vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Hali kadhalika tutaendelea kutoa pesa zitakazoboresha miundombinu ya shule na nyumba za walimu. Kwa upande wa walimu tumefanikiwa kutosheleza mahitaji ya walimu wa masomo ya sanaa kwa shule zote za sekondari. Kwa baadhi ya Wilaya kuna ziada ya walimu hao. Hii ndiyo hali ilivyo kote nchini. Hata hivyo, kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi jambo ambalo ni tatizo la kitaifa.
Mkoa wa Dodoma una mahitaji ya walimu 4,076. Waliopo ni walimu 3,250, kati yao walimu 2,482 wa sanaa na 645 wa sayansi. Kuna jumla ya upungufu wa walimu 949 wa sayansi na ziada ya walimu 123 wa sanaa. Walimu wa ziada kwa masomo ya sanaa wapo Wilaya za Mpwapwa (34), Bahi (55), Dodoma Mjini (86) na Kongwa (92). Upungufu wa walimu wa sanaa upo Wilaya za Chamwino (103), Chemba (9), na Kondoa (32). Upungufu wa walimu wa sayansi upo wilaya zote. Hivi sasa kitaifa tuna pengo la walimu 23,500 na uwezo wa vyuo vyetu ni kuzalisha wanafunzi 2,500 kwa mwaka. Tumedhamiria kulikabili tatizo hili kwa nguvu zote na maarifa yetu yote. Sina wasiwasi kwamba tutafanikwia kama ilivyokuwa kwa changamoto nyingine nyinig.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za Sekondari za Kata, narudia kuwakumbusha viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Dodoma kwamba muda wa miaka miwili tuliopeana mwaka 2012 unaisha mwezi Novemba, 2014. Na, kupitia kwenu nawakumbusha viongozi wa Mikoa yote na Wilaya zote nchini ifikapo Novemba mwaka huu tutaulizana. Hatutaacha kubanana na kama hapana budi kuwajibishana.
Tunaendelea kuboresha upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Mpaka sasa uwiano wa kitabu kwa wanafunzi umefikia 1:3. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili kila mwanafunzi awe na kitabu chake. Suala la nyumba za walimu nalo ni jambo ambalo tunalipa umuhimu. Tunaendelea kuanzia mwaka wa jana kutekeleza mpango wa kuzipatia shilingi milioni 500 kila Halmashauri kwa ajili ya ujenzi huo. Halmashauri za Wilaya ya Mkoa wa Dodoma zitaingizwa kwenye awamu zinazofuata na fedha pia zitaongezwa.
Nimefurahishwa na utekelezaji wa mpango wa utoaji chakula cha mchana kwa wanafunzi mashuleni katika Wilaya za Chamwino, Bahi, Kondoa, Mpwapwa na Chemba. Huu ni mpango unaofadhiliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP). Hapa nchini Mpango wa Chakula wa WFP za Mikoa 4 ya Dodoma, Singida, Arusha na Manyara. Jumla ya shule 640 za mikoa hiyo zinafaidika na mpango huu upo katika Wilaya 16. Ni mpango mzuri ambao manufaa yake ni kuwaongezea watoto mazingira mazuri ya kufuatilia na kuelewa masomo. Hivyo, tuusimamie vizuri ufanikiwe. Ni vizuri viongozi wa Mkoa na kila Halmashauri mkajipanga vizuri ili mpango huu mzuri uweze kuwepo kila Wilaya na uweze kuendelea punde WFP watakapoacha kugharamia mpango huo. Maana jukumu la kuhakikisha lishe ya watoto wetu ni letu wenyewe.
Mkoa wenu unakabiliwa na tatizo kubwa sana la watoto wanaoanza darasa la kwanza kutomaliza darasa la saba na wanaoanza kidato cha kwanza kutomaliza kidato cha nne. Tatizo hili lipo katika kila Wilaya. Takwimu za Mkoa zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 54,301 waliosajiliwa darasa la kwanza mwaka 2007, ni wanafunzi 39,387 tu ndiyo walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2013. Hii ina maana kuwa wanafunzi 14,914 hawakufanya mtihani ambao ni sawa na asilimia 27.5. Na kwa upande wa sekondari, kati ya wanafunzi 16,023 walioandikishwa kidato cha kwanza mwaka 2010, ni wanafunzi 12,693 ndiyo waliofanya mtihani mwaka 2013. Wanafunzi 3,330 hawakufanya mtihani huo, sawa na asilimia 21. Idadi hii ni kubwa mno, haikubaliki. Haiwezi kuachwa kuendelea lazima ikomeshwe.
Narudia kusisitiza agizo langu nililotoa mwezi uliopita kwamba, kuanzia sasa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni lazima watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu. Maafisa Elimu wa Wilaya nao watalazimika kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ambae nae atawasilisha kwenye vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo. Halmashauri hazina budi kuchukua hatua stahiki, kijamii na kisheria, kuhakikisha kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa watoto hao au mtu ye yote atakayebainika kuhusika na utoro huo abanwe ipasavyo.
Maji
Kama mjuavyo, kuwapatia wananchi wa Tanzania maji safi na salama karibu na wanapoishi ni moja ya malengo ya msingi ya Sera na shughuli za serikali na Chama tawala. Katika ziara yangu nimeshuhudia utekelezaji wake. Nimeweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi ya maji na nimezindua miradi ya maji iliyokamilika. Jitihada zetu hizo zimetuwezesha kuwapatia maji asilimia 75.4 ya wakazi wa Mijini na asilimia 50.6 ya wakazi wa vijijini mkoani Dodoma. Lengo la kitaifa ni kuwapatia maji asilimia 90 ya wakazi wa mijini na asilimia 65 ya wakazi wa vijijini ifikapo 2015.
Kwa hapa Dodoma kiwango hicho cha upatikanaji maji kina maana ya kufanya kazi ya ziada ili kuweza kufikia lengo. Miradi inayoendelea kutekelezwa sasa mijini na vijijini hapa Mkoani itakapokamilika itawezesha kufikia lengo. Rai yangu kwa viongozi ni kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate maji safi na salama mapema.
Vile vile, nawaomba kusimamia na kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla wake. Viongozi, waache kulalamika juu ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Sheria zipo, mamlaka mnayo chukueni hatua ili kulinusuru taifa letu dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Umeme
Tumeongeza, maradufu, juhudi za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme nchini. Shabaha yetu ni kuwawezesha asilimia 30 ya Watanznaia waweze kupata umeme ifikapo mwaka 2015. Tayari tumeshavuka lengo hilo kwa kufikia asilimia 36. Kwa Mkoa wa Dodoma katika mwaka huu wa fedha shilingi bilioni 43.8 zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini. Fedha hizi zitawezesha zaidi ya vijiji 193 kupatiwa umeme katika Mkoa huu. Kila Wilaya niliyoitembelea kuna miradi kadhaa ya umeme inayoendelea kutekelezwa. Ndugu zetu Wilaya ya Bahi walinilalamikia kuwa wao wamepewa vijiji vinne tu. Nikawasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambae ameahidi kuwa watafanya masahihisho stahiki. Maombi yangu kwa viongozi wenzangu wahimizeni wananchi waunganishe umeme majumbani na kwenye shughuli zao za kiuchumi na kibiashara.
Barabara
Ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, umeme na simu ni mambo tuliyoyapa kipaumbele cha juu. Nilisema hivyo katika hotuba yangu ya kwanza tarehe 30 Desemba, 2005 na kurudia katika kupindi chote cha uongozi wangu mpaka sasa. Kwa upande wa barabara lengo letu ni kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami na kuimarisha baraba za mikoa, wilaya na Vijiji ziweze kupitika wakati wote. Katika ziara yangu ya Mkoa wa Dodoma nimeshuhudia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa lengo hilo. Nimeweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mayamaya hadi Bonga. Hali kadhalika, nilizindua kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Dodoma hadi Fufu. Nimeambiwa kuwa zimebaki kilometa 25 kwa upande wa Fufu hadi Iringa ili kukamilisha ujenzi wa barabara yote ya Iringa hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 260 kwa kiwango cha lami. Bila ya shaka mtakubaliana name kuwa ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati unatoa fursa ya iana yake kwa maendeleo ya mji wa Dodoma na Mkoa huu kwa jumla. Jipangeni kuitumia fursa hiyo.
Kule Kongwa niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbande, Kongwa hadi Mpwapwa na Kibakwe. Napenda kurudia kuwatoa hofu ndugu zangu wa Mpwapwa na Kibakwe kuwa ujenzi wa barabara ile unaendelea na ndiyo maana pale njia panda ya Kongwa tulifanya shughuli za kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbande, Kongwa, Mpwapwa na siyo uzinduzi wa barabara ya lami kutoka pale hadi Kongwa.
Nimefarijika sana kuona jinsi barabara za mkoa na Wilaya zikiendelea kuimarishwa. Kwa kweli ilikuwa jambo la faraja kubwa kwangu kusikia kuwa vijiji vyote vya mkoani vinafikika kwa barabara. Ni ushindi mkubwa. Napenda kuwaahidi kuwa tutaendelea kuwapatia fedha kutoka Mfuko wa Barabara ili mzidi kuziimarisha barabara zenu. Bahati nzuri Mfuko huo tumeuongezea sana uwezo wake kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 751.7 hivi sasa.
Tulipokuwa wilayani Mpwapwa niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja jipya la Gulwe linalounganisha majimbo ya mpwapwa na Gulwe. Tulipokuwepo pale palijitokeza mawazo mazuri kuhusu namna ya kuikinga reli ya kati ambayo imekuwa inaharibiwa mara kwa mara wakati wa mvua katika maeneo ya Godegode, Gulwe, Msagali na Kilosa. Ulitolewa ushauri kwamba kama yakijengwa mabwawa katika mito inayovuka reli hiyo katika maeneo hayo. Mabwawa hayo yatapunguza wingi na kasi ya maji hivyo kuinusuru reli. Nilivutiwa na mawazo hayo na kuufikisha ujumbe kwa Waziri wa Uchukuzu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe ambaye aliniambia kuwa ni jambo linalofanyiwa kazi. Nilizungumza pia na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda asimamie kuhakikisha kuwa jambo hili muhimu linafanyika. Tulikubaliana kuwa Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika nao washiriki katika mpango huu kwani ni wadau muhimu wa mabwawa hayo. Hali kadhalika viongozi wa Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Manyara wahusike.
Natambua kuwepo maombi ya kutaka barabara kadhaa za Wilaya ziwe za mkoa ili zisimamiwe na TANROADS. Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Magufuli amesikia na zipo baadhi ambazo amezitolea majibu ya kukubali na nyingine anaendelea kutafakari nini afanye. Bila ya kuingilia atakachoamua napenda kusisitiza kuwa msingi mkuu unaoifanya barabara kuwa ya mkoa na hivyo kushughulikiwa na TANROADS ni kuunganisha Wilaya moja na nyingine. Barabara inayoanzia na kuishia ndani ya Wilaya haina sifa hiyo hata kama ni ndefu kiasi gani. Nalisema hili kwa sababu umeanza kuzuka mtindo wa Halmashauri kutaka kukwepa wajibu wao. Pale ambapo wamezidiwa ujuzi na uwezo waseme TANROADS itawasaidia lakini wasikwepe majukumu yao.
Kilimo na Mifugo
Masoko ya Mazao ya Kilimo
Viongozi, Wazee wangu na Ndugu Wananchi;
Hongereni kwa mafanikio mliyopata mwaka huu katika kilimo. Mkoa umezalisha tani 687,122 za mazao ya chakula wakati mahitaji yenu ni tani 494,331. Hivyo kuna ziada ya tani 192,791. Hiki ni kielelezo tosha kwamba juhudi zenu za kuleta mageuzi ya kilimo zinafanikiwa. Mkoa wenu una zaidi ya matrekta makubwa na madogo 1,756. Kati ya matrekta hayo Wilaya ya Kongwa ina matrekta 728. Hongereni sana na endeleeni kuongeza matumizi ya zana bora na pembejeo za kisasa za kilimo mpate mafanikio makubwa zaidi.
Nilipoingia mkoa huu kutokea mkoa wa Morogoro kilio kikubwa cha wakulima kilikuwa soko la mahindi kwa maana ya kukosekana mnunuzi anayetoa bei nzuri kwa wakulima. Wapo watu binafsi wanaonunua mahindi ya wakulima kwa bei ndogo sana. Kilio hicho nilikikuta Mkoa wa Morogoro na Tanga kabla ya hapo. Nilizungumza na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mheshimiwa Mhandisi Chiza kuhusu jambo hilo. Akamtuma Katibu Mkuu Mama Sofia Kaduma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula Ndugu Walwa waje kujiunga na msafara. Ndugu Walwa alieleza kuwa walichelewa kuanza ununuzi katika ukanda wa kati lakini sasa wako tayari kufanya hivyo. Ni matumaini yangu kuwa hatua hiyo italeta nafuu kwa wakulima. Naomba tufanye kazi kwa karibu na NFRA tuwasaidie panapobidi ili wafanikishe jukumu lao. Ni jambo lenye maslahi kwa wakulima, kwa Wakala na Taifa kwa jumla.
Migogoro ya Wakulima na Wafugaji
Wazee wangu;
Nilipokuwa Kibaigwa, Kongwa nilipokea malalamiko yenye mvumo mkubwa kutoka kwa ndugu zetu wanaofanya shughuli za kilimo katika Wilaya ya Kiteto. Wanalalamikia kufukuzwa, kupigwa, kuuawa, kuchomewa moto nyumba, matreka na kuporwa na kunyang’anywa mali zao na ndugu wa jamii ya wafugaji. Wapo waliokuwa wanadai kuwa walikuwa wanaishi huko kwa zaidi ya miaka thelathini hivyo kujikuta wanaambiwa ondoka, nyumba zinachomwa moto, mali zinaharibiwa ni mambo magumu sana kuelewa. Nilipokuwa Mkoa wa Morogoro nilipokea malalamiko kutoka kwa wakulima dhidi ya wafugaji kwamba mifugo imekuwa mingi mno kupita kiasi na kwamba wanaharibu mazao ya wakulima.
Nilipokuwa Morogoro nilisema mambo ambayo ningependa kuyarudia tena leo. Kwanza, kwamba, ardhi hainongezeki lakini watu wanaongezeka na shughuli zinazohitaji kutumia ardhi zinaongezeka. Kwa sababu hiyo wanadamu hawataweza kufanya kila kitu anachotaka katika ardhi hiyo hiyo aliyonayo. Hivyo analazimika kupanga matumizi bora ya ardhi. Yaani anatakiwa kupanga atafanya nini, wapi katika ardhi yake. Kwa ajili hiyo nimewataka viongozi wa vijiji, Wilaya na Mkoa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya uongozi. Kwa upande wa ardhi inayotengwa kwa ufugaji hawana budi kujua ina uwezo wa kubeba mifugo mingapi na ya aina gani. Mgao huo ukishafanywa lazima usimamiwe kwa dhati. Ikifanyika hivyo mtakuwa na hakika na kila hatua ya maendeleo inayochukuliwa na kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Hapatakuwa na migogoro kwa sababu kila mmoja atakuwa na eneo lake la kutosha kufanyia shughuli zake. Pia hapatakuwa na migogoro kwa vile baada ya ukomo wa uwezo wa mifugo inayoweza kubebwa na ardhi iliyotengwa kujulikana na kuzuia mifugo zaidi isiruhusiwe kuingia.
Najua wakati mwingine wenye mifugo wakiambiwa hivyo wanaona wanabaguliwa na kunyimwa haki yao kama raia. Si hivyo, hawajanyimwa haki ya uraia ya kuishi po pote upendapo. Kilichofanyika ni kuweka utaratibu mzuri wa raia kutumia haki yake hiyo kwa manufaa yake na jamii yote. Inampa fursa za uhakika kustawisha mifugo yake na kumuepusha na ugomvi na wengine.
Jambo la pili, nililolisisitiza kule Morogoro ambalo napenda kulirudia tena hapa leo ni kuwa ndugu zetu wanaofuga wahakikishe kuwa mifugo yao haili mazao ya wakulima. Kwa kweli jambo kubwa linalozua chuki, uadui na ugomvi baina ya wakulima na wafugaji ni mifugo kula mazao ya wakulima shambani. Kama hili halitokei sioni mazingira ya kuwepo mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Kila mmoja ataendelea na shughuli zake na kuwa rafiki wa mwenzake. Nilipokuwa Morogoro niliwaomba wafugaji wapitishe azimio kuwa mwaka huu hakuna hata robo eka ya shamba itakayoliwa na kuteketezwa. Ikiwa hivyo, sidhani kama kutakuwa na mgogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Kuhusu yaliyotokea Kiteto kati ya wakulima na wafugaji nalo ni suala la uhusiano na uongozi. Kama watu wameishi huko na kufanya shughuli zao kwa zaidi ya miaka 30 kuna namna bora zaidi za wao kuondoka au kuwaondoa. Viongozi wanayodhamana kubwa ya kuona kuwa watu wa nchi hii hawafanyiwi vile. Nimezungumza na Waziri Mkuu ili tuangalie uwezekano wa mkutano kati ya viongozi wa Mikoa ya Manyara, Morogoro na Dodoma inayojumuisha Wilaya za Mpakani wakutane na kuzungumza namna ya kuondoa uadui na kuwafanya watu waishi pamoja na kushirikiana.
Afya
Nawapongeza kwa hatua kubwa mliyopiga katika kuboresha sekta ya afya kwa kupeleka huduma karibu zaidi na wananchi. Mkoa wa Dodoma una mtandao wa hospitali 8, vituo vya afya 41 na zahanati 316. Nafurahishwa pia na jitihada za kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vipya ili kutimiza azma yetu ya kusogeza huduma za afya ndani ya eneo la mzingo wa kilometa 5 wanapoishi wananchi.
Huko nyuma niliagiza kwamba kila Halmashauri ya Manispaa, Mji na Jiji ambayo iko Makao Makuu ya Mkoa, ijenge hospitali yake ili kuiwezesha hospitali ya Mkoa kufanya shughuli za rufaa za Mkoa. Manispaa ya Dodoma mko nyuma katika kutekeleza agizo langu hili. Tengeni eneo la ujenzi wa hospitali ya Manispaa na wekeni kwenye bajeti yenu ili tuijenge.
Pia upo wajibu wa kisera kuhakikisha kuwa kila Wilaya ina hospitali ya Wilaya. Katika Mkoa wa Dodoma Wilaya za Kongwa, Bahi, Chamwino, Chemba na Dodoma Mjini hazina hospitali za Wilaya. Nimewataka waanze ujenzi wa hospitali hizo. Waweke mahitaji yao kwenye mipango ya maendeleo ili itafutiwe fedha.
Nawapongeza kwa jitihada mnazofanya za kuhamasisha akina mama kujifungua katika zahanati, vituo vya afya na hospitali. Taarifa yenu inaonesha kwamba asilimia 79 ya akina mama wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kisasa vya kutoa huduma ya afya na chanjo ya watoto mmefikisha asilimia 96. Msibweteke ongezeni uhamasishaji ili akina mama wote wajifungulie kwenye vituo vya afya na watoto wote wapate chanjo. Kwa ajili hiyo, napenda kushauri kuwa ujenzi wa sehemu ya akina mama wajawazito kusubiria kabla ya kujifungua (maternity waiting homes) ufikirieni kwa uzito unaostahili. Wenzenu wa Morogoro wamelifanya kuwa sehemu ya mipango yao ya kuendeleza afya ya akina mama wajawazito. Inasaidia kuokoa maisha ya mama wajawazito kunaweza kusaidia Mkoa huu pia na kwingineko nchini.
Aidha, tuendelee kuhimiza mapambano dhidi ya ugonjwa ya UKIMWI katika maeneo yetu. Japo takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya UKIMWI kimkoa yanapungua toka asilimia 3.4 mwaka 2008 hadi asilimia 2.9 mwaka 2012, lengo letu ni kutokuwa na maambukizi mapya kabisa. Ongezeni juhudi ili lengo letu hilo tulifikie.
Nawapongeza pia kwa kuvuka lengo letu la kuhakikisha kwamba asilimia 30 ya Watanzania wanajiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ifikapo 2015. Ninyi mmekwishafikisha asilimia 47.9. Hata hivyo, ziko Wilaya kama za Kondoa, Chemba na Manispaa ya Dodoma ambazo ziko chini sana. Ongezeni jitihada ili wananchi wengi zaidi wapate huduma ya mfuko huo.

Ugonjwa wa Ebola
Ndugu wananchi;
Tangu mwezi Aprili, 2014 nchi za Afrika Magharibi hususan nchi ya Guinea, Siera Leone, Liberia na Nigeria zimekumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa hatari wa Ebola. Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa tayari watu 3,500 wameambukizwa na tayari zaidi ya vifo 1,900 vimetokea. Asilimia 40 ya vifo hivi vimetokea ndani ya wiki tatu hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2014. Ebola ndiyo virusi hatari zaidi duniani kuliko hata UKIMWI. Ndiyo maana Shirika la Afya Duniani limeutangaza ugonjwa huu kuwa ni janga la dunia, na inatarajiwa athari zake zinaweza kuongezeka. Ugonjwa huu husababishwa na virusi vya Ebola na husababisha wagonjwa wengi kufa kwa vile ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo.
Wataalam wanatuambia kwamba virusi vya Ebola hubebwa na ndege aina ya popo na wanadamu huupata kupitia kwa wanyama walioambukizwa kwa kuwagusa au kuwala. Wanyama hao ni pamoja na sokwe, nyani na swala. Maambukizi kutoka kwa mgonjwa huenda kwa mtu mwingine kwa kugusa damu au majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo au kwa kugusa maiti ya mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa huo. Ugonjwa huu ni hatari sana kiasi kwamba hata watoa huduma za afya kama madaktari na wauguzi kama hawakuchukua tahadhari zinazotakiwa wanaweza kuambukizwa na hata kufa. Mpaka hivi sasa Daktari mmoja aliyekuwa anawahudumia wagonjwa wa Ebola kule Liberia amekufa.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mgonjwa kuwa na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, kuumwa na kichwa, kuumwa na misuli na kutokwa na vidonda kooni. Dalili hizi zinaweza kuambatana na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele, kutokwa na damu ndani na nje ya mwili na kushindwa kufanya kazi kwa figo na ini. Dalili za ugonjwa huu hujitokeza katika siku 2 hadi 21 baada ya kuambukizwa.
Tunamshukuru Mungu kwani mpaka sasa hapa nchini hajapatikana mtu yeyote mwenye ugonjwa huu. Pamekuwepo na wagonjwa wanne waliohisiwa kuwa na Ebola ambao uchunguzi ulionesha hawakuwa na ugonjwa huo. Watatu kati ya wagonwja hao walikuwa ni wagonjwa wa malaria na mmoja uchunguzi wake bado unaendelea. Wagonjwa wawili ni kutoka Dar es Salaam na wawili ni kutoka Geita na Nkasi. Wagonjwa hawa waliohisiwa walihudumiwa na walifanyiwa uchunguzi kwa kufuata tahadhari zote za ugonjwa wa Ebola. Hii imeonesha utayari wetu wa kukabiliana na janga hili. Pamoja na kutokuwepo kwa mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitika kuwa na ugonjwa huu.
Tumejipanga vizuri kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini. Tumechukua tahadhari na kujiandaa vilivyo kukabiliana na janga hili kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(i) Tunacho Kikosi Kazi cha Taifa kinachoongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donald Mbando cha kukabiliana na ugonjwa huu katika ngazi ya taifa hadi Wilaya.
(ii) Tumekamilisha mpango wa kitaifa “Ebola Contingency Plan” na tumetenga Shilingi milioni 500 ikiwa ni fedha za awali za utekelezaji wa mkakati huo.
(iii) Tumeshaagiza Timu za Maafa za mikoa na wilaya kutekeleza mpango huo.
(iv) Tumesambaza vifaa “personal protective equipment” kwa watumishi wa afya katika mikoa yote, wilaya zote, hospitali zote za Rufaa na kanda 37, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar. Tumesambaza pia dawa.
(v) Tumetenga kituo maalum tengefu (isolation unit) cha Wilaya ya Temeke na vituo vingine tengefu mikoani.
(vi) Tumechukua tahadhari kubwa kwenye viwanja vya ndege. Tumekwishafunga mitambo maalum ya vipima joto na dalili za wagonjwa wa Ebola katika viwanja vya Mwalimju Nyerere (2), Mwanza (1), Zanzibar (1) na kituo cha Namanga (1). Tumeagiza pia scanners 5 ambazo zimekwishawasili na zitafungwa katika viwanja vyetu.
(vii) Tumetoa mafunzo kwa watumishi wa afya wa mipakani na viwanja vya ndege. Tumetoa mafunzo hayo kwa watumishi 100 wa Dar es Salaam na 45 kutoka mikoa ya Arusha, Kagera, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, Kigoma na Zanzibar. Tumepeleka watumishi watatu nchini Jamhuri ya Kongo kupata mafunzo maalum.
(viii) Tumeanza maandalizi ya kuboresha maabara zetu ili tuweze kufanya uchunguzi wa sampuli hapa hapa nchini. Kwa sasa, eneo zima la Afrika Mashariki tunategemea na tunatumia maabara ya Nairobi.
Viongozi wa ngazi zote hizi wamepatiwa mwongozo wa utekelezaji. Tunachoomba ni ushirikiano wa wananchi wote katika kuchukua tahadhari na kutoa taarifa mapema iwezekanavyo mara tu mnapogundua dalili za ugonjwa huu kwa mtu ye yote.
Mchakato wa Katiba
Nilipozungumza na Taifa mwishoni mwa mwezi Julai, nilizungumzia mchakato wa Katiba. Nilielezea utayari wangu wa kufanya kila liwezekanalo kusaidia kufanikisha mchakato wa Katiba unaonndelea sasa. Kwa moyo huo, sikusita, nilipoombwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (Umoja wa Vyama vyenye Uwakilishi Bungeni) Mhe. John Momose Cheyo kukutana nao na kufanya mazungumzo ya mashauriano. Kama mnavyojua tulikutana tarehe 31 Agosti, 2014 Mjini Dodoma. Tumekuwa na mazungumzo mazuri. Tumepeana kazi ya kufanya na tumekubaliana kukutana tena tarehe 08 Septemba, 2014 kuendelea na mazungumzo yetu. Kinachotia moyo ni ule ukweli kwamba kila upande umeonesha kiu na utayari wa kuzungumza. Tuyape nafasi mazungumzo haya yatutoe hapa tulipo na kutusogeza mbele kwa umoja na mshikamano.
CDA
Mwisho, suala la CDA: Wakati wa kuzundia barabara ya Dodoma – Fufu Mbunge wa Dodoma Mheshimiwa Malole alielezea kwa uchungu matatizo ya CDA. Nimewaagiza Wadau wakae tutakutana tarehe 07 Septemba, 2014 tupokee ushauri. Naomba muwe na subira.
Hitimisho
Wazee wangu;
Narudia tena kuwashukuru ndugu zangu wa Dodoma kwa mapokezi mazuri na ratiba nzuri iliyonipa nafasi ya kujifunza mengi kuhusu mkoa wenu. Naondoka nikiwa na kumbukumbu ya mambo mazuri yanayoendelea kufanyika hapa mkoani kuinua hali za maisha ya wananchi. Tafadhali ongezeni bidii. Mimi na wenzangu Serikalini tutaendelea kuwaunga mkono.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.