Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kuja
kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kuadhimisha Siku ya Sheria
kwa mwaka 2012. Nakushuru pia kwa kunipa nafasi ya kutoa salamu
kwa hadhara hii ya mabingwa wa sheria na watoaji haki.
Lazima nikiri kuwa baada ya kusikiliza nasaha maridhawa zilizotolewa katika hotuba yako nzuri na nyinginezo za walionitangulia mimi sintokuwa na mengi ya kusema. Hakika tumepata darasa la kutosha. Hivyo, nitasema machache. Niruhusuni nianze kwa kutakiana heri ya Mwaka Mpya. Naungana na viongozi wa dini waliotuombea dua hapa leo hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuumaliza mwaka uliopita salama na tunamuomba atujaalie neema na baraka tele mwaka huu wa 2012.
Tumuombe atujaalie ndoto zetu zitimie na tunayopanga yafanikiwe.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nakupongeza sana wewe binafsi kwa kazi yako nzuri uifanyayo ya
kusimamia na kuuongoza mhimili wa Mahakama. Wahenga walisema
‘nyota njema huonekana asubuhi’. Katika kipindi kifupi ulichokuwa
Jaji Mkuu umeonyesha kuwa wewe ni kiongozi mahiri na mtetezi shupavu wa maslahi ya mhimili wa Mahakama na haki za raia.
Aidha, umekuwa daraja imara kati ya mihimili yetu mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Kupitia kwako, mafanikio mengi
yamepatikana na heshima na taswira ya Mahakama katika jamii inazidi
kuboreka. Nakushukuru sana.
Nawapongeza, pia, Majaji wa Rufaa, Majaji wa Mahakama Kuu,
Mahakimu pamoja na watumishi wengine wote wa Mahakama. Kwa
kweli wamefanya kazi kubwa na nzuri pamoja na kuwepo changamoto
mbalimbali. Mimi na wenzangu Serikalini pamoja na wananchi walio
wengi tunatambua na kuthamini mchango wenu muhimu katika utoaji
wa haki. Jitihada zenu ndizo zimewezesha Mahakama kupata
mafanikio ambayo tunayazungumzia leo. Mimi naamini kuwa
mwelekeo wetu wa siku za usoni unaleta matumaini makubwa.
Ujumbe wa Mwaka
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nawapongeza sana kwa mada nzuri ya maadhimisho ya Siku
ya Sheria mwaka huu inayosema “Adhabu Mbadala Katika Kesi
za Jinai na Faida zake katika jamii”. Kwa hakika huu ni ujumbe
ambao umekuja wakati muafaka kabisa.
Jambo hili ni muhimu sana. Ni ukweli ulio wazi kwamba
mfumo wetu wa sasa wa adhabu unasisitiza adhabu ya kifungo jela
badala ya adhabu mbadala ambazo zipo katika sheria. Kama adhabu
mbadala zingekuwa zinatolewa, idadi ya wafungwa gerezani
ingepungua na hata tatizo la msongamano katika magereza
lisingekuwepo au lingepungua sana.
Hatuna budi kutumia adhabu mbadala kama sheria ya The
Community Act inavyoruhusu kwa makosa yanayostahili. Sheria hiyo
inajenga dhana kwamba jukumu la kuwarekebisha wahalifu haliko
mikononi mwa Serikali pekee na kwamba jamii wanakotoka wahalifu
nayo ina wajibu wa kushiriki katika kuwarekebisha wahalifu.
Sheria ya kufanya kazi ya kijamii ililenga kuwaepusha na adhabu ya kifungo wale wafungwa ambao wameonyesha tangu awali kwamba waliteleza, wametubu na kuomba msamaha.
Utekelezaji wa sheria hizi una changamoto zake ambazo
Mheshimiwa Jaji Mkuu umezieleza kwa ufasaha. Moja ya changamoto
hizo ni ile ya jamii kukubali ukweli kwamba wahalifu wanarekebishika.
Adhabu zinazotolewa zina lengo la kumrudi na kumrekebisha mhalifu.
Inapodhihirika kuwa mwenendo wa mhalifu una muelekeo mzuri na
hasa unapopima uzito wa kosa alilofanya ni dhahiri kwamba ni kwa
manufaa ya mfungwa kurekebishwa na jamii badala ya kumtenga kwa
kumfunga gerezani. Hii ni namna nyingine ya kumpa mhalifu fursa ya
kujirekebisha katika jamii yake.
Hata hivyo, kuna changamoto ya jamii kutambua na kukubali
kuwa inao wajibu mkubwa katika kusaidia kuwarekebisha wahalifu.
Naelewa ugumu uliopo kwa jamii kulielewa jambo hili kwani wengi
wanaamini kwamba adhabu pekee ya mhalifu ni kumfunga gerezani.
Hivyo, ipo kazi kubwa ya kutoa elimu ili watu nao waelewe kuwa
wanao wajibu wa kusaidia kuwarekebisha wafungwa wawe na tabia
njema.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Changamoto nyingine ni jinsi jamii itakavyojipanga kufanya kazi
ya kuwarekebisha wahalifu katika jamii zao. Ingefaa wadau muhimu,
kama vijiji, Halmashauri na Mamlaka nyingine wabuni kazi na kutenga
maeneo ya kufanya kazi zenye manufaa kwa umma. Kazi hizo zisiwe
za kukwaza, bali ziwe za kuwarekebisha wahalifu. Ni muhimu kwa ajili
hiyo basi, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wengine wa Serikali za
Mitaa wakahusishwa kwa ukamilifu katika utekelezaji wa adhabu
mbadala. Tukifanya hivyo mpango huu utakuwa umepewa msukumo
wa pekee na kupata mafanikio.
Kuhusu suala la msongamano wa wafungwa, baada ya kutembelea
magereza ya Keko, Ukonga na Segerea na kuyaona niliyoyaona,
nimeshawishika tuchukue hatua. Nimetoa maagizo kwa wahusika
kuandaa maoni yao. Baadhi wamekamilisha na wengine wanamalizia.
Hivi karibuni tutakutana kujadili hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja
kuongeza magereza, kuharakisha kusikiliza na kumaliza kesi, kupata
nakala ya hukumu, kukamilisha upelelezi haraka na kuiwezesha
Mahakama kwa watu na rasilimali.
Mwisho
Mheshimwa Jaji Mkuu,
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuzungumzia baadhi
ya mambo uliyoyataja katika hotuba yako. Kwa upande wa mgao wa
fedha kuwa kati ya asilimia 60 na 70 ya lengo, hilo halikuwa tatizo lenu
pekee. Karibu Serikali nzima ilikuwa hivyo. Sababu kubwa ni jukumu
la kulipa malimbikizo ya madeni ya mwaka wa fedha 2010/2011 ambayo
tulilazimika kuyalipa katika mwaka huu wa fedha. Bahati nzuri mzigo
huo wa madeni umepungua sana hivyo katika nusu hii ya pili ya mwaka
wa fedha 2011/2012 hali itakuwa bora zaidi.
Aidha, napenda kukuarifu kuwa bajeti ya Mahakama, kwa
maagizo yangu, imewekewa wigo wa kutolewa kama ilivyoidhinishwa
na Bunge. Hivyo basi, toeni hofu kwani kile chote kilichopangwa
kitapatikana. Kuhusu baadhi ya stahili za Majaji ambazo hazijalipwa
suala hilo linashughulikiwa na tumefikia mahala pazuri.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Kuhusu ajira ya Majaji wapya, nasikitika kwamba imechukua
muda mrefu. Taratibu za kirasimu karibu zinafikia ukingoni na bila
shaka zoezi litakamilika muda si mrefu. Kwa upande wa upungufu wa
Mahakimu, Serikali inalitambua tatizo hilo na nimekwishamuelekeza
Waziri wa Sheria hatua za kuchukua ili mgawo wa nafasi za ajira za
Mahakimu uongezeke.
Bahati nzuri hivi sasa ipo idadi ya kuridhisha ya Mahakimu
waliohitimu kutoka katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama kule
Lushoto. Mwaka jana nilipohudhuria Mahafali ya 11 ya Chuo na
nilishuhudia jinsi Chuo kinavyofanya kazi kubwa na nzuri ya
kusomesha Mahakimu wengi. Hivyo basi, tatizo la uhaba wa Mahakimu
litamalizika muda si mrefu. Ni matumaini yangu kwamba ongezeko la
Majaji na Mahakimu litasaidia sio tu kusajili kesi nyingi
zinazowasilishwa Makahamani, bali pia litawezesha kesi
zinazopokelewa Mahakamani kusikilizwa na kumalizika kwa wakati.
Baada ya kusema maneno yangu hayo mengi kwa mara nyingine
tena nawatakia kazi njema mwaka huu, nawatakia kila la heri katika
kuboresha mfumo wetu wa adhabu tusiwaache wananchi wetu mbali ili
waukubali mfumo huu na wauunge mkono.
Asanteni kwa kunisikiliza