HOTUBA YA RAIS JAKAYA KIKWETE KWENYE MAADHIMISHO YA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU NA KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS NYERERE OKTOBA 14, 2012
Dk. Fenella Mukangara (Mb) Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu Omari, Waziri wa Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto – Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Mheshimiwa Ali Nassoro Lufunga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga;
Mama yetu mpendwa Mama Maria Nyerere;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Ndugu Wananchi;
Shukrani
Ndugu wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana tena mwaka huu kuadhimisha kilele cha Mbio za Mwenge, kumkumbuka Baba yetu wa Taifa, na Wiki ya Vijana. Naungana na viongozi waliotangulia kuwashukuru viongozi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na wananchi wote wa mkoa huu kwa mambo mawili. Kwanza kwa kukubali kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya. Ni jukumu kubwa na zito, lakini wenzetu mmelipokea kwa mikono miwili na kulitekeleza kwa ufanisi mkubwa. Asanteni sana. Pili, nawashukuru kwa mapokezi mazuri. Naomba radhi kwa kushindwa kufika jana kutokana na matukio yaliyotokea Dar es Salaam.
Namshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mheshimiwa Zainabu Omari, Waziri mwenzake kutoka Zanzibar kwa kunialika kuja kuungana nanyi na Watanzania wengine popote walipo kushiriki kwenye maadhimisho haya adhimu kwa taifa yanayofanyika hapa Shinyanga mwaka huu.
Ndugu Wananchi;
Nawapongeza pia Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na watumishi wote wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, bila kuwasahau wajumbe wote wa kamati mbalimbali, walioshiriki katika kuratibu mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu. Mipango yao mizuri na umakini wao katika utekelezaji ndio imewezesha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu kufanyika nchi nzima kwa mafanikio makubwa. Hongereni sana.
Ndugu Wananchi;
Kwa namna ya pekee nawapongeza kwa dhati vijana wetu waliokabidhiwa jukumu la kukimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu. Wamefanya kazi kubwa na nzuri. Mwenge wameufikisha salama, unang’ara kama walivyokabidhiwa. Pia, wamefikisha ujumbe wa Mwenge kwa ufasaha mkubwa. Nimeambiwa mbio za mwaka huu zimefana sana. Kila mahali Mwenge wa Uhuru ulipokelewa vizuri na wananchi walijitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za Mwenge ikiwa ni pamoja na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapongeza wananchi wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu. Hamasa yenu inatupa nguvu na kutufanya tuongeze bidii zaidi ya kuboresha Mbio za Mwenge miaka ijayo. Navipongeza sana vyombo vya habari nchini kwa kuwa pamoja nasi katika kutangaza msafara wa Mwenge na kuwahimiza wananchi washiriki kwenye za Mbio za Mwenge wa Uhuru. Wenzetu hawa wametusaidia sana kufikia malengo yetu. Asanteni sana.
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Ndugu wananchi;
Kama nilivyosema awali, pamoja na kuwa ni Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, siku ya leo pia tunaadhimisha miaka kumi na tatu tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotangulia mbele ya haki. Miaka hiyo ni mingi kwa mwanadamu kusahaulika baada ya kufariki, lakini siyo hivyo kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hasahauliki na kamwe hatasahaulika kwa sababu ya mema mengi aliyoifanyia nchi yetu na watu wake. Ameongoza harakati za kudai uhuru wa nchi yetu kwa njia ya amani mpaka ukapatikana. Kwa miaka 23 ameongoza juhudi za kujenga taifa jipya la Tanganyika na baadaye la Tanzania. Ametuachia nchi nzuri ya watu wenye umoja, upendo, mshikamano, amani na utulivu licha ya watu wake kuwa na tofauti za rangi, kabila, dini, hali zao za kiuchumi na maeneo watokayo.Na licha ya kuwa nchi yetu imetokana na nchi mbili kuungana.
Ndugu Wananchi;
Tofauti hizo miongoni mwa raia wa nchi hii ni sababu tosha ya watu kuwa na migawanyiko, uhasama baina yao na ukosefu wa amani na utulivu. Bahati nzuri, na kwa mshangano wa wengi, nchi yetu imekuwa kisiwa cha amani na utulivu. Wahenga walisema “usione vinaelea vimeundwa”. Hakuna mtu mwingine wa kushukuriwa na kutambuliwa kwa kuifanya hali hiyo iwe, zaidi ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alibuni na kutekeleza Sera nzuri zilizowajumuisha Watanzania wote katika shughuli muhimu zihusuzo nchi yao bila ya ubaguzi. Sera nzuri zilizohakikisha raia wote wanapata haki zao za msingi kwa usawa bila ya kubaguliwa kwa sababu ya rangi zao, makabila yao, dini zao au maeneo watokayo. Sera nzuri zilizopinga na kuzuia dhuluma, unyanyasaji, ukandamizaji na uonevu dhidi ya raia. Hiyo ndiyo siri ya utulivu na amani ya Tanzania.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hakuna jambo kubwa na la heshima kubwa tunayoweza kumfanyia katika kumkumbuka Baba wa Taifa siku ya leo zaidi ya kuzingatia sera hizo za msingi zilizojenga umoja, amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Barani Afrika ambazo hazizalishi wakimbizi bali tumekuwa tunapokea wakimbizi. Hivyo basi lazima tuzienzi na kuzidumisha sera hizo kama tunataka amani na utulivu vidumu. Tusiwape nafasi watu wanaotaka au kufanya vitendo vya kutuvurugia sera hizo nzuri, wawe ni watu binafsi, kikundi cha watu au vyama vya siasa. Watu hao hawaitakii mema nchi yetu na watu wake. Tukiwapa nafasi na tukawaendekeza tutaingia kwenye maangamizi sisi wenyewe.
Nafarijika sana kuona Watanzania wakiendelea kukataa ushawishi wa kugawanywa kwa rangi, makabila na dini bali wamekuwa wanasisitiza kuwa wamoja na wenye mshikamano licha ya tofauti zao hizo. Na huo ndiyo ujumbe mkuu wa Mwenge tangu kuasisiwa kwa wazo la kuwasha Mwenge kabla ya uhuru na kuwepo kwa Mbio za Mwenge baada ya Uhuru.
Ndugu Wananchi;
Jana kule Dar es Salaam nilitembelea makanisa yaliyovunjwa na wanaharakati wa Kiislamu kufuatia tukio la kusikitisha la kijana mmoja kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu, yaani “Quran Tukufu”. Kijana huyu alifanya kosa kubwa pamoja na mazingira ya utoto wake na mwenzake. Waislamu wanayo haki ya kukasirika. Lakini pamoja na kukasirishwa kwao, na wao kuvamia makanisa matano kuyabomoa, kuharibu vifaa pamoja na magari, haikuwa sahihi hata kidogo. Kijana huyo hakutumwa na Kanisa wala na mtu yeyote. Ni matokeo ya ubishani wake na mtoto mwenzake. Isitoshe tayari alikuwa mikoni mwa Polisi kwa hatua zipasazo za kisheria.
Watu kwenda Kituo cha Polisi kutaka wakabidhiwe mtoto yule wamuadhibu wao haikuwa sawa. Nchi yetu inaongozwa kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, tuache sheria ichukue mkondo wake. Na baada ya hapo watu kuvamia makanisa na kufanya uharibifu niliouona nalo lilikuwa ni kosa la kusikitisha na lisilokuwa na maelezo yanayotosheleza. Nilisema jana, na napenda kurudia tena leo kuwa ndugu zangu tujiepushe na matendo ya namna ile. Hayajengi bali yanabomoa. Hayatoi jawabu kwa matatizo yanayotukabili bali yanakwaza wahusika, waathirika na jamii kwa ujumla. Yanaleta ugumu katika kupata ufumbuzi wa matatizo yenyewe. Isitoshe yanaleta wasiwasi usiostahili kuwepo katika jamii na nchi kwa jumla. Niliwasihi viongozi wa dini wa pande zote mbili kujiepusha na jazba na kulipiza kisasi. Niliwaomba Waache vyombo vya sheria vifanye kazi yake. Yule kijana yuko mikononi mwa Polisi, halikadhalika na wanaharakati 122 wa Kiislamu nao hivyo hivyo.
Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Kama tulivyomsikia Mheshimiwa Waziri akitueleza muda mfupi uliopita, kila mwaka Mbio za Mwenye huwa na ujumbe maalum. Mwaka huu ujumbe ulikuwa “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo Yetu, Shiriki Kuhesabiwa Tarehe 26 Agosti 2012”. Kauli mbiu hii ilikuwa muafaka kabisa kwani kama mtakavyokumbuka kuwa tarehe 26 Agosti hadi 1 Septemba, 2012 katika nchi yetu kulifanyika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Zoezi hilo lilifanyika kwa mafanikio makubwa pamoja na kuwapo kwa changamoto ndogo na kubwa. Bila ya shaka, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu na Kauli mbiu yake hiyo imechangia katika mafanikio haya.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na ujumbe huu wa jumla, Mwenge wa Uhuru uliendelea kuwahimiza wananchi kushiriki katika mambo muhimu kwa mustakabali mwema wa taifa letu na jamii. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na wananchi kushiriki katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba na kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, dawa za kulevya na rushwa. Masuala haya yote yalielezwa vizuri na viongozi wa msafara wa Mbio za Mwenge na ujumbe uliwafikia walengwa.
Mabadiliko ya Katiba
Ndugu wananchi;
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba ametoa taarifa hivi majuzi kuwa zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na makundi mbalimbali linaendelea vizuri. Katika awamu ya kwanza na ya pili, Tume imefanya mikutano 842 katika mikoa 15; miwili ya Zanzibar na 13 ya Tanzania Bara. Katika mikutano hiyo, watu 517,427 walihudhuria na waliotoa maoni yao moja kwa moja ni watu 29,514 na waliotoa kwa njia ya maandishi ni 102,404.
Katika awamu ya tatu inayoendelea sasa, Wajumbe wa Tume wanakusanya maoni katika mikoa tisa yaani miwili ya Visiwani na saba ya Bara. Kama mambo yataenda vizuri kama ilivyo sasa, huenda Tume ikamaliza kazi ya kukusanya maoni mwezi Disemba, 2012. Baada ya hapo itafuata hatua nyingine ya kuandaa rasimu ya Katiba. Dhamira yetu ni kuona kuwa katika uchaguzi ujao nchi yetu itakuwa na Katiba mpya inayokidhi mahitaji ya sasa na miaka mingi ijayo.
Ndugu Wananchi;
Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Makamu Mwenyekiti Jaji Agustino Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu, Wajumbe wote wa Tume pamoja na Maofisa wa Tume kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Nawaomba waendelee na moyo huo wa kuchapa kazi mpaka watakapokamilisha jukumu lao kubwa na la kihistoria kwa nchi yetu.
Nawaomba wananchi wa Mikoa iliyosalia waendelee kujitokeza kwa wingi kama wanavyojitokeza sasa wenzao kutoa maoni yao pindi wajumbe wa Tume watakapotembelea katika maeneo yao. Watoe maoni yao kwa uhuru bila woga wala vitisho. Msikubali kutishwa wala kulishwa maneno ya kusema na mtu yeyote. Msikubali kugeuzwa radio kaseti au santuri ya mtu. Toeni maoni yenu mpendavyo nyie.
Ugonjwa wa UKIMWI
Ndugu wananchi;
Kuhimiza Watanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI umekuwa ni ujumbe wa kudumu kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru tangu mwaka 2007. Tumeamua iwe hivyo kwa sababu ya ukubwa wa tatizo na haja ya kuzidisha mapambano hayo. Huu ni mwaka wa 29 tangu maradhi ya UKIMWI yalipogunduliwa kuwepo nchini kwa mara ya kwanza. Tangu wakati huyo mpaka sasa watu wengi wameambukizwa na wanaendelea kuambukizwa. Watu wengi wamepoteza maisha na wengi wanaugua hivi sasa.
Maradhi haya yamekuwa na gharama kubwa kwa taifa kwa maana ya tiba, kupoteza nguvu kazi na mzigo wa kulea yatima. Jitihada kubwa zimekuwa zinafanywa kupambana na maradhi haya na mafanikio makubwa yamepatikana. Bado jitihada zaidi zinahitajika.
Ndugu Wananchi;
Kuzuia maambukizi mapya ndilo hasa lengo kuu la mkakati wa kupambana na maradhi haya nchini. Tunataka walioambukizwa wabaki hao hao tuwashughulikie lakini wale ambao walio salama wabakie salama. Kwa ajili hiyo, kazi kubwa imekuwa inafanyika kuelimisha umma kuhusu UKIMWI. Hivi sasa, karibu kila Mtanzania anajua kuwepo kwa ugonjwa wa UKIMWI, jinsi unavyoambukiza na namna ya kujikinga. Elimu ya kujikinga na UKIMWI tumeielekeza pia kwa watoto wetu mashuleni ili wapate ufahamu mapema na kujinga. Hivi sasa, inawafikia asilimia 65 ya wanafunzi wa Shule za Msingi na asilimia 80 ya Shule za Sekondari. Elimu kwa vijana wetu ndiyo matumaini makubwa ya kutokomeza janga hili siku za usoni.
Ndugu Wananchi,
Pamoja na hayo, tumeelekeza nguvu zetu katika kuwahamasisha Watanzania kupima afya zao ili kujua kama wako salama au wana maambukizi. Nafurahi kwamba tangu tuzindue kampeni ya kitaifa ya upimaji UKIMWI kwa hiari, Julai 2007 zaidi ya watu milioni 14.2 wamejitokeza kupimwa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa upimaji wa hiari. Kutokana na zoezi hilo, imethibitika kuwa kiwango cha maambukizi nchini kimeshuka kutoka zaidi ya asilimia 15 miaka ya tisini hadi asilimia 5.7 hivi sasa.
Haya ni mafanikio makubwa sana. Hata hivyo bado watu watano katika kila watu 100 kuwa wameambukizwa ni wengi mno. Tunataka tufikie siku ambapo hakuna hata mtu mmoja mwenye maradhi haya. Inaleta faraja kuona kuwa, maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 25.
Ndugu Wananchi;
Katika zoezi la upimaji wa hiari linaloendelea, tumeweza kupata sura ya kuaminika zaidi ya watu wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini. Kati ya hao, asilimia 57 tayari wanapatiwa dawa za kurefusha maisha na asilimia 43 waliosalia watahudumiwa hali zao za ugonjwa itakapofikia hatua ya kuhitaji dawa. Jitihada zinaendelea kufanywa kuhakikisha kuwa mahitaji muhimu yakiwepo ya dawa na fedha yanapatikana.
Napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupima kwa hiari. Inasaidia kujua kama uko salama ili ujihadhari na kama umeambukizwa ujue namna ya kuishi kwa matumaini na kuepuka kuambukiza wenza wao. Aidha, napenda kuwahakikishia kuwa tumejipanga vizuri, wale wote walioathirika watapata dawa.
Ndugu Wananchi;
Narudia kuwakumbusha Watanzania wenzangu kufanya kila wawezalo kujiepusha kupata maambukizi ya UKIMWI. Hili ni jambo linalowezekana iwapo watu watazingatia masharti yake. Wahenga wamesema penye nia pana njia, haya shime tuazimie kwa dhati kukataa kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Ziko njia kadhaa za kuambukizwa lakini kubwa zaidi ni ile tunayoijua sote. Kila moja wetu aamue kushinda udhaifu wa moyo wake, jambo ambalo hatuwezi kusema haliwezekani. Linawezekana. Ndiyo maana bado sina shaka Tanzania bila UKIMWI inawezekana. Sisi serikalini tutaendelea kuimarisha jitihada zetu ili kupunguza maambukizi mapya na kuwahudumia vizuri zaidi walioathirika. Pia naomba tuache tabia ya kuwabagua na kuwanyanyapaa wenzetu walioathirika.
Dawa za Kulevya
Ndugu wananchi;
Taifa letu liko katika mapambano makubwa na magumu dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Biashara imekuwa kubwa na idadi ya watumiaji imeongezeka sana na maeneo yenye tatizo hili hapa nchini nayo yameongezeka. Zaidi ya bangi na mirungi, watu sasa wanatumia dawa za kulevya ngeni kutoka nje kama vile heroin, cocaine, na nyinginezo.
Matumizi ya dawa za kulevya huambatana na athari mbaya za kiafya, kijamii na kiuchumi. Baadhi ya athari hizo ni magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya akili, moyo, figo, kifua kikuu na UKIMWI. Vilevile matumizi ya dawa za kulevya yanasababisha uhalifu kuongezeka, nguvu kazi muhimu ya taifa kupotea, watoto wa mitaani kuongezeka na vifo vinavyoweza kuepukika. Kinachosikitisha zaidi ni ule ukweli kwamba waathirika wengi wa dawa za kulevya ni vijana wakiwemo pia wanafunzi katika shule na vyuo.
Ndugu Wananchi;
Serikali, kupitia kwa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Kikosi Kazi na vyombo vingine vya dola inaendelea kukabiliana na tatizo hili. Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana japokuwa bado changamoto zipo nyingi. Kwa mwaka huu 2012 hadi kufikia Agosti, Tume kwa kushirikiana na Kikosi Kazi na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kukamata kilo 250 za heroin, kilo 150 za cocaine, kilo 45,458 za bangi kavu, kilo 6,215 za mirungi na kuteketeza ekari 184 za mashamba ya bangi. Aidha, kati ya Januari hadi Agosti, 2012, watu 44 wakiwemo Watanzania na raia wa kigeni wamekamatwa na dawa za kulevya za cocaine, heroin na kadhalika na kesi zao zipo Mahakamani.
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa tutaendeleza mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini bila kuchoka. Hatutakubali kushindwa. Hatuwezi kuacha taifa letu liangamie na kuwa na vijana wengi mazezeta. Hata hivyo ili tufanikiwe kwenye vita hii, tunahitaji sana ushirikiano wa wananchi wote. Wananchi mnawafahamu vizuri waagizaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya. Wengine mnaishi nao, marafiki, jirani, ndugu na hata watoto wenu. Tafadhali pelekeni taarifa mzijuazo kwenye taasisi na vyombo vinavyohusika ili zifanyiwe kazi na hatua stahili zichukuliwe dhidi ya wahalifu hao. Tusiwaonee muhali, ni hatari kwa taifa na hasara kwa jamii na familia.
Rushwa
Ndugu wananchi;
Changamoto nyingine inayolikabili taifa letu ambayo Mwenge wa Uhuru umekuwa unaimulika ni rushwa. Sote tunafahamu kuwa taifa lolote lile duniani haliwezi kuendelea bila kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. Rushwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya taifa na utoaji wa haki. Hivyo hatuna budi kupambana kwa dhati na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa nchini mwetu.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ndicho chombo cha mstari wa mbele katika mapambano haya. Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri na kujenga uwezo wa kiutendaji wa TAKUKURU ili iweze kutimiza ipasavyo wajibu wake. Nafurahi kuwa kazi inakwenda vizuri na mafanikio yanazidi kupatikana. Idadi ya kesi za rushwa kubwa na ndogo zinazopelekwa mahakamani imeongezeka.
Pamoja na mafanikio hayo bado tatizo la rushwa lipo hivyo hatuna budi kuendeleza mapambano kwa nguvu zaidi. Napenda kutumia nafasi hii kukumbushana kuwa vita hii sio ya Serikali na TAKUKURU peke yake. Ni vita ya kila mtu hapa nchini, walio raia na wasiokuwa raia wa Tanzania. Narudia kuwasihi watu wote kushirikiana na Serikali na TAKUKURU kupiga vita rushwa. Uhakika wa mafanikio katika vita hii utapatikana pale watu watakapokuwa jasiri kukataa kutoa rushwa au kukataa kupokea rushwa wanapoombwa kufanya hivyo. Mafanikio yatakuwa makubwa zaidi pale watu watakapotoa taarifa kwa TAKUKURU au vyombo vya dola husika kwa hatua zipasazo kuchukuliwa dhidi ya wahalifu. Kulalamikia rushwa imezidi bila ya kuwasema waombaji, watoaji na wapokeaji rushwa haitoshi. Haitasaidia kumaliza tatizo hili ambalo sote tunalolichukia sana.
Wiki ya Vijana Kitaifa
Ndugu wananchi;
Siku ya leo pia ni kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa iliyoanza tarehe 8 Oktoba, 2012. Mbio za Mwenge, ni shughuli ya vijana. Tangu zilipoanzishwa na Baba wa Taifa aliwakabidhi vijana kukimbiza Mwenge, na kwenye wiki kabla ya kumalizika kwa mbio hizo vijana hupata fursa ya kufanya na kuonyesha shughuli mbalimbali wazifanyazo. Nafurahi kwamba utaratibu huu umedumishwa na naomba tuendelee kuudumisha.
Hapa Shinyanga programu mbalimbali za vijana ziliandaliwa ikiwa ni pamoja na maonesho na midahalo, kama sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Vijana. Kabla ya kuja hapa nimepata fursa ya kutembelea maonesho ya vijana pamoja na ya wadau wengineo katika Viwanja vya Sabasaba mjini hapa. Nimejionea mwenyewe jinsi vijana wanavyofanya kazi kwa bidii na maarifa kuinua hali zao za maisha na kuchangia maendeleo ya nchi yao. Maonesho haya yamebainisha wazi kuwa vijana wanao uwezo wa kulifanya taifa letu kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za uchumi na utoaji wa huduma.
Ndugu Wananchi;
Kinachotakiwa kutoka kwetu, yaani wazazi, Serikali na jamii ni kuwajengea vijana wetu mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao.
Kwa kutambua ukweli huo Serikali imewekeza katika kuwapatia vijana fursa za elimu na mafunzo ya stadi za kazi. Kadhalika, kuna mifuko ya kuwasaidia vijana kupata mikopo kutoka Serikalini, taasisi za fedha na kupitia mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali. Natambua kuwa mahitaji ni makubwa kuliko rasilimali zilizopo. Ahadi yangu kwenu tutaendelea kuongeza mafungu kwa ajili hiyo. Aidha, tutaendelea kuhimiza vijana kupewa kipaumbele katika fursa mbalimbali zitakazojitokeza. Napenda kuwahimiza vijana wote nchini wachangamkie fursa zitakapojitokeza na wafanye kazi kwa bidii na maarifa. Waache uvivu na uzembe, waache kushinda vijiweni na kulalamika bali wajitume. Mifano ya wenzao wanaojituma ipo hata leo tumeona. Waige mifano hiyo. Serikali ipo nao bega kwa bega, ipo tayari kuwasaidia.
Maji Mkoani Shinyanga
Ndugu wananchi;
Niruhusuni nimalizie yangu hotuba yangu kuzungumzia mambo mawili: Jambo la kwanza ni tatizo la uhaba wa maji safi na salama Mkoani Shinyanga na Simiyu. Serikali, kwa kutambua hilo, iliamua kuchukua maji ya Ziwa Victoria na kuyafikisha miji ya Kahama na Shinyanga. Katika mradi huo uliokamilika mwezi Desemba, 2008 pamoja na kuhudumia Manispaa ya Shinyanga na mji wa Kahama, vijiji 45 vya mkoa huu na Mwanza vimenufaika. Kazi ya upanuzi wa mradi inaendelea ili kupeleka huduma ya maji safi kwenye vijiji 104 vilivyosalia.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 vijiji vinne vya Nyangomango, Isesa, Igenge na Mbalika vimefanyiwa usanifu na ujenzi wa miundombinu unatarajiwa kuanza hivi karibuni. Vile vile, vijiji vya Chibuji, Ndambi na Nyang’ohonge vilivyoko wilayani Kwimba viko katika hatua ya mwisho za kuunganishwa katika mtandao ili viweze kupata huduma hiyo.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka za zabuni zimekamilika kwa ajili ya kupata Mkandarasi wa kupeleka maji kwenye mji wa Muhunze ambao ni makao makuu ya wilaya ya Kishapu. Hivi sasa taratibu za kupata fedha za kutekeleza mradi huo zinaendelea. Vile vile, maandalizi yanaendelea ya kupata Mhandisi Mshauri wa kufanya usanifu wa mradi wa kupeleka maji kutoka Kahama kwenda Kagongwa hadi Tinde kupitia Isaka na vijiji vya njiani. Mambo yakienda kama ilivyopangwa kazi inategemewa kuanza mwezi Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Serikali imebuni mradi mpya wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kutoka kijiji cha Nasa na kuyasambaza kwenda Miji ya Bariadi, Maswa mpaka Mwanhuzi. Tathmini ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi hiyo imekamilika. Mhandisi Mshauri anatarajia kuanza kazi hiyo mwezi Januari, 2013. Baada ya hapo tutatafuta fedha za kutekeleza mradi huo. Hivyo ndugu zangu wa Shinyanga na Simiyu vuteni subira, Serikali inatambua kilio chenu cha miaka mingi na jitihada za kutafuta ufumbuzi zinaendelea vizuri. Subira yavuta heri.
Bei ya Pamba
Ndugu wananchi;
Jambo la pili, ninalotaka kulizungumzia ni tatizo la bei ya zao la pamba katika msimu wa mwaka huu ulioanza tarehe 2 Julai, 2012 ambao sasa unaelekea ukingoni. Haukuwa msimu mzuri sana pamoja na mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa ya ununuzi wa pamba. Mpaka sasa jumla ya makampuni 37 yanaendelea kununua na kuchambua pamba mbegu. Aidha, zaidi ya tani 309,560 za pamba-mbegu zimenunuliwa kutoka Kanda ya Magharibi. Na zaidi ya tani 1,700 zimenunuliwa Kanda ya Mashariki. Ununuzi bado unaendelea katika Wilaya mbali mbali ambapo inakadiriwa kiasi cha tani 30,000 za pamba bado hazijanunuliwa toka kwa wakulima katika Wilaya za Bariadi, Maswa na Meatu.
Ndugu Wananchi;
Kwa ujumla, ununuzi wa pamba msimu huu ulikabiliwa na changamoto kubwa ya bei kwa mkulima kuwa ndogo tofauti na mwaka wa jana. Kiini cha tatizo hilo ni kuporomoka kwa bei ya pamba katika soko la dunia. Mwaka wa jana bei ya pamba katika soko la dunia ilikuwa Dola ya Marekani 1.45 sawa na shilingi 2,276 kwa ratili wakati mwaka huu ilianzia senti 83 ya dola ya Marekani sawa na shilingi 1,303 kwa ratili na iliendelea kushuka. Kwa sababu hiyo bei ya mkulima mwaka wa jana ilikuwa shilingi 1,100 kwa kilo wakati mwaka huu ilikuwa shilingi 660 kwa kilo. Tena, bei hiyo ilifikiwa baada ya juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali ikishirikiana na Chama cha Wanunuzi wa Wachambuaji wa Pamba, Chama cha Wakulima wa Pamba (TACOTA) pamoja na viongozi wa siasa hususan Wabunge. Wanunuzi wa pamba walitaka kununua kwa shilingi 525 kwa kilo.
Katika jitihada za kutaka bei iongezeke njia mbalimbali zilifikiriwa. Mojawapo ilikuwa ile ya Serikali kufidia tofauti ya bei. Njia hiyo ilishindikana kwani ilikuwa inaibebesha bajeti ya nchi mzigo mkubwa mno ambao haingeumudu. Iwapo ingeamuliwa iwe hivyo mipango mingi ya maendeleo iliyopangwa ingebidi isimame. Baada ya njia hiyo kushindikana, ikaonekana tuangalie uwezekano wa kupunguza baadhi ya tozo zilizokuwa kwenye zao la pamba. Tulikubaliana kupunguza ushuru wa Halmashauri kutoka asilimia 5 hadi 2, faida ya wachambuaji kutoka asilimia 10 hadi 2. Pia, tuliondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye viwanda vya nguo. Hatua hizo ndizo zilizopandisha bei kutoka shilingi 525 kwa kilo hadi shilingi 660 kwa kilo. Bado bei hiyo ni nafuu kidogo, lakini ni chini mno ukilinganisha na ile ya mwaka wa jana. Hata hivyo, ni vigumu kumlazimisha mnunuzi kulipa bei kubwa kuliko ile atakayouzia katika soko la dunia.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;
Ni vyema tukatambua kuwa hatuna uwezo wa kudhibiti bei katika soko la dunia. Kuna miaka huwa nzuri kama mwaka jana na mingine huwa mbaya kama mwaka huu. Lakini tatizo la bei safari hii limetufundisha mengi. Kwanza inatupasa tuanze kuchuna bongo kutafuta mfumo mzuri wa kuleta utulivu wa bei kwa wakulima wakati wa misukosuko mbalimbali ya kiuchumi ndani na nje ya nchi. Nimeshatoa maelekezo kwa Wizara husika kuanza kufanya kazi hiyo. Pili, kwamba tupunguze kutegemea mno soko la nje kuuza pamba ghafi na tuanze safari ya kuuza pamba iliyoongezwa thamani au bidhaa zitokanazo na pamba. Hii ina maana ya kuwa tuwe na viwanda vingi vya nyuzi, nguo na mavazi hapa nchini vinavyotumia pamba yetu. Jambo hilo litawezesha wakulima kupata bei nzuri kwa pamba yao bila ya wanunuzi kuathirika vibaya.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuhitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu wa 2012 napenda kuwapongeza vijana walioshiriki kwenye halaiki. Nawapongeza pia walimu wao. Narudia pia kuwashukuru wote walioshiriki kwa namna mbalimbali kufanikisha sherehe hizi ambazo zimefana mno. Kwenu nyote nasema asanteni sana.
Baada ya kusema hayo sasa natamka rasmi kwamba shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2012 zimefikia kilele chake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Asanteni sana