HOTUBA YA RAIS JAKAYA KIKWETE AKILIVUNJA BUNGE LA 10 DODOMA

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Spika Anne Makinda alipokuwa akilihutubia Bunge.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Spika Anne Makinda alipokuwa akilihutubia Bunge.

HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAGANA NA BUNGE NA KULIVUNJA BUNGE LA KUMI LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA TAREHE 9 JULAI, 2015

Mheshimiwa Spika;
Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuishuhudia siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu na nchi yetu. Hatimaye siku ya kuvunja Bunge la Kumi imewadia ili kuwezesha hatua husika za mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ziweze kutekelezwa.
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kunipatia nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili niweze kutimiza wajibu wangu huo wa msingi Kikatiba. Lakini, shukrani zangu kubwa ni kwa uongozi wako mahiri na shupavu. Umeliongoza Bunge vizuri. Najua haikuwa kazi rahisi. Penye wengi pana mengi. Lakini kwa uhodari mkubwa umeweza kulifikisha jahazi bandarini salama salmini. Hakika wewe ni nahodha makini na jemedari hodari, uliyethibitisha uhodari na umakini wako katika uwanja wa medani. Wewe ndiwe mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga sheria na umeidhihirishia dunia kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza.
Mheshimiwa Spika;
Niruhusu pia nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wao wa Kikatiba wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila ya ninyi Wabunge wetu na Bunge hili, tusingeweza kupata mafaniko na maendeleo tuliyoyapata. Mmejijengea, nyinyi wenyewe na Bunge letu heshima kubwa mbele ya wananchi. Mmeitendea haki demokrasia ya Tanzania na kuliletea heshima kubwa Bunge letu nchini, kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 30 Desemba 2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Tarehe 16 Julai, 2010 wakati wa kuvunja Bunge hilo nilielezea mafanikio tuliyopata na changamoto zilizotukabili katika kipindi hicho. Tarehe 28 Novemba, 2010 wakati wa kuzindua Bunge hili la Kumi niliainisha vipaumbele vya Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi changu cha pili cha uongozi wa nchi yetu na kuahidi kuvitekeleza kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Kama ilivyo ada, leo tunafikia mwisho wa uhai wa Bunge la Kumi, naomba kutumia fursa hii kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale mambo ambayo tuliahidi na kupanga kufanya.
Umoja, Amani na Usalama
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi kuwa katika kipindi cha uongozi wangu nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, dini, makabila, mahali watokako, na ufuasi wa vyama vya siasa. Pia, kwamba nchi yetu itaendelea kuwa yenye amani, usalama na utulivu.
Leo tunapoagana, ninyi na mimi, ni mashuhuda kuwa Tanzania na Watanzania tumebakia kuwa wamoja. Hata hivyo, katika kipindi hiki kumekuwepo na matukio ya hapa na pale madogo na makubwa, yaliyotishia umoja wa nchi yetu na watu wake. Yapo mambo yaliyopandikizwa kuleta chuki baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, baina ya Wakristo na Waislamu na baina ya maeneo fulani ya nchi na wengine.
Bahati nzuri, msimamo thabiti wa viongozi wakuu wa Serikali zetu mbili wakisaidiwa na viongozi wengine pamoja na ushirikiano na viongozi wa dini na wa jamii na uelewa wa wananchi, vimeliwezesha taifa letu kushinda changamoto hizo na matishio yote hayo. Changamoto hizi zimethibitisha ubora wa mazungumzo. Ni kweli kabisa kwamba wanaozungumza hawagombani na wanaozungumza humaliza tofauti zao bila kugombana.
Mheshimiwa Spika;
Niruhusuni, nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa mara nyingine viongozi wakuu wenzangu, Makamu wa Rais, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, viongozi wa dini, viongozi wa jamii na wananchi wote kwa ushindi tulioupata katika kudumisha umoja wetu. Hata hivyo, tahadhari kubwa lazima iendelee kuchukuliwa kwani watu wenye nia mbaya kwa nchi yetu au na umoja wetu hawajaisha na hawajafurahi kwamba hawajafaulu. Huenda wakajaribu tena. Tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kushikamana ili hata wakijaribu tena washindwe.
Muungano Wetu Umeimarika Zaidi
Mheshimiwa Spika;
Nafurahi kwamba namaliza kipindi changu cha uongozi tukiwa tumeweza kudumisha na kuuimarisha Muungano wetu adhimu na adimu Barani Afrika. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kufungua Bunge la Tisa nilisisitiza umuhimu wa viongozi wa pande zetu mbili kukutana mara kwa mara kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu. Nafurahi kwamba jambo hili limefanyika chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais, akisaidiwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, Waziri Kiongozi katika awamu yangu ya kwanza na Makamu wa Pili wa Rais katika awamu hii.
Mafanikio yaliyopatikana ni makubwa. Masuala mbalimbali ya zamani na mapya yamezungumzwa, yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, hadi mwaka 2005 zilikuwa zimebakia kero 13 za Muungano zilizoainishwa na Tume ya Shelukindo, hivi sasa zimebaki kero nne. Tayari ufumbuzi wa kero moja unakamilishwa kiutawala na tatu zimeshughulikiwa kwa ukamilifu katika Katiba Inayopendekezwa. Kama kura ya maoni ingekuwa imefanyika na Katiba hiyo kupitishwa kungekuwa hakuna kiporo cha kero za Tume ya Shelukindo. Lakini kwa vile kura ya maoni haijafanyika ndiyo maana tunaendelea kuzitaja. Hata hivyo, Serikali zetu mbili zimezungumza na kukubaliana tutafute njia ya kumaliza suala la rasilimali ya mafuta na gesi. Ndiyo maana katika Muswada wa Petroli hoja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kusimamia uchimbaji wa mafuta na kumiliki mapato yake ilijumuishwa. Natoa shukrani nyingi kwa Bunge lako tukufu kwa kupitisha Muswada huo. Moja ya kero kubwa katika Muungano tumeimaliza.

Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar
Mheshimiwa Spika;
Mtakumbuka kuwa nilizungumzia kusononeshwa kwangu na mpasuko wa kisiasa uliokuwepo Zanzibar wakati ule na kuelezea utayari wangu wa kusaidia kuuondoa. Kama mjuavyo mazungumzo yalifanyika ndani ya CCM na CUF na baina ya vyama hivyo na muafaka ukapatikana. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikaundwa na mpasuko wa kisiasa ukawa umepatiwa tiba. Matokeo ya yote hayo ni kuwa mazingira ya kisiasa na kijamii yamekuwa bora zaidi siku hizi kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo.
Ni matumaini yangu kuwa ndugu zetu wa Zanzibar watayadumisha mafanikio haya ili waendelee kuishi kwa amani, upendo na udugu. Natambua kuwepo kwa changamoto za hapa na pale katika uendeshaji wa Serikali hiyo. Jambo linalonipa faraja ni kuwa matatizo yenyewe hayahusu muundo wa Serikali bali yanaletwa na watu kupishana kauli au kutofautiana katika uendeshaji wa baadhi ya mambo. Mimi naamini hayo ni mambo yanayoweza kumalizwa kwa wadau kukaa kitako na kuzungumza kama ilivyokuwa kabla ya muafaka.
Amani na Usalama
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu iko salama, mipaka iko salama kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu. Katika kipindi hiki tumewekeza sana katika kuliimarisha Jeshi letu kwa vifaa na zana za kisasa za kivita na mafunzo. Tumeimarisha Kamandi za Nchi Kavu, Anga na Majini. Utayari kivita wa jeshi letu ni mzuri tena wa hali ya juu. Weledi na nidhamu ya Wanajeshi wetu ni ya hali ya juu. Tumeboresha maslahi na makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya za kuishi. Utekelezaji wa mpango wa kuwajengea nyumba 10,000 unaendelea vizuri. Hadi hivi sasa nyumba 6,064 zinaendelea kujengwa nchi nzima na kati yake nyumba 3,096 zimekamilika. Namaliza kipindi changu cha kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kujiamini kwamba “Tupo vizuri”. Pamoja na hayo kazi ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka 15 wa kuimarisha JWTZ lazima iendelezwe ili kulifikisha Jeshi letu pale tulipopakusudia.
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka 10 hii tumefanya jitihada kubwa ya kupambana na uhalifu ili kulinda usalama wa maisha na mali za watu waishio Tanzania. Mtakumbuka kuwa mwaka 2005 na mwanzoni mwa 2006 kulikuwa na matukio mengi ya ujambazi. Niliahidi wakati wa kampeni na katika hotuba yangu Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi waendelee kutamba. Hali ile imedhibitiwa. Ingawaje matukio ya ujambazi hayajaisha, lakini hayako kama ilivyokuwa wakati ule.
Hali kadhalika, matukio ya uhalifu wa kuwania mali yamepungua kutoka 53,268 mwaka 2005 hadi 43,808 mwaka 2014. Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kufanya. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani. Lazima tuendelee kuzitafutia muarobaini wake. Niruhusuni niwatambue na kuwashukuru Inspekta Jenerali (mstaafu) Omari Mahita, Inspekta Jenerali (mstaafu) Said Mwema na Inspekta Jenerali Ernest Mangu aliyepo sasa kwa uongozi wao mzuri.
Mafanikio haya ni matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika utakelezaji wa mpango wa maboresho ya Jeshi la Polisi uliobuniwa wakati wa uongozi wa Ndugu Saidi Mwema, IGP mstaafu. Jeshi la Polisi linaendelea kuwezeshwa kwa zana, vifaa na mafunzo. Taratibu zimekamilika za kulipatia Jeshi hilo magari ya kutosha ili kuongeza ufanisi.
Pia, tumeendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kuishi Maafisa na Askari. Kwa ajili hiyo tumekarabati baadhi ya nyumba zilizopo, tumejenga nyumba kadhaa mpya za ghorofa, za kawaida na mabweni. Mipango imekamilika ya kuwezesha ujenzi wa nyumba 10,000 ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa nyumba za kuishi katika Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika;
Jeshi letu la Magereza nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na kurekebisha tabia zao. Aidha, huduma za malazi, mavazi, chakula na usafiri kwa wafungwa zimeendelea kuboreshwa. Changamoto kubwa ni msongamano wa wafungwa Magerezani. Naamini mipango ya kujenga magereza mapya na kupanua yaliyopo ikitekelezwa tatizo litaisha. Aidha, mpango wa maboresho ya Jeshi la Magereza ukikamilika na kutekelezwa, utaboresha mazingira ya kufanyia kazi na kuishi maafisa na askari, hivyo kupandisha morali wao na kuongeza ufanisi.
Jeshi la Kujenga Taifa
Mheshimiwa Spika;
Ahadi yangu ya kuanzisha upya utaratibu wa kuchukua vijana wa mujibu wa Sheria katika Jeshi la Kujenga Taifa imetimia. Mpaka hivi sasa vijana 38,200 wamekwisha hitimu mafunzo hayo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge walioshiriki kwa kuongoza kwa mfano. Imesaidia sana utaratibu huo kuanza upya bila vipingamizi. Ni matumaini yangu kuwa Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa watakaa pamoja kujadili namna ya kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zilizopo. Naamini zinaweza kumalizwa, vijana wetu wakashiriki mafunzo bila matatizo yoyote.

Utawala Bora
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha miaka kumi hii tumetekeleza dhamira yetu ya kujenga na kuimarisha utawala bora kwa sera, sheria, mifumo, taasisi na kwa rasilimali watu. Tumefanya hivyo katika maeneo yote muhimu yakiwemo yale yahusuyo haki za binadamu, demokrasia, mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya viongozi, ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mgawano wa madaraka hati ya mihimili.
Bunge la Jamhuri ya Muungano
Mheshimiwa Spika;
Serikali imetimiza ipasavyo wajibu wake kwa mhimili mkuu wa dola wa Kutunga Sheria. Tulianzisha Mfuko wa Bunge na kuongeza fedha katika bajeti ya Bunge toka shilingi bilioni 30.58 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 173.76 mwaka 2015/16. Pia tumeanzisha Mfuko wa Jimbo ili kuwawezesheni Wabunge kuchangia katika kutatua changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi wa majimbo yao. Bunge letu limetekeleza ipasavyo majukumu yake kupitia Kamati zake za kudumu na pale ilipolazimu Kamati teule zilizoundwa.
Katika kipindi hiki miswada 163 imepitishwa, maswali ya msingi 7,544 na ya nyongeza 22,632 yameulizwa na kujibiwa. Kamati teule 2 ziliundwa. Haya ni mafanikio makubwa kwa Bunge letu. Bunge hili limefanya kazi kubwa na kazi ya kutukuka. Michango na ushauri wake umekuwa chachu ya baadhi ya hatua na mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na Serikali. Kwa kweli mnastahili pongezi nyingi. Huwezi kutaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne bila kutambua mchango wa Bunge hili.
Mchakato wa Katiba
Mheshimiwa Spika;
Kama sote tujuavyo, kupitia Sheria iliyotungwa na Bunge hili, mwaka 2013 tulianzisha mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kuipatia nchi yetu Katiba mpya iliyo bora zaidi kuliko iliyopo sasa. Nafurahi kwamba mchakato huo ulituwezesha kupata Katiba Inayopendekezwa ambayo imekidhi matarajio hayo. Narudia kutoa pongezi za dhati kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Hatua iliyobaki ni Kura ya Maoni ambapo sote tunasubiri maelekezo ya Tume ya Uchaguzi. Mimi naamini iwapo itapitishwa, Katiba Inayopendekezwa itaimarisha zaidi taifa letu.
Vyama vya Siasa
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumeshuhudia vyama vya siasa vikiendelea kuimarika na kujijenga nchini. Idadi ya vyama vya siasa imeongezeka kutoka 18 hadi 24. Vyama vya siasa vimefanya shughuli zake kwa uhuru. Viongozi na wanachama wao wamefanya mikutano mingi na hata maandamano kote nchini. Baraza la Vyama vya Siasa na TCD vimekuwa vyombo muhimu vilivyofanya kazi nzuri ya kujenga ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa. Yamekuwa majukwaa muhimu ya mashauriano baina ya vyama vya siasa kwa masuala mbalimbali. Matatizo na changamoto nyingi zimeweza kupatiwa ufumbuzi. Ni matumaini yangu kuwa vyombo hivi viwili vitaendelezwa na kuimarishwa miaka ijayo.
Huu ni mwaka wa Uchaguzi, na vyama vya siasa ndiyo wahusika wakuu. Ni matumaini yangu kuwa vyama vya siasa vitaheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi. Hii itasaidia kuwepo kwa utulivu na amani katika mchakato wa uchaguzi.
Uchaguzi Mkuu
Mheshimiwa Spika;
Habari kubwa hapa nchini sasa ni uchaguzi mkuu. Tayari Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) zimekwisha tangaza tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwa ni siku ya kufanyika uchaguzi mkuu. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri. Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa mfumo mpya wa teknolojia ya Biometric Voters Register (BVR). Hadi sasa zoezi la uandikishaji limekamilika katika mikoa 13 na linaendelea katika mikoa 11 na katika mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar uandikishaji unategemea kuanza mwezi huu. Kwa taarifa za Tume ya Uchaguzi, tayari wamekwisha andikisha hadi sasa wapiga kura milioni 11 kati ya lengo la kuandikisha wapiga kura kati ya milioni 21 hadi 23.
Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuiwezesha Tume kutimiza wajibu wake. Napenda kuwahakikishia kuwa kila Mtanzania mwenye haki ya kupiga kura atapata fursa ya kuandikishwa. Shime tuhimize watu wajitokeze kujiandikisha ili wasikose haki yao hiyo.

Uhuru wa Habari
Mheshimiwa Spika;
Mtakubaliana nami kuwa katika kipindi hiki uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao umepanuka sana. Tanzania kuna magazeti ya kila siku 16 na kati ya hayo ya Serikali ni 2 (Daily News, Habari Leo). Pia magazeti ya kila wiki yapo 62. Aidha, kuna vituo vya redio 115 na vya televisheni 29. Serikali haifanyi uhakiki wa habari kabla ya kuchapishwa au kuandikwa. Tumeamua hivyo kwa imani yangu kwamba ustawi wa demokrasia hutegemea sana uhuru wa vyombo vya habari. Pili, kwa vile tunatambua manufaa ya vyombo vya habari kuelimisha jamii, kupambana na maovu na kuhimiza uwajibikaji.
Pamoja na hayo, hatukusita wala kuchelea kuchukua hatua pale uhuru huo ulipotumiwa vibaya na kutishia kuvuruga amani, umoja na usalama wa jamii au taifa. Au, pale ambapo Sheria za nchi zimekiukwa. Huo ni wajibu wetu wa kikatiba ambao mimi na wenzangu tuliapa kuutimiza.
Mheshimiwa Spika;
Katika kuongeza uwazi na mawasiliano na wananchi mwaka 2007 tulianzisha tovuti ya wananchi. Tovuti hiyo imeshapokea hoja 117,243 na kati ya hizo zilizohusu Serikali zilikuwa 78,258 na zote zimeshughulikiwa.
Katika kuboresha mfumo wa mawasiliano, Tanzania imeshahama kutoka mfumo wa analogia na kuingia kwenye mfumo wa digitali. Hii ni hatua kubwa muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini. Jambo ambalo nasikitika kuwa hatukuweza kulikamilisha ni utungaji wa Sheria ya Haki ya Upatikanaji wa Habari na Sheria ya Vyombo vya Habari. Miswada imekamilika na kusomwa mara ya kwanza hapa Bungeni lakini mchakato wake haukuweza kufika mwisho. Tunawaachia wenzetu wajao washughulike nayo katika Bunge la 11.

Vita dhidi ya Rushwa
Mheshimiwa Spika;
Vita dhidi ya rushwa ni eneo jingine ambalo tulilivalia njuga katika Awamu ya Nne. Tumepata mafanikio ya kutia moyo katika mapambano dhidi ya rushwa ingawaje kazi bado ni kubwa. Tumefanya mambo matatu. Kwanza, tumetunga Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo imeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya uovu huu. Idadi ya makosa ya rushwa iliongezwa kutoka 4 mpaka 24 na wigo wa wakosaji pia, kwa kuhusisha watu katika sekta binafsi. Mifumo ya upelelezi na uendeshaji mashitaka nayo imeimarishwa.
Tumeunda chombo kipya TAKUKURU badala ya TAKURU ambacho kimepewa majukumu ya kuzuia na kupambana na rushwa badala ya kuzuia peke yake. TAKUKURU imepewa mamlaka zaidi katika kuongoza mapambano haya. Taasisi imeendelea kuimarishwa kwa kuipatia zana na vifaa vya kufanyia kazi pamoja na rasilimali watu na mahitaji mengine. Tumeiwezesha TAKUKURU kufungua ofisi katika Mikoa na Wilaya zote.
Mheshimiwa Spika;
Maboresho haya yamewezesha idadi ya kesi za tuhuma za rushwa zinazofikishwa mahakamani kuongezeka kutoka kesi 50 mwaka 2005 hadi 1,900 mwaka 2014. Jumla ya shilingi bilioni 87.8 ziliokolewa. Watumishi wa Serikali 97 wameachishwa kazi kwa tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi zao baada ya ushahidi wa kijinai kukosekana. Kwa upande wa kupambana na rushwa kwenye shughuli za uchaguzi, tumetunga Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi Na. 6 ya mwaka 2010 ili kutoa majibu ya kilio cha siku nyingi dhidi ya watu wanaotumia fedha kununua kura.
Mapato na Matumizi ya Fedha na Mali za Serikali
Mheshimiwa Spika;
Nilieleza katika hotuba yangu ya Kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba, 2005 kuwa tutatoa kipaumbele cha juu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya Serikali. Leo miaka kumi baadae ninaona fahari tumepata mafanikio makubwa. Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka shilingi bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi takriban shilingi bilioni 850. Hii imewezesha bajeti ya Serikali kukua kutoka trilioni 4.13 mwaka 2005/2006 hadi trilioni 22.49 mwaka 2015/2016. Isitoshe imetuwezesha kupunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya Serikali mwaka 2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na tumejipa lengo la kushusha zaidi hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika;
Mafanikio haya yametokana hasa na kazi kubwa tuliyoifanya ya kuimarisha Mamlaka ya Mapato ambao wanastahili pongezi zetu nyingi. Bado naamini tunaweza kufanya vizuri zaidi ya hivi, kama tukiongeza udhibiti kwa mianya ya kupoteza mapato na kuimarisha zaidi TRA na mamlaka nyingine za ukusanyaji mapato ya Serikali. Bado ukusanyaji wa mapato yasiyokuwa ya kodi katika Halmashauri za Wilaya na Miji na katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali uko chini ya lengo. Huku kuendelee kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za Serikali tulielekeza nguvu zetu katika kuimarisha utaratibu wa manunuzi Serikalini na ukaguzi wa hesabu za Serikali. Kwa upande wa ununuzi wa bidhaa na huduma, tumeendelea kuimarisha Sheria na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma ili iweze kuhakikisha kuwa kuna usimamizi thabiti wa sheria hiyo na kanuni zake. Kama mjuavyo sehemu, kubwa ya fedha za Serikali hutumiwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma, hivyo kuwepo usimamizi mzuri ni jambo jema. Ukikosekana, wizi na rushwa hutawala.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa ukaguzi wa hesabu za Serikali, tumechukua hatua za makusudi za kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Tumetunga Sheria mpya inayoipa nguvu na uhuru zaidi Ofisi hiyo. Aidha, tumewaongezea bajeti, vitendea kazi na rasilimali watu. Ofisi 8 za Mikoa zimejengwa na 2 zinaendelea kujengwa.
Nafurahi kwamba maagizo yangu kwa viongozi na watendaji katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupewa uzito linazingatiwa. Taarifa hizo sasa zinasomwa, zinajadiliwa na hatua kuchukuliwa kwa kasoro zilizoonekana. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali imefanya kazi nzuri. Wezi na wabadhirifu wanaobainika kuchukuliwa hatua za kisheria mara makosa yanapogundulika. Kitaifa taarifa hiyo hujadiliwa Bungeni kwa muda wa kutosha.
Mheshimiwa Spika;
Niliamua pia kuanzisha Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali na kuwaweka Wakaguzi wa Ndani wote wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa chini ya Mamlaka yake na kuwajibika kwake. Ofisi hii imesaidia kuhakikisha sheria na kanuni za matumizi ya fedha na mali ya umma zinaheshimiwa. Pia, katika ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG. Uimarishaji wa ukaguzi wa ndani na ule wa CAG umesaidia kuboresha hesabu za Serikali kuwa nzuri zaidi siku hizi. Hati safi zimeongezeka na hati chafu zinazidi kupungua Serikalini. Kwa mfano katika Halmashauri za Wilaya na Miji, hati safi zimeongezeka kutoka 56 mwaka 2006 hadi 150 mwaka 2014. Hati zenye mashaka ni 13 na hakuna Hati isiyoridhisha. Kazi ya kuimarisha ukaguzi na nidhamu ya matumizi lazima iendelezwe.

Maadili ya Viongozi wa Umma
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka 10 hii tumeimarisha mfumo wa kusimamia maadili ya viongozi. Tumefanya hivyo kwa kutambua kuwa maadili mema ni sifa ya msingi ya kiongozi na huiletea heshima Serikali. Tumeendeleza Kamati ya Maadili na kuunda Baraza la Maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya 1995. Tumepanua wigo na kwamba sasa mali za viongozi na familia zao hutolewa taarifa na kiongozi katika Tamko la Mali la kila mwaka. Hii inasaidia kuondoa uwezekano wa kiongozi kuficha mali kwa mgongo wa mwenza wake au mtoto.
Mheshimiwa Spika;
Kamati ya Maadili sasa si tu inapokea fomu na kuzihifadhi, bali inafanya ukaguzi wa mali za viongozi na kuzifuatilia. Kikwazo chao ni kupata rasilimali fedha. Hili litazamwe zaidi. Pale inapoonekana kuna makosa ya kimaadili wahusika hufikishwa kwenye Baraza la Maadili. Sote tumeshuhudia kazi nzuri iliyofanywa na Baraza hilo wakati wa sakata la Escrow. Bado kazi ya kuimarisha Kamati ya Maadili kwa rasilimali fedha, vitendea kazi, majengo ya ofisi na rasilimali watu haina budi kuendelezwa.
Muhimili wa Mahakama
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha miaka 10 hii tumefanya jitihada kubwa za kuimarisha mhimili wa Mahakama. Miongoni mwa mambo mengine, tumefanya mambo muhimu kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu lake la msingi la utoaji haki.
Kwanza, tumetenganisha shughuli za kutoa haki na za utawala. Tumeunda Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya kushughulikia mambo ya fedha na utawala. Hivyo basi, Wasajili wa Mahakama wanabaki na jukumu la kutoa haki. Mpaka sasa mabadiliko haya yamekuwa ya manufaa makubwa kwa Mahakama kwani yameboresha utekelezaji wa majukumu katika Mahakama. Pili, tumeanzisha Mfuko wa Mahakama ambao unaipa Mahakama uhuru katika kuendesha shughuli zake. Sambamba na hilo tumeongeza bajeti ya Mahakama kutoka shilingi bilioni 36.6 mwaka 2006/07 hadi shilingi bilioni 87.6 mwaka 2014/15. Jambo linalohitaji kuboreshwa ni Hazina kutoa fedha kwa wakati ili shughuli zifanyike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu, ni kwamba tumeongeza idadi ya Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Lengo letu ni kuongeza nguvukazi ya kusikiliza na kuamua mashauri. Kwa upande wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wameanza kuteuliwa watu wenye Shahada ya Sheria. Hivi sasa itawawezesha watu wenye mashauri katika Mahakama hizo kupata utetezi wa Mawakili. Kati ya mwaka 2005 na 2015 tumeongeza Majaji wa Rufani kutoka 8 mwaka 2005 hadi 16, na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 37 hadi 81 katika kipindi hicho. Hali kadhalika, tumeongeza idadi ya Majaji wanawake. Katika Mahakama ya Rufani wapo 5 na katika Mahakama Kuu wapo 32 na kufanya jumla yao kuwa 37. Hivi sasa tunao jumla ya Mahakimu Wakazi 1,266 katika ngazi zote za Mahakama. Kati ya hao 534 sawa na asilimia 35 ni wanawake. Idadi ya Majaji na Mahakimu wanawake hivi sasa ni kubwa kuliko wakati wowote uliopita.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na mipango mizuri iliyowekwa na Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman Mahakama zimepiga hatua kubwa katika kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani. Majaji wamejiwekea malengo kwa kila Jaji asikilize na kuamua mashauri yasiyopungua 220 kwa mwaka na kila Hakimu Mkazi mashauri 250 na wale wa Mahakama ya Mwanzo mashauri 260 kwa mwaka. Kwa sababu hiyo, kuanzia Julai, 2014 hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2015 yalifunguliwa mashauri 177,586 na Mahakama ilisikiliza na kuamua mashauri 179,962. Maana yake ni kuwa zimesikilizwa zote na nyingine zilizobakia miaka ya nyuma. Bila shaka kwa kasi hii sasa mrundikano wa kesi utabakia kuwa historia katika kipindi kifupi kijacho. Nawapongeza sana Majaji na Mahakimu kwa kazi nzuri waifanyayo.
Kwa upande wa ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu, wamekamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu za Divisheni ya Kazi pamoja na majengo ya Mahakama Kuu Mikoa ya Shinyanga na Kagera. Aidha, majengo mawili ya Mahakama za Wilaya na 12 ya Mahakama za Mwanzo nayo yamekamilika. Hivi sasa, ujenzi unaendelea wa majengo ya Mahakama Kuu 9 za mikoa iliyosalia, Mahakama za Wilaya 9 na za mwanzo 25.
Maboresho ya Mfumo wa Utoaji Haki
Mheshimiwa Spika;
Jambo lingine ambalo tumefanya katika nia ya kuongeza uwajibikaji, ufanisi, na kupunguza malalamiko ya wananchi na ucheleweshaji wa mashauri ni kutenganisha kazi ya upelelezi wa makosa ya jinai na uendeshaji wa mashtaka hayo Mahakamani. Polisi waliokuwa wanafanya yote sasa watashughulikia upelelezi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ndiyo inayoendesha mashauri. Tayari Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka zimekwishafunguliwa katika kila Mkoa na sasa tunaenda wilayani. Aidha, tumeboresha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa ofisi hiyo muhimu sana. Kuna haja ya kuendelea kuongezea rasilimali fedha na vitendea kazi ili ufanisi uongezeke zaidi.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki, tumeimarisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuiwezesha kwa nyenzo, rasilimali fedha na watu. Tume sasa inafanya kazi katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano. Aidha, kutokana na utumiaji wa mfumo wa elektroniki malalamiko ya wananchi mengi zaidi yanafikishwa kwenye Tume na mengi yanapatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, idadi ya malalamiko yaliyowasilishwa Tume yameongezeka kutoka 9,455 mwaka 2006 hadi 25,921 mwaka 2014 na uwezo wa Tume kushughulikia malalamiko kwa mwaka umeongezeka kutoka malalamiko 3,021 mwaka 2005 hadi malalamiko 18,501 mwaka 2014.
Utendaji Serikalini
Maeneo ya Utawala
Mheshimiwa Spika;
Kwa nia ya kusogeza huduma, mwaka 2010 tulianzisha mikoa mipya 4 ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi na wilaya mpya 19. Pia, tulianzisha Halmashauri 45, kata 1,432, vijiji 1,949, Mitaa 1,379 na vitongoji 8,777. Nimeamua kuanzisha mkoa mpya wa Songwe kutoka mkoa wa Mbeya na Wilaya sita kama ifuatavyo: Tanganyika mkoani Katavi, Kigamboni na Ubungo mkoani Dar es Salaam, Songwe mkoani Mbeya, Kibiti mkoani Pwani na Malinyi mkoani Morogoro. Najua tulikuwa na maombi mengi lakini kwa sasa tufanye haya.
Maslahi ya Wafanyakazi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Nne imelipa umuhimu wa juu suala la kuboresha maslahi ya watumishi wa Serikali. Karibu kila mwaka tumekuwa tunaongeza kima cha chini cha mshahara. Kwa sababu hiyo, kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 mwaka 2005 hadi shilingi 265,000 mwaka wa jana. Mwaka huu tumefikia shilingi 300,000. Najua bado hakikidhi mahitaji lakini ukilinganisha na tulikokuwa kipindi hiki tumeongeza sana mishahara ya wafanyakazi. Vile vile, tumeendelea kupunguza kodi ya mapato kwa mfululizo kutoka asilimia 18 mwaka 2005 hadi asilimia 11 mwaka huu. Dhamira yetu ni kutaka kutoa nafuu zaidi kwa wafanyakazi. Vile vile, tumewapandisha vyeo watumishi 233,876 na kulipa malimbikizo ya watumishi 422,348 ya kiasi cha shilingi bilioni 384.8.
Mheshimiwa Spika;
Tumetekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wilaya jambo ambalo limelazimu kuongeza rasilimali fedha na watu kwa Halmashauri za Wilaya na Miji. Kwa ajili hiyo ruzuku kwa Halmashauri zetu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 780 mwaka 2005/2006 hadi shillingi trilioni 4.69 mwaka 2015/2016. Aidha, tumeimarisha utumishi katika Halmashauri kwa kuajiri watumishi wengi wa kada mbalimbali.
Usawa wa kijinsia
Mheshimiwa Spika;
Mwaka 2005 niliahidi wakati wa kampeni na wakati wa kuzindua Bunge la Tisa, kuwa tutaongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli na nyanja mbalimbali za maisha ya watu wa nchi yetu ikiwemo nafasi za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwamba tumetimiza ahadi hiyo. Idadi ya Wabunge wanawake imeongezeka kutoka 62 mwaka 2005 hadi 127. Hivi sasa hamsini kwa hamsini ni rasmi katika Katiba Inayopendekezwa. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na Bunge letu tumepata Spika mwanamke Mheshimiwa Anne Semamba Makinda.
Wanawake wameongezeka katika ngazi zote kuu za uamuzi. Kwa mfano, tunao Mawaziri wanawake 10, Naibu Mawaziri wanawake 5, Majaji wanawake 37 na Wakuu wa Wilaya wanawake wako 53. Kwa upande wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi Watendaji n.k. pia wameongezeka. Katika elimu nako tuna usawa wa kijinsia kwa upande wa idadi ya wanafunzi wa kike na wa kiume katika shule za msingi na sekondari. Katika vyuo vya elimu ya juu, idadi ya wanafunzi wa kike imeongezeka kwa kasi kutoka 10,039 mwaka 2005 hadi 78,800 mwaka 2014.

Hali ya Uchumi
Mheshimiwa Spika;
Wakati ninaingia madarakani mwaka 2005 niliwaahidi Watanzania wenzangu kuwa tutafanya kila tuwezalo kujenga uchumi ulio imara na shirikishi. Hususan, nilisema nitaendeleza sera za mageuzi ya kiuchumi na kuweka misingi madhubuti ya kukuza uchumi, kuongeza ajira, kuongeza Pato la Taifa na kupunguza umaskini. Katika miaka kumi iliyopita tumeendelea kusimamia kwa kiwango kizuri sera za uchumi jumla na sera za uchumi katika ngazi ya chini zinazogusa wananchi wa kawaida.
Jitihada zetu hizo zimezaa matunda ya kutia moyo. Katika kipindi hiki, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa takriban asilimia 7. Nchi yetu ni miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. Pato ghafi la Taifa limeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka shilingi trilioni 14.1 mwaka 2005 hadi kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014. Hivyo basi, pato la wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka shilingi 441,030 mwaka 2005 hadi shilingi 1,724,416 mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika;
Mauzo yetu ya nje yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.67 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani bilioni 8.76 mwaka 2014 na kutunisha akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kuagiza bidhaa na mahitaji ya nchi kutoka nje kwa kipindi cha miezi 4.1 kama tulivyopanga. Mfumuko wa bei ni asilimia 6.1.
Mheshimiwa Spika;
Kama mjuavyo, mwaka 2000 nchi yetu ilijiwekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya hadi mwaka 2025. Mwaka 2010 tulitengeneza Mpango wa Muda Mrefu (Long Term Perspective Plan) wa (2010 – 2025) wa kuongoza utekelezaji wa Dira kwa miaka 15 iliyobaki. Tuligawa utekelezaji wake katika Mipango mitatu ya Maendeleo ya Miaka Mitano kila mmoja. Tuko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mpango wa Kwanza, (2011/12 – 2015/16) na kuandaa mpango wa pili (2016/17 – 2021/22).
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
Mheshimiwa Spika;
Kwa madhumuni ya kuboresha utendaji wa Serikali nilianzisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Huu ni mfumo mpya wa kupanga, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa malengo na shughuli za Serikali kwa nia ya kuhakikisha kuwa kilichokusudiwa kinafanyika, tena kwa wakati. Tuliamua kuanza na sekta sita za Elimu, Nishati, Kilimo, Uchukuzi, Maji na Mapato ya Serikali. Baadae sekta ya afya na uboreshaji mazingira ya uwekezaji ziliongezwa.
Katika kipindi hiki kifupi Mpango umethibitisha kuwa wenye manufaa. Mambo katika sekta zilizojumuishwa katika BRN yameanza kwenda vizuri. Changamoto yetu kubwa imekuwa ni upatikanaji wa fedha zinazohitajika kwa wakati kutoka Hazina. Kama changamoto hiyo isingekuwepo mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa Spika;
Kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji katika kukuza uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato na kupunguza umaskini, Serikali yetu imekuwa inachukua hatua thabiti za kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuchagua Tanzania kuwa nchi inayofaa kuwekeza.
Mwaka 2010 tumetengeneza Sera na kutunga Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership—PPP). Lengo letu ni kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuvutika kushirikiana na Serikali katika shughuli za kiuchumi na maendeleo. Faida kubwa ya utaratibu huu ni kuipunguzia Serikali mzigo wa kuwekeza katika baadhi ya shughuli ambazo sekta binafsi inaweza kubeba sehemu ya gharama. Hii siyo tu inaongeza kasi ya maendeleo, bali kuiwezesha Serikali kuokoa fedha ambazo inaweza kuzitumia kwa shughuli nyingine.
Juhudi zetu za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinaendelea kuzaa matunda mema. Kati ya 2005 na 2014, Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 154.274. Kati ya miradi hiyo asilimia 49.38 ni ya wawekezaji wa ndani, asilimia 23.41 ni wawekezaji wa kutoka nje na asilimia 27.18 ni miradi ya ubia baina ya Watanzania na wawekezaji wa kigeni. Ajira 16,000 zilipatikana. Ukuaji huu wa uwekezaji umeongeza mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya uwekezaji iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Viwanda na Biashara Duniani (UNCTAD) ya mwaka 2015, Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji. Ilipata Dola za Marekani bilioni 2.142 sawa na asilimia 31.5 ya uwekezaji wote katika Jumuiya yetu.

Sekta za Uzalishaji
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika;
Kuendeleza kilimo ilikuwa ni moja ya mambo tuliyoyapa kipaumbele cha juu. Shabaha yetu kuu ni kutaka kuongeza tija ili uzalishaji uongezeke, wakulima wapate mavuno mengi, masoko ya uhakika yawepo na bei iwe nzuri ili mapato yao yaongezeke na umasikini uwapungukie. Vile vile wao na taifa lijitosheleze kwa chakula.
Kwa ajili hiyo mwaka 2006 tuliasisi Programu ya miaka 7 ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme—ASDP). Katika Programu hiyo, matatizo yanayofanya tija na uzalishaji katika kilimo kuwa mdogo yalitambuliwa na kutengenezewa mpango wa kuyatatua. Serikali pia ilianzisha mikakati, programu na mipango mingine ya kuongeza msukumo katika kuleta mageuzi ya kilimo. Miongoni mwa hiyo ni mkakati wa Kilimo Kwanza, Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (TAFSIP), Sera ya Umwagiliaji tuliyoitunga mwaka 2010 na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na hayo, tumeongeza pia bajeti ya sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 233.3 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 1,084.7 mwaka 2014/15. Kuongezwa kwa bajeti kumewezesha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo kuongezeka kutoka shilingi bilioni 7.5 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 299.3 mwaka 2013/14. Matrekta makubwa na madogo yameongezeka kutoka 7,491 mwaka 2005 hadi 16,412 mwaka 2014. Kwa sababu hiyo matumizi ya jembe la mkono yamepungua kutoka asilimia 70 hadi asilimia 62. Tumeongeza maafisa ugani kutoka 3,379 mwaka 2005 hadi 7,974 mwaka 2014.
Vituo vya utafiti wa kilimo tumeviongezea rasilimali fedha, watu na vitendea kazi. Aidha, tumeanza safari ya kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuzalisha mbegu. Aidha, tumeimarisha Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency – ASA) na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 10,477.17 mwaka 2005 hadi tani 32,340 mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika;
Juhudi za Serikali kuendeleza kilimo zimezaa matunda mazuri. Tija katika uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula imeongezeka. Kwa upande wa mazao ya chakula uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2014. Ongezeko hili limeliwezesha taifa letu kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 125 mwaka 2014 ikilinganishwa na asilimia 95 mwaka 2005. Uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara umeongezeka toka tani 427,738 mwaka 2005 hadi tani 569,054 mwaka 2014 na uzalishaji wa mbegu za mafuta umeongezeka karibu ya mara 4 toka tani 1,389.9 mwaka 2005 hadi tani 5,545.6 mwaka 2014. Aidha, uzalishaji wa matunda nao umeongezeka toka tani milioni 1.2 mwaka 2005 hadi tani milioni 4.4 mwaka 2014 na maua toka tani 5,862 hadi tani 10,790.
Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima bado ni changamoto. Pia kuna tatizo la upungufu wa maghala ya kuhifadhi mazao. Jitihada zinaendelea kupata mkopo au wabia wa kujenga maghala ya kisasa nchi nzima. Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushiriki ilianzishwa ili kutatua tatizo la masoko. Aidha, tumeanza maandalizi ya kuanzisha soko la bidhaa (Commodity Market Exchange) kwa nia hiyo hiyo. Naamini misingi mizuri tuliyoijenga pamoja na kuenea kwa SACCOS na kuanza kwa Benki ya Kilimo ikiendelezwa itatoa mchango mkubwa katika kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo.

Mifugo
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa mifugo, dhamira yetu ilikuwa kuanza safari ya kuleta mageuzi katika sekta hii. Safari hiyo tumeianza kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo. Changamoto zinazochangia maendeleo duni ya sekta hii zimeainishwa na kutengenezewa mkakati wa utekelezaji. Katika kipindi hiki malambo 1,008, majosho 2,364 na maabara 104 za mifugo zimejengwa. Visima virefu 101 vimechimbwa, malambo 370 na majosho 499 yamekarabatiwa katika kipindi hiki cha miaka 10.
Ukarabati na ujenzi wa majosho umeongeza idadi kutoka 2,177 mwaka 2006 hadi 3,637 mwaka 2015. Tumeongeza Maofisa Ugani kutoka 2,270 mwaka 2005 hadi 6,041 mwaka 2014. Kuhusu uhamilishaji, tumeongeza vituo kutoka kituo 1 mwaka 2005 hadi vituo 8 mwaka 2015 na kuwezesha ng’ombe 955,360 kuhamilishwa katika miaka 10 hii.
Mheshimiwa Spika;
Mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi tuliyoyajenga yamewezesha viwanda vya kusindika nyama, maziwa na vyakula vya mifugo kuongezeka. Viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka 2015. Viwanda vya kuzalisha vyakula vya mifugo vimeongezeka kutoka viwanda 6 mwaka 2005 hadi 80 mwaka 2015 vikiwa na uwezo wa kusindika tani milioni 1.4 za vyakula hivyo kwa mwaka. Aidha viwanda na machinjio ya kisasa 9 vimejengwa katika kipindi hiki. Usindikaji wa ngozi pia umeongezeka kutoka vipande 790,000 mwaka 2005 hadi vipande milioni 3.78 mwaka 2014. Hivi sasa kwa mfano, uzalishaji wa malisho ya mifugo (hei) umefikia marobota 957,860 ikilinganishwa na marobota 178,100 mwaka 2005.
Safari yetu ya kuanza kuondoka kwenye uchungaji kwenda kwenye ufugaji imeanza. Vijiji vingi vimeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na hivyo vimetenga maeneo ya kilimo na ya ufugaji. Tuendelee kuhimiza vijiji vyetu kutekeleza mipango hiyo ili wafugaji wapate maeneo ya malisho mbali na mazao ya wakulima. Pia, tuhimize uhamilishaji kama mlango wa kuingilia kwenye kuboresha kosafu za mifugo yetu.
Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Wakati nazindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba 2005 nilisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itatoa kipaumbele kwenye kuendeleza sekta ya uvuvi. Katika kutekeleza hayo tumefanya yafuatayo. Kwanza, nimeunda Wizara mpya ya Mifugo na Uvuvi. Pili, tulifuta kodi ya zana za uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kupata zana bora na za kisasa kwa bei nafuu zaidi. Tatu, tumeimarisha vyuo vya uvuvi na hivi sasa vina uwezo wa kudahili wanafunzi 1,215 ikilinganishwa na wanafunzi 127 mwaka 2005. Hii imetuwezesha kuongeza wagani wa uvuvi kutoka 103 mwaka 2005 hadi 540 mwaka 2014. Nne, tumeongeza sana juhudi za kupambana na uvuvi haramu ili kutunza mazingira, mazalia ya samaki na kuzuia kuvuliwa au kuuawa kwa samaki wadogo.
Tumeimarisha maabara ya Taifa ya Samaki pale Nyegezi kwa vifaa vya kisasa na wataalamu ili iende na wakati. Tano, tumeongeza msukumo wa kuhimiza ufugaji wa samaki na kuwezesha mashamba ya samaki kuongezeka kutoka 13, 011 mwaka 2005 hadi 20, 325 mwaka 2014.
Uvuvi haramu unapungua. Mapato ya sekta ya uvuvi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 351.6 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.8 mwaka 2013. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika sekta hii ili kuongeza tija na mapato ya wavuvi na taifa.
Utalii
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa utalii, tumeendelea na jitihada za kuiendeleza sekta hii muhimu. Tumeongeza kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu katika masoko makubwa duniani. Sekta ya utalii imekua kwa wastani wa asilimia 7.1 na imechangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni. Idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 612, 754 mwaka 2005 hadi watalii 1,140,156 mwaka 2014. Idadi ya vitanda katika mahoteli imeongezeka kutoka 15,828 hadi 21,929. Mapato pia yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 823.05 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani bilioni 2 mwaka 2014. Ajira za moja kwa moja zimeongezeka kutoka 32,673 hadi 686,130 na zisizokuwa za moja kwa moja kutoka 165,883 hadi 1,318,109. Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumekabiliana na tukio kubwa la ujangili wa wanyamapori hasa wa ndovu kutokana na kushamiri kwa biashara ya meno ya ndovu na bei kuwa kubwa katika nchi za Mashariki ya Mbali. Vuguvugu la ujangili lilifikia kiwango cha kutishia kumaliza ndovu nchini na dunia nzima. Tukaamua kuchukua hatua za kuidhibiti hali hiyo. Tumefanya operesheni tatu kukabiliana na tishio hili. Ya kwanza, iliendeshwa na Idara ya Wanyamapori na Misitu wakishirikiana na TANAPA na Ngorongoro Conservation Area. Hii hasa ilihusu kupambana na ujangili katika hifadhi na mapori ya Kaskazini mwa Tanzania. Mafanikio makubwa yalipatikana.
Mheshimiwa Spika;
Operesheni ya pili ni ile iliyohusisha Jeshi la Polisi katika hifadhi na sehemu nyingine za Tanzania. Operesheni Kipepeo kama ilivyoitwa nayo ilipata mafanikio. Na ya tatu, Operesheni Tokomeza iliyohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Pamoja na changamoto zake operesheni hizi zimesaidia sana kupunguza kasi ya ujangili nchini. Matokeo yake katika sensa ya ndovu iliyofanyika mara ya mwisho, ukiacha Ruaha, hali katika hifadhi na mapori mengine ina muelekeo mzuri.
Kuundwa kwa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) yenye mamlaka makubwa zaidi ya kusimamia sekta ya wanyamapori nako kutaimarisha uhifadhi na mapambano ya ujangili. Kwa mipango na program zilizopo Wizarani, naamini mambo yatakuwa mazuri zaidi muda si mrefu.
Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka kumi hii, sekta ya viwanda imeendelea kukua kwa kasi nzuri ya kutia moyo. Viwanda vikubwa, vya kati na vidogo vimeongezeka kutoka 11, 544 mwaka 2005 hadi viwanda 51,224 mwaka 2015. Kati ya mwaka 2005 na 2014 na miradi 751 imepewa leseni za kudumu na BRELA ya kuanzisha viwanda. Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.3 mwaka 2014 kutoka asilimia 6.8 mwaka 2005. Mchango wa viwanda kwenye mauzo ya nje umeongezeka kutoka asilimia 9.3 mwaka 2005 hadi asilimia 23.3 mwaka 2014.
Tunategemea ukuaji mkubwa wa viwanda katika Mpango wa Pili wa maendeleo wa miaka 5 kutokana na misingi imara tuliyoijenga katika Mpango wa Kwanza. Ujenzi wa kiwanda cha chuma kule Liganga na makaa ya mawe cha Mchuchuma, unatarajiwa kuanza mwaka huu na kiwanda cha kuchakata gesi pale Lindi unatarajiwa kuanza baada ya taratibu za kuwapatia ardhi zitakapokamilika. Hivi ni viwanda vya msingi na mama ambavyo vitachochea kasi ya ukuaji wa viwanda nchini na uchumi kwa jumla.
Madini
Mheshimiwa Spika;
Sekta ya Madini ndiyo ya pili baada ya utalii kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni. Kama nilivyoahidi, tulipitia upya sera, sheria na mikataba ya madini iliyokuwepo na kutengeneza sera na sheria mpya. Halikadhalika, tulianzisha mazungumzo na baadhi ya makampuni ambayo hatimaye yalizaa marekebisho ya mikataba yao na hivyo kuboresha maslahi ya taifa.
Kufuatia marekebisho hayo, makampuni husika ya madini yanalipa kodi ya mapato. Bila ya hivyo huenda mpaka leo yangekuwa hayajaanza kulipa kodi. Kutumika kwa Sheria mpya ya Madini, viwango vipya vya mrahaba na kupunguzwa kwa misamaha ya kodi vimeongeza mapato ya Serikali. Aidha, tuliunda Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ambao umewezesha kukagua mahesabu ya migodi kuhusu uwekezaji na mauzo ya madini na kuwawezesha TRA kutoza kodi stahiki kutoka kwa makampuni hayo.
Mheshimiwa Spika;
Mabadiliko haya pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta hii yamewezesha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2014. Thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi pia imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 655.5 mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.794 mwezi Desemba 2014. Mambo yangekuwa mazuri zaidi kama bei ya dhahabu isingeshuka katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika;
Serikali ilifanya uamuzi wa kulifufua na kuliwezesha Shirika letu la Madini (STAMICO) kuanza tena kazi ya utafutaji na uchimbaji wa madini kupitia kampuni zake tanzu. STAMICO kwa kupitia kampuni yake ya STAMIGOLD imeanza kuzalisha dhahabu na kuuza nje. Vilevile, tumejiunga na Mpango wa Uwazi wa Uvunaji wa Maliasili (EITI) ambao umesaidia sana katika kuongeza uwazi katika biashara ya madini na kusaidia katika ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye makampuni ya madini.
Katika kipindi hiki, migodi mitatu mipya ilianzishwa nayo ni Migodi ya dhahabu wa Buzwagi (Shinyanga) na New Luika (Mbeya) na mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka (Ruvuma). Aidha, miradi mikubwa mingine 8 imeendelezwa na kufikia hatua ya kuanzisha mgodi ukiwemo Mradi wa Urani wa Mkuju (Ruvuma), Mradi wa Chuma Liganga na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma (Njombe). Pia, ajira rasmi kwenye migodi mikubwa nchini imeongezeka kutoka waajiriwa 3,517 mwaka 2005 hadi waajiriwa 15,000 mwaka 2014. Hali kadhalika, makampuni ya madini yameongeza unununzi wa bidhaa na huduma hapa nchini (local procurement) kutoka Dola za Marekani milioni 230.41 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani milioni 536.56 mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki pia, tumetenga maeneo 8 kwa ajili ya wachimbaji wadogowadogo. Maeneo haya yamewezesha wachimbaji wadogo kuchimba madini bila bughudha. Aidha, Wizara imenunua mitambo miwili kwa ajili ya uchorongaji wa miamba kusaidia utafiti wa madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Tumeanzisha mfuko wa kuwakopesha wachimbaji wadogo pale Wizarani ili kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao.

Nishati
Mheshimiwa Spika;
Wakati naanza kazi ya uongozi wa nchi yetu, Tanzania ilikuwa inakabiliwa na ukame mkubwa uliosababisha upungufu mkubwa wa chakula. Pia kulikuwa na upungufu mkubwa wa umeme kwa sababu ya mabwawa ya kuzalisha umeme kukosa maji ya kutosha. Serikali ililazimika kulisha watu zaidi ya milioni 3,776,000 na kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Kwa siku za usoni tuliamua kuchukua hatua thabiti ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na vyanzo vingine kama vile makaa ya mawe, mionzi ya jua na upepo.
Ujenzi umekamilika wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Songo Songo litakaloongeza kiasi cha gesi kuja Dar es Salaam na kuwezesha uzalishaji wa megawati 3000 za umeme. Wakati huo huo kazi ya kujenga vituo vya kufua umeme inaendelea pale Kinyerezi, Dar es Salaam. Umeme huo utakidhi mahitaji ya umeme sasa na miaka kadhaa ijayo.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tuliunda Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambao wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kusambaza umeme kwa vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 nchini. Kazi kubwa iliyofanyika vijijini inapochanganywa na ile ya mijini imeongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme kutoka asilimia 10 hadi asilimia 40 mwaka 2015. Uamuzi uliofanywa katika Bajeti ya mwaka huu wa kukusanya fedha kwa ajili ya umeme vijijini kupitia mafuta ya petroli, utasaidia sana kuongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini.
Gesi Asilia
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Kuanzia mwaka 2010 nchi yetu imepata bahati ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi bahari kuu. Mpaka sasa zimegundulika futi za ujazo trilioni 47.08. Ukijumlisha na futi za ujazo trilioni 8 zilizogunduliwa takriban miaka 40 iliyopita kule Songo Songo na Msimbati jumla ya rasilimali ya gesi asilia nchini ni futi za ujazo trilioni 55.08. Kazi ya utafutaji inaendelea na wataalamu wanasema kuwa Tanzania inaweza kuwa na akiba ya futi za ujazo trilioni 200. Kiasi cha gesi kilichogunduliwa mpaka sasa ni kikubwa na kufanya Tanzania kuwa mahala papya pa kuipatia dunia nishati hii.
Gesi asilia tuliyonayo ikisimamiwa na kutumiwa vizuri itaiwezesha nchi yetu na watu wake kupata maendeleo makubwa na kuondokana na umaskini. Ni fursa ya aina yake ya kuipatia Serikali mapato makubwa na kuiwezesha kutimiza kwa uhakika majukumu yake na mipango yake. Lakini, ili hayo yaweze kufanyika hapana budi pawepo usimamizi mzuri wa hatua zote muhimu za mnyororo wa thamani: yaani utafutaji, uchimbaji, usafirishaji, uuzaji wa gesi asilia na matumizi yake nchini kama nishati na mali ghafi ya viwanda upande mmoja. Upande mwingine inategemea sana matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Ni kutokana na kutaka kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa hivyo ndiyo maana tumetunga Sera ya Gesi Asilia na kuwasilisha katika Bunge hili ile Miswada miwili yaani wa Sheria ya Petroli na ule wa Matumizi ya Mapato ya Mafuta na Gesi. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuipitisha Miswada hii nami nitaitia saini mara nitakapoletewa.
Usafirishaji na Uchukuzi
Barabara
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Nne, imetoa kipaumbele cha juu kwa uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi nchini. Hii ni pamoja na barabara, reli, bandari, usafiri wa majini na usafiri wa angani. Tumeendeleza kazi ya kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini kwa mafanikio makubwa. Karibu barabara kuu zote nchini na zile zinazounganisha mikoa zimekamilika kujengwa au kazi ya ujenzi inaendelea. Kwa sababu hiyo hivi leo kutokea po pote nchini kwenda Dar es salaam unafika siku hiyo hiyo, tofauti na ilivyokuwa zamani watu walichukua zaidi ya siku moja. Adha ya kupita Kenya na Uganda kwa watu wa Mikoa ya Ziwa tumeimaliza.
Katika mkakati wetu wa kupanua mtandao wa barabara za lami nchini, tulitambua barabara za urefu wa kilomita 11,474 za kujengwa kwa kiwango cha lami. Baadae tuliongeza barabara nyingine na kufikisha kilomita 17,742 katika mpango huo. Utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali. Tayari ujenzi wa kilomita 5,568 kwa upande wa barabara kuu na kilomita 535 kwa barabara za mijini umekamilika. Ujenzi wa kilomita 3,873 unaendelea. Upembuzi yakinifu na usanifu umekamilika kwa barabara za urefu wa kilometa 4,965 kinachosubiriwa ni kupatikana fedha ujenzi uanze. Baadhi ya barabara hizo zimo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. Barabara za urefu wa kilometa 3,336 zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki pia, madaraja madogo 7,200 na makubwa 12 yamejengwa na mengine 16 yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miongoni mwa madaraja makubwa yaliyokamilika ni daraja la Mto Malagalasi na yanayojengwa ni daraja la Kigamboni na lile la Mto Kilombero. Madaraja haya yalikuwa miongoni mwa matano yaliyopangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano mara baada ya uhuru. Madaraja mawili yaani la Kirumi lilijengwa mwaka 1985 na la Rufiji mwaka 2003. Kwa upande wa vivuko, tumeongeza vipya 15 na kufikisha idadi ya 28 kote nchini mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika;
Tumeongeza sana fedha katika mfuko wa barabara kutoka shilingi bilioni 73.08 mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 866.63 mwaka 2015/16. Hii itasaidia katika matengenezo ya barabara za lami tulizojenga na kujenga nyingine mijini. Hali kadhalika itatumika kuimarisha barabara za udongo na changarawe wilayani na vijijini ziweze kupitika wakati wote. Katika kipindi hiki barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilometa 9,424 hadi kilometa 22,089.
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka kumi hii idadi ya vyombo vya moto yaani magari, bajaji na pikipiki imeongezeka kutoka 1,696,088 mwaka 2005 hadi 3,313,254 hivi sasa. Ongezeko hili linalotokana na hali ya kiuchumi ya watu wengi kuwa nzuri limezua tatizo la msongamano wa magari katika miji mingi nchini. Katika jiji la Dar es Salaam ambako tatizo ni kubwa zaidi na Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kupunguza ukali wake. Tunapanua ukubwa wa baadhi ya barabara, kujenga barabara za mzunguko (ring roads) na sasa tunaanza ujenzi wa barabara za juu ya nyingine (flyovers). Tulianzisha matumizi ya treni katika reli za TAZARA na TRC kusafirisha abiria. Hivi sasa reli hizo zinasafirisha abiria milioni 2,804,269 kwa mwaka ambao wangehitaji daladala 253 kwa siku. Mpango mkubwa wa kuendeleza matumizi ya reli, Dar es Salaam umeandaliwa na tumeanza kuutafutia fedha.
Usafiri wa Reli
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumetumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili reli zetu za TAZARA na TRC. Kimsingi reli hizo zimekuwa zinakabiliwa na matatizo ya uchakavu wa miundombinu na uongozi na uendeshaji usioridhisha. Kwa sababu ya matatizo hayo reli hizi ambazo kila moja inaweza kusafirisha tani milioni 5 kwa mwaka zinasafirisha kati ya tani 200,000 na 300,000 tu. Hivyo basi, mizigo mingi husafirishwa kwa barabara na kutishia uhai wa barabara ambazo tumezijenga kwa gharama kubwa.
Kwa upande wa reli ya kati, uboreshaji wa reli kati ya Dar es Salaam na Tabora unakaribia kukamilika na utaendelea mpaka Kigoma na Mwanza. Wakati huo huo mchakato wa ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa (standard gauge) unaendelea. Ujenzi unaweza kuanza mwaka huu kutegemea kukamilika kwa majadiliano na mabenki yaliyoonyesha utayari wa kutukopesha pesa za ujenzi.
Mheshimiwa Spika;
Azma yetu ya kufufua reli ya TAZARA nayo tumeiwekea mkakati. Sisi na Zambia tumekubaliana kushirikiana kwa karibu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili reli yetu hiyo. Bahati nzuri marafiki zetu wa China nao wamekubali kutusaidia katika mipango yetu hiyo. Ni matumaini yangu kuwa safari hii tutapata ufumbuzi wa kudumu kwa matatizo yanayoathiri ufanisi wa reli hii yenye umuhimu wa aina yake kwa uhai na ustawi wa uchumi wa nchi zetu na watu wake.
Bandari
Mheshimiwa Spika;
Tumeboresha na kuimarisha huduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa. Mwaka 2014 bandari yetu ilihudumia tani milioni 14.4 ukilinganisha na tani milioni 6.7 mwaka 2005. Mwaka huu inaweza kufikia tani milioni 18. Siku hizi huduma hutolewa kwa saa 24 na kasi ya kupakua, kupakia na kutoa mizigo imeongezeka sana na wizi umepungua sana. Hata wale walioacha kuitumia bandari yetu wameanza kurudi.
Mheshimiwa Spika;
Kuanza kutumika kwa mfumo wa Single Custom’s Territory unaorahisisha upakuaji na upakiaji mizigo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kumeongeza zaidi ufanisi. Tuko katika majadiliano na DRC na Zambia ambao nao wameonyesha nia ya kuingia katika mfumo huu.
Kuongezeka kwa usafirishaji wa mizigo inayopita nchini kuna faida kwani sekta ya usafirishaji inachangia zaidi ya asilimia 15 ya pato la taifa. Hali kadhalika, ujenzi wa gati za 13 na 14 katika bandari ya Dar es Salaam unaotegemewa kuanza mwezi huu utawezesha huduma ya makasha kuongezeka kutoka makasha 600,000 hadi makasha 1,200,000. Mipango ya kuboresha bandari za Mtwara, Tanga na zile zilizo kwenye Maziwa yetu makuu na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo zitaiwezesha Tanzania kunufaika na fursa ya jiografia yake.
Usafiri wa Anga
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumefanya jitihada kubwa ya kuwekeza kwenye ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege nchini. Tumekarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ambao umeongeza uwezo wa kuhudumia kutoka ndege 7 hadi 30 hivi sasa. Aidha tunajenga jengo la tatu la abiria kwenye uwanja huo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5. Ujenzi huo unategemewa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu. Kukamilika kwake kutauwezesha uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhudumia abiria milioni 6 na ndege nyingi zikiwemo ndege kubwa za kisasa za Airbus 380.
Mheshimiwa Spika;
Vile vile, tumeufanyia ukarabati na upanuzi Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro ambao ni muhimu sana kwa sekta ya utalii ya ukanda wa kaskazini. Uwanja mpya wa ndege wa Songwe kule Mbeya umekamilika na hivi sasa unatumika. Hali kadhalika, tumeviboresha upya viwanja vya ndege vya Arusha, Mafia, Mpanda, Kigoma, Tabora, Mwanza na Bukoba.
Ujenzi, upanuzi na ukarabati huu tulioufanya, umechangia sana katika ongezeko kubwa la safari za ndege na abiria nchini. Safari za ndege kuja nchini zimeongezeka toka safari 78 mwaka 2005 zilizokuwa zinatolewa na kampuni 29 za usafiri wa ndege hadi safari 175 zinazotolewa na kampuni 55 mwaka 2014. Aidha, abiria wanaoondoka na kuwasili katika viwanja vya ndege wameongezeka kutoka 2,172,519 mwaka 2005 hadi abiria 4,670,380 mwaka 2013. Siku hizi Watanzania wanaopanda ndege wanaongezeka kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Spika;
Jambo ambalo hatukuweza kufanikiwa ni lile la kufufua Shirika letu la Ndege. Tumefanikiwa kulifanya lisife lakini hatukuweza kulihuisha lirejee hata kwenye ile hali yake ya zamani. Hata hivyo, fikra na mawazo kuhusu mkakati wa kulijenga upya shirika hilo yapo. Kwa sasa Menejimenti imepewa jukumu la kuandaa mpango wa biashara unaoeleweka na unaokopesheka, kisha Serikali itaona namna ya kulisaidia shirika.

Utabiri wa Hali ya Hewa
Mheshimiwa Spika;
Sambamba na hayo, tumeboresha huduma za utabiri wa hali ya hewa. Mamlaka ya Hali ya Hewa imepatiwa vifaa vipya ambavyo vimeongeza ufanisi na usahihi wa utabiri unaotolewa. Mwezi Februari 2014 Mamlaka hiyo ilipata cheti cha utoaji wa huduma bora cha ISO na hivyo kuufanya taarifa zake kutambuliwa kimataifa.
Mawasiliano
Mheshimiwa Spika;
Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Tumejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilometa 7,560 unaounganisha miji mikuu ya mikoa yote ya Tanzania Bara isipokuwa mkoa mpya wa Simiyu. Kwa Mikoa ya Unguja na Pemba, ujenzi wake utakamilika mwezi ujao. Katika Awamu ya Pili, Mkoa wa Simiyu na wilaya zote nchini zitaunganishwa.
Ujenzi wa mkongo huu umechangia katika kuongeza ubora na kasi ya mawasiliano, na kushusha gharama za mawasiliano. Kwa mfano, gharama za kupiga simu zimeshuka kutoka shilingi 115 kwa dakika mwaka 2005 hadi shilingi 34.92 mwaka 2014 na gharama za intaneti zimeshuka kutoka wastani wa shilingi 36,000 kwa Gigabyte moja mwaka 2005 hadi wastani wa shilingi 9,000 kwa Gigabyte moja (GB 1) mwaka 2014. Hii imeshusha pia gharama za biashara kwa kurahisisha mawasiliano na malipo kati ya mabenki na kwa njia ya mtandao na simu.
Kwa upande wa laini za simu, zimeongezeka kutoka laini milioni 2.96 mwaka 2005 hadi milioni 28 mwaka 2014. Watu wanaotumia intaneti wameongezeka toka milioni 1.6 hadi milioni 9.3 mwaka 2014. Kukua kwa mawasilino ya simu kumewezesha watumiaji milioni 12.3 kupata huduma ya fedha kupitia simu za mkononi. Kati ya Julai 2013 na Aprili 2014 jumla ya miamala milioni 972.6 ilifanyika yenye thamani ya shilingi trilioni 28. Huu ni wastani wa zaidi ya shilingi trilioni 2 kwa mwezi na kufanya Tanzania kuongoza duniani kwa huduma hii.
Mheshimiwa Spika;
Tulitambua kuwa makampuni binafsi ya simu hayapendi kuwekeza vijijini ambako biashara si kubwa kama mijini. Kwa kutambua umuhimu wa huduma ya mawasiliano kwa maendeleo, Serikali iliamua ibebe mzigo huo. Kwa sababu hiyo tumeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao utawezesha kata na vijiji vyote nchini kufikiwa na huduma za mawasiliano. Mfuko huo umekwisha wezesha jumla ya kata 52 na vijiji 314 kufikiwa na huduma hizo. Upelekaji wa huduma za mawasiliano kupitia Mfuko huo zinaendelea kwa kata nyingine 163 zenye vijiji 922, ambapo wananchi milioni 1.2 watanufaika.
Mheshimiwa Spika;
Tumechukua hatua ya kuhakikisha kuwa mianya ya kodi inazibwa na kwamba makampuni yanalipa kodi stahiki kwa kununua na kufunga mtambo wa Kusimamia Mawasiliano ya simu nchini. Mtambo huo unaowezesha Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kukusanya takwimu halisi za mawasiliano yanayofanywa. Tangu kuanza kutumika kwa mtambo huo, mwaka jana Serikali imeweza kukusanya shilingi bilioni 24.6 ambazo vinginevyo zisingepatikana. Aidha, tumekuwa nchi ya kwanza Afrika ya Mashariki kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda digitali. Karibu tutakamilisha kwa mikoa yote. Tunazipokea nchi kadhaa zinazokuja kujifunza kwetu juu ya uendeshaji wa zoezi hili.
Ardhi na Makazi
Mheshimiwa Spika;
Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kuboresha makazi ya watu. Sote tunafahamu kuwa makazi ni hitajio la msingi la binadamu. Lengo letu la kuboresha huduma za ardhi, nyumba na makazi limepata mafanikio makubwa. Tumepeleka huduma za utawala wa ardhi karibu zaidi na wananchi kwa kuanzisha Kanda nane za kusimamia upangaji, upimaji na utoaji hatimiliki. Uamuzi huu umepunguza lile tatizo la watu kuchelewa kupata hati miliki. Toka 2006 hadi sasa jumla ya hati 164,275 zimetolewa, vijiji 10,500 vimepimwa na kati yake vijiji 10,341 vimepatiwa hatimiliki.
Mheshimiwa Spika;
Tumetunga Sheria kwa ajili ya kuwezesha upatatikanaji wa mikopo ya ujenzi na ununuzi wa nyumba. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mikopo ya Nyumba (Mortage Finance) na Sheria ya Kutambua Milki ya Sehemu ya jengo haswa kwenye maghorofa (Unit Tittles Act) ya mwaka 2008. Sheria hizi kwa ujumla wake zimewezesha watu wengi zaidi kupata mikopo ya kujenga au kukarabati nyumba zao na kuwawezesha watu kupata umiliki wa sehemu ya jengo.
Mabadiliko hayo pia yamewezesha sekta ya nyumba kukua kwa kasi kubwa na majengo na nyumba za kisasa kujengwa katika kipindi cha miaka 10 hii. Dar es Salaam ya leo na ile ya 2005 ni tofauti kabisa. Shirika la Nyumba la Taifa, Wakala wa Nyumba za Serikali, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nayo imefanya uwekezaji mkubwa sana katika ujenzi wa nyumba katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa watumishi wa serikali kuwa na nyumba mwaka 2008 tulianzisha Mfuko wa Mkopo kwa watumishi wa umma ambao hadi sasa umetoa mikopo ya shilingi bilioni 5.4 kwa watumishi 1,169. Pia, tumeanzisha Kampuni ya Mikopo ya Nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma ambayo tayari imeanza kazi.
Mheshimiwa Spika;
Ninayo furaha kueleza kuwa makazi ya wananchi pia yameendelea kuwa bora. Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, inaonyesha kuwa idadi ya nyumba zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2002 hadi asilimia 65 mwaka 2012. Kwa lugha nyingine nyumba zilizoezekwa makuti na nyasi zimezidi kupungua. Haya ni mafanikio makubwa ya kutia moyo na hatua muhimu katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Utafiti
Mheshimiwa Spika;
Jambo lingine ambalo tumeliwekea msingi mzuri ni eneo la utafiti. Hili ndilo eneo ambalo ilitalivusha taifa letu kwenda katika maendeleo makubwa zaidi. Niliamua Serikali ichukue hatua za makusudi za kufufua shughuli za utafiti ambazo zilikuwa zinapita katika kipindi kigumu. Niliamua kuwa Serikali ianze safari ya kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utafiti. Tulianza na shilingi bilioni 10 na kuendelea kuongeza mwaka hadi mwaka na kufika shilingi bilioni 60 mwaka 2014, katika kipindi cha kujitahidi kufikia asilimia 1 ya bajeti ya Serikali na hatimaye asilimia 1 ya pato la Taifa kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kutumia kiasi hiki kidogo kilichopo wanasayansi wetu 344 wamepata ufadhili wa masomo ya shahada ya Uzamili na 173 wa shahada ya Uzamivu. Miradi 70 ya utafiti imefadhiliwa, kati ya hiyo 22 ni ya kilimo. Fedha hizi pia zimewezesha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kuanzisha viatamizi vya teknohama ambavyo vimewezesha vijana wetu kubuni na kuvumbua teknolojia zenye manufaa kwa maendeleo ya jamii na taifa. Wamezalisha ajira na kunufaisha watu wengi. Kampuni ya Max Malipo ni mfano mmojawapo mzuri wa matokeo mazuri ya viatamizi hivi.
Huduma za Jamii
Elimu
Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa mwaka 2005 nilisema kuwa, “Hakuna Taifa lililopata maendeleo bila kuendeleza elimu. Hivyo kuendeleza elimu nchini itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne”. Tumetimiza ahadi. Katika kipindi chote cha miaka kumi bajeti ya sekta ya elimu ndiyo iliyokuwa kubwa kuliko za sekta nyingine zote. Mwaka huu 2015 bajeti ya elimu imefikia shilingi trilioni 3.4 ikilinganishwa na shilingi bilioni 669.5 za mwaka 2005.
Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu ndani ya miaka 10 hii ni ya kutia moyo. Tumeongeza shule za msingi kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015 na wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892. Upanuzi huu umewezesha asilimia 98 ya watoto wanostahili kupata elimu ya msingi sasa kuandikishwa.
Kwa kushirikiana na wananchi na sekta binafsi tumeongeza Shule za Sekondari kutoka Shule 1,745 mwaka 2005 hadi Shule 4,753 mwaka 2015. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,804,056 mwaka 2015. Katika kipindi hiki pia vyuo vya Ufundi vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015 na wanafunzi katika vyuo hivyo wameongezeka kutoka 40,059 hadi 145,511 mwaka 2015. Haya ni mafanikio makubwa sana.
Kwa nia ya kuongeza ubora wa elimu, tumechukua hatua thabiti za kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, maabara za sayansi na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Tumepanua mafunzo ya ualimu wa Cheti, Stashahada na Shahada. Hii imetuwezesha kuongeza idadi ya walimu wa Shule za Msingi kutoka 135,013 mwaka 2005 hadi 202,752 mwaka 2015, na walimu wa Shule za Sekondari kutoka 18,754 mwaka 2005 hadi 88,908 mwaka 2015. Uhaba wa walimu wa masomo ya sanaa si tatizo tena, tunao wa kutosha. Tuna upungufu wa walimu 20,141 wa masomo wa sayansi na hisabati. Ninaamini, hata hivyo, kwa programu za kusomesha walimu wa sayansi vyuoni zilizopo, katika miaka michache ijayo tatizo hili nalo tutalipatia ufumbuzi. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dodoma, mwaka 2014 kimeanza kudahili wanafunzi 5,000 wa ualimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa maabara za sayansi, katika shule za sekondari za kata tayari maabara 5,979 zimejengwa na nyingine 4,410 ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Hivi sasa tunashughulikia upatikanaji na usambazaji wa vifaa kwa matumizi ya maabara hizo. Kwa upande wa vitabu tumeweza kuboresha upatikanaji wake kwa mwanafunzi wa Shule za Msingi kutoka uwiano wa 1:5 mwaka 2005 hadi 1:3 mwaka 2015. Katika shule za sekondari uwiano ni 1:2 ukilinganisha na 1:8 mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki pia tumeshuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu nchini. Idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kutoka vyuo 26 mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015. Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma na cha Nelson Mandela cha Arusha ambavyo vimejengwa na Serikali ya Awamu ya Nne. Tumeanza mchakato wa kujenga Chuo Kikuu cha Julius Nyerere cha Kilimo kule Butiama. Vyuo hivi ni fahari ya nchi yetu kwani tumevijenga kwa fedha zetu wenyewe bila msaada kutoka kwa wafadhili. Ongezeko la vyuo vikuu limefanya idadi ya wanafunzi kuongezeka kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi 218,959 mwaka 2014. Idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo nayo imeongezeka kutoka wanafunzi 16,345 mwaka 2005 hadi wanafunzi 99,590 mwaka huu.
Afya
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa kuboresha na kupanua huduma ya afya nchini. Tuliazimia kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu kwa kujenga vituo vya kutoa huduma ya afya vipya na kuimarisha vilivyopo. Kati ya mwaka 2005 na 2014 vituo vya kutolea huduma za afya 2,175 vimejengwa. Kati yake hospitali 19, vituo vya afya 168 na zahanati 1,883 zimejengwa.
Tumeimarisha hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Wilaya kwa kuzipatia vifaa vya tiba na uchunguzi (MRI, CT Scan, X ray, Ultra Sounds, Maabara n.k). Tumejenga maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ambayo inatumika kama maabara ya Kimataifa ya Rufaa kwa nchi za SADC. Tumeimarisha maabara za mikoa kwa majengo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa. Maabara yetu ya Mbeya sasa ina uwezo wa kubaini virusi vya Ebola jambo ambalo miezi michache iliyopita tulikuwa tunapeleka sampuli Nairobi. Hivi sasa hospitali za wilaya zinaweza kufanya uchunguzi wa mwenendo wa figo na ini.
Mheshimiwa Spika;
Tumeboresha huduma ya Afya ya Kinywa katika Hospitali ya Muhimbili kwa kufunga mashine 26 za kisasa za tiba ya meno na maabara ya kisasa ya kutengeneza meno bandia. Pia tumeimarisha huduma ya afya ya kinywa kwa kuweka vifaa vya tiba ya meno kwenye Halmashuri 91. Hivi sasa hospitali 136, vituo vya afya 63 na zahanati 3 zinatoa huduma hiyo nchini.
Tumeanza kupata mafanikio katika dhamira yetu ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kuchunguza na kutibu maradhi ya figo, moyo, saratani na mishipa ya fahamu ambayo tumekuwa tunapeleka wagonjwa wengi nje. Kwa mfano, tangu Taasisi ya Moyo ianze kutoa huduma pale Muhimbili wagonjwa 71,963 wamepatiwa matibabu wakiwemo 692 waliofanyiwa upasuaji. Watu hao wangepelekwa nje taifa lingelipa pesa nyingi. Uwezo wetu utaongezeka sana hospitali ya Mloganzila itakapokamilika.
Mheshimiwa Spika;
Tumebadilisha utaratibu wa kusambaza dawa kutoka Bohari ya Dawa. Tumeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka shilingi bilioni 40.6 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 147 mwaka 2014. Idadi ya watu wanaonufaika na Mfuko wa Afya ya Jamii na Mfuko wa Bima ya Afya wameongezeka kutoka asilimia 3 mwaka 2005 hadi asilimia 19 mwaka 2014.
Katika kipindi hiki tumetoa msukumo mkubwa katika kupambana na maradhi makubwa ya kuambukiza yanayosababisha vifo vya watu wengi. Tumeendesha kampeni ya kupambana na malaria nchi nzima kwa kubadilisha dawa ya kutibu malaria na kugawa vyandarua 26,371329 kwa watoto chini ya miaka mitano, kwa akina mama wajawazito na katika kila kaya. Aidha, tumepulizia dawa ya kuua mbu ndani ya nyumba katika mikoa ya kanda ya ziwa. Matokeo ya jitihada hizo ni kupungua kwa maambukizi ya malaria kwa asilimia 51 na vifo kwa asilimia 71. Baada ya kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu pale Kibaha kuanza uzalishaji, safari ya kutokomeza malaria hapa nchini ni ya uhakika.
Mheshimiwa Spika;
Juhudi zetu katika kupambana na ukimwi zimewezesha kushuka kwa maambukizi ya ukimwi kutoka asilimia 7.7 mwaka 2005 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012. Idadi ya watu waliopima virusi vya ukimwi imeongezeka kutoka 365,189 mwaka 2005 hadi 25,468,564 mwaka 2014. Aidha, tumewezesha vituo 5,244 na asilimia 97 ya vituo vyote vinavyotoa huduma ya uzazi kutoa huduma ya kuzia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mheshimiwa Spika;
Kati ya mwaka 2005 na 2014 tumeongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya afya kutoka 3,025 mwaka 2005 hadi 11,807 mwaka 2014. Katika kipindi hicho wataalamu wa afya 55,608 wameajiriwa. Aidha, tumeongeza ajira ya kada mbalimbali za afya. Kwa sababu hiyo idadi ya madaktari imeongezeka kutoka madaktari 1,048 mwaka 2006 hadi madaktari 2,325 mwaka 2014. Halikadhalika, madaktari wasaidizi wameongezeka kutoka 1,223 hadi 1,914, wauguzi kutoka 15,961 hadi 22,942 wataalamu wa Maabara kutoka 1,277 hadi 2,378 mwaka 2014. Hivi sasa uwiano wa Daktari kwa wagonjwa ni 1:6,666 ikilinganishwa na 1:35,714 mwaka 2005. Na, uwiano wa Muuguzi kwa wagonjwa umeshuka kutoka 1:2,347 mwaka 2005 hadi 1:2,008 mwaka huu.
Mheshimiwa Spika;
Tumeendesha kampeni ya kuboresha lishe nchini na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Lishe (2011-2016). Kwa ajili hiyo mwaka 2013 tulizindua Programu ya Uongezaji wa Virutubishi. Matokeo ya jitihada zetu hizo yameanza kuonekana. Udumavu umepungua toka asilimia 44 mwaka 2005 hadi asilimia 35 mwaka 2014 na uzito pungufu toka asilimia 17 hadi asilimia 13.
Kwa jumla juhudi zetu za kuboresha huduma ya afya zimezaa matunda ya kuridhisha. Wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka toka miaka 49 mwaka 2005 hadi miaka 62 hivi sasa. Vifo vya watoto wachanga vimepungua toka vifo 68 kwa kila vizazi hai 1000 hadi vifo 21 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2014. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 112 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2005 hadi vifo 54 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2014, na vifo vya akinamama wajawazito vimepungua toka vifo 578 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 432 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2012. Haya ni mafanikio ya kutia moyo ingawaje bado tunatakiwa kuendeleza juhudi zaidi mara dufu ili vifo vipungue zaidi na zaidi.
Maji
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Nne imefanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama na usafi wa mazingira katika kipindi hiki. Tumekamilisha miradi ya maji katika miji mikuu ya mikoa 8, Wilaya 6 na Miji midogo 2. Aidha, miradi katika miji mingine 13 ya mikoa, 27 ya Wilaya na Miji midogo inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa miradi hii umewezesha kiwango cha upatikanaji maji mijini kufikia wastani wa asilimia 86 kwa mwaka 2014 kutoka asilimia 73 mwaka 2005. Na kwa Vijijini imefikia asilimia 67.6 Mwaka 2014 ukilinganisha na asilimia 53 mwaka 2005. Tumevuka lengo letu la kuwapatia maji asilimia 65 ya wakazi wa vijijini.
Aidha, miradi inayoendelea kutekelezwa hivi sasa itakapokamilika katika mwaka huu wa fedha upatikanaji wa maji mijini utafikia asilimia 90 ambalo ndilo lengo la Ilani ya uchaguzi ya CCM. Vijijini inaweza kufikia asilimia 70 ambayo ni juu ya lengo la asilimia 65.
Aidha, tumeboresha huduma za uondoaji wa maji taka katika miji ya Tanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Songea, Tabora na Morogoro. Uboreshaji huu wa huduma za utoaji wa maji taka ni mwanzo mzuri katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na mipango mizuri ya maji taka mijini.
Uwezeshaji wa Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ilikuwa ni moja ya dhima kuu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Katika kutekeleza dhamira hii, Serikali imeendeleza kwa mafanikio makubwa mifuko ya kutoa mikopo kwa vijana, wanawake, wajasiriamali wadogo na kuanzisha fursa nyingine mpya. Watu wengi wamenufaika na wao wenyewe kuwa chachu ya kuzalisha ajira, kupunguza umasikini na kuinua hali za maisha ya watu walioguswa na fursa zilizopatikana.
Tumeiwezesha Benki ya Wanawake kuanza na kuendelea kutoa huduma. Kama mjuavyo niliamua Serikali ichangie mtaji wa mwanzo na inaendelea kuchangia mtaji huo. Tayari Benki hiyo imeshakopesha watu 125,000 na kati yao wanawake ni asilimia 82. Hali kadhalika, nilifanya uamuzi wa makusudi wa kuifufua Benki ya Rasilimali (TIB). Dhamira yangu ni kutaka iwepo Benki ya maendeleo itakayotoa mikopo ya muda mrefu na wa kati kwa wawekezaji wazawa. Hii itawezesha kuanzisha na kuendesha shughuli za viwanda, madini, utalii na biashara kwa urahisi.
Tumeiwezesha Benki ya Rasilimali kwa mtaji, rasilimali watu na vitendea kazi na kuifanya iwe moja ya benki ya kutumainiwa nchini. TIB imeshatoa mikopo kwa makampuni 365 yenye thamani ya shilingi bilioni 512. Aidha, imetoa mikopo kwa miradi 201 yenye thamani ya shilingi bilioni 156 kupitia dirisha dogo la kilimo. Natoa pongezi maalum kwa viongozi na watumishi wa Benki ya Rasilimali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya katika kipindi hiki kifupi. Naomba waendelee na moyo huo kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika;
Tumetimiza ahadi yetu ya kuimarisha ushirika nchini kama nguzo kuu ya kuunganisha nguvu za wanyonge kujiletea maendeleo. Katika kipindi hiki, idadi ya Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali nchini imeongezeka kutoka 5,832 mwaka 2005 hadi 9,604 mwaka 2015.
Kwa upande mwingine, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), vimeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka vyama 1,875 mwaka 2005 hadi 5,559 mwaka 2014. Akiba, hisa na amana za wanachama zimeongezeka kwa zaidi ya mara tano kutoka Shilingi bilioni 85.6 mwaka 2005/2016 hadi Shilingi 463 bilioni mwaka 2014 na mikopo kwa wanachama imekua mara 13 toka shilingi bilioni 65.7 hadi shilingi bilioni 893 mwaka huu. Kwa hakika haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia. Watu wengi wamewezeshwa kupunguza umasikini wao na wengine kuondoka katika lindi la umasikini.
Sanaa na Michezo
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi kusaidia kukuza michezo na sanaa nchini. Kwa upande wa michezo niliahidi kuwa Serikali italipia makocha. Nilitimiza ahadi yangu kwa michezo ya soka, netiboli na ngumi. Kwa upande wa riadha tuliwapeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa. Timu yetu ya taifa ya soka haijafanya vizuri sana. Kwa upande wa soka tulianza kupata matumaini lakini baadae yakafifia. Timu yetu ya taifa ya soka haijafanya vizuri sana pamoja na kubadili makocha. Hata vilabu vyetu pia havifanyi vizuri. Kwa kweli lazima Watanzania tukae chini na kujiuliza kwa nini hatufanyi vizuri na tufanye nini tufanikiwe.
Mheshimiwa Spika;
Nilifanya uamuzi wa kurejesha michezo mashuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA). Nia yetu ni kutaka vipaji vya michezo vya vijana viibuliwe wakiwa bado wadogo na kuendelezwa. Uamuzi huu umerejesha uhai na matumaini kwamba siku za usoni tutaona matunda yake.
Kwa dhamira hiyo hiyo, kwa kushirikiana na Kampuni ya Symbion Power na Klabu ya Soka ya Sunderland kituo cha kuandaa wanamichezo wadogo kinajengwa pale Kidongo Chekundu, Dar es Salaam. Kituo hiki kinatarajiwa kuwa tayari ifikapo mwezi Septemba, 2015. Kikitumiwa vizuri huenda ikawa ndiyo mwanzo wa safari ya uhakika ya kuendeleza soka hapa nchini. Tukifanikiwa Kidongo Chekundu, vituo vingine kama hivyo vinaweza kuanzishwa sehemu nyingine nchini na wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya kuridhisha kwa upande wa sanaa za filamu na muziki. Vijana wetu wa tasnia hizi wamekuwa wanafanya vizuri kiasi kwamba leo hii Bongo Flavor na Bongo Movie zimevuka mipaka ya Tanzania. Zinaitangaza sanaa ya Tanzania, lugha ya Kiswahili pamoja na nchi yetu. Vijana hawa wameitoa kimasomaso Tanzania na kutufutia unyonge tunaopata kwenye michezo. Tasnia hizi zimeajiri vijana wengi, wanalipa kodi na wanasaidia sana katika kuhamasisha na kufikisha ujumbe kwa mambo muhimu katika jamii.
Mheshimiwa Spika;
Kwa nia ya kutaka kuendeleza ujuzi, mbinu na maarifa kwa wasanii wetu mwaka wa jana niligharimia timu ya watu wazoefu wa fani za muziki na filamu kutoka Marekani kuja nchini kutoa mafunzo ya muda mfupi. Ninafanya mipango waje tena kwani mafunzo ya mara kwa mara yatawaimarisha wasanii wetu.
Kwa wasanii wa muziki niliwatimizia maombi yao ya kutaka kuwa na mastering studio. Kwa wote nimefanya jitihada kubwa ya kutafuta majawabu kwa tatizo sugu la kupata malipo ya haki kwa kazi wazifanyazo. Tumetunga Kanuni ambazo zimewezesha kazi za wasanii kutambuliwa na kulindwa. Halikadhalika, tumeweza kuanza utaratibu mpya wa kusambaza kazi za wasanii ambapo wao wenyewe wana sauti nazo. Nitajitahidi katika kipindi kifupi kilichobaki niyasukume kwa kasi masuala yaliyosalia ili niwaache wasanii wetu mahali pazuri. Nataka wapate malipo ya haki kwa vipaji vyao na jasho lao ili wainue hali zao za maisha.

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
Wakati nalihutubia Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba 2005 niliahidi kwamba Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania inakuwa na uhusiano mzuri na mataifa mengine duniani, na mashirika ya kimataifa na kikanda. Leo, miaka 10 baadae napenda kuwahakikishia kuwa ahadi yetu tumeitekeleza, tena vizuri kuliko tulivyotegemea. Tanzania ni rafiki wa kila nchi na kila shirika la kanda na kimataifa. Hadhi yetu katika uso wa kimataifa imepanda sana. Tunaheshimiwa, tunasikilizwa, tunathaminiwa na kuaminiwa na mataifa makubwa na madogo.
Katika kipindi hiki tumetembelewa na wageni wengi mashuhuri kutoka mabara yote. Tumeweka historia kwa kutembelewa mfululizo na Marais wawili wa Marekani yaani Rais George W. Bush mwaka 2008 na Rais Barack Obama mwaka 2013, na Marais wawili wa China Rais Hu Jintao mwaka 2009 na Rais Xi Jinping mwaka 2013. Pia tulitembelewa na Wafalme, Marais, Mawaziri Wakuu na Mawaziri kutoka nchi za Mabara yote duniani. Aidha, tumetembelewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Benki ya Dunia n.k.
Tumeshirikishwa katika shughuli nyingi na mikutano mingi. Nimepata fursa ya kushiriki katika mikutano mbalimbali ya kimataifa pamoja na miwili ya G8 kuwakilisha Afrika. Nimewahi kushiriki na kupewa dhamana ya uongozi katika kamati na Tume kadhaa za Afrika na dunia. Nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (2008), Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Mjumbe wa Danish Africa Commission, Mwenyekiti wa ALMA. Hivi karibuni nimeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Mataifa Kupendekeza Namna Bora kwa Dunia Kushughulikia Majanga ya Afya.

Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumefungua Balozi mpya 5 katika nchi za Oman, Malaysia, Brazil, Uholanzi na Comoro. Hii inafikisha idadi ya Balozi zetu kuwa 35. Pamoja na ufinyu wa bajeti jitihada zimekuwa zinafanyika kuboresha huduma kwa Balozi zetu na wanadiplomasia wetu. Tumejenga jengo la Ubalozi New Delhi na kununua majengo ya ofisi ya kitega uchumi Washington DC, New York na Ufaransa. Tumeanzisha Kurugenzi ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni katika maendeleo ya nchi yetu.
Ushirikiano wa Kanda
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imeendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha na kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Katika miaka 10 hii tumefanikiwa kukamilisha utekelezaji wa Umoja wa Forodha tarehe 1 Januari, 2010 na tarehe 1 Julai, 2010 tulianza utekelezaji wa Soko la Pamoja ambao unaendelea hivi sasa. Tumetia saini Itifaki ya Umoja wa Sarafu Novemba 2013 ambayo utekelezaji wake unaendelea vizuri. Matunda ya utekelezaji wa utengamano kiuchumi yameanza kuonekana. Kwa mfano, mauzo yetu katika soko la Afrika Mashariki yameongezeka kutoka bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 161 mwaka 2005 hadi bidhaa za Dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2014. Uwekezaji nchini Tanzania kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki umeongezeka toka miradi 35 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 39.5 hadi miradi 244 yenye thamani ya Dola za Marekani milion 676.5. Haya yote ni mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC). Tumeendelea kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli za umoja huo. Tumeshiriki kwenye kutafuta suluhisho la Visiwa vya Comoro, Madagascar, Zimbabwe na DRC.
Salamu za Kuaga
Mheshimiwa Spika;
Tulipanga kufanya mengi na tumefanikiwa mengi, lakini hatukuweza kuyamaliza yote kwa sababu ya changamoto mbalimbali na kubwa zaidi ni uhaba wa rasilimali fedha na wakati mwingine rasilimali watu na vitendea kazi. Hata hivyo tumeweza kutekeleza zaidi ya asilimia 88 ya ahadi zetu zilizomo kwenye Ilani za Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na mipango ya Serikali.
Siku moja nikiwa Marekani mwandishi mmoja wa habari aliniuliza, je, utakapomaliza uongozi wako utapenda Watanzania wakukumbuke kwa lipi? Nikamjibu, nitapenda Watanzania waseme, “Rais Kikwete alitukuta kuleee! na sasa anatuacha hapa palipo juu”. Mimi na ninyi ni mashahidi kuwa tulipo leo ni bora zaidi ya kule tulipokuwa jana.
Changamoto za nchi haziishi kila siku zinaibuka mpya. Kila ukimaliza moja inazaa changamoto nyingine. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa baba wa taifa ambaye naye hakumaliza changamoto zote, ndivyo ilivyokuwa kwa Mzee Mwinyi na hivyo ndivyo alivyoniachia Rais Mkapa. Nami namwachia anayekuja, naye afanye yake na yatakayobakia atamwachia atakayemfuatia. Jambo linalonipa faraja ni kuwa nami nimetoa mchango wangu kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Shukrani
Mheshimiwa Spika;
Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipokushukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Ghalib Bilal kwa msaada wako, ushauri wako na ushirikiano wa karibu ulionipatia katika kipindi hiki cha miaka 5. Nakutakia kila la heri katika maisha yako baada ya mimi na wewe kumaliza kipindi chetu cha uongozi. Namshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kipindi changu cha kwanza. Nakushukuru kwa ushirikiano wako mkubwa, msaada wako na ushauri wako wa hekima na busara ambao umewezesha mafanikio tuliyoyapata katika kujenga nchi yetu na katika kuimarisha muungano wetu.
Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda, Waziri Mkuu na Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni kwa kazi nzuri na ya kutukuka uliyoifanya katika kipindi cha miaka 8. Umepita katika misukosuko mingi, na wakati mwingine umebebeshwa lawama isiyokuwa yako. Daima umeonyesha ukomavu, uimara na kutotetereka. Napenda pia kumtambua Mheshimiwa Edward Lowassa ambaye katika kipindi kifupi alichokuwa Waziri Mkuu alifanya kazi kubwa na nzuri.
Nawashukuru pia Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji na watumishi wote wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa mchango wao katika kufanikisha majukumu ya Awamu ya Nne. Mmenisaidia sana. Kwa kweli mafanikio haya tunayozungumza leo yameletwa na juhudi zenu.
Nawashukuru viongozi wa dini, asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa kuniunga mkono mimi na Serikali yangu na kwa mchango wenu muhimu. Nawaomba muendelee kuilea amani ya nchi yetu na watu wake.
Nakishukuru Chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini, kuniunga mkono na kunisaidia kwa karibu, katika miaka yote hii kumi. Wakati wote CCM imekuwa pamoja nami na Serikali. Kimetoa uongozi wa nchi na kuisimamia Serikali kutekeleza Ilani.
Mwisho lakini sio mwisho wa umuhimu, naishukuru sana familia yangu. Namshukuru mke wangu Bi. Salma Kikwete kwa mchango wake mkubwa ulionipa utulivu wa kutekeleza majukumu yangu. Upo msemo kwamba, “kwa kila mwanaume mwenye mafanikio, yuko mwanamke”, nawaambia ni kweli. Shukrani zangu, pia, kwa wanangu na wajukuu zangu kwa kunivumilia pale walipomkosa baba yao na babu yao. Karibuni mambo yatakuwa tofauti mtaniona mara kwa mara kiasi kuwa huenda mkanichoka.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Ninapoagana na Bunge letu natambua kuwa baadhi ya Wabunge mnarudi kutetea viti vyenu nawatakia kila la kheri. Nimewahi kuwa Mbunge, hivyo naelewa hofu na mashaka mliyonayo. Mwenyezi Mungu awape utulivu na subira. Nawatakia mapumziko mema kwa wale ambao mmeamua kustaafu. Wale wanaogombea Urais waliomo humu nawatakia kila la kheri, na nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu.
Kwa ndugu zangu Watanzania wenzangu, nawashukuruni kwa kuniamini na kunichagua mara mbili kuwa kiongozi wa nchi yetu. Nawashukuru kwa kuniunga mkono wakati wote wa uongozi wangu. Mmenipa heshima kubwa ambayo sitakaa nisahau maishani mwangu. Ninamaliza kipindi changu cha uongozi nikiwa nawapenda sana na nitaendelea kuwapenda mpaka siku Mwenyezi Mungu atakaponiita. Nitawa-miss kama mtumishi na kiongozi wenu mkuu lakini tutakutana kwa urahisi zaidi nikiwa raia. Baada ya hotuba yangu ndefu, sasa natangaza kuwa Bunge la 10 limevunjwa rasmi, lakini linabakia kuwa hai mpaka tarehe itakayotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Katiba.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza!