HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM, RAIS WA TANZANIA, DK. JAKAYA KIKWETE, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NANE WA UVCCM MJINI DODOMA OKTOBA, 23, 2012

Mkutano wa UVCCM ukiendelea

HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM, RAIS WA TANZANIA, DK. JAKAYA KIKWETE, KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NANE WA UVCCM MJINI DODOMA OKTOBA, 23, 2012

Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa;
Katibu Mkuu wa CCM;
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Nane wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Nakushukuru sana Kaimu Mwenyekiti na viongozi wenzako wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya Mkutano wenu. Nyota njema huonekana asubuhi. Bila ya shaka mambo yataenda vizuri na vijana watapata fursa ya kuchagua viongozi wao wanaowataka wao kwa ajili yao na kwa maslahi ya Jumuiya yao na ya Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Katika Ibara ya 5 ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi imeelezwa kuwa malengo na madhumuni ya CCM ni: “Kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Mitaa, Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Mitaa katika Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa pili“…
Kwa mujibu wa Ibara hiyo basi, sisi katika Chama cha Mapinduzi tunataka Mwenyekiti wa Kitongoji awe wa CCM, Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji awe wa CCM, Serikali ya Mtaa au Kijiji iwe ya CCM, Diwani awe wa CCM, Halmashauri ya Wilaya au Mji iwe ya CCM, Mbunge au Mwakilishi awe wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar wawe wa CCM na Serikali zetu mbili ziwe za CCM.
Ndugu Mwenyekiti;
Tunapozungumzia Serikali tangu ngazi ya vitongoji mpaka taifa kuwa ni ya CCM, tunazungumzia kushinda katika uchaguzi katika ngazi hizo. Tena basi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi tuna maana ya CCM kupigiwa kura nyingi zaidi na wananchi kuliko vyama vingine vya siasa vitakavyoshiriki. Kama mjuavyo, idadi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu imefikia 20 pamoja na CCM.
Ndugu Mwenyekiti;
Jumuiya za Chama cha Mapinduzi zimeundwa kuisaidia CCM kukubalika na kuungwa mkono na wananchi. Kila Jumuiya inapaswa kufanya kazi na makundi maalum katika jamii licha ya jukumu la jumla kwa watu wote wa Tanzania. Jumuiya ya Vijana imekabidhiwa kufanya kazi hiyo miongoni mwa vijana wa nchi hii popote walipo.
Ndugu wajumbe;
Chama cha Mapinduzi kinaitegemea Jumuiya yake hii kufanya kazi ya siasa miongoni mwa vijana wa Tanzania kuwashawishi wakubali kuwa wanachama na wapenzi wa CCM. Na kubwa zaidi kuwafanya vijana waunge mkono, wapiganie na kuwapigia kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi nyakati za uchaguzi. Kwa muhtasari nasema kuwa Chama cha Mapinduzi ni Chama cha siasa kilichoundwa kwa ajili ya kukamata uongozi wa dola. Aidha, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ni chombo cha siasa kilichoundwa kukirahisishia na kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kutimiza malengo na madhumuni yake hayo kwa kupitia vijana.
Hayo ndiyo matumaini makubwa na ya msingi zaidi kuliko yote ya Chama cha Mapinduzi kwa Jumuiya yake hii. Pili, Jumuiya hii inalo jukumu la ulinzi na utetezi wa Chama cha Mapinduzi. Chama chetu hakina walinzi wengine zaidi ya UVCCM. Kwa ajili ya kutimiza majukumu hayo mawili hamna budi kujipanga vizuri kifikra na kimkakati kuijenga na kuiimarisha Jumuiya. Safari hiyo inaanzia kwenye kupata uongozi ulio bora. Hii ndiyo fursa mliyonayo leo, msiipoteze.
Kaimu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Hakikisheni kuwa mnapata Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na safu ya viongozi wazuri ambao wataiongoza vyema Jumuiya ya Umoja wa Vijana na kuiwezesha kutimiza ipasavyo malengo na madhumuni yake. Viongozi watakaoongoza juhudi za kuendeleza, kutetea na kulinda maslahi ya Chama chetu kupitia kwa vijana. Viongozi watakaoiwezesha CCM kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Kumbukeni kuwa mnachagua viongozi wa kuongoza Jumuiya yenu kwa miaka mitano ijayo. Mkifanya kosa sasa mtalijutia kwa miaka mitano ijayo. Majuto ni mjukuu. Hivyo, hamna budi kuwa makini kwa kuwachagua viongozi wanaofaa kupewa dhamana hiyo nzito. Kwa kuwa ninyi wenyewe mnajuana, natumaini hamtafanya ajizi.
Chagueni viongozi wanaoijua na kuipenda Jumuiya na wenye mapenzi ya dhati kwa Chama cha Mapinduzi. Viongozi waaminifu, waadilifu na wachapakazi hodari. Watu mtakaokuwa nao wakati wa jua na mvua na kuwavusha kuwapeleka kwenye neema na mafanikio. Chagueni watu kwa kufaa kwao na sio kwa urafiki wenu au kufadhiliana.
Jambo muhimu la kuzingatia msimchague mtu anayetoa rushwa, mtu anayewarubuni kwa ahadi za uongo. Nawasihi vijana wakataeni watu hao, wanyimeni kura zenu. Anayetoa rushwa na ahadi za uongo hafai, hana uwezo wa kuongoza, hafai kupewa nafasi ya uongozi. Vijana lazima muongoze kukitoa Chama chetu kwenye taswira ya rushwa.
Ndugu Wajumbe;
Chagueni mtu anayeweza kuiongoza vyema Jumuiya ili itimize ipasavyo wajibu na majukumu yake kwa maslahi ya vijana wa Tanzania. Chagueni mtu atakayewavuta vijana wote wa mijini na vijijini, wasomi na wasio wasomi waitumainie UVCCM kama chombo chao, kimbilio lao, nguzo yao, mpiganaji na mkombozi wao. Mtu atakayewaunganisha vijana wa Tanzania badala ya kuwatenganisha. Na, mwisho mtu mtakayemchagua awe na uwezo wa kuiimarisha Jumuiya yenu ili ipate mafanikio zaidi kuliko yaliyopatikana sasa.
Ndugu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Mkimaliza uchaguzi jipangeni vizuri kutimiza wajibu wenu kwa wanachama wenu, kwa Chama cha Mapinduzi chenye Jumuiya yake. Jengeni na imarisheni Jumuiya yenu kwa kina, marefu na mapana yake. Kazi yenu ya awali katika kufanya hayo ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na kati ya viongozi na wanachama na miongoni mwa wanachama. Katika historia ya Chama chetu na mila na desturi ya demokrasia ndani ya Chama, uchaguzi ndiyo njia tunayoitumia kupata viongozi. Kwa kweli ni njia bora kuliko zote na haina badala yake. Lakini, ina hatari zake na iliyo kubwa ni ile ya kusababisha mgawanyiko au hata mpasuko miongoni mwa wanaogombea, wapenzi wao na miongoni mwa viongozi na wanachama wa Jumuiya, Chama na hata jamii.
Kwa kutambua ukweli huo, ndiyo maana nawakumbusha kuwa mara unapomalizika uchaguzi, msisahau kazi ya kuziba nyufa na migawanyiko iliyotokana na uchaguzi. Kazi hii muipe kipaumbele cha juu ili mpate utulivu utakaowapa fursa ya kupanga na kutekeleza mipango ya kujenga na kuimarisha Jumuiya.

Ndugu Mwenyekiti;
Naomba mambo matatu kwenu. La kwanza, msisahau msemo wa wahenga usemao “asiyekubali kushindwa si mshindani”. Nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti ni moja na kwamba atashinda mmoja tu na wawili hawatapata. Kila aliyegombea ana imani au anatumaini kuwa yeye atakuwa ndiyo huyo mshindi. Lakini, atambue pia kuwa anaweza kuwa miongoni mwa wale wawili ambao hawatabahatika. Ajiandae hivyo na wapenzi wake nao wajiandae hivyo pia. Bahati mbaya sana wengi wetu tunaogombea na hata wanaotuunga mkono hatuko tayari kufikiria hivyo. Tunafikiria kushinda tu na hivyo tunaposhindwa tunapata taabu kukubali ukweli huo na wengine hufikia kufanya mambo yasiyostahili. Kukataa matokeo na baya zaidi kufanya vurugu au kutishia au hata kuondoka kundini.
Ndugu Mwenyekiti;
Napenda kutumia nafasi hii kuomba (na hili ndilo ombi langu la pili), kuwa muwe na moyo wa ustahamilivu na ukomavu wa kisiasa. Muwe na moyo mpana wa kukubali matokeo hata yale yasiyopendeza. Lazima ukubali kuwa mmoja wenu tu atapata na wawili watakosa na kati ya hao unaweza kuwa wewe wa kupata au kukosa. Kubali ukweli huo na songa mbele kujenga Jumuiya yako na kupigania Chama chako kwa mapenzi yale yale yaliyokufanya ujitokeze kuomba kukitumikia.
Ndugu Wajumbe;
Mtu mwenye mapenzi ya dhati na Jumuiya yake na Chama chake hatanuna au kufanya vitendo vya hujuma ati kwa sababu tu yeye kashindwa uchaguzi. Hataamua kuzamisha au kuacha jahazi lizame kwa sababu hakuchaguliwa. Akifanya hivyo yeye si muumini wa dhati, ni mwanachama cheo. Akikosa hana hamu tena na Chama chenu. Ninaposema hayo, nisieleweke kuhalalisha watu kufanyiwa dhuluma au hata rushwa. Lakini hata ikiwa hivyo zipo taratibu zake za kufuatwa.

Ndugu Mwenyekiti;
Ombi langu la tatu kwenu ni kuwataka nyote mtambue kuwa kugombea ni haki ya kila mwanachama wa Jumuiya, tena ipo kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Jumuiya. Kila baada ya miaka mitano uchaguzi hufanyika, hivyo, hakuna sababu ya kumchukia mwanachama aliyejitokeza kugombea. Pia si dhambi kwa mwanachama kumuunga mkono au kumpigania mgombea ye yote anayemuona yeye anafaa. Ni haki yake ya msingi.
Ukimchukia au kumuona adui mtu aliyeamua kugombea nafasi unayogombea au kutokukuunga mkono wewe katika uchaguzi na akamuunga mkono mgombea mwenzako, unadhihirisha una upungufu mkubwa wa maadili ya kidemokrasia. Siyo mtakuwa hamuwatendei haki wenzenu bali pia mtakuwa mnathibitisha kuwa hamtoshi. Mnaonesha kuwa ni watu wabinafsi wa hali ya juu, wenye tabia ya kujikweza isivyostahili na wapenda makuu na kuabudiwa.
Ndugu Wajumbe;
Watu wa aina hiyo watakuwa viongozi wa makundi na ni wenye kulipiza visasi. Na, kwa tabia hiyo ukishashindwa au hata ukishinda, Chama au Jumuiya itakuwa na mifarakano na misuguano isiyoisha. Narudia kuwaomba na kuwakumbusha kuwa lazima muoneshe ukomavu wa kisiasa, na kwa ajili hiyo muwe wavumilivu na watulivu hata pale mambo yakienda msivyotaka yawe.
Uchaguzi ukiisha nyote mshikamane na mshirikiane kujenga Jumuiya yenu. Wale watakaoshinda ndiyo waongoze njia kuwajumuisha wenzao. Mkishinda, msigeuze Jumuiya mali ya walioshinda. Hii ni Jumuiya ya wote, walioshinda na walioshindwa. Msiwatenge, hawana Jumuiya yao nyingine. Na, watakaoshindwa wawe mfano wa kuwa tayari kufanya kazi na wenzao. Tukumbuke rai ya wahenga “yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo”
Kaimu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Mkiziyangatia hayo, naamini mtatoka kwenye uchaguzi huu mkiwa na nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya ya kutimiza wajibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM. Moja ya jukumu la msingi la UVCCM ni kufanya kazi ya siasa miongoni mwa vijana wana-CCM na hasa wasiokuwa wana-CCM. Lengo likiwa kuwafanya wakubali kuiunga mkono CCM. Kwa ajili hiyo, ningependa kuona Jumuiya yetu inajishughulisha zaidi na changamoto zinazowakabili vijana wa Tanzania. Napenda kuona UVCCM mkiwa mstari wa mbele kutambua na kuwasemea vijana mashuleni na vyuoni kwa matatizo na changamoto zinazowakabili. Napenda kuona UVCCM ikiwa mstari wa mbele kuwasemea na kuwatetea vijana wamachinga wapatiwe maeneo mazuri ya kufanyia kazi.
Napenda kuona Umoja wa Vijana wa CCM ukiwasaidia vijana wasanii kuendeleza vipaji vyao na kuwapigania wapate malipo ya haki kwa kazi zao wazifanyazo. Napenda kuona UVCCM wakiwa mstari wa mbele kuendeleza vipaji vya michezo ya vijana na kuwa karibu na vijana wana michezo. Aidha, napenda kuona Umoja wa Vijana ukijihusisha na masuala ya ajira kwa vijana. Wasemeeni kwa sauti kubwa lakini pia wasaidieni pale mnapoweza wapate ajira. Wasemeeni wanaotaka kujiajiri ili waweze kusaidiwa kujiajiri. Wasaidieni kwa kadri muwezavyo vijana wanaotaka kujiajiri waweze kutimiza ndoto zao.
Ndugu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Sina budi kutoa pongezi kwako na viongozi wenzako kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya ya kuwawezesha vijana kupitia Tanzania Youth Microfinance (TYM). Vijana wengi wamekuwa wananufaika kupitia SACCOS zao na vikundi vyao vya uzalishaji mali na huduma. Endelezeni juhudi zenu hizo mpaka TYM siku moja ije iwe Benki ya kutumainiwa siyo tu na vijana bali na watu wote. Mimi nawahakikishia kuendelea kuwaunga mkono kwangu na msaada wangu nitakaojaliwa. Nawaomba pia muendelee kuwahamiza vijana kujiunga na kuanzisha SACCOS. Ni mkombozi wao katika jitihada zao za kujikwamua kimaisha kama ilivyo kwa Watanzania wote.
Ndugu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa uongozi wa Umoja wa Vijana unaomaliza muda wake kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya ya kuijengea Jumuiya yenu uwezo wa kujitegemea. Nafurahi kwamba mmeendeleza kazi iliyoanzishwa na uongozi uliowatangulia wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi. Jengo sasa linaelekea kukamilika. Tena linapendeza sana na kumfanya Baba yenu CCM kuona fahari ya mafanikio yenu. Si hivyo tu mmempa baba changamoto ya kufikiria urefu na ubora wa majengo itakayoamua kujenga. Wakati nawapongeza kwa mafanikio haya, nawaomba muendeleze maradufu juhudi za uwekezaji. Fursa mnazo nyingi zitumieni.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa katika miaka mitano iliyopita, Jumuiya imezidi kuimarika na uwezo wa kiutendaji unaongezeka. Vilevile Jumuiya inazidi kupata umaarufu na kupendwa na vijana wengi zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Wanachama wapya wameongezeka sana. Siku hizi wasomi wengi wanajitokeza kuwa wanachama wa Jumuiya yenu na kuomba uongozi. Kwa kweli napata faraja kwamba hatma ya CCM ina matumaini.
Kilicho muhimu sasa ni kuimarisha safu ya uongozi wa vijana kwa kuwapatia mafunzo. Bahati nzuri Chuo cha Ihemi kipo. Nimezungumza na Katibu Mkuu Martin Shigela kuwa tengenezeni mpango kabambe wa kukarabati chuo na kukipanua. Nimemhakikishia kuwa nitawatafutia uwezo wa kufanya hivyo. Nataka Chuo cha Ihemi kiwe ndicho Chuo cha CCM na Jumuiya zake kwa ajili ya kutayarisha makada. Pia, kiwe kitovu cha kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama na Jumuiya zake.
Ndugu Mwenyekiti;
Chama kimeunda Jumuiya ya Vijana kuwa kama kikosi chake cha dafrau cha kuondoa vizuizi na kusafisha njia kwa CCM kupita na kupata ushindi. Tunategemea viongozi na wanachama wa UVCCM kukisemea, kukitetea na kukipigania Chama cha Mapinduzi kwa kauli zenu na matendo yenu. Hatutegemei muwe tofauti. Naomba uongozi mpya muyazingatie haya. Muangalie wenzenu walifanikiwa wapi na walikosea wapi. Imarisheni na endelezeni mafanikio yaliyopatikana na sahihisheni kasoro zilizojitokeza. Anzeni ukurasa mpya wa kujenga na kuimarisha UVCCM.
Ndugu Mwenyekiti;
Kabla sijamaliza hotuba yangu napenda kutoa rai moja kwenu. Nawaomba mhimize viongozi na wanachama wenu wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba watakapotembelea maeneo yao. Pia na nyie kaeni chini kama Umoja wa Vijana toeni mapendekezo yenu. Kilio kina mwenyewe. Mambo ya vijana wenyewe vijana. Hii ni fursa adimu na adhimu kwa vijana, kusema yao wanayoyataka yawemo katika Katiba yao. Wahamasisheni vijana wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao na nyie toeni yenu. Huu ndio wakati wake.
Kaimu Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe;
Natambua kwamba wengi wenu hivi sasa mnawaza kuhusu uchaguzi, hivyo kila ninavyoendelea kusema mnasema mioyoni huyu mzee atamaliza lini tumalize kazi. Naona sasa nimalize kwa kusema tena kwamba nawashukuru kwa kunialika. Sisi katika CCM tunayo matumaini na matarajio makubwa kwenu kwani tunajua mmelelewa vizuri katika Chama hiki chenye historia kubwa na chenye dhamana kubwa ya uongozi wa nchi yetu. Tunategemea mtaupa uzito unaostahili uchaguzi wenu ili tupate viongozi bora.
Hivyo nawaomba mtumie fursa ya Mkutano Mkuu huu wa Nane wa Taifa kuchagua Viongozi wa Jumuiya watakaokidhi matumaini yetu na yenu ya kutekeleza majukumu ya UVCCM na ya Chama cha Mapinduzi.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa natamka kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa UVCCM umefunguliwa rasmi. Nawatakia Mkutano mwema na uchaguzi mwema wenye mafanikio tele.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.