UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
1. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Tano wa Bunge lako Tukufu ulioanza tarehe 08 Novemba 2011. Tuna kila sababu ya kumshukuru kwa kuwa tumetekeleza majukumu yote yaliyopangwa kwenye Ratiba kwa Amani, Utulivu na Ufanisi Mkubwa. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kuwa, kwa pamoja tumefanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
2. Napenda nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo la Igunga kwa kura nyingi kupitia Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika tarehe 02 Oktoba 2011. Kuchaguliwa kwake kunadhihirisha imani kubwa waliyonayo Wananchi wa Igunga kwake na kwa Chama Cha Mapinduzi. Vilevile, kunadhihirisha kwamba Chama Cha Mapinduzi bado ni Chama imara, Chama cha Wakulima na Wafanyakazi na Chama chenye Mvuto Mkubwa kwa Watanzania. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mohammed Said Mohammed kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Muungano kupitia Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
3. Tangu tulipohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu, kumekuwa na matukio mbalimbali yaliyosababisha majeruhi na kupoteza maisha ya ndugu, jamaa na marafiki zetu. Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole wote walioathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na matukio hayo. Aidha, kwa wale waliopoteza maisha,
namwomba Mwenyezi Mungu aziweke Roho za Marehemu wote Mahali Pema Peponi. Amen. Kipekee, napenda kutumia nafasi hii pia kuwatakia kheri Waheshimiwa Wabunge wote ambao katika kipindi hiki wamepata misukosuko ya maradhi na baadhi yao bado wako Hospitalini Ndani na Nje ya Nchi kwa matibabu. Napenda kuungana na Familia zao kumwomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka na awape nguvu ya kurejea katika afya zao ili waweze kujiunga na Familia, Wapiga Kura wao na Watanzania wote kwa ujumla katika ujenzi wa Taifa letu.
Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu wa Tano, jumla ya Maswali ya Msingi 123 na ya Nyongeza 289 yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 8 ya Msingi na 5 ya Nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Miswada
Mheshimiwa Spika,
5. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Miswada ifuatayo:
i) Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2011 [The Public Procurement Act, 2011]; na
ii) Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 [The Constitutional Review Act, 2011].
Taarifa Mbalimbali
Mheshimiwa Spika,
6. Vilevile, katika Mkutano huu, zilitolewa Taarifa mbili ambazo ni Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini juu ya Uendeshaji wa Sekta Ndogo ya Gesi Nchini na Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge.
Kauli za Serikali
Mheshimiwa Spika,
7. Katika Mkutano huu pia, Serikali ilitoa Tamko kuhusu Fujo na Vurugu Zilizojitokeza hivi karibuni katika Mikoa ya Mbeya na Tabora.
8. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote walioshiriki katika Mijadala ya Miswada na Taarifa hizo.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya Tarehe 18 Novemba 2011
Mheshimiwa Spika,
9. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Hotuba aliyoitoa jana tarehe 18 Novemba 2011 katika Ukumbi wa Karume, Viwanja vya Mwalimu Nyerere – Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam. Mheshimiwa Rais amefafanua kwa kina maeneo muhimu yanayohusu Mwenendo wa Uchumi katika Nchi yetu, hususan Mfumuko wa Bei, Kushuka kwa Thamani ya Shilingi na kupanda kwa Bei ya Mafuta na Chakula katika Soko la Dunia. Vilevile, alielezea vizuri suala la matumizi ya Fedha za Kigeni katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali hapa Nchini.
10. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais, suala la Mdororo wa Kiuchumi uliopo na kupanda kwa Bei ya Mafuta na Chakula katika Soko la Dunia kumeathiri siyo Tanzania pekee, bali Nchi nyingi Duniani zikiwemo za Ulaya na Afrika, na hata jirani zetu. Ili kupata uelewa mpana kuhusu suala hili tumekubaliana kwamba Gavana wa Benki Kuu ataandaa Semina kuhusu masuala hayo itakayofanyika wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge ambapo tutapata fursa ya kujadili kwa kina hali ilivyo ya Mwenendo wa Viashiria vya Uchumi wa Nchi yetu athari zake na hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
11. Katika Hotuba yake, Mheshimiwa Rais alizungumzia pia kwa kina Mchakato wa Maandalizi ya Mabadiliko ya Katiba ambapo Bunge lako Tukufu limepitisha Muswada wa Sheria wa Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 jana tarehe 18 Novemba 2011. Ninaamini kwa dhati kabisa kuwa maelezo yale ya Mheshimiwa Rais yatatoa Majibu sahihi na uelewa wa pamoja kwa Watanzania wenzangu kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Uelewa huo wa pamoja, kwa maoni yangu, utatuwezesha Watanzania wote kujiandaa na kushiriki kwenye hatua zinazofuata katika Mchakato huo kwa Utulivu, Amani, Umoja na Mshikamano.
12. Kwa namna ya pekee, napenda kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa jinsi ulivyoongoza Mjadala huu. Ninawashukuru pia Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi walivyosimamia na kuongoza Mjadala pale ulipojadiliwa.
Mheshimiwa Spika,
13. Muswada tulioupitisha ulisimamiwa kwa umahiri mkubwa na Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge. Kwa moyo wa dhati naishukuru Kamati kwa kazi nzuri ya kuchambua na kutoa ushauri kwa Serikali na hivyo kuonesha njia iliyo bora katika kutekeleza jukumu hili muhimu tulilohitimisha jana. Kipekee, ninawashukuru Mheshimiwa Pindi Chana, Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati; na Mheshimiwa Anjellah Kairuki, Mbunge na Makamu Mwenyekiti wa Kamati kwa kuongoza na kusimamia mjadala wa kuandaa Muswada uliopitishwa jana na Bunge lako Tukufu. Hawa wote ni kina Mama na kina Mama wakipewa nafasi wanaweza.
14. Napenda pia kuchukua nafasi hii kuishukuru kwa moyo wa dhati kabisa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa iliyoutoa wakati wote wa uandaaji na Mjadal wa Muswada huo.
15. Napenda pia kuwashukuru Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani, Mbunge wa Ulanga Mashariki na Waziri wa Katiba na Sheria; na Mheshimiwa Jaji Frederick Mwita Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi chote cha maandalizi na Majadiliano ya Muswada huo. Ninawashukuru pia Watendaji wote wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa utaalam na ushirikiano mkubwa waliouonesha ambao uliwawezesha Viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
16. Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, Muswada huo ulipitiwa pia na Wasomi, Wanataaluma, Makundi mbalimbali ya Jamii na Wadau wengi ambao siyo rahisi kuwataja wote hapa. Itoshe tu kusema, Serikali inawapongeza Wadau wote kila moja kwa nafasi yake kwa namna walivyoshiriki katika kufanikisha mjadala wa Muswada uliopitishwa na Bunge lako Tukufu jana.
17. Kwa ujumla wenu mmeandika historia mpya katika kulitumikia Taifa letu kwa kufanikisha hatua ya Mwanzo na ambayo ninaamini ilikuwa ngumu katika kuelekea Uundaji wa Katiba Mpya. Katiba ambayo kama alivyosema Mheshimiwa Rais, itaendana na Mafanikio na Changamoto za Miaka 50 ya Uhuru, Miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Miaka 47 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ambayo italipeleka Taifa letu Miaka 50 mingine ijayo kwa Utulivu, Amani, Umoja na Mshikamano. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kujadili Muswada huo na hatimaye kuupitisha.
Kazi tuliyonayo mbele yetu ni kutekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais ameyaelekeza kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika hatua zinazofuata.
Mheshimiwa Spika,
18. Nitumie nafasi hii pia kuwaomba Watanzania wote kwamba sasa tuungane kwa pamoja kutekeleza hatua itakayofuata ambayo ni kutoa Maoni yetu kwa Tume itakayoundwa na Waheshimiwa Ma-Rais wetu wa pande zote mbili – Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, nawaomba Viongozi na Wanachama wa Vyama vyote vya Siasa kupongeza hatua iliyofikiwa na kukubali Muswada huu ambao tayari umepitishwa kwa maslahi ya Taifa letu.
Wito wangu kwa Wananchi wote ikiwa ni pamoja na Vyama vya Siasa ni kuungana kwa pamoja katika hatua muhimu inayokuja ambayo itahusisha Watanzania wote ya kutoa Maoni ya Katiba tunayoitaka. Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatia yale yote aliyotuasa Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ili hatua zote kueleza Katiba Mpya zifanyike kwa Amani na Utulivu. Kwa pamoja tutaweza kufikia lengo tulilojiwekea na kuandika historia mpya ya Nchi yetu.
HALI YA CHAKULA
Mheshimiwa Spika,
19. Nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na hali ya ukame wa mara kwa mara kwa muda mrefu, hususan tangu mwaka 2006. Hali hii imesababisha upungufu wa Chakula katika baadhi ya Mikoa ambayo imekuwa ikiathirika zaidi na ukame. Hata hivyo, Chakula ambacho kimekuwa kinazalishwa katika maeneo yenye Mvua za kutosha kimewezesha Nchi yetu kuendelea kujitosheleza kwa Chakula, kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, katika mwaka 2010/2011 uzalishaji wa mazao ya Chakula unakadiriwa kufikia Tani Milioni 12.81 ikilinganishwa na mahitaji ya jumla ya Tani Milioni 11.50 za Chakula kwa mwaka 2011/2012. Uzalishaji huu unatosheleza mahitaji ya Chakula kwa Asilimia 111, sawa na ziada ya Tani Milioni 1.31. Ziada hiyo kwa kiasi kikubwa inatokana na mazao yasiyo ya Nafaka. Hivyo, uhaba wa Nafaka ni kiasi cha Tani 410,000 Nchini kote na upungufu huo wa Nafaka upo zaidi kwenye baadhi ya Mikoa inayokabiliwa na ukame.
20. Tathmini ya kina ya hali ya Chakula na Lishe Nchini iliyofanywa mwezi Agosti na Septemba, 2011 inaonesha kuwepo kwa jumla ya Watu 1,062,516 katika Wilaya 52 za Mikoa 15 wanaokabiliwa na upungufu wa Chakula (Acute Food Insecurity) kwa viwango mbalimbali.
Wananchi hao wanahitaji Tani 38,843 za Chakula cha msaada kwa kipindi cha Miezi mitatu kuanzia Mwezi Oktoba hadi Desemba 2011. Hadi tarehe 31 Oktoba 2011, jumla ya Tani 13,905 za Chakula zilikuwa zimechukuliwa kutoka maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na kusambazwa katika maeneo hayo yenye uhaba wa Chakula, na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Spika,
21. Pamoja na jitihadi za Serikali za kupeleka Chakula cha Msaada katika maeneo yenye upungufu wa Chakula, natoa Wito kwa Wananchi kwenye maeneo yaliyo na upungufu wa Chakula kutumia Mvua kidogo zinazonyesha Nchini hivi sasa kulima Mazao yanayostahimili ukame kama vile Mtama, Viazi, na Mihogo ili kujiongezea Chakula.
HALI YA UNUNUZI WA MAHINDI
Mheshimiwa Spika,
22. Serikali inazingatia kuhakikisha kunawepo na akiba ya kutosha ya Chakula kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa Chakula Nchini. Hadi tarehe 30 Juni 2011, Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) ulikuwa na akiba ya Tani 154,506 za Mahindi na Tani 1.96 za Mtama. Wakala umelenga kununua Tani 200,000 za Mahindi katika kipindi cha msimu wa mwaka 2011/2012.
Hadi kufikia tarehe 30 Oktoba 2011, Wakala ulikuwa umenunua jumla ya Tani 114,117 kutoka Mikoa iliyozalisha ziada ya Nyanda za Juu Kusini. Katika kipindi hicho, jumla ya Tani 49,792 za Mahindi zilikuwa zimepelekwa kwenye Mikoa yenye upungufu wa Chakula inayohudumiwa na Maghala ya Wakala yaliyopo Arusha, Shinyanga na Dodoma na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Spika,
23. Zoezi la kununua, kuhifadhi na kusafirisha Mahindi kutoka maeneo yenye ziada kwenda maeneo yenye upungufu linakabiliwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo ni pamoja na ufinyu wa Bajeti,
uwezo mdogo wa kuhifadhi nafaka zinazonunuliwa na kasi ndogo ya kusafirisha Mahindi kutoka katika maeneo yenye ziada kwenda kwenye maeneo yenye upungufu.
Mheshimiwa Spika,
24. Bajeti iliyotengwa na Serikali katika Mwaka wa Fedha 2011/2012 kwa ajili ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) haitoshi kutekeleza malengo ya Wakala. Kati ya Tani 114,117 za Mahindi ambazo zimepokelewa katika Vituo vya ununuzi, Wakala umeweza kulipia Tani 80,615 tu na kushindwa kulipia Tani 33,492 zilizopokelewa.
Kufikia tarehe 30 Oktoba 2011, Wakala ulikuwa unadaiwa jumla ya Shilingi Bilioni 13.62 na Wakulima waliouza Mahindi yanayohifadhiwa na Wakala katika Vituo vya Makambako, Songea na Sumbawanga.
Mheshimiwa Spika,
25. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeiruhusu NFRA kukopa Shilingi Bilioni 20 kutoka katika Mabenki ya Biashara Nchini na mazungumzo na Mabenki hayo yanaendelea. Pamoja na hatua hiyo, Serikali pia imeiruhusu NFRA kuuza Mahindi Tani 50,000 kwa Shirika la Chakula Duniani (WFP), ambapo tayari Tani 10,000 zimenunuliwa. Pia NFRA imeruhusiwa kuuza Tani 40,000 kwa Wafanyabiashara Binafsi.
26. Hatua hizi zitawezesha Wakala kulipia madeni ya Wakulima, kuendelea na ununuzi, uhifadhi na usafirishaji wa Mahindi kwenda katika maeneo yenye upungufu wa Chakula. Kuhusu kasi ya kusafirisha Mahindi, Serikali inaangalia uwezekano wa kuiwezesha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuongeza kasi ya kusomba Mahindi kutoka kwenye Maghala ya Sumbawanga na Mpanda kwenda Shinyanga. Aidha, Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika usafirishaji wa Mazao haya. Ni imani ya Serikali kuwa jitihada hizi zitasaidia kukabiliana na uhaba wa Chakula kwenye maeneo yenye ukame.
MPANGO WA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA KILIMO, NA USALAMA WA CHAKULA (TAFSIP)
Mheshimiwa Spika,
27. Ili Nchi yetu ijitosheleze katika Chakula na Lishe na kuongeza kipato katika Kaya pamoja na Kukuza Uchumi wa Nchi, Tanzania inatekeleza Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula yaani “Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan” (TAFSIP). Huu ni Mpango wa Miaka 10 kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2020/2021 ambao unawaleta pamoja Wadau wote katika Sekta pana ya Kilimo Tanzania Bara na Visiwani.
28. Utekelezaji wa Mpango huu utaiwezesha Sekta ya Kilimo kukua kwa Asilimia 6 au zaidi kwa mwaka. Katika kufanikisha mpango huu, Serikali imeridhia kuongeza Bajeti ya Kilimo hadi kufikia Asilimia 10 kwa kuzingatia utekelezaji wa Azimio la Maputo la mwaka 2003 ambapo Wakuu wa Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania walikubaliana kuwa kila Nchi itaongeza Bajeti yake katika Sekta ya Kilimo angalau kufikia Asilimia 10 ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
29. Wadau mbalimbali walishiriki kuandaa Mpango huu ikiwa ni pamoja na Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi, Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi, Wanataaluma mbalimbali, Jumuiya za Uchumi za Kikanda, Umoja wa Afrika, Ubia Mpya wa Maendeleo ya Afrika (New Partnership for Africa’s Development-NEPAD) na Programu ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme-CAADP). Aidha, mchakato wa kutengeneza Mpango huu ulihusisha mikutano mbalimbali ya kukusanya maoni katika Kanda zote Tanzania Bara na Visiwani ambapo wadau mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia katika uundwaji wa mpango huu.
30. Serikali, Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi, Sekta Binafsi, NGOs, Jumuiya za Uchumi za Kikanda na Wakulima wadogo kwa wakubwa watashiriki katika utekelezaji wa Mpango huu. Katika kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016, Mpango huu unategemea kutumia kiasi cha Shilingi Trilioni 8.75, sawa na Wastani wa Shilingi Trilioni 1.7 kwa mwaka. Uwekezaji huo utakuwa katika maeneo yafuatayo:
i) Kuongeza uzalishaji, tija na Kilimo cha Kibiashara (Shilingi Trilioni 6.22);
ii) Kutekeleza mipango ya Umwagiliaji na Matumizi Bora na Endelevu ya Ardhi na Maji (Shilingi Trilioni 1.2);
iii) Kufanya Maboresho ya Sera na kujenga uwezo wa Taasisi mbalimbali (Shilingi Bilioni 681.13);
iv) Kuendeleza Miundombinu ya Vijijini, Masoko na Biashara (Shilingi Bilioni 357.26);
v) Kuwezesha kufikiwa kwa Usalama wa Chakula na Lishe (Shilingi Bilioni 211.4);
vi) Kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi na Majanga ya Asili (Shilingi Bilioni 66.31); na
vii) Kuendeleza Sekta Binafsi (Shilingi Bilioni 15.56).
Mheshimiwa Spika,
31. Hivi karibuni Mkutano wa Kazi (Business Meeting) kwa ajili ya Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (TAFSIP) ulifanyika tarehe 10 – 11 Novemba 2011, katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam. Mkutano huo uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 10 Novemba 2011 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 11 Novemba 2011. Mkutano huo ulihudhuriwa na Wadau mbalimbali toka Wizara na Taasisi za Serikali, Taasisi za Wakulima, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kiraia na Wabia wa Maendeleo.
Katika Mkutano huo makubaliano yalifikiwa kuhusu maeneo ya Kipaumbele ya Mpango, gharama za Mpango na Ratiba ya Utekelezaji wake. Katika Mpango huu, mbinu na msukumo mpya kupitia uratibu, ukusanyaji wa Rasilimali na ushirikishaji wa Sekta Binafsi vitatumika katika kuongeza kasi katika utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Nchini (Agricultural Sector Development Programme – ASDP) pamoja na Miradi na Programu mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa katika Sekta ya Kilimo hapa Nchini.
Mheshimiwa Spika,
32. Kama ilivyo katika utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Nchini (ASDP) kwa upande wa Tanzania Bara na Mpango wa Sekta ya Kilimo (ASP) kwa upande wa Tanzania Zanzibar, utekelezaji wa Programu ya TAFSIP utahusisha kwa karibu Mipango ya Maendeleo ya Wilaya kama ilivyo sasa. Ni matumaini ya Serikali kwamba utekelezaji wa Mpango huu utaiwezesha Sekta ya Kilimo kuchangia katika Ukuaji wa Uchumi Nchini, Kuongeza Pato la Mkulima na kuhakikisha kwamba Taifa linajitosheleza kwa Chakula na Lishe.
MAANDALIZI YA MSIMU WA KILIMO WA MWAKA 2011/2012
Mheshimiwa Spika,
33. Serikali imefanya Maandalizi muhimu ya Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2011/2012 ambapo imejikita katika upatikanaji na usambazaji wa Mbolea na Mbegu, maandalizi ya Vocha kwa ajili ya Pembejeo za Ruzuku na upatikanaji wa Madawa ya Kudhibiti uharibifu wa Mazao.
Upatikanaji na Usambazaji wa Mbolea
34. Mahitaji ya Mbolea Nchini yanakadiriwa kufikia Tani 400,000 kwa mwaka. Hadi kufikia tarehe 3 Novemba 2011, jumla ya Tani 246,454 za Mbolea, sawa na Asilimia 61.6 ya mahitaji zilikuwa zimesambazwa katika Mikoa mbalimbali Nchini. Kati ya hizo, Tani 81,294 ni Mbolea ya kupandia ambayo inatosheleza mahitaji ya Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Mikoa ya Kigoma, Kagera, Manyara na Mwanza ambayo Wakulima huanza kupanda mwezi Novemba kila mwaka. Kwa Wakulima wa Mikoa inayopanda mwezi Januari na Februari kila mwaka, Tani 129,711 za Mbolea ya kupandia zitakazotumika katika Mikoa hiyo zinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi Desemba 2011.
Upatikanaji na Usambazaji wa Mbegu Bora
Mheshimiwa Spika,
35. Mahitaji ya Mbegu Bora za Nafaka na Mikunde Nchini yanakadiriwa kufikia Tani 30,000 kwa mwaka. Hadi tarehe 3 Novemba 2011, jumla ya Tani 23,437, sawa na Asilimia 78 ya mahitaji zilikuwa zimesambazwa katika Mikoa mbalimbali Nchini. Kiasi cha Mbegu kilichopo kinatosheleza mahitaji ya Wakulima wanaopanda Mazao hayo katika mwezi wa Novemba kila Mwaka. Aidha, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaendelea kuwasiliana na Makampuni ya Mbegu ili kiasi cha Mbegu kilichobaki kipatikane kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
36. Katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2011/2012, jumla ya Tani 18,157 za Mbegu bora za mazao ya Mpunga na Mahindi zitasambazwa kwa Wakulima kwa utaratibu wa Vocha. Vilevile, Tani 180,000 za Mbolea ya kupandia na kukuzia mazao hayo zitasambazwa kwa utaratibu huo huo kwa Wakulima 1,800,000. Mapendekezo ya mgawanyo wa Vocha katika Mikoa 20 na Wilaya 96 zinazohusika na Ruzuku hiyo yamekamilika na wahusika wameshapatiwa taarifa. Vilevile, Ruzuku ya Mbegu Bora za Mtama kiasi cha Tani 356 zitatolewa kwa Wakulima 127,300 wa Mikoa yenye ukame ya Singida, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Dodoma na Mara. Pia, Ruzuku ya Mbegu bora za zao la Alizeti kiasi cha Tani 50 zitatolewa kwa Wakulima 10,392 wa Mikoa ya Singida na Shinyanga. Jumla ya Vocha 5,400,000 zitasambazwa katika Mikoa 20.
Mheshimiwa Spika,
37. Pamoja na taarifa hii, naomba nitumie fursa hii kutoa Taarifa ya Upatikanaji na Usambazaji wa Mbegu za Pamba kwa Msimu wa 2011/2012. Hadi kufikia tarehe 16 Novemba 2011, Tani 15,000 za Mbegu za Pamba zimesambazwa Vijijini, kati ya Tani 20,000 zilizopangwa kusambazwa msimu huu.
38. Pamoja na hali hii, limejitokeza kundi la Walanguzi wa Mbegu za Pamba katika Wilaya za Bariadi, Maswa, Magu, Meatu na Kishapu ambao wanapita Vijijini wakinunua Mbegu za Pamba walizosambaziwa Wakulima kwa kuwapa bei kubwa ili kununua Mbegu hizo na kuuza kwa bei kubwa. Kwa kuwa Mkulima akishauza Mbegu zake hawezi kupata mbegu zingine tena; jambo hili ni la hatari sana kwa Wakulima, zao la Pamba na Uchumi wa Taifa. Aidha, kwa Mkulima mwenyewe, kuuza mbegu yake ya Pamba ni kujiua yeye mwenyewe.
39. Mbinu nyingine inayotumika ni kwa Walanguzi wa Mbegu na baadhi ya Viongozi kupanga watu wengi katika Vituo vya kununulia Mbegu wakijifanya kuwa ni Wakulima, kwa lengo la kuwakusanyia mbegu nyingi ili waiuze kwa bei kubwa.
Mheshimiwa Spika,
40. Serikali imepokea majina ya Walanguzi wengi wa Mbegu katika Wilaya za Meatu, Bukombe, Bariadi, Bunda, Magu na Kishapu na operesheni ya kuwakamata inaendelea. Hivyo, Serikali inawatahadharisha wote (Walanguzi, Wakulima na wengine) wanaoshiriki katika hujuma hii, kuacha mara moja. Hatua kali za Kisheria zitachukuliwa kwa wote wanaouza na wale wanaonunua Mbegu za Pamba kinyume cha Sheria.
Madawa ya Kudhibiti Uharibifu wa Mazao
Mheshimiwa Spika,
41. Hadi tarehe 3 Novemba 2011, tayari lita 3,072 za Madawa ya kudhibiti Viwavi Jeshi, Lita 2,000 za Madawa ya kudhibiti Ndege aina ya Kwelea Kwelea na Kilo 1,200 za kudhibiti Panya zilikuwa zimesambazwa katika Mikoa mbalimbali Nchini. Aidha, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imeandaa zabuni itakayowezesha kuingizwa Nchini Lita 4,000 za Dawa za kudhibiti Ndege aina ya Kwelea Kwelea; Lita 7,000 za kudhibiti Nzige Wekundu; Lita 5,000 za kudhibiti Viwavi Jeshi; na Kilo 1,400 za kudhibiti Panya.
Mheshimiwa Spika,
42. Kwa kuzingatia maandalizi hayo ya Kilimo yaliyofanyika na ili kupata ufanisi katika uzalishaji katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2011/2012, suala la usimamizi wa dhati litazingatiwa. Viongozi kuanzia ngazi ya Wizara hadi ngazi ya Vijiji wasimamie upatikanaji, usambazaji wa pembejeo na upatikanaji wa ushauri wa kitaalam kwa Wakulima wetu Vijijini. Vilevile, Wataalam wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, TAMISEMI na Halmashauri zote Nchini wanapaswa kutoka Maofisini waende Vijijini kufuatilia na kusimamia Kilimo. Mikoa na Halmashauri yenye Maafisa Ugani wengi katika ngazi ya Makao Makuu wahamishiwe kwenye ngazi ya Kata na Vijiji ili kuwasaidia kwa karibu Wakulima Vijijini.
HALI YA AJIRA
Mheshimiwa Spika,
43. Viongozi na Jamii kwa ujumla wamekuwa wakizungumzia tatizo la Ajira hasa kwa Vijana. Athari za ukosefu wa Ajira hususan kwa Vijana ni kubwa na ni mbaya katika mustakabali wa Taifa letu. Tatizo hili linachangia kwa kiasi kikubwa umaskini Nchini kwani yeyote asiyekuwa na Ajira hana kipato. Watu wasio na ajira ni rahisi kujikuta wanaishi kwa njia zisizokubalika katika Jamii zikiwemo za Wizi, Unyang’anyi, Biashara za Ngono, Matumizi ya Dawa za Kulevya, Uhalifu na kadhalika.
44. Katika mwaka 2001, kiwango cha ukosefu wa Ajira Nchini kilikuwa Asilimia 12.9. Kwa matokeo ya utafiti wa Nguvu Kazi na Ajira ya mwaka 2006, Nguvu Kazi Nchini ilikuwa Watu Milioni 18.8. Kati yao, Watu Milioni 2.2 walikuwa hawana ajira sawa na Asilimia 11.7 ya Nguvu Kazi yote Nchini. Makadirio ya kiwango cha ukosefu wa Ajira Nchini katika mwaka 2011 ni Asilimia 10.7 ya Nguvu Kazi ya Taifa ya Watu Milioni 22.2. Kwa kiwango hicho inakadiriwa kuwa Idadi ya Watu wasiokuwa na Ajira kwa sasa ni Milioni 2.4.
Takwimu pia zinaonesha kuwa mwaka 2006 wakati wa utafiti wa Nguvukazi (Labour Force Survey) Watu Milioni 14.9 walikuwa wameajiriwa kwenye Sekta Rasmi na Watu Milioni 1.7 walikuwa wameajiriwa katika Sekta Isiyo Rasmi. Kwa mwaka 2011 inakadiriwa kuwa Watu Milioni 17.3 wameajiriwa kwenye Sekta Rasmi na Watu 2.5 wameajiriwa kwenye Sekta Isiyo Rasmi. Sekta ya Kilimo (kwa tafsiri pana) ndiyo inayoongoza kwa kuajiri Asilimia 75 ya Nguvu Kazi. Sekta Isiyo Rasmi inaajiri Asilimia Tisa, Serikali Asilimia 2.4 na Mashirika Asilimia 0.4.
45. Utafiti unaonesha pia kuwa ukosefu wa ajira unawaathiri zaidi Vijana wa umri kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 ambao wanamaliza Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Aidha, tatizo hili ni kubwa zaidi kwa Wanawake kuliko Wanaume. Ongezeko kubwa la Watu wasiyo na kazi linatokana na kasi kubwa ya ongezeko la Watu wenye umri wa kufanya kazi ikilinganishwa na kasi ndogo ya ongezeko la nafasi za ajira ambalo limekuwepo kwa miaka mingi sasa.
Mheshimiwa Spika,
46. Hata hivyo, suala hili la ukosefu wa Ajira siyo la Tanzania tu, bali ni la Nchi nyingi Duniani. Kwa mfano, kwa mwaka 2011, wakati kiwango cha ukosefu wa Ajira Tanzania ni Asilimia 10.7, Nchi ya Afrika Kusini ni Asilimia 25.0, Hispania Asilimia 21.5, Ureno ni Asilimia 12.4, Iran ni Asilimia 11.5, Ufaransa ni Asilimia 9.5, na Marekani ni Asilimia 9.
Mheshimiwa Spika,
47. Serikali inatambua kuwepo kwa mahitaji makubwa ya ajira Nchini. Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 inatambua kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa ajira. Sera hiyo inalenga pamoja na mambo mengine kuandaa mazingira wezeshi kwa wasiokuwa na ajira kujiajiri wenyewe na kuainisha maeneo ya kiuchumi yanayoweza kukuza ajira na kuweka mikakati ya kutumia maeneo hayo kukuza Uchumi. Aidha, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 inalitambua suala hili. Kwa mfano, Ibara ya 77 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaeleza ifautavyo:
“Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwamba katika kipindi hiki suala la ajira hususani Ajira ya Vijana imekuwa nyeti. Hii ni kwa sababu idadi ya Vijana wanaofuzu Elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu kila mwaka ni kubwa sana. Idadi hiyo inakuzwa pia na Vijana wanaomaliza Mafunzo ya JKT. Vijana wote hawa ni Nguvukazi ya Taifa ambayo inaweza kutumika katika kazi na shughuli halali za ujenzi wa Nchi”.
Aidha, Ibara ya 78 inaainisha mambo yanayotakiwa kushughulikiwa na Serikali ili kujenga fursa za Ajira hasa kwa Vijana.
Mheshimiwa Spika,
48. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo hili. Serikali yenyewe imekuwa ni miongoni mwa Waajiri wakubwa Nchini na itaendelea kuajiri Vijana wengi kadri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu. Aidha, Serikali itaendelea kujenga mazingira ya kupunguza ukosefu wa ajira kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha Sekta ya Kilimo ambayo inaajiri Asilimia kubwa ya Nguvu Kazi na kuchangia katika kutoa huduma za Ardhi, kupanda, kuvuna, kutunza na kuuza mazao. Hatua nyingine ni kupanua mafunzo ya VETA; kupanua na kuboresha Elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ufundi na Vyuo Vikuu na kuimarisha mitaala ya Elimu ili Wahitimu waweze kujiajiri. Vilevile, Wananchi watahamasishwa kujiunga katika SACCOs na VICOBA na kuwawezesha kimtaji, kuweka mazingira mazuri ya kukuza Sekta Binafsi na Uwekezaji, na kuvutia Wawekezeji wa Ndani na Nje ya Nchi. Aidha, Serikali itandelea kuwawezesha Waajiri na wale wanaotafuta kazi kupata taarifa za hali ya Soko la Ajira.
49. Ningependa tukumbushane kuwa tunapozungumzia ajira hatuna maana ya ajira za kulipwa mishahara tu bali ni pamoja na ajira binafsi katika Kilimo, Uvuvi, Ufugaji, Biashara na kadhalika. Hivyo, suala la kupunguza ukosefu wa ajira si suala la Serikali pekee bali ni pamoja na Sekta Binafsi. Kila mmoja wenu afanye kila liwezekanalo kuongeza Ajira Nchini. Tukiwa na dhamira ya pamoja tutaweza.
HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
50. Hali ya Usalama katika Nchi yetu ni shwari ikiwa ni pamoja na maeneo ya Mipakani na eneo la Bahari ya Hindi, licha ya kuwepo kwa matishio ya Uharamia katika Pwani ya Nchi za Afrika Mashariki. Tarehe 3 Oktoba 2011, Maharamia wenye asili ya Somalia walivamia ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Mafia kwa lengo la kutaka kuteka meli inayotumika katika utafiti wa mafuta.
Jaribio hilo lilidhibitiwa na Wanajeshi wetu wa Jeshi la Wanamaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Katika jaribio hilo, Maharamia Saba (7) walikamatwa na hatua za Kisheria dhidi yao zinaendelea kuchukuliwa. Vilevile, kulikuwa na matukio mengine matatu ya uharamia ambapo yalidhibitiwa na hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa upande wa Tanzania.
51. Napenda kutumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Wananchi kwa kazi nzuri inayofanya kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti vitendo vya Uharamia katika Pwani ya Nchi za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika,
52. Kama mnavyofahamu, kwa sasa katika Ukanda wa Afrika Mashariki kumekuwa na matishio ya Ugaidi, hususan katika Nchi jirani. Hivi karibuni kumezuka matishio ya Kigaidi Nchini Kenya kufuatia Serikali ya Kenya kufunga Mpaka wake na Somalia kama njia ya kupambana na Kikundi cha Wapiganaji wa Kundi la Al-Shabab. Kutokana na hali hii, Nchi yetu imeimarisha Ulinzi katika mipaka yake yote ambapo Idara ya Uhamiaji imewaelekeza Maafisa Uhamiaji wa Mikoa yote na Vituo vyote vya kuingia Nchini kuimarisha Doria na misako katika maeneo yao ili kuzuia Wahamiaji Haramu, hususan Raia wa Somalia wengi wao wakitokea Kenya kuingia Nchini. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Dola wameweka mikakati ya kukubaliana na tishio hili, ikiwa ni pamoja na kuweka Boti za Doria katika Pwani ya Bahari ya Hindi na Askari wa Doria katika maeneo ya Mipakani.
53. Natoa wito kwa Watanzania wote, hasa wale wanaoishi maeneo ya mipakani mwa Nchi yetu kutoa taarifa katika Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama pale watakapoona Mtu au Watu ambao nyendo zao hazieleweki. Aidha, niwatake Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji kuendelea na zoezi la kuhakiki watu katika maeneo yao na kuchunguza Watu wanaokuja na kuishi katika Vijiji na Mitaa yao bila ya kutoa taarifa kwa Viongozi wa maeneo hayo.
Kazi ya kulinda Nchi yetu na mipaka yake itafanikiwa endapo Wananchi wote watashirikiana kwa karibu na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kutoa taarifa pale inapobidi.
KUIBUKA KWA MATUKIO YA UHALIFU KWA WATU WENYE WALEMAVU WA NGOZI
Mheshimiwa Spika,
54. Mwaka 2007, Nchi yetu ilikumbwa na tatizo la imani za kishirikina kwamba Viungo vya Watu Wenye Walemavu wa Ngozi (Albino) vinaweza vikaleta utajiri. Imani hiyo potofu ilisababisha kuibuka kwa kasi kwa vitendo vya mauaji na unyama wa kukata viungo vya Ndugu zetu Walemavu wa Ngozi. Vitendo hivyo vilisikitisha sana, kuona Watu wachache kwa tamaa za kupata utajiri wanawageuza Binadamu wenzao kama Wanyama. Suala hili lilichafua jina na Sifa ya Tanzania ambayo siku zote imekuwa ni Nchi ya Amani, Umoja na Mshikamano.
Mheshimiwa Spika,
55. Serikali kwa kushirikiana na Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali, Taasisi mbalimbali za Ndani na Nje ya Nchi na Madhehebu ya Dini kwa pamoja tulisimama kidete kupambana na vitendo hivyo. Vilevile, Serikali kupitia Vyombo vya Dola ilichukua hatua kali dhidi ya wahusika. Kwa kuzingatia hilo, Watuhumiwa 94 walikamatwa na Kesi 11 za Mauaji ya Walemavu wa Ngozi zilifikishwa Mahakamani. Kati ya hizo, Kesi Tisa (9) zimekwisha sikilizwa na Kesi Sita (6) zimeshatolewa hukumu ambapo Watuhumiwa Nane (8) wamehukumiwa Kunyongwa. Kutokana na jitihada hizo, Matukio ya Mauaji na Kujeruhiwa kwa Walemavu wa Ngozi yalionekana kupangua sana.
56. Pamoja na hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali, bado hivi karibuni kumeripotiwa matukio mawili ya uhalifu yaliyohusisha kukatwa kwa Viungo vya Watoto wawili Wenye Ulemavu wa Ngozi kwa nyakati tofauti. Matukio hayo yalitokea Mikoa ya Mwanza na Shinyanga ambapo tarehe 14 Oktoba 2011 Mtoto wa Darasa la Tatu,
Adam Robert, mwenye Miaka 13 mkazi wa Kijiji cha Nyaluguguna, Kata ya Nyijuda, Wilayani Geita alivamiwa na kukatwa vidole vitatu vya mkono wa kulia mbele ya Wazazi wake na mhusika kutoweka navyo. Katika tukio la pili, tarehe 22 Oktoba 2011, Mtoto Kulwa Lusana, mwenye Miaka 16 Mkazi wa Kijiji cha Mbizi, Kata ya Mega Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga alikatwa mkono wa kulia na mhusika kutoweka nao. Watoto hawa wote wanaendelea kupata Matibabu, mmoja katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na mwingine Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
57. Katika Matukio haya mawili Watu wa karibu na majeruhi hawa wanahisiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine na matukio haya wakiwemo Wazazi wao ambao wamekamatwa na Upelelezi wa Mashauri yao unaendelea.
58. Unyama huu unaofanywa na Watu wachache wenye uchu wa utajiri wasiokuwa na utu, unachafua jina zuri la Tanzania Duniani kote na kudhalilisha Watanzania wote. Hivyo, Wadau wote tunahitaji kukemea vitendo hivyo, kuvilaani na kuhakikisha uhalifu huo unatokomezwa.
59. Napenda kusisitiza tena kwamba Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi ni Binadamu kama walivyo Binadamu wengine. Wanastahili haki ya kuishi kwa amani na kufurahi katika Nchi yao. Hakuna Mtu, Kikundi chochote ambacho kina haki ya kumfanya Mlemavu wa Ngozi aishi kwa wasiwasi au kwa hofu katika Nchi yake kwa sababu yoyote ile.
60. Narudia tena kuagiza Vyombo vya Dola kuongeza Nguvu katika kuhakikisha Vitendo vya uhalifu dhidi ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi vinadhibitiwa ipasavyo na Wadau wote tushirikiane kuhakikisha Ndugu zetu hawa wanalindwa. Aidha, natoa wito kwa Wananchi wote, Wazazi, Vijana na Wadau wengine kwamba suala la ulinzi wa Ndugu zetu Walemavu wa Ngozi ni letu sote.
Ni wajibu wa kila mmoja wetu kutoa taarifa juu ya Watu wanaonesha kuwa na mwenendo unaotia mashaka kuhusiana na Ndugu zetu hawa. Tunahitaji ushirikiano katika suala hili, hata kama wanaohisiwa ni Wazazi tafadhali toeni taarifa. Viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini, Viongozi wa Serikali na Wazee Maarufu, katika maeneo yenu Kemeeni imani hii potofu inayosababisha Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi na kuwaeleza madhari ya Imani za Kishirikina kwa Ndugu zetu hawa.
61. Aidha, Viongozi wa Serikali za Mitaa, mna jukumu la kubaini makazi ya Walemavu wa Ngozi na kuwapatia ulinzi kila inapobidi. Aidha, ni muhimu kupata namba za simu za Wazazi/Walezi wao ili waweze kufuatiliwa. Kwa upande wa Ndugu zetu Walemavu wa Ngozi, nawaomba ninyi pia toeni taarifa pale mnapoona kufuatwa fuatwa na Watu ambao mnahisi wana nia mbaya, au kutia mashaka.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Timu ya Mpira wa Miguu – TAIFA STARS
Mheshimiwa Spika,
62. Watanzania wote tunafahamu na kutambua kuwa Timu yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu –TAIFA STARS – ilicheza na Timu ya Taifa ya Chad huko N’djamena, Chad tarehe 11 Novemba, 2011. Matokeo ya mechi hiyo yalikuwa ni ushindi kwa Timu yetu kwa kuifunga Timu ya Taifa ya Chad Mabao 2-1.
63. Mechi ya marudiano ilifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2011 na matokeo yalikuwa Chad 1 na Tanzania 0. Kwa matokeo hayo, Timu ya Taifa imefaulu kusonga mbele na hivyo kuingia katika kundi C ambalo lina Timu za Morroco, Ivory Coast na Gambia. Mechi hizo ni muhimu sana kwa Taifa kwa kuwa ni maandalizi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka 2014. Pamoja na kwamba Timu yetu imefuzu kuingia katika Makundi, lakini ukweli ni kwamba safari yetu bado ni ngumu na ndefu.
Timu tulizopangwa nazo ni ngumu na ni magwiji wa Soka Barani Afrika. Ili kukabiliana na Timu hizo na kupata ushindi tunahitaji maandalizi ya kutosha na Michezo ya kujipima nguvu kwa Timu yetu. Napenda kuwaasa Vijana wetu kuwa, hata kama tungekuwa na Kocha Mzuri kama kiasi gani, lakini kama hawatafanya Mazoezi ya kutosha, kujituma kwa hali na mali kutambua kuwa wanabeba Bendera ya Taifa bado hatutashinda.
Mheshimiwa Spika,
64. Wakati wa mechi za ugenini na zile ya nyumbani, Timu yetu inahitaji kutiwa moyo, kusaidiwa kisaikolojia na zaidi ya yote kuungwa mkono kifedha ili iweze kushinda.
Ninawasihi Watanzania wenzangu tuiunge mkono Timu yetu ya Taifa kwani Ushindi wa Timu yetu ni Ushindi wa Taifa; Ni Ushindi wa Watanzania Wote, Ni Njia ya Kuitangaza Tanzania Duniani na Sote Kama Watanzania Tutapata Sifa na Kujivunia Ushindi Huo.
65. Nawaomba Watanzania, kila mmoja kwa nafasi yake tuisaidie Timu yetu kwa hali na mali ili iweze kuibeba na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa ujasiri mkubwa.
Mlima Kilimanjaro
Mheshimiwa Spika,
66. Kuna suala la Mlima Kilimanjaro ambalo nalo pia haliwezi kuachwa hivi hivi. Tutakumbuka kuwa miezi ya karibuni kulikuwa na kampeni ya kuupigia kura Mlima Kilimanjaro ili uweze kuchanguliwa na kuwa miongoni mwa Maajabu Saba Mapya ya Dunia. Kulikuwa na vivutio 28 vilivyochaguliwa kutoka vivutio 77 kutoka Nchi 220 zilizoshindanishwa mwaka 2007. Tangu Julai 2009, kura zilikuwa zikipigwa na hatima yake ilikuwa ni tarehe 11 Novemba 2011. Matokeo rasmi ya kura hizo yatatangazwa mwanzoni mwa mwaka 2012 lakini katika matokeo ya awali, Mlima Kilimanjaro haukupata nafasi ya kushinda na kuwemo katika Maajabu Saba ya Dunia. Hata hivyo, ulipata nafasi ya kupita katika mchujo wa kwanza na kuwa miongoni mwa vivutio 14 kati ya 28, vilivyoshinda kura za awali. Hili ni jambo la kujivunia na naomba nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania wote ambao walishiriki kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) ama emails zao kuupigia kura Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika,
67. Kwa kuwa Maajabu hayo Saba yalikuwa yameamuliwa kwa kura, ninaamini, na ni maoni yangu kuwa Watanzania wengi hawakutumia nafasi hiyo vizuri kuupigia Mlima Kilimanjaro kura. Aidha, taarifa ya kushindanishwa kwa Mlima Kilimanjaro hazikutolewa na kutangazwa mapema na Wizara yenye dhamana na Taasisi zake. Hii ni Changamoto kwetu sote lakini zaidi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo kimsingi ilikuwa na jukumu la kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha Wananchi kuhusu Mashindano hayo tangu suala hili lilipojulikana mapema mwezi Julai 2011. Pamoja na kwamba hatukupata nafasi, naomba nichukuwe nafasi hii kuzipongeza Kampuni za Simu za Airtel na VODACOM kwa kukubali kufanyakazi na Serikali kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu kuupigia Kura Mlima Kilimanjaro. Matarajio ni kwamba Kampuni zingine nazo zitashiriki katika maeneo mengine ya Maendeleo kwa nyakati zijazo.
68. Ninawapongeza Wananchi wote wa Ndani na Nje walioitikia wito wa kuupigia Kura Mlima Kilimanjaro. Aidha, nitumie fursa hii kuzitaka Wizara zote kujipanga vizuri wakati wote kunapotokeza Mashindano ya Kimataifa katika Sekta zao kwa kuweka Uzalendo mbele na kuwa tayari kuipigania Nchi yetu. Ufahamu wa Wananchi upewe kipaumbele na Wananchi washirikishwe kikamilifu.
KUVUTIA UWEKEZAJI KIKANDA
Mheshimiwa Spika,
69. Serikali imedhamiria kuongeza kasi ya kuhamasisha na kuvutia Wawekezaji wa Ndani na wa Nje kuwekeza Nchini ili hatimaye tuweze Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa haraka. Dhamira hiyo inaendana na matakwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano hadi 2015 ambao unasisitiza na kutoa kipaumbele katika kuvutia Uwekezaji Nchini. Aidha, ili kuleta uwiano wa maendeleo endelevu Nchini, Serikali inahimiza Mikoa na Wilaya kuunganisha nguvu na kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji Kikanda kwa kuzingatia Jiografia, Hali ya Hewa, Miundombinu na fursa za Uwekezaji zilizopo katika Mikoa husika.
Mheshimiwa Spika,
70. Ili kutekeleza Azma hiyo, tarehe 17 Oktoba 2011, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifungua Kongamano la Uwekezaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika unaojumuisha Mikoa ya Rukwa, Kigoma na Mkoa tarajiwa wa Katavi. Kongamano hilo ni la kipekee na la aina yake kufanyika katika Mikoa hiyo, ambayo iko nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Mikoa ya Kaskazini, lilikuwa na lengo la kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizopo katika Ukanda huo kwa Wawekezaji wa Nje na wa Ndani. Miongoni mwa mambo muhimu ambayo Wadau na Washiriki wa Kongamano hilo, walijifunza na kupata uzoefu ni pamoja na:
i) Mikoa hiyo mitatu ina fursa za kipekee na Rasilimali nyingi zenye tija kubwa na zinazofanana katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Utalii, Madini, Misitu na Ufugaji Nyuki. Aidha, Mikoa hiyo ina ardhi nzuri yenye rutuba, Hali ya Hewa inayofanana, imeunganishwa na Reli ya Kati na yote ipo kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Hivyo, ina fursa kubwa ya kuunganisha nguvu na kuvutia Wawekezaji wa ndani na nje kwa pamoja ili kuongeza kasi ya maendeleo katika Ukanda huo;
ii) Mikoa hiyo na Wilaya zake imetenga maeneo maalum ya Uwekezaji na Ardhi kwa ajili ya kuvutia Uwekezaji katika Sekta zenye fursa kubwa za Kiuchumi. Sekta hizo ni za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Makazi, Madini, Viwanda na Biashara.
Hatua hii ni nzuri kwa kuwa itapunguza urasimu katika kuwawezesha Wawekezaji kupata ardhi kwa ajili ya Uwekezaji;
iii) Aidha, Serikali kwa upande wake inajitahidi kuweka Mazingira wezeshi ya kuvutia Uwekezaji ili kufungua Milango zaidi ya Uwekezaji katika maeneo hayo. Mfano wa jitihada ambazo Serikali imeanza kuzifanya ni kuwekeza katika Miundombinu muhimu, hususan Barabara za Mikoa ya Kigoma na Rukwa na kuziunganisha na Mikoa mingine na Nchi Jirani. Miundombinu mingine ni kuimarisha Reli ya Kati, Viwanja vya Ndege, Nishati ya Umeme, Madaraja, Usafiri wa Majini na kushirikiana na Sekta Binafsi kuhakikisha kunakuwepo Hoteli nzuri kwa ajili ya Watalii katika Hifadhi za Taifa za Katavi, Gombe na Mahale;
iv) Zaidi ya hayo ilionekana kuwa upo umuhimu mkubwa kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhamasisha Wawekezaji wengi wa ndani kuchangamkia fursa za Uwekezaji zilizopo Nchini ili waweze kunufaika na Vivutio vingi vinavyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania; na
v) Viongozi wa Mikoa na Wilaya wakijipanga vizuri wanaweza kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji kuandaa na kuendesha Makongamano ya Kikanda ya kutangaza kwa pamoja fursa za Kuvutia Wawekezaji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika,
71. Kwa kuzingatia uzoefu huo, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri wote Nchini kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji kuanza kuandaa Mipango ya Uwekezaji na kutenga maeneo ya Uwekezaji katika maeneo yao ili kuwarahisishia Wawekezaji wa Ndani na Nje kuwekeza kulingana na fursa zilizopo katika Mikoa na Halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika,
72. Sambamba na hatua hiyo, moja ya Maazimio ya Kongamano la Uwekezaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika ni kuendeleza utaratibu huo katika Kanda nyingine. Kwa kuzingatia Azma hiyo, narejea wito nilioutoa wakati nilipofanya Majumuisho ya Ziara yangu katika Mkoa wa Mara mwezi Septemba 2011 ambapo nilishauri Viongozi wa Mkoa huo wawasiliane na Mikoa jirani kuona uwezekano wa kufanyika kwa Kongamano la Uwekezaji katika Kanda ya Ziwa Victoria. Mimi naamini kuwa Mikoa ya Kanda hiyo inayojumuisha Mikoa ya Mara, Mwanza,
Kagera, Shinyanga na Mikoa tarajiwa ya Geita na Simiyu ina Vivutio vingi na fursa nyingi za Uwekezaji zinazofanana katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Utalii, Madini, Maliasili, n.k. Vilevile, Mikoa hii ina Jiografia, Hali ya Hewa inayofanana na shughuli nyingi za Kibiashara na Kijamii zinazowiana. Hivyo, Mikoa hii inaweza kuunganisha nguvu katika kutangaza na Kuvutia Uwekezaji kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika,
73. Mikoa mingine iliyopendekezwa kuunganisha nguvu na kuvutia Uwekezaji kwa pamoja ni ile ya Kanda ya Pwani inayojumuisha Mikoa ya Tanga, Pwani na Morogoro. Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Viongozi wa Mikoa niliyoitaja na mingine kujipanga vizuri Kikanda, kuibua fursa za Uwekezaji na kuunganisha nguvu katika kutangaza Vivutio vya Uwekezaji katika maeneo yao. Aidha, nawashauri kutumia kikamilifu uzoefu wa Mikoa ambayo tayari imefanya Makongamano ya Kuvutia Uwekezaji, ikiwemo Kilimanjaro, Tanga, Rukwa na Kigoma.
Mheshimiwa Spika,
74. Katika Hotuba ya Ufunguzi ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kongamano la Uwekezaji wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika, alisema na kusisitiza (kwa lugha aliyoitumia siku hiyo) kuwa:
“It is a statement of fact that Investment is Key to Economic Growth. There is no Growth without Investment. ……… Therefore, where there is growth, know for sure that, there has been Investment at the place. Conversely where there is no growth it is evident that there has been little or no Investment in that place. For these reasons, if we want growth to happen, one thing that we must ensure is continuous and increased Investment”.
Kwa kifupi tafsiri isiyokuwa rasmi ya Kiswahili anachosema ni kwamba:
Ni ukweli usiopingika kwamba Uwekezaji ni Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi. Kwani Bila Uwekezaji Hakuna Maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana na Uchumi hauwezi Kukua. Kwa hiyo, ukiona Uchumi unakua, utambue kuwa kuna Uwekezaji umefanyika mahali hapo. Kinyume cha hapo, ni kwamba mahali pasipokuwa na Maendeleo ni Ushahidi tosha kwamba umefanyika Uwekezaji Kidogo au hakuna kabisa Uwekezaji. Kwa mantiki hiyo, kama tunahitaji Maendeleo na Uchumi wetu Ukue ni lazima kuhakikisha kuwepo na Ongezeko la Uwekezaji na Uwekezaji huo uwe endelevu.
75. Hivyo, suala la Kuvutia Uwekezaji wa Ndani na Nje ni Agenda kubwa ya Serikali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba chimbuko la maendeleo katika Nchi zote Duniani limetokana na Uwekezaji uliofanyika katika Nchi hizo. Kwa kuzingatia kuwa Nchi yetu ina Rasilimali nyingi, na fursa kubwa za Kuvutia Uwekezaji. Serikali itaendelea kushirikiana na Wawekezaji wa Ndani na Nje kuwekeza Mitaji ili tutumie kikamilifu Rasilimali zetu tuweze Kupunguza Umaskini, Kuongeza Ajira na Kukuza Uchumi wa Taifa letu. Tukifanya hivyo tutaweza kuwanufaisha Watanzania walio wengi zaidi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, katika kuvutia Wawekezaji wa Ndani na Nje tunatarajia kupata Mitaji, Teknolojia Mpya, Rasilimali Watu na fursa za Masoko zitakazotuwezesha Kukuza Uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
76. Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia Wawekezaji Nchini. Aidha, tutajitahidi kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu na faida za Uwekezaji ili nao washiriki kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika maeneo yao na kujiletea maendeleo. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kuunga mkono jitihada hizi za Serikali za Kuvutia Uwekezaji Nchini ili kuongeza Ajira, Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini.
ZOEZI LA UTOAJI WA VITAMBULISHO
Mheshimiwa Spika,
77. Moja ya mambo makubwa ambayo kwa sasa Serikali inayafanyia kazi ni kutekelezwa kwa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa. Mapema mwaka huu, Serikali ilisaini Mkataba na Mkandarasi aliyeshinda Zabuni ya kutengeneza Vitambulisho vya Taifa. Hivyo, kazi kubwa iliyopo mbele yetu kwa sasa ni kutengeneza Mfumo na kuweka Utaratibu mzuri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ili Wananchi waweze kusajiliwa na hatimaye kupewa Vitambulisho.
Mheshimiwa Spika,
78. Mradi huu una faida nyingi Kisiasa, Kiuchumi, Kiusalama, Kiulinzi na Kijamii. Zipo faida kubwa ambazo tunaweza kuzitaja kama ifuatavyo:
Kwanza: Uboreshaji Daftari la Wapiga Kura. Iwapo zoezi la kutoa Vitambulisho vya Taifa litakamilika kama ilivyopangwa, Serikali itapunguza gharama zinazotumika katika kuboresha Daftari la Wapiga Kura, kwani tayari kutakuwa na Taarifa za Watanzania wenye Sifa za Kupiga Kura, vivyo hivyo tatizo la kughushi Kadi ya Kupigia Kura, litakwisha kwani Kitambulisho kitaweza kutambulisha uhalali wa mtu kupiga kura au la;
Pili: Kwa kuwa Serikali sasa iko katika maandalizi ya utekelezaji wa zoezi la Sensa litakalofanyika mwezi Agosti 2012 kuwepo kwa Vitambulisho vya Taifa, kutahuisha takwimu za Sensa, kwani mbali ya kujua Idadi, Taifa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa litakuwa na Idadi kamili ya Watanzania, shughuli zao na mahitaji yao ya msingi na hivyo kuirahisishia Serikali kazi katika kuweka Mipango yake, vikiwemo vipaumbele vya Huduma za Jamii;
Tatu: Kuiongezea Serikali wigo wa ukusanyaji mapato na hivyo kuboresha huduma muhimu za kijamii kama vile afya, elimu pamoja na ulinzi na usalama wa raia na mali zao; na
Nne: Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo hivi sasa ni Muungano wa Nchi Tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda kumeongeza kwa kiasi kikubwa umuhimu wa kuwa na Vitambulisho. Aidha, kuna makubaliano kwamba Wananchi wa Nchi hizi wawe wanaweza kutembeleana bila ya vikwazo na bughudha kwa kutumia Kitambulisho cha Uraia. Tanzania na Uganda ndizo Nchi pekee katika Jumuiya ambazo hazina Vitambulisho vya Taifa. Hata hivyo tayari Uganda wameshaanza mchakato wa kuwa na Vitambulisho vyao.
Mheshimiwa Spika,
79. Kwa taarifa nilizonazo, Vitambulisho vya kwanza vitatolewa kuanzia mwezi Aprili 2012, wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Muungano. Ombi langu kwenu Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wananchi kwa jumla ni kuunga mkono jitihada hizi za Serikali na kuelimisha Umma faida za zoezi hili Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii. Suala la Kitambulisho cha Taifa halina Chama, wala itikadi. Hivyo, suala hili ni la Taifa zima. Sisi sote tuungane pamoja kuhakikisha kwamba mafanikio ya zoezi hili yanapatikana kwa wakati uliopangwa. Vilevile, niwaombe Watendaji wote, kuanzia Serikali za Mitaa, ngazi za Vijiji, Kata, Wilaya, Mikoa hadi Taifa kuwa Wazalendo katika kuthibitisha nani ni Mtanzania na nani si Mtanzania kwa kutoa taarifa sahihi bila uonevu, kwa kuzingatia misingi ya Haki na Sheria ya Nchi. Napenda kuwaasa Watanzania wote kuwa wakweli wakati wote wa kuandikisha na kutoa Vitambulisho ili kujiepusha na Madhara ya Udanganyifu. Hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kudanganya katika zoezi hili.
MAANDALIZI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012
Mheshimiwa Spika,
80. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti 2012. Sensa hii itakuwa ya Tano tangu tulipopata Uhuru mwaka 1961. Sensa zilizotangulia zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na mwaka 2002. Lengo kubwa la Sensa ya mwaka 2012 ni kuchangia katika uboreshaji wa maisha ya Watanzania kwa kutoa takwimu sahihi na kwa wakati kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo. Taarifa hizi zitasaidia katika kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo kama ifuatavyo:
i) Kutoa Takwimu za Idadi ya Watu, taarifa za Kiuchumi na Kijamii katika ngazi zote za Mipango;
ii) Kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na ile ya Zanzibar ya mwaka 2020;
iii) Kutumika katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) – Tanzania Bara na MKUZA – Tanzania Zanzibar);
iv) Kutumika kutathmini hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015;
v) Kusaidia Serikali kufanya tathmini juu ya ongezeko la idadi ya watu, makazi yao, shughuli zao na athari zake kwa mazingira ili kuwezesha kuweka Sera na Mipango madhubuti ya uboreshaji wa Makazi ya Watu na utunzaji wa Mazingira na pia kusaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha mahitaji halisi ya miuondombinu na huduma nyingine za Kijamii kama vile Jiji la Dar es Salaam na Miji mingine; na
vi) Kuimarisha Utawala Bora na ukuaji wa Demokrasia Nchini kwa kutumia Takwimu hizo katika kuamua Mipaka mipya ya Majimbo ya Uchaguzi pamoja na Mipaka mingine ya Kiutawala.
Mheshimiwa Spika,
81. Maandalizi ya Sensa hii yalianza mwaka 2004 kwa kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia Watu yajulikanao kitaalamu kama Enumeration Areas. Lengo kubwa la kazi hii ni kuitenga Nchi nzima katika maeneo madogo madogo ya kuhesabia Watu ili ifikapo mwezi Agosti 2012 Watu wote watakaolala Nchini waweze kuhesabiwa mara moja tu.
Hadi mwezi Oktoba 2011, kazi hii ilikuwa imeshakamilika kwa Asilimia 85 na inategemewa kukamilika mwezi Februari, 2012 kama Ratiba ya Sensa inavyoonesha.
82. Kazi nyingine ambayo imeshakamilika ni Sensa ya Majaribio iliyofanyika mwezi Oktoba, 2011 ambayo ilikuwa na lengo la kutathmini utendaji na muundo mzima wa kuendesha zoezi la Sensa mwakani. Lengo lingine la zoezi hilo lilikuwa kutathmini mtiririko mzima wa Maswali yatakayoulizwa kwa Watu wote watakaolala Nchini usiku wa kuamkia usiku wa Sensa pamoja na Teknolojia ya Kisasa itakayotumika katika uchambuzi wa Takwimu.
Mheshimiwa Spika,
83. Changamoto kubwa tuliyo nayo tangu Serikali ianze maandalizi ya Sensa hii mwaka 2004 ni gharama kubwa itakayotumika kujipanga kuhesabu Watu na kuchukua taarifa zao muhimu zikiwemo taarifa za umri, uraia, elimu, hali ya kazi, uzazi, vifo, hali ya ulemavu na mahali waliposhinda (day population) kwa muda usiopungua siku tatu na hususan katika Miji mikubwa. Serikali imejipanga kutenga Rasilimali Fedha za kutosha na kupata Rasilimali Watu ambao ni Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari. Lengo ni kujihakikishia kuwa Wananchi hawapotezi muda mrefu kuwasubiri Makarani wa kuhesabu Watu kuwatembelea katika Kaya zao, hususan katika Jiji la
Dar es Salaam. Serikali itajipanga vizuri kupitia Kamati Kuu ya Sensa ambayo inajumuisha Wizara zote na hususan Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuona namna ya kuweza kuwapata Walimu watakaohitajika.
84. Changamoto nyingine ni kuwepo kwa baadhi ya sehemu Nchini ambazo hazifikiki kwa urahisi, hasa sehemu zenye miinuko mikali, wanyama wakali, visiwa vingi vinavyokaliwa na wavuvi na sehemu zenye Watu wanaohamahama. Juhudi zinafanyika kuandaa namna bora ya kufika sehemu hizo kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia ndege, magari maalum, na vyombo vya kuaminika vya majini.
Mheshimiwa Spika,
85. Nichukue nafasi hii kuwashukuru Wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika hatua tuliyofikia ya Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Pia niwaombe tena, kuendelea na ushirikiano huo wa kuhakikisha Sensa ya mwaka 2012 inafanikiwa ili kuiwezesha Serikali kupanga Mipango endelevu ya Maendeleo. Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge ambao mpo karibu na Wananchi ni kuwaomba kuwaelimisha Wananchi katika Majimbo yenu kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ili waweze kushiriki kwa kikamilifu katika Sensa hii. Aidha,
niwakumbushe Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutimiza wajibu wao kama wasimamizi wakuu wa zoezi hili katika Mikoa na Wilaya zao.
UWAZI NA UWAJIBIKAJI KATIKA SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
86. Nchi yetu imeridhia kujiunga na Mpango wa Ubia katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi yaani “Open Government Partnership”. Mpango huu ambao ni juhudi mpya za Kimataifa katika kuendesha Serikali kwa uwazi na ushirikishwaji mkubwa wa Wananchi, ulizinduliwa rasmi na Viongozi wa Nchi za Marekani, Brazil, Indonesia,
Mexico, Norway, Philippines, Afrika ya Kusini na Uingereza mnamo tarehe 20 Septemba 2011 wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani. Msisitizo mkubwa wa Mpango huu ni kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali, kuwawezesha Wananchi kupata taarifa sahihi na kuzitumia kwa maendeleo yao, Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kusisitiza matumizi ya Teknolojia na Ubunifu katika kuimarisha Utawala Bora. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imeamua kutekeleza kwa uwazi shughuli zake,
tumedhamiria kushirikiana na Wadau katika ngazi zote kuhakikisha kwamba habari muhimu za utendaji wa Serikali zinatolewa kwa Wananchi na kuwashirikisha katika kufuatilia na kutoa taarifa katika ngazi husika pale wanapoona utendaji hauridhishi.
Mheshimiwa Spika,
87. Ili kuwa Mwanachama wa Mpango huo, Nchi zinatakiwa kuunga mkono Azimio la Uwazi katika Kuendesha Serikali; kuandaa Mpango Kazi kwa kushirikiana na Wananchi na kuweka utaratibu wa uwazi wa kutoa taarifa za utekelezaji wa Mpango Kazi huo.
Napenda kupitia Bunge lako Tukufu kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wote kwamba maandalizi ya Mpango Kazi Shirikishi umeanza kwa kushirikisha Wadau mbalimbali. Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora amezungumza na Waandishi wa Habari na kueleza kwa undani kuhusu Mpango huo. Vilevile, tarehe 15 Novemba 2011, Serikali ilikutana na Wadau kutoka Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia ambapo kwa pamoja walijadili kwa uwazi aina ya Mpango Kazi wa Kitaifa wanaoutaka na kubainisha maeneo ya kuanzia ili kutekeleza Mpango huo wa Uwazi. Mawasiliano zaidi na Wananchi yataendelea kupitia njia za barua, barua pepe,
simu za mkononi na tovuti ambazo anwani zake zimeshatolewa kwa Wananchi. Nawasihi Wananchi washiriki kikamilifu kutoa maoni yao kwa uwazi ili hatimaye tuwe na Mpango Kazi wa Kitaifa kwa manufaa yetu wote. Nawahakikishia Watanzania kwamba, maoni yenu yataheshimiwa na kuzingatiwa ipasavyo katika Mpango huo.
Mpango wa Kuboresha Lishe
Mheshimiwa Spika,
88. Kama nilivyolielezea Bunge lako Tukufu wakati wa Hotuba yangu ya Bajeti mwezi Juni 2011, Serikali imedhamiria kwa dhati kupambana na tatizo la Lishe Duni hapa Nchini. Katika kutekeleza Azma hiyo, tarehe 20 Septemba 2011, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliungana na Viongozi mbalimbali Duniani kujadiliana juu ya kuboresha Lishe hasa kwa Nchi zinazoendelea. Katika Mkutano huo, Viongozi hao walionesha dhamira ya kushirikiana na Serikali yetu ili kuongeza kasi ya kupambana na tatizo la lishe Duni hasa kwa siku 1,000 za kwanza za maendeleo ya Mtoto muda ambao Kitaalam ni muhimu sana katika maendeleo yote ya msingi ya Binadamu. Aidha, tarehe 19 Septemba 2011, nilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Lishe ambao utakuwa ndiyo Dira ya kutekeleza shughuli zote za kuboresha Lishe hapa Nchini.
Hivi sasa unaandaliwa Mpango wa Utekelezaji wa Mkakati huo utakaoweka malengo na viashiria vitakavyopimika na kuongoza ufuatiliaji na tathmini.
89. Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kwamba, suala la kuboresha Lishe linapewa umuhimu mkubwa na kuanzia Mwaka wa Fedha wa 2012/2013, Kasma maalum ya Lishe itaanzishwa kwenye Bajeti zetu. Nawasihi Wananchi kushirikiana na Serikali katika ngazi zote, ili kukabiliana na tatizo hili la Lishe Duni.
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA
Mheshimiwa Spika,
90. Kama Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wanavyofahamu tarehe 9 Desemba 2011, Taifa letu litahitimisha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa uzito unaostahili. Maadhimisho hayo yalianza mwezi Juni mwaka huu, ambapo Wizara, Taasisi, Mikoa pamoja na Sekta Binafsi zimekuwa zikifanya Maonesho kwenye maeneo yao na sehemu mbalimbali Nchini kuelezea mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na matarajio ya Miaka 50 ijayo kwa ajili ya Kumbukumbu ya Vizazi vijavyo. Utaratibu huo unafanyika kwa zamu baina ya Wizara na Mikoa na utaendelea hadi tarehe 30 Novemba 2011. Kuanzia tarehe 1 hadi 9 Desemba 2011, Maonesho hayo yatahamia Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam ambapo Wizara zote, Taasisi pamoja na Wadau wengine watashiriki.
Mheshimiwa Spika,
91. Napenda kutumia fursa hii kwa mara nyingine tena kuwatakia Watanzania wote Kheri na Mafanikio katika Kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Nawaomba Wananchi kuendelea kutembelea maonesho yanayofanyika kwa sasa katika sehemu mbalimbali Nchini ili kujielimisha juu ya mafanikio tuliyopata katika kipindi cha Miaka 50 ya Uhuru wetu wa Tanzania Bara pamoja na kutambua Changamoto zake. Tutambue kuwa tuna kila sababu kama Taifa kujivunia maendeleo tuliyoyapata kwa Miaka 50 kwa kuwa Tumethubutu, Tumeweza na Tunazidi Kusonga Mbele.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
92. Napenda kuhitimisha Hotuba yangu kwa kurejea machache kama ifuatavyo:
Moja: Tunayo kazi kubwa iliyoko mbele yetu ya kuunganisha nguvu kukabiliana na athari za Msukosuko wa Uchumi Duniani kwa kujenga Uchumi tulivu na kuhakikisha kuwa tunadhibiti Mfumuko wa Bei na Kushuka kwa Thamani ya Shilingi. Tushirikiane wote katika kila Nyanja zikiwemo Taasisi zetu za Fedha kwa kutekeleza maelekezo yatakayotusaidia kukabiliana na matatizo hayo;
Pili: Jukumu la Kuandaa Katiba ni letu sote Watanzania bila kujali Kabila, Rangi, Jinsia, Dini ama Itikadi za Kisiasa na Vyama. Kwa hili, Watanzania wote tuungane kulinda Umoja wetu, Amani yetu, Utulivu wetu na Mshikamano wetu uliodumu kwa Miaka 50 ya Uhuru wetu;
Tatu: Tumeanza vizuri katika maandalizi ya Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2011/2012. Tuwahimize Wakulima na wote wanaohusika na Upatikanaji na Usambazaji wa Mbolea, Mbegu na Pembejeo kuhakikisha kwamba zinawafikia Wakulima kwa wakati. Tuwahimize Wakulima kutumia Mvua zilizoanza kunyesha katika baadhi ya maeneo Nchini kwa kupanda mapema, kwani “Mvua za Kwanza ni za Kupandia”;
Nne: Tunalo jukumu la kuvutia na kufanya Uwekezaji mkubwa katika Nchi yetu. Nawaomba, tuunganishe nguvu zetu kutangaza fursa zilizopo Kikanda kwa ajili ya Uwekezaji katika maeneo yetu. Kila Mkoa utenge Ardhi kwa ajili ya Uwekezaji na kutangaza fursa zilizopo Kikanda ili kuleta msukumo wa pamoja katika kuvutia Wawekezaji kwenye maeneo hayo;
Tano: Bado tunalo tatizo la Vitendo vya Uhalifu Nchini, ikiwa ni pamoja na Uhamiaji Haramu na uhalifu kwa Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.
Nawaomba Wananchi wote kushirikiana na Vyombo vya Dola kuongeza Nguvu katika kuhakikisha Vitendo hivyo vinakomeshwa;
Sita: Serikali imefikia hatua za mwisho za kukamilisha Zoezi la kuandaa Vitambulisho vya Taifa. Tushirikiane kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa suala hili ambalo halina Chama wala Itikadi. Tuungane kuhakikisha kwamba mafanikio ya zoezi hili yanapatikana na kila Mtanzania anapata haki yake kwa kupata Kitambulisho cha Taifa; na
Saba: Maandalizi ya Sensa itakayofanyika mwezi Agosti 2012 yanaendelea. Tushirikiane kuwaelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa zoezi hilo.
Mheshimiwa Spika,
93. Nimalizie kwa kuwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Tano wa Bunge. Nikushukuru kipekee wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge hili. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Namshukuru Katibu wa Bunge, na Wasaidizi wake kwa huduma mbalimbali ambazo zilifanikisha Mkutano huu. Ninawashukuru Maafisa wote wa Serikali pamoja na Madereva waliotuleta hapa salama na ambao wataturudisha kwenye maeneo yetu ya Makazi na Kazi. Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, ninaushukuru Uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Vyombo vya Dola kwa kutuangalia vizuri tangu tulipofika hapa Mkoani. Kwa wote, nasema Asanteni Sana!
Mheshimiwa Spika,
94. Nitumie nafasi hii sasa kuwatakia wote safari njema kurudi katika maeneo yenu ya kazi. Vilevile, niwatakie wote Maadhimisho mema ya Miaka 50 ya Uhuru, Sikukuu Njema ya Krismas na Kheri ya Mwaka Mpya wa 2012.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu atufikishe sote salama mwaka 2012 ili tuweze sote kukutana katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
95. Baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi siku ya Jumanne tarehe 7 Februari, 2012, Saa Tatu Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa Sita hapa Mjini Dodoma.
96. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.