Na Zamaradi Kawawa, MAELEZO, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajiwa kulihutubia Bunge Maalum la Katiba Kati ya Jumanne na Jumatano wiki ijayo. Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta ameliambia bunge Mara baada ya kuapishwa na kukabidhiwa kiti chake jana jioni.
Alisema kazi ya kuwaapisha wabunge wote iliyoanza jana jioni itakuwa ikifanyika hadi saa 3 usiku na kukamilika Jumapili hii Machi 16, 2014. Jumatatu wiki ijayo saa 10 jioni bunge hilo litakabidhiwa rasmi rasimu ya katiba na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba.
Sitta ameliambia bunge hilo kuwa wabunge watakuwa na mjadala wa jumla kwa siku tatu kuhusu malengo na muelekeo wa Katiba mpya kabla ya kugawanyika katika Kamati mbali mbali kwa kazi rasmi.
Mwenyekiti Sitta amemshukuru na kumpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kwa ustahimilivu, busara, hekima na uvumilivu aliouonesha wakati akiliongoza bunge hilo kuandaa kanuni zake kwa kipindi cha wiki tatu.
Alisema kazi ya kuandaa kanuni ilifanywa bila kanuni hivyo baadhi ya wabunge walitumia fursa hiyo kufanya vitendo visivyokubalika. aliwakumbusha wabunge kuwa kanuni zimepatikana na hivyo wazifuate vinginevyo wasije wakamlaumu pale atakapochukua hatua kwa ukiukwaji wa kanuni hizo.
Akiwaaga wabunge wa bunge, Kificho aliwaasa kuwa na hekima, busara, subira na hoja zenye mashiko wakati wakifanya kazi hiyo na kuangalia zaidi maslahi ya taifa ili kuwapatia wananchi Katiba ambayo haitawagawa bali itakayoimarisha umoja na mshikamano wao.
Mwenyekiti, Sitta na Makamu wake, Bi. Samia Suluhu Hassan waliapishwa jana jioni na Katibu wa Bunge la Katiba, Bw. Yahya Khamis Hamad aliyekuwa na Naibu wake, Bw. Thomas Kashililla.