Hotuba ya JK Katika Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete


HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI,
TAREHE 12 MEI, 2014 – MKOANI ARUSHA

Mheshimiwa Dkt. Kebwe Stephen Kebwe(Mb) – Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mheshimiwa Stanslaus Magesa Mulongo – Mkuu wa mkoa wa Arusha;
Ndugu Paul Magesa – Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania;
Ndugu Clavery Mpandana – Muuguzi Mkuu wa Serikali;
Daktari Khadija Malima, Mwenyekiti wa Baraza la Wauuguzi Tanaznia na Chama cha Wauguzi Tanzania;
Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Ndugu Rais na viongozi wenzako wa Chama cha Wauguzi na Wakunga (TANNA) kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuja kujumuika nanyi katika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Wauguzi Duniani. Nakupongeza pia Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na wananchi wote wa Arusha kwa kutupokea vizuri na kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hii na kushiriki kwa ukamilifu katika kufanikisha maandalizi yake.
Nawapongeza nyote kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho haya. Hakika yamefana sana. Nimefurahishwa na maonesho kuhusu baadhi ya shughuli zinazofanywa na wauguzi katika kuwahudumia Watanzania. Maonesho ya aina hii husaidia sana kukuza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yenu, wajibu wenu na mchango wenu katika kuimarisha afya za Watanzania. Pamoja na kutembelea mabanda ya maonyesho, nimeshuhudia maandamano yenu na kusoma ujumbe kwenye mabango ya washiriki. Pia nimesikiliza Risala yenu iliyosomwa kwa ufasaha na utulivu mkubwa na Rais wa Chama cha Wauguzi Ndugu Paul Magesa. Kwa ujumla, maadhimisho haya yanadhihirisha kuwa wauguzi ni kiungo muhimu sana katika utoaji na maendeleo ya huduma ya afya nchini na ni nguvu thabiti ya mabadiliko.
Kauli Mbiu
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi na ndugu wananchi;
Nilipopata mwaliko kutoka kwenu sikusita kukubali kuja kujumuika nanyi siku ya leo kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kwamba wauguzi ni kada muhimu sana katika utoaji na maendeleo ya huduma ya afya nchini. Bila ya kuwepo wauguzi huduma ya afya itayumba. Natambua kuwa Wauguzi ni zaidi ya asilimia 60 ya watumishi wote wa sekta ya afya na hutekeleza asilimia 80 ya shughuli zote za afya. Aidha, Muuguzi ndiye mwenye kuandaa mazingira mazuri kwa daktari kutekeleza majukumu yake. Daktari anapomaliza kumuona mgonjwa, na kutoa maelekezo yake, Muuguzi husimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na tiba yenyewe. Muuguzi ndiye anayefanya kazi ya kuuguza mgonjwa. Sote ni mashahidi kuwa wagonjwa wanatumia wakati mwingi zaidi mikononi mwa wauguzi kuliko muda wanaoutumia mikononi mwa wahudumu wengine wa afya.
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Sababu ya pili ni kwamba nimevutiwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo; “Wauguzi ni Nguvu ya Mabadiliko na Rasilimali Muhimu ya Afya”. Ni kauli mbiu sahihi na mwafaka kabisa. Ni ukweli ulio wazi kuwa wauguzi wanayo nafasi maalum katika maendeleo ya huduma ya afya na sekta yenyewe kwa jumla. Ni chachu muhimu ya mabadiliko katika sekta ya afya, na ndiyo rasilimali ya kuwezesha mabadiliko hayo kutokea na kufanikiwa.
Huwezi kuzungumzia mabadiliko katika sekta hii bila kutambua mchango wa Wauguzi na kuwahusisha. Ujenzi wa miundombinu ya vituo vya kutoa huduma ya afya, ununuzi na usambazaji wa madawa, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa katika hospitali zetu vitakuwa na maana tu pale ambapo wauguzi wapo na wanatimiza wajibu wao ipasavyo. Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa hakuna mbadala wa wauguzi.
Ndugu Wananchi;
Uangalizi unaotolewa na wauguzi, upendo na huruma yao husaidia sana kurejesha matumaini ya wagonjwa na watu wengine wanaojishughulisha na maendeleo ya huduma ya afya. Huongeza ari ya mapambano dhidi ya maradhi na kuleta matumaini kwamba ushindi utapatikana. Ninyi ndiyo kioo cha huduma ya afya. Ndiyo watu wa kwanza mnaokutana na wagonjwa wanapofika hospitali, na ni watu wa mwisho kuwaona wanapotoka baada ya matibabu.

Mheshimiwa Naibu Waziri;
Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi na ndugu Wananchi;
Kuboresha huduma ya afya ni moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ninayoiongoza na ndiyo maagizo ya Ilani ya Uchanguzi ya Chama Tawala – CCM. Kwa sababu hiyo tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulitoa umuhimu wa pekee kwa zoezi la kupitia upya Sera ya Afya ya mwaka 1997 kwa lengo la kuihuisha. Matokeo yake ni kupatikana kwa Sera Mpya ya Afya ya mwaka 2007 na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi wa mwaka 2007 uliotengenezwa maalum kuongoza utekelezaji wa Sera hiyo.
Kama mjuavyo huu ni mpango wa miaka kumi mpaka mwaka 2017 unaolenga kuleta mageuzi na maendeleo makubwa katika sekta ya afya. Kwa muhtasari tumepanga kufanya mambo makuu mawili. Kwanza, kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi wananchi kwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya. Pili, kuimarisha ubora wa huduma ya afya inayotolewa kwa wananchi kwa kuvipatia vituo hivyo vifaa vya uchunguzi na tiba vilivyo bora pamoja na dawa za kutosha. Pia kuvipatia rasilimali watu, kwa maana ya Madaktari, Waganga, Wauguzi, Wakunga na Wataalamu wengine wa afya.
Ndugu Wauguzi na Ndugu Wanannchi;
Leo miaka karibu saba baadae ninyi ndiyo mashahidi wa mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Mpango huu. Tumefanikiwa kwa kiasi cha kutia moyo ingawaje bado tunayo kazi kubwa mbele yetu. Kwanza kabisa tumeongeza sana bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.4 mwaka 2013/2014. Imekuwa bajeti ya tatu kwa ukubwa baada ya elimu na miundombinu kutoka ya sita. Kwa sababu ya ongezeko hilo tumeshuhudia mambo mengi mazuri yakifanyika katika kuboresha huduma ya afya nchini. Kwa mfano, zahanati ziko 5,960 ukilinganisha na 4,930 zilizokuwepo mwaka 2007. Vituo vya afya viko 716 ukilinganisha na 565 na hospitali ziko 249 ukilinganisha na 230 wakati ule.
Kazi kubwa imefanyika kuimarisha hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kazi bado inaendelea na tunaweza kusema ndiyo kwanza imechanganya. Miundombinu imeongezwa na majengo mengine yanaendelea kujengwa. Huduma zinaendelea kuboreshwa na nyingine ambazo hazikuwepo zimeanzishwa. Hali kadhalika vifaa tiba na uchunguzi vya kisasa vimeendelea kuwekwa na uwezo wa hospitali kuchunguza na kutibu maradhi umekuwa mkubwa.
Tumeendelea kupanua fursa za mafunzo na ajira kwa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wengine wa afya. Kwa upande wa mafunzo kwa mfano Madaktari waliojiunga na mafunzo wameongezeka kutoka 520 mwaka 2005 hadi 1,057 hivi sasa. Kwa Wauguzi na Wakunga wameongezeka kutoka 1,586 mwaka 2005 hadi 3,569 hivi sasa, kwa jumla kila kada imeongezeka. Ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili pale Mloganzila itaongeza sana uwezo wetu wa kufundisha Madaktari na Wauguzi kutoka Chuo hicho kutoka 3,000 mpaka 15,000. Ukiongeza na wanafunzi 5,000 wa Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma tatizo la rasilimali watu nchini litapatiwa ufumbuzi miaka michache ijayo. Tayari ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia ya vitanda 600 umeanza pale Mloganzila. Hospitali hiyo nayo itaimarisha ubora wa huduma ya uchunguzi na tiba ya maradhi kwa namna yake hapa nchini. Hali kadhalika ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia pale UDOM unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Hivyo hivyo, kwa upande wa ajira nako kumekuwa na ongezeko. Idadi ya Madaktari waliosajiliwa imeongezeka kutoka 1,339 mwaka 2006 hadi 3,133 na Wauguzi kutoka 20,115 mwaka 2007 hadi 34,740 hivi sasa. Aidha, katika kipindi cha miaka 3 iliyopita, tumeajiri wauguzi 8,659 na tunatarajia kuajiri wengine 1,152 kabla ya Julai, 2014. Tutaendelea kufanya hivyo mwaka ujao wa fedha na miaka inayofuatia. Hii itasaidia kupunguza mzigo wa kazi mlio nao sasa hivi ambao mmeutaja kwenye risala yenu.
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Kwa upande wa maslahi nako, tumejitahidi kuboresha, najua bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Bado mishahara ni midogo lakini hatujafika mwisho, tunaendelea kuboresha. Tumekuwa tunaongeza kila mwaka na tutaendelea kufanya hivyo mwaka huu na miaka ijayo.
Risala ya Wauguzi
Ndugu Wauguzi,
Nimesikiliza kwa makini risala yenu iliyowasilishwa vizuri na Ndugu Paul Magesa, Rais wa Chama cha Wauguzi na Wakunga. Namna ambavyo ameiwasilisha, lugha aliyotumia kuiwasilisha na jinsi mlivyoishangilia inathibitisha kuwa risala hii ni shirikishi, na yaliyosemwa ni mambo muhimu kwa wauguzi kwa ujumla wenu. Ni risala iliyosheheni ukweli kuhusu mafanikio tuliyoyapata na mambo yanayowatatiza mnayotaka yapatiwe ufumbuzi. Kuna ushauri mzuri uliotolewa kuhusu nini kifanyike kuboresha mazingira ya kazi ya Wauguzi na huduma ya afya nchini. Lazima nikiri kuwa nimeguswa sana na ahadi yenu ya kuendelea kufanya kazi kwa mujibu wa viapo vyenu, licha ya changamoto zilizopo.
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inaelewa mchango wenu muhimu na inauthamini sana hivyo basi, sisi tutakuwa watu wa mwisho kupuuza mambo ya wauguzi. Kama kuna jambo halijafanyika haitokani na kupuuza au ukosefu wa dhamira ya kuyashughulikia bali kuna sababu fulani fulani za msingi zinazotukwaza katika utekelezaji wake.
Nimefurahishwa sana na dhamira yenu njema ya kutaka kuona mabadiliko yanafanyika katika sekta ya afya na ninyi kuwa sehemu kamili ya mabadiliko hayo. Ndiyo maana sehemu kubwa ya risala yenu ina mapendekezo ya mambo ya kubadilisha ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya. Nawaunga mkono kwa msimamo wenu huo. Nimefarijika sana kusikia kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara nyingine za Serikali kuwa mambo mengine yametekelezwa na yapo ambayo tunaendelea kuyatekeleza. Hata hivyo, bado yapo mambo ambayo tunayavutia pumzi kwa maana ya kujenga uwezo wa kuyatekeleza.
Ndugu Wauguzi;
Hii ni mara ya tatu napata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Wauguzi. Mara ya kwanza ilikuwa Mnazi Mmoja mwaka jana, mara ya pili Ikulu tarehe 29 Aprili, 2014 na leo ndiyo mara ya tatu hapa Arusha. Jambo mojawapo muhimu nililojifunza ni kuwa mambo mengi yanayowatatiza wauguzi, ambayo pia yameainishwa katika risala yenu leo, yanaweza kumalizwa kwa kuboresha mawasiliano na mahusiano kati yenu na Wizara zinazohusika na kati yenu (wauguzi) na kada nyingine katika sekta ya afya. Naamini kama hayo yakifanyika mambo mengi yatapatiwa ufumbuzi na kwamba yatabaki machache yanayohitaji msaada wa ngazi za juu. Hii itasaidia kuondoa kutiliana mashaka, kutokuaminiana na hisia za kupuuzwa kwa wauguzi. Nimeona nitumie fursa ya maadhimisho haya ya leo kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala tuliyozungumza siku zilizopita na yaliyoibuliwa hapa leo kwenye mabango na risala.
Madai ya Wauguzi
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi,
Katika risala yenu mmezungumzia mambo yahusuyo muundo wa utumishi, mafunzo, posho, huduma ya makazi na mambo mengineyo muhimu. Mambo yote haya ni ya msingi na napenda kuwahakikishia kuwa tutayachukulia kwa uzito unaostahili na tutayafanyia kazi ipasavyo ili tuwatengenezee mazingira mazuri ya kufanya kazi zenu.
Muundo wa Utumishi wa Uuguzi
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
NduguWauguzi;
Kwanza kabisa nawapongeza kwa kukamilisha mapendekezo ya Muundo wa Utumishi. Nitawasaidia kufuatilia kwa mamlaka husika ili uamuzi ufanyike mapema iwezekanavyo. Kukamilika kwa zoezi hilo kutatoa ufumbuzi kwa mambo mengi yanayowatatiza hivi sasa. Itayaweka sawa masuala ya upandishaji wa vyeo. Itawezesha kutambuliwa ipasayo kwa wauguzi wanaomaliza shahada za uzamili na uzamivu. Kwa kweli nashangaa kwa nini watu waliojiendeleza kiasi hicho wapate taabu ya kutambuliwa inavyostahili katika utumishi wa uuguzi.
Hivyo hivyo nashangaa tena napata taabu kuamini kuwa mtumishi akienda masomoni kuongeza ujuzi anasimama kupanda cheo au hata kushushwa cheo. Haya ni ya kustaajabisha mambo ambayo hayastahili kufanyika. Naomba Wizara na mamlaka husika zihakikishe kuwa uonevu huu hauendelei kufanyika. Iweje leo kujiendeleza iwe ni balaa kwa mfanyakazi na mwajiri badala ya kuwa jambo jema kwa wote.
Ndugu Wauguzi;
Nadhani suala la uanzishwaji wa Kurugenzi ya Uuguzi ndani ya Wizara ya Afya limefikia hatua nzuri. Nimeambiwa kuwa Wizara iliridhia maombi yenu na kuyawasilisha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Wataalamu wa Mifumo katika Idara Kuu ya Utumishi walichoshauri ni kuwa Sehemu ya Uuguzi sasa ipandishwe hadhi na kuwa Kitengo cha Uuguzi kitakachoongozwa na Mkurugenzi. Nimeambiwa pia kwamba Wizara ya Afya imekubali na tayari imefanya marekebisho na kuwasilisha upya pendekezo hilo. Nimesikia kuwa jambo hili litakamilishwa muda si mrefu na huenda muundo huo ukaanza tarehe 1 Julai, 2014 hivyo kuhitimisha maombi yenu. Niruhusuni niwapongeze kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa.
Maslahi ya Watumishi
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, hususan mishahara na posho mbalimbali ni mambo ambayo Serikali imeyapa kipaumbele. Tumekuwa yunafanya hivyo kila mwaka na tutaendelea kufanya hivyo. Maombi yenu tumeyapokea na tutayafanyia kazi. Napenda kusema hata katika Bajeti ya mwaka ujao wa fedha hatua kiasi fulani zitachukuliwa.
Nimesikia kilio chenu kuhusu posho zilizoamuliwa kutokutekelezwa na ile ya sare za kazi ambayo imeahidiwa na kuongezwa kutoka shilingi 150,000 na kuwa Shilingi 300,000 kutokamilishwa mpaka sasa. Nitatoa maagizo kwa mamlaka husika katika Serikali kufuatilia na kuwabana, watakaokaidi. Hivyo hivyo, kwa posho ya kufanya kazi usiku, kama ilishaamuliwa ilipwe, mamlaka husika zitatakiwa kutekeleza bila ajizi.
Nyumba za Wauguzi
Serikali inatambua umuhimu wa wauguzi kuwa na makazi karibu na maeneo yao ya kazi. Kwa kutambua umuhimu huo Serikali imekuwa inatenga fedha za kujenga nyumba za madaktari na wauguzi kila mwaka. Hata hivyo kasi ya ujenzi ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa mahitaji kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Tutatafuta njia nyingine za kuharakisha ujenzi wa nyumba hizo. Mipango hiyo ikikamilika mtaona matokeo yake. Kwa sasa tutaendelea na kazi ya ujenzi wa nyumba katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Tabora na Mara.
Nimelipokea pendekezo lenu la kutaka msaidiwe kupata viwanja vya kujenga nyumba. Nitaagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wawasaidie. Miaka miwili iliiyopita niliagiza utengenezwe mpango maalum wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa umma. Matayarisho yanaendelea, ukikamilika utasaidia wafanyakazi wa umma wakiwemo Wauguzi kujipatia nyumba za kuishi.

Udhamini wa Mafunzo
Ndugu Rais wa Wauguzi;
Ndugu Wauguzi,
Nimesikia rai yenu ya kutaka Serikali itoe udhamini kwa wanafunzi wanaosomea shahada ya kwanza ya uuguzi kama tunavyofanya kwa wale wanaosomea udaktari. Nakubali maombi yenu, nitaagiza mamlaka husika walifanyie kazi. Kama hivi sasa wanafunzi hao siyo wengi tunaweza kuanza hata bajeti ijayo lakini kama ni wengi itabidi tuanze mwaka wa fedha wa 2015/16 lazima tujipange vizuri kwani inahusu pesa.
Naamini uamuzi huu utahamasisha wauguzi kujitokeza kwa wingi kujiendeleza kitaaluma. Wauguzi wasiishie kwenye Cheti na Diploma bali waende zaidi ya hapo. Napenda kuwahakikishia pia kwamba pamoja na uamuzi huu, Serikali bado itaendelea kudhamini wauguzi wanaosomea shahada ya uzamili na uzamivu kama tufanyavyo sasa. Nimesikia utayari wenu wa kupewa nafasi za uongozi katika Wizara ya Afya na kwingineko kama tulivyofanya kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Wito kwa Wauguzi
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi,
Tunapoadhimisha siku ya wauguzi, tunakumbuka pia siku ya kuzaliwa kwa Bi. Frorence Nightlingale, mwanzilishi wa taaluma na fani hii adhimu ya uuguzi. Mama Nightlingale aliyeishi kati ya mwaka 1820 hadi 1910 ndiye aliyeanzisha shule ya kwanza ya wauguzi huko London katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas. Alianzisha huduma hii baada ya uzoefu wake katika kuwashughulikia majeruhi wa kivita, na wanajeshi wagonjwa wakati wa vita.
Sifa yake kubwa ilikuwa ni wito na moyo wa kujitolea na huruma vitu ambavyo aliamini ndio misingi ya kuwa muuguzi. Alipata kunukuliwa akisema, “Kama muuguzi atakacha kutoa huduma kwa sababu yoyote ile au kusema haimuhusu, basi uuguzi kwake sio wito”. Kutokana na maisha yake ya kuwaangazia nuru wagonjwa na kuwatembelea usiku akiwa na taa ya kandili kuwafariji na kuwahudumia, alipewa jina la “Mwanamke Mwenye Kutembea na Nuru”.
Ndugu Wauguzi;
Ninyi ni watu wenye dhamana kubwa juu ya maisha ya watu na mnategemewa sana. Nawapongeza kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo. Kwa sababu yenu mmeokoa maisha ya watu wengi na kuwapunguzia maumivu wagonjwa. Wakati mwingine moyo wenu kuonyesha kujali, upendo na huruma hutoa matumaini kwa mgonjwa na kumrejeshea siha yake. Hivyo, nawaomba muendelee kuwa na kauli nzuri na nyuso zenye tabasamu na nyoyo za huruma na upendo kwa wagonjwa. Tabia hiyo ni tiba ya aina yake.
Nimeona niikumbushe hadithi ya muasisi Mama Florence Nightngale ili kuwaomba wakati wote iwaongoze na muendelee kukumbushana kuizingatia. Minong’ono kuwa mienendo ya baadhi yenu inalalamikiwa na wagonjwa kuwa hailingani na mafundisho ya muasisi wa kazi hii adhimu inanisumbua sana. Kama nilivyosema awali, ninyi ndiyo watu wa kwanza mnaokutana na mgonjwa akifika hospitali na ni watu wa mwisho anapotoka hospitali baada ya matibabu. Ikiwa mtakuwa na nyuso za ukatili na ulimi mkali au wa kebehi, mtakuwa mnawakwaza wagonjwa na hata kuongeza ukali wa maumivu yao. Wengine wanaweza kukata tamaa na hata kupoteza uhai. Msifanye watu wajutie kufika zahanati au hospitali. Narudia kuwasihi mzingatie kiapo chenu na maudhui ya kauli mbiu yenu ya kutaka mabadiliko. Kwa maana nyingine naomba mtambue kuwa kauli mbiu yenu ya mabadiliko inawahusu na nyie pia kama inavyotuhusu sote. Lazima mabadiliko yaanze na ninyi wenyewe.
Homa ya Dengue
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba nizungumzie ugonjwa mpya wa Homa ya Dengue uliojitokeza katika jiji la Dar es Salaam hivi karibuni. Huu si ugonjwa asili kwetu. Ni ugonjwa wa huko Asia na Bara la Amerika lakini ndiyo umeshafika. Kwa mara ya kwanza ugonjwa huu ulijitokeza Jijini Dar es Salaam mwaka 2010 na kuathiri watu 40 ambao walipatiwa matibabu na kupona. Ugonjwa huu ulitoweka lakini ukaibuka tena Mei na Juni, 2013 ulipojitokeza tena na kuwakumba watu 172. Mwaka huu ugonjwa huo umerudia tena kwa kasi kubwa zaidi. Kati ya Januari na Aprili 6, mwaka huu wagonjwa 399 wamethibitika kuugua katika Jiji la Dar es Salaam. Kati ya wagonjwa hao 322 walitoka Wilaya ya Kinondoni, 61 Wilaya ya Ilala na 16 Wilaya ya Temeke. Kwa bahati mbaya wawili kati yao walipoteza maisha.
Ndugu wananchi;
Wataalamu wa afya wanasema kuna aina tatu za ugonjwa wa dengue. Aina ya kwanza ni Homa ya Dengue, aina ya pili ni Dengue ya Damu na aina ya tatu ni Dengue ya Kupoteza Fahamu. Hapa kwetu Homa ya Dengue ndiyo ugonjwa uliothibitika kuathiri wagonjwa wote. Homa hii ina dalili kubwa tatu: homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa, na maumivu ya viungo au uchovu. Kwa vile dalili za ugonjwa huu zinafanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria, ipo hatari kwa watu waliozoea kutumia dawa bila kupima kumeza dawa za malaria wakati wanaugua Homa ya Dengue. Wakifanya hivyo watahatarisha maisha yao. Natoa wito kwa mtu yeyote anayejisikia dalili hizi aende hospitali akapimwe; asinywe dawa bila kupima kama baadhi yetu tulivyozoea. Ni hatari kwa maisha yetu.
Ndugu Wananchi;
Ugonjwa huu unaambukizwa na mbu aina ya Aedes akishamuuma binadamu. Tena huuma mchana. Hatua za kupambana na mbu huyu ni sawa na zile zinazochulikuwa kupambana na mbu wa Anopheles anayeambukiza malaria. Watu waendelee kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kupaka dawa za kuzuia kuumwa na mbu na kuharibu maeneo ya mazalia ya mbu.
Nimetoa maelekezo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa Bohari Kuu ya Madawa ya Serikali (MSD) wanaleta kits za kupimia maradhi haya (Dengue Rapid Test Kits) za kutosha na kuzisambaza kwenye hospitali na vituo vya afya. Nimeambiwa hivi sasa vipimo hivi havipo vya kutosha. Hii ni dharura ya kitaifa ambayo lazima ipewe uzito na uharaka unaostahili na Wizara ya Afya na Hazina.
Hitimisho
Ndugu Rais wa Chama cha Wauguzi;
Ndugu Wauguzi;
Niruhusuni nimalize hotuba yangu kwa kurudia kuwashukuru kwa kunialika na kwa risala yenu nzuri. Nimejifunza mengi na kama nilivyosema, nakwenda kuifanyia kazi risala yenu na yote niliyosikia na kuona yanayohitaji kuchukuliwa hatua. Yale masuala ya kimuundo na mengineyo nitakwenda kuyakwamua huko yalikokwama, ili utekelezaji uanze. Yale yahusuyo posho, kama nilivyoeleza, baadhi yake yatashughulikiwa katika bajeti ijayo na mengine tutaendelea kuyashughulikia kadri uwezo utakavyoruhusu.
Ninachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kuwa tunawapenda, tunatambua umuhimu wenu na tunawathamini sana. Katu hakuna upungufu wa dhamira bali tunakwazwa na uwezo mdogo wa mapato ya Serikali kuweza kutosheleza mahitaji yote ya kuboresha huduma ya afya na maslahi kwa watumishi wa afya nchini. Narudia kusisitiza kuwa kamwe sio kutokana na kukosekana kwa utayari wa kutatua changamoto zinazowakabili wauguzi au watumishi wengine wa umma.
Upo ushahidi wa wazi wa juhudi za Serikali ninayoiongoza ya kufanya mambo mengi makubwa na madogo ya kuboresha mazingira ya kazi kwa kila kada na sekta kadiri uwezo unavyoruhusu. Mtakubaliana nami kuwa hali ya kada ya wauguzi ilivyo leo, si sawa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. Tumepiga hatua kiasi chake lakini bado tuna safari ndefu na tutaendelea kufanya zaidi. Ni dhahiri kwamba tumesogea kutoka pale tulipokuwa, ingawa hatujafika tunapodhamiria kwenda. Kwa vile msimamo na muelekeo wetu ni sahihi, naamini baada ya muda si mrefu tutafika. Penye nia pana njia. Inawezekana Timiza Wajibu wako.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.