Hotuba ya Dkt Jakaya Wakati wa Uzinduzi wa Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa

Nawapongeza sana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya Chakula na Dawa, kwa hatua kubwa mliyofikia ya kuwa na maabara ya kisasa ya uchunguzi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba inayotambuliwa kimataifa

HOTUBA YA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA UZINDUZI WA MAABARA YA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA TAREHE 18 MACHI, 2013

Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi (Mb.), Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Mheshimiwa Said Meck Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam;
Mheshimiwa Margaret Sitta (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii;
Bw. Hiiti Sillo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa;
Viongozi wa Serikali na Wawakilishi wa Wadau wa Maendeleo Mliopo Hapa;
Wakurugenzi na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana:

Kwanza kabisa napenda kutumia fursa hii kumshukuru Dkt. Hussein Mwinyi na uongozi wa TFDA kwa kunishirikisha kwenye tukio hili la kihistoria la kuzindua maabara ya kisasa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa. Nilikuwa na shauku kubwa ya kuja kuiona maabara hii baada ya kusikia sifa zake.
Nawapongeza sana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya Chakula na Dawa, kwa hatua kubwa mliyofikia ya kuwa na maabara ya kisasa ya uchunguzi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba inayotambuliwa kimataifa. Sasa TFDA imekamilika. Mnao uwezo mkubwa wa kuchunguza na kutambua kwa uhakika ubora na usalama wa bidhaa hizo. Kazi yenu inawezesha Serikali na mamlaka husika kuchukua hatua zinazostahili kuzuia athari mbaya kutokea na pale inapotokea kukabili athari zake. Naungana na Mheshimiwa Waziri kuwashukuru kwa dhati washirika wetu wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa wa kuimarisha maabara hii pamoja na mifumo ya udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa iliyojengwa TFDA.
Mabibi na Mabwana;
Nimefurahishwa sana na kazi nzuri zinazofanywa na TFDA katika kutekeleza majukumu yake. Mmepata mafanikio makubwa na kuwafanya kuwa moja ya taasisi bora na ya mfano Barani Afrika. Ninawapongeza sana kwa mafanikio mliyopata ikiwa ni pamoja na maabara ya TFDA kuwa ya kwanza barani Afrika miongoni mwa maabara za Serikali za udhibiti wa bidhaa kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Endeleeni kupeperusha bendera ya nchi yetu.
Aidha, nawapongeza kwa kupata hati ya ithibati kwenye uchunguzi wa chakula na mikrobiolojia kwa kiwango cha kimataifa kutoka “Southern African Development Community Accreditation Services” (SADCAS). Hii itasaidia sana kuhakiki ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini ambazo zinapelekwa kwenye soko la nje ya nchi. Ubora wake ukipitishwa hapa hakuna maabara nyingine itakayosema vinginevyo.
Mabibi na Mabwana;
Sote tumesikia hapa kwamba kutokana na kutambuliwa kimataifa nchi mbalimbali zimeanza kuitumia maabara hii kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa ubora na usalama wa bidhaa zao. Ni vyema na sisi wenyewe tukaitumia vizuri maabara hii. Natoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, kwa wenye viwanda, wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha kuwa wanaitumia maabara hii kwa ajili ya kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa zao. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii isaidie kutangaza maabara hii ndani na nje ya nchi ili wananchi na wadau wote waweze kuifahamu na kutumia huduma zake.
Nawaomba wafanyakazi wa TFDA kuzingatia viwango vya kimataifa katika utendaji wenu. Mafanikio hayo yawe chachu ya kuongeza ufanisi kiutendaji ili kufikia dira mliyojiwekea ya kuwa Mamlaka inayoongoza barani Afrika katika udhibiti wa ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba kwa wote. Mkifikia dira hiyo, mtakuwa mmetekeleza kwa ukamilifu jukumu mlilopewa na Serikali la kulinda afya ya jamii ya Watanzania na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wangu sina shaka kuwa mtaendelea kuwa mfano mzuri kwa taasisi nyingine za umma hapa nchini. Hivyo, dumisheni weledi na uadilifu mafanikio haya ili mlinde heshima na sifa nzuri ya TFDA ndani na nje ya nchi. Endelezeni ushirikiano na wadau mbalimbali katika kutekeleza majukumu mliyopewa na Serikali. Ongezeni nguvu katika udhibiti wa bidhaa bandia na zenye ubora duni ambazo zimekuwa zikijitokeza katika soko na hivyo kuhatarisha afya za watumiaji.
Napenda kuwaahidi kuwa Serikali itawasaidia kukabili changamoto zinazowakabili na kuboresha mazingira yenu ya kazi. Tutawasaidia mjenge mtandao mpana kote nchini na kusaidia upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika ikiwa ni pamoja na watu na vifaa. Lengo letu ni kuona Mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Tutaongeza juhudi kuhakikisha wataalamu wa kuhudumia vifaa vya maabara hapa nchini wanaongezeka kwa kupanua mafunzo hayo kwenye vyuo vyetu vya afya. Aidha, tutaendelea kuongeza fedha za kununulia vifaa vya kupimia viuatilifu na vifaa tiba pamoja na kuimarisha mafunzo ya wataalamu wenu.
Baada ya kusema hayo, sasa ninayo furaha kuzindua rasmi Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa.
Aksanteni sana kwa kunisikiliza.