HOTUBA YA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA (MARA DAY), BUTIAMA-MARA
TAREHE 15 SEPTEMBA 2015
Waheshimiwa Mawaziri kutoka Tanzania na Kenya;
Makatibu Wakuu wa Wizara;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Magavana wa Majimbo;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Caunt kutoka Kenya;
Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria;
Wataalam kutoka Wizara, Taasisi mbalimbali Kenya na Tanzania;
Wadau wa Maendeleo;
Wawakilishi wa Jumuiya za Watumiaji Maji;
Ndugu Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana
Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na kutuwezesha kukusanyika hapa siku ya leo kushuhudia tukio hili muhimu. Napenda nitumie nafasi hii pia kuwashukuru waandaji wa shughuli hii, kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika siku hii ya pekee ambayo wadau wa Bonde la Mto Mara, wanakutana katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day). Nimepokea mwaliko huu kwa mikono miwili, nasema; Asanteni Sana! Nitumie fursa hii pia kuwakaribisha mkoani Mara, hususani hapa Butiama, wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania. Nasema Karibuni Sana Butima. Jisikieni mpo nyumbani. Hili ni eneo lenye historia kubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla kwani ndipo alipozaliwa na alipolala, Baba wa Taifa letu na Mtetezi wa Wanyonge Barani Afrika na Duniani kwa ujumla, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi). Napenda pia nitumie nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa sherehe hizi na wadau mbalimbali waliochangia kwa namna moja ama nyingine kufanikisha shughuli hii. Endeleni na moyo huo, fanyeni kila linalowezekana kuzidi kuboresha jambo hili mwaka hadi mwaka.
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Tukio la leo linatoa fursa kwa wadau kutoka nchi mbili, Tanzania na Kenya zinazopitiwa na Bonde la Mto Mara, kukutana pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya uhifadhi na matumizi endelevu ya Mto Mara na kutafakari mustakabali wa Bonde hili kwa ujumla.
Hifadhi za Mto Mara zina umuhimu mkubwa kiuchumi kwa nchi hizi mbili kutokana na mapato yatokanayo na utalii. Wanyama waliopo katika hifadhi za Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara kwa upande wa Kenya, hutegemea sana maji ya Mto Mara kwa maisha yao. Aidha siku hii inakwenda sanjari na msimu wa uhamaji wa wanyamapori jamii ya nyumbu ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya nyumbu Milioni mbili wanahama na kurudi kutoka mbuga za Serengeti- Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya kwa kipindi cha Julai na Oktoba kila mwaka.
Kaulimbiu ya Madhimisho ya mwaka huu ni “Mto Mara: Maisha yangu, Maendeleo yangu”. Kaulimbiu hii ni nzuri kwani inalenga kusisitiza dhamira ya dhati ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji na nyinginezo katika Bonde la Mto Mara. Fanyeni kila linalowezekana kuhakikisha mnabadilisha Bonde hili na kuwa mfano katika shughuli za maendeleo ikiwa pamoja na kufungua milango na fursa zaidi za uwekezaji. Ni wajibu wa wadau wote wa Bonde hili kuhakikisha chini ya Ushirikiano mzuri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, vitega uchumi mbalimbali vinawekezwa katika Bonde hili ili kusaidia wananchi wa nchi hizi mbili kuondokana na umasikini .
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Mto Mara ni mto wa kimataifa unaounganisha nchi mbili za Tanzania na Kenya. Wananchi na wadau mbalimbali wa nchi hizi waishio katika Bonde la Mto Mara wanatumia maji na rasilimali zingine kama ardhi na misitu katika bonde hili kwa ajili ya kuendeleza maisha yao ya kijamii na kiuchumi kwa nia ya kupunguza umasikini. Hata hivyo kadri ya miaka inavyokwenda, hali ya rasilimali hizi imekuwa ikipungua kutokana na matumizi mbalimbali.
Hivi sasa tunashuhudia matumizi ya rasilimali hizi yakiongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ikiwa ni pamoja na ongezeko la fursa za kiuchumi. Kwa upande mwingine tunashuhudia rasilimali hizi zikipungua na kuharibika hivyo kupunguza fursa ya nchi hizi na jamii, kujikwamua kiuchumi na kupunguza umasikini. Wakazi wa Bonde hili sasa wanashuhudia kupungua kwa maji na uchafuzi wa maji, kuzidi kupungua kwa misitu kunakosababishwa na ukataji holela wa miti, uharibifu wa ardhi na uharibifu mkubwa wa mazingira kwa ujumla unaosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wito wangu kwenu tunapoadhimisha Siku hii ya Mara, ni wajibu wa kila mmoja wetu kutafakari juu ya changamoto za msingi zinazopaswa kuchukuliwa katika kuboresha matumizi endelevu na usimamizi wa Bonde hili. Sote tunafahamu kuwa Bonde la Mto Mara lina umuhimu mkubwa kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha linatunzwa na kuendelezwa ili lisadie wananchi wetu kupata maisha bora na kuondokana na umasikini.
Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatilia mkazo suala la utunzaji mazingira katika Bonde hili. Uharibifu wa Mazingira ni moja ya tatizo linalotishia kwa kiasi kikubwa uhai wa Bonde hili. Tusipotilia mkazo utunzaji mazingira katika eneo hili tutaathiri kwa kiasi kikubwa rasilimali zilizomo katika Bonde hili na kukwamisha juhudi za wakazi wa eneo hili kujikwamua na umasikini. Tukiendelea kuharibu mazingira ya Bonde hili tutasababisha matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiasi kikubwa cha maji kwenye Mto Mara. Jambo hili halitaathiri wanyama tu bali linaweza hata kusababisha migogoro ya wanaotumia maji hayo katika nchi hizi mbili. Rai yangu kwa wadau wote wa Bonde la Mto Mara ni kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Mara kila mwaka yawe chombo cha kuhakikisha kuwa hatufiki huko. Naamini kwamba Serikali za nchi zote mbili Tanzania na Kenya zina sera, sheria na mikakati mizuri inayolenga kuhifadhi na kuhakikisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali mbalimbali za Mto Mara kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla. Lazima tuwe na chombo chenye malengo ya pamoja ya kusimamia Sera na Sheria hizo.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu kwa mara nyingine naomba niwashukuru wadau wote mliofanyikisha Maadhimisho haya, bila kuwasahau ndugu zetu kutoka Jamhuri ya Watu Kenya kwa namna mlivyojitoa kufanikisha shughuli hii. Asanteni Sana! tuzidi kushirikiana na Karibuni tena na tena.
Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa na taadhima sasa natamka rasmi kuwa; Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mara, zimefungwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.