HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, KATIKA SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA 36 YA CCM KWENYE UWANJA WA CCM LAKE TANGANYIKA KIGOMA
TAREHE 3 FEBRUARI 2013
Ndugu Walid Amani Kaburu, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kigoma;
Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara;
Mwenyekiti wa CNDD;
Katibu Mkuu wa PPRD;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mliopo;
Ndugu Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa;
Watendaji Wakuu wa Serikali na Viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali;
Wanachama wenzangu wa CCM;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote niruhusuni nianze kwa kuwashukuru viongozi, wana-CCM na wakazi wa Kigoma kwa mapokezi
mazuri sana mliyonipa mimi na mke wangu Salma MNEC wa Lindi Mjini tangu tulipowasili mkoani hapa. Nawapongeza kwa kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe za Kuadhimisha Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Lakini pongezi kubwa kwa kuandaa sherehe hii kwa mafanikio makubwa. Utaratibu mpya wa Katibu Mkuu na Wajumbe wa Sekretariet kutembelea matawi, kuzungumza na wanachama na wananchi ni wa aina yake. Ni mzuri na unafaa kuigwa.
Ni jambo la faraja na kujivunia kwamba tunasherehekea Chama chetu kufikisha umri wa miaka 36 wakati kikiwa imara na nguvu za kutosha za kupambana na kushinda katika mfumo wa vyama vingi uliodumu kwa miongo miwili. Pia kwamba, nchi yetu na watu wake bado ni wamoja, na kuna amani na utulivu licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo na kubwa zinazotishia umoja na mshikamano wetu. Ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kwamba tunasherehekea miaka 36 ya Uhai wa CCM wakati nchi ya Tanzania ikiendelea kupiga hatua kwa kasi katika kujiletea maendeleo. Tena maendeleo yaliyo dhahiri na yanayoonekana na wote isipokuwa, labda, wale ambao hutembea wakiwa wamefumba macho.
Wana CCM wenzangu;
Uimara wa Chama cha Mapinduzi na maendeleo yanayopatikana nchini chini ya uongozi wake ni uthibitisho wa ubora wa sera zake na umakini wa viongozi wa CCM kuongoza Chama na kusimamia serikali katika kutekeleza Sera na hasa Ilani za Chama cha Mapinduzi. Wana-CCM wenzangu tunayo kila sababu ya kujipongeza na kutembea kifua mbele kwa mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa na yale yanayoendelea kupatikana ndani ya Chama na katika taifa. Wananchi wa Tanzania nao hawana budi kujipongeza kwa uamuzi wao wa busara wa kukiamini Chama cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi yetu. Nawaomba waendelee na imani hiyo hiyo kwa miaka mingi ijayo. Mimi nawaahidi kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi, tena kwa kujiamini kuwa hatutawaangusha.
Ndugu zangu, Wana-CCM wenzangu;
Tuendelee kwa ari zaidi na nguvu zaidi kujenga na kuimarisha Chama chetu. Hayo ndiyo maagizo ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM uliofanyika tarehe 11 mpaka 13 Novemba, 2012 kule Kizota, Dodoma. Hayo ni maagizo kwa Chama chenyewe na kwa Jumuiya zake. Maagizo ya kujijenga na kujiimarisha yameainishwa vizuri katika Maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita. Lakini, hii si mara ya kwanza ni maagizo ya Mikutano Mikuu yote iliyopita, ya mradi wa Kuimarisha Chama III na ya Mageuzi ya Ndani ya Chama yaliyoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa katika Kikao chake cha Aprili, 2011.
Maombi yangu kwa viongozi na wanachama wenzangu wa CCM kote nchini ni kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ukamilifu maagizo hayo. Kwanza tuyasome na kuyaelewa vizuri na kupanga mipango na programu nzuri za utekelezaji wake. Viongozi wa Chama tunao wajibu maalum wa kuwaongoza viongozi walio chini yetu na wanachama wote katika kuelewa na kutekeleza Maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita, Mradi wa Kuimarisha Chama na Mageuzi ya Ndani ya Chama.
Ndugu zangu;
Tunayotakiwa kufanya si mageni. Ni mambo tunayoyajua na tumekuwa tunayafanya lakini tunakumbushwa na kusisitiziwa kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anayafanya, tena kwa ufanisi wa hali ya juu. Chama ni wanachama. Hivyo basi lililo la awali kabisa ni kutambua kuwa lazima tuendelee kuongeza wanachama. Wanachama ndiyo Jeshi letu la kutuletea ushindi. Ndizo kura zetu za uhakika za kuanzia. Hivi sasa kitaifa CCM ina wanachama 6,042,791. Hizi ni kura nyingi kwa kuanzia. Tujitahidi tufikishe wanachama milioni 8 mpaka 10 mwaka 2015. Hakuna wa kutushinda. Hivyo basi ni muhimu kuwa na wanachama wengi wenye imani ya dhati kwa Chama chao. Wanachama wenye ufahamu mzuri wa Sera za Chama na Serikali yake, wasiokuwa na ajizi katika kutekeleza Sera na maagizo ya CCM na walio tayari kukisemea na kukitetea Chama cha Mapinduzi. Kuwa na viongozi na wanachama ambao imani yao kwa Chama ni nusu nusu au uelewa wao wa mambo ni mdogo na si makini katika kutekeleza wajibu wao ni jambo la hatari.
Kwa sababu hiyo viongozi wenzangu na wanachama wenzangu hatuna budi kuongeza wanachama na kuhakikisha kuwa tunawatayarisha vizuri kuelewa vyema Sera za Chama na wajibu wao kwa Chama chao. Lazima tujipange vyema kuzitekeleza na kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wake. Suala la elimu kwa wanachama wetu na kujipangia majukumu ya kufanya ndani ya Chama na katika jamii lilisisitizwa sana katika Mkutano Mkuu wa Taifa uliopita na katika mradi wa kuimarisha Chama na malengo ya mageuzi ya ndani ya Chama. Haya shime tutekeleze.
Viongozi kutembelea wanachama wetu na kuzungumza nao, kuwaelimisha na kufafanua mambo mbalimbali ya Chama na Serikali na kuwaelekeza wajibu wao ni jambo la lazima kufanya. Hali kadhalika, viongozi lazima tuwatembelee wananchi kufafanua Sera za Chama chetu na masuala yahusuyo nchi yetu na serikali. Pia tuwasikilize mambo wanayotaka kupatiwa ufumbuzi au ufafanuzi. Yale mambo tunayoyaweza tuyajibu na yale tusiyoyaweza tuondoke nayo tukayatafutie majibu kisha tuwape taarifa. Ni kwa kufanya hivyo tu Chama chetu kitajijengea uhalali wa kuendelea kuongoza taifa kwani watu watatuamini na kutupenda. Tusipowatembelea wananchi na kuzungumza nao tunaacha ombwe linalojazwa na wale wasiokitakia mema Chama cha Mapinduzi. Watu wanaopotosha wananchi na kupandikiza chuki dhidi ya Chama chetu na serikali yake. Wengine wanaweza hata kuchukua sifa zetu isivyostahili na kujifanya ni wao waliofanya au kusababisha yawepo.
Hali kadhalika tuhakikishe kuwa vikao vinafanyika ili viongozi wapate fursa ya kuzungumza mambo yahusuyo ujenzi wa Chama chao na kupanga mikakati na mbinu za kutekeleza wajibu wao. Miongoni mwa mambo ambayo Chama chetu lazima kiyape kipaumbele cha juu ni pamoja na kujenga uwezo wa kujitegemea katika kila ngazi. Jambo hili tumelisemea kwa muda mrefu lakini hakuna kitu cha maana kinachoonekana kufanyika. Wakati umefika wa kulipa uzito unaostahili suala la kujitegemea. Tusilipuuze jambo hili muhimu kwa uhai wa Chama chetu vinginevyo mambo mengi yatatushinda kufanya na Chama kitadorora na kudhoofika.
Wapo baadhi ya wenzetu wamefanikiwa katika hili ndani ya Chama na Jumuiya. Tuwatambue na kuwasiliana nao ili watupe maarifa ya kufanya hivyo. Jambo hili si la hiari tena. Ni lazima tuhakikishe tunaulizana katika kila kikao.
Viongozi wenzangu na Wana-CCM wenzangu;
Miongoni mwa maagizo na maelekezo makuu na ya msingi sana ya Mkutano Mkuu wa Taifa ni Umoja wa Chama chetu. Mkutano Mkuu wa Taifa umetutaka viongozi tuwe wamoja, wanachama tuwe wamoja na viongozi na wanachama hali kadhalika. Tushikamane kwa pamoja kujenga Chama chetu kueneza sera, kutekeleza sera na kukipigania Chama chetu. Ndiyo maana kauli mbiu ya Chama chetu iliyotoka katika mkutano ule ilikuwa Umoja ni Ushindi. Ndiyo Kauli Mbiu ya maadhimisho haya ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM na ndiyo Kauli Mbiu mpaka itakapotengenezwa nyingine.
Umuhimu wa umoja hauhitaji kuelezwa kwa muda mrefu. Sote tunaijua misemo ya wahenga isemayo Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu au Nguvu ya Mnyonge ni Umoja na kadhalika. Umoja ndiyo uliowawezesha wazee wetu kuongoza harakati za kudai uhuru wa nchi yetu na kushinda. Kina Saadani, Abdul Kandoro, Alhaji Tawakal Karago na wenzao wengi hawakuwa na nguvu za fedha wala silaha bali umoja wao ndiyo uliyoiletea nchi yetu uhuru. Wakati mwingine husononeka sana ninapoona viongozi na wana-CCM wakifanya vitendo vinavyovuruga umoja na mshikamano ndani ya Chama. Nawaomba wenzangu tulinde umoja wa ndani ya Chama cha Mapinduzi kama mboni ya macho yetu. Tukiwa na umoja wana-CCM tutapendana, tutazungumza lugha moja, tutashirikiana vyema kupigania Chama chetu na kuwapigania wagombea wa Chama chetu kwenye chaguzi za dola.
Pasipokuwa na umoja yote hayo hayawezekani. Na ninyi wa Kigoma mnajua ukweli wa athari zake. Tumepoteza majimbo matano kwa sababu ya mifarakano ndani ya Chama chetu. Tunataka kuyakomboa majimbo yetu. Tutafanya hivyo tu iwapo tutakuwa wamoja na tuna mshikamano ndani ya Chama chetu. Tunataka kuyakomboa majimbo yetu. Tutafanya hivyo tu iwapo tutakuwa wamoja na tuna mshikamano wa dhati. Ni imani yangu kuwa sherehe hizi na kazi nzuri aliyofanya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dkt. Asha-Rose Migiro na Katibu wa Uenezi Nape Moses Nnauye itakuwa chachu itakayotufikisha katika matumaini yetu hayo.
Ndugu Viongozi na Wana-CCM wenzangu;
Jambo lingine muhimu sana ambalo hatuna budi kulisimamia kwa ufanisi mkubwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ahadi za Chama chetu na wagombea wetu wakati wa uchaguzi na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi. Lazima tukumbuke kuwa Ilani ya Uchaguzi ndiyo mkataba rasmi baina ya wananchi wa Tanzania na Chama cha Mapinduzi walipotuchagua mwaka 2010 tuendelee kuongoza nchi yetu.
Ilani ya Uchaguzi hujumuisha mambo ambayo tumewaahidi Watanzania tutayafanya. Wakatuamini wakatuchagua. Ahadi ni deni, lazima tulipe. Lakini pia zipo ahadi za papo kwa papo nilizotoa mimi, alizotoa mgombea mwenza, walizotoa wagombea wetu wa ngazi mbalimbali na viongozi wa Chama wa ngazi mbalimbali. Hizo nazo lazima tuzitimize. Jambo lililo muhimu ni kuzitambua ahadi hizo na kuzitengenezea mipango ya kuzitekeleza. Mimi hufurahi sana viongozi na wananchi wanaponikumbusha ahadi za papo kwa papo tulizotoa ili tuzitekeleze.
Wana-CCM wenzangu;
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunaitekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi mliyonikabidhi mimi na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Ghalib Bilal na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kuinadi na baada ya ushindi kuitekeleza. Nawaahidi kuwa hatutawaangusha katika hilo kwani hatupendi kusutwa na wala hatupendi Chama chetu tunachokipenda sana kinyooshewe kidole au kilaumiwe kwa kutokutimiza ahadi.
Tunaendelea kwa mafanikio makubwa kutekeleza mambo tuliyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi. Tumepanua sana fursa ya elimu katika ngazi zote kuanzia ya msingi, sekondari, ufundi stadi na vyuo vikuu. Tuelekeze nguvu zetu katika kuimarisha ubora wa elimu kwa maana tumeongeza vyuo vya ualimu na idadi ya wahitimu ili kukabili upungufu wa walimu nchini. Tunaendelea kuongeza maabara, vifaa vya kufundishia na vitabu ili kuboresha elimu inayotolewa. Vilevile tunaendelea kusogeza kwa wananchi huduma ya afya kwa kuongeza idadi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali. Tumeanza kuona dalili njema kwani vifo vya watoto na wajawazito imeanza kupungua. Hivi sasa juhudi kubwa zinafanyika kudhibiti magonjwa yanayoua watu wengi kama vile Malaria na UKIMWI.
Sambamba na juhudi hizo, tunaendelea kuboresha miundombinu na upatikanaji wa umeme, maji na huduma nyingine za jamii. Tunaelekea kufikia lengo letu la barabara kuu zote kuwa za lami na kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami. Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 11, 154 kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa na madogo unaendelea katika sehemu mbalimbali hapa nchini. Ninyi wa Kigoma ni mashahidi wa kazi hiyo. Barabara ya Kigoma – Kidahwe – Uvinza inaendelea kujengwa. Daraja la Mto Malagarasi, ujenzi wake unakwenda vizuri. Na kwa upande wa Tabora nako ujenzi wa barabara za lami umeanza mambo ambayo yanaihakikishia Kigoma barabara nzuri kutokea Pwani. Hatujaisahau barabara ya Kidahwa-Nyakanazi. Tunaendelea kutafuta fedha kutoka kwa marafiki lakini wenyewe tutaanza kidogo kidogo mwaka huu kuelekea Kasulu. Hapa mjini tutaendelea kuongeza barabara za lami. Nafahamu kuwa ujenzi wa barabara Gungu-Airport, Job Lusinde na Mji Mwema umechelewa. Nimehakikishiwa kuwa kasi itaongezeka. Pia tutaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Gungu-Tibirizi.
Ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege unaendelea katika mikoa mbalimbali. Kiwanja cha Songwa kimekamilika na kesho nitaweka jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma.
Ndugu Wananchi;
Kama alivyoeleza Waziri Harrison Mwakyembe mipango yetu haiishii hapa. Tutaendelea kukipanua kiwanja hiki hadi kifikie kilometa 3 ili ziweze kutua ndege kubwa zaidi. Narudia kusema nia yangu ya kuona siku moja Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kinakuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa nchi za Maziwa Makuu. Inshallah heri. Safari za treni ya Reli ya Kati zimeanza na tayari mipango ya kuagiza mabehewa mapya na vichwa vya treni vipya kutoka nje inakamilishwa ili kuboresha huduma hiyo. Kama mambo yataenda kama tunavyotarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu hali ya usafiri itakuwa bora sana. Pia tunaendelea kuboresha reli yenyewe na tuna mipango ya kujenga reli mpya pana zaidi itakayofika mpaka Msongati, Burundi kutokea Uvinza.
Vile vile tumeendelea kuchukua hatua za kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Tunaendelea kutekeleza lengo la Ilani ya Chama chetu ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe wamefikiwa na huduma ya umeme. Hivi sasa tumefikia asilimia 18 kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Ninyi ndugu wa Kigoma mmenufaika na mpango huu. Kigoma, Kasulu na Kibondo mmepata mitambo mipya ya kuzalisha umeme. Mwaka huu tutaanza kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Kibondo kwenda Kakonko. Suala la umeme kwa upande wa Uvinza nimelisikia nitawatuma wahusika wafuatilie ili umeme upatikane saa 24 na kwa bei nafuu. Nawaomba viongozi wa CCM muwe mstari wa mbele kuyasemea mafanikio haya. Msiposema wapo wanaosema na kuchukua sifa yetu wakabeba wao.
Ndugu wananchi;
Jana jioni nilipokea risala ya wazee wa Kigoma. Katika risala yao wazee wamenipongeza kwa kasi ya maendeleo inayopata Mkoa wa Kigoma katika nyanja mbalimbali. Nawashukuru kwa maneno ya faraja inatupa moyo; kwani wapo wenzetu wengine hapa nchini tumewafanyia mambo mengi lakini wagumu hata kusema asante. Wamebakia kulaumu kwa yale mapya wanayoyataka, tena kwa lugha chafu. Wazee pia wameniomba nihamie Kigoma nitakapostaafu, au nijenge nyumba ya kupumzikia hapa Kigoma. Nawashukuru kwa moyo wao wa upendo na ukarimu nitafikiria ingawaje sijajua nani atanipa eneo la kujenga.
Ndugu wananchi;
Katika risala yao wazee wameelezea pia kwamba hali ya upatikanaji wa maji bado haijatengemaa.Watu wanapata maji kwa mgao na Mbunge akaongezea kuwa bei imepanda sana na watu hutakiwa kulipa hata kama maji hawakupata inavyostahili. Nilimuita Mkurugenzi Mkuu wa KUWASA kutaka maelezo na mipango ya kupata ufumbuzi.
Katika maelezo yake Mkurugenzi wa KUWASA amekiri kuwepo kwa mgao wa maji na kupanda kwa bei ya maji. Mgao upo kwa sababu ya chanzo kilichopo sasa kuwa kidogo hivyo kuleta maji kidogo kuliko mahitaji. Mahitaji ya maji kwa mji wa Kigoma/Ujiji ni mita za ujazo 26,000 kiasi kinachopatikana sasa ni mita za ujazo 15,000. Hivyo kuna upungufu wa mita za ujazo 11,000.
Lakini Mkurugenzi alinipa habari njema kwamba upo mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia ikishirikiana na Wizara ya Maji utakaomaliza tatizo hilo. Kitajengwa chanzo kipya cha kutekea na kusafishia maji katika eneo la Amani. Upatikanaji wa maji utaongezeka na kufikia mita za ujazo 42,000 hivyo kuzidi mahitaji ya sasa kwa mita za ujazo 16,000 ambazo zitatosheleza mahitaji ya mji wa Kigoma mpaka mwaka 2030. Yatajengwa matanki ya kuhifadhi na kusambaza maji matano huko Mnarani, Chungu, Kigoma Sekondari, Mlole na Mji Mwema. Pia mabomba mapya makubwa ya urefu wa kilometa 70 yatatandazwa kote mjini na watu 10,000 kuunganishwa na kufungiwa mita. Kuhusu bei ya maji alisema malalamiko yataisha pindi kila mtumiaji atakapofungiwa mita na kulipa kadri anavyotumia. Heri sasa wamewafikia asilimia 54 ya wateja na mipango ya kuwafungia mita watumiaji waliosalia inaendelea.
Ndugu wananchi;
Wazee wetu hao pia walilalamikia bei ya viwanja kuwa kubwa mno kwa mtu wa kawaida kumudu, pembejeo za kilimo za ruzuku kutokutosheleza mahitaji na kuchelewa kupatikana na mengineyo. Nimeahidi kuwa mamlaka husika zitataarifiwa kuyatafutia ufumbuzi masuala hayo. Vile vile wazee wa Kigoma walitahadharisha kuhusu kuwepo migogoro kidogo na kuhatarisha amani ya Mkoa na taifa kwa ujumla. Nakubaliana nao kwamba ni kweli ipo na inaelekea kuibuka kila kukicha na ni kweli kwamba ni hatari kwa amani na utulivu hapa nchini. Nimelisema jambo hili mara baada ya Uchaguzi wa 2010 lakini wapo waliojaribu kunibeza na kudai kuwa si kweli. Watanzania wenzangu haitasaidia kujifanya haipo wakati ipo tunaiona na kuisikia. Nilisemea jambo hili tena katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka kuomba viongozi wa dini watusaidie. Kama wao watawakemea na kuwakataza waumini wao, magazeti yao na radio zao zisilete mifarakano ya kidini haitatokea. Niliwaomba wafufue utaratibu mzuri wa mazungumzo baina ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Ulikuwa utaratibu wao si wa serikali. Ukitumika vizuri utatuepusha na mengi. Nawaomba waione haraka ya kufanya hivyo. Serikali itatimiza wajibu wake wa kulinda amani kama hapana budi. Lakini, mzuie tusifikie hapo.
Ndugu wananchi;
Kabla ya kumaliza napenda kuwasihi viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha kushabikia siasa za kuigawa nchi yetu katika makundi ya dini, rangi, kabila na mahali anapotoka mtu. Naomba tushabikie sera zinazojenga umoja na mshikamano badala ya migawanyiko na mifarakano. Ni siasa na sera ambazo hazina faida yeyote kwa nchi yetu na watu wake. Ni siasa za maangamizi na mifano ipo mingi duniani na hata nchi jirani ya kuthibitisha hayo. Inashangaza kuona baadhi ya wanasiasa wanafanya siasa za chuki kuwa mtaji wao wa kisiasa. Nawaambia hawatafika popote. Nawaomba Watanzania wenzangu msikubali kutumiwa na wanasiasa au mtu yoyote mwenye sera za aina hiyo. Wanaendeleza maslahi yao binafsi na siyo ya taifa. Msikubali kuweka rehani maisha yenu na amani ya nchi yetu kwa ajili ya maslahi ya mtu au kikundi fulani. Jiulizeni hivi, nchi hii ikichafuka mimi na familia yangu tutaokolewa na nani?
Ndugu viongozi na wanaCCM wenzangu;
Mwisho, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana wenyeji wetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Ndugu Kaburu, na wale wote walioshiriki kuandaa sherehe hizi ambazo zimefana sana. Nawashukuru pia wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki matembezi ya mshikamano leo asubuhi na sasa katika kilele cha sherehe hizi. Sina neno zuri la kushukuru zaidi ya kusema asanteni sana.
Nawapongeza tena viongozi, wanachama, makada, wapenzi na wakereketwa wa CCM kwa kutimiza miaka 36 ya uhai wa CCM. Nawasihi tutoke hapa tukiwa na ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ya kwenda kukijenga Chama chetu kote nchini na kuwatumikia wananchi. Daima tukumbuke Umoja ni Ushindi na kwa pamoja tutashinda. Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.