HIPZ kuiendeleza Hospitali Kivunge Zanzibar

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

MRADI wa Kuendeleza huduma za Afya Zanzibar (HIPZ), umeeleza azma yake ya kuangalia uwezekano wa kuiendeleza hospitali ya Kivunge iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ili ipate mafanikio kama ilivyo hospitali ya Makunduchi hivi sasa.

Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka hospitali ya Tauton nchini Uingereza na Mwenyekiti Mwanzilishi wa Mradi wa Kuendeleza huduma za Afya Zanzibar (HIPZ) Dk. Ru Macdonagh, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Dk. Mcdonagh alimueleza Rais Dk. Shein kuwa hospitali ya Makunduchi imepata mafanikio makubwa katika kutoa huduma kwa jamii hivyo ameona haja ya kupanua wigo kwa hospitali ya Kivunge.

Alisema kuwa Mradi wa HIPZ umedhamiria kuiendeleza hospitali hiyo ya Kivunge na kueleza hatua zote muhimu zitasimamiwa na mradi huo ili hospitali hiyo ya Kivunge iweze kutoa huduma kama zile zinazotolewa katika hospitali ya Makunduchi hivi sasa.

Dk. Macdonagh alifuata na Dk. Jon Rees ambaye ni Mjumbe wa HIPZ kutoka Briston Uingereza, alisema kuwa mradi huo unaoendeshwa kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umepata mafanikio makubwa katika kutoa huduma kwa jamii sanjari na kuijengea uwezo hospitali ya Makunduchi katika utoaji huduma za afya.

Alisema kuwa miongoni mwa mafanikio yaliopatikana katika hospitali ya Makunduchi hivi sasa ni pamoja na uwezo wa kufanya upasuaji wa uzazi pamoja na kusaidia damu katika hospitali hiyo ambapo pia wamekarabati chumba hicho cha upasuaji.

Aidha, alisema kuwa asilimi 75 ya akina mama wamekuwa wakijifungua katika hospitali ya Makuduchi hatua ambayo imekuwa ikichangiwa kwa kuwepo gari maalum ya kuchukulia wagonjwa ambayo hutoa huduma kwa akina mama katika eneo lote la kusini bila ya malipo.

Alieleza kuwa tayari vifaa mbali mbali vya tiba vimewekwa katika hospitali hiyo, pamoja na kufanya ukarabati chumba cha kungolea meno pamoja na vifaa vyake, kutoa tiba ya kisukari, presha, maradhi ya moyo, kiharusi na mengineyo.

Kutokana na hatua hiyo, ndipo mradi wa HIPZ ukaona haja ya kuendeleza huduma hizo katika hospitali ya Kivunge ili kuweza kutoka huduma kwa wakaazi wa Kaskazini Unguja na kuipunguzia mzigo hospitali ya MnaziMmoja.

Nae Mohamed Shein alitoa pongezi kwa ujio wa Daktari huyo bingwa pamoja na mashirikiano makubwa anayotoa katika kuimarisha huduma za afya hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa ni azma ya Serikali ya Mapinduzin Zanzibar kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuziimarisha hospitali pamoja na vituo vyote vya afya hapa nchini.

Aidha, alieleza azma ya kuzipa hadhi ya Wilaya Hospitali za Makunduzi na Kivunge kwa upande wa Unguja na Vitongoji na Micheweni kwa upande wa Pemba.

Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza matumaini yake ya kuimarika utoaji huduma kwa hospitali hizo ikiwa ni pamoja na kuweza kufanya upasuaji kwa maradhi tofauti kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na serikali hivi sasa.

Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa mtandao mzuri wa barabara nchini nako kumeweza kurahisisha utoaji huduma kwa jamii katika eneo hilo la Kusini mwa Unguja pamoja na maeneo mengineyo. Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya mafanikio kwa mradi huo katika eneo hilo la Kaskazini mwa Unguja pamoja na maeneo mengine ya Zanzibar huku akiahidi mashirikino kutoka serikalini yataimarisha.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana vyema na Mradi huo wa HIPZ ambao umeweza kupata mafanikio makubwa katika kuiimarisha hospitali ya Makunduchi pamoja na juhudi zake katika uimarishaji wa sekta ya afya nchini.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mohammed Jidawi, alieleza kuwa Mradi wa HIPZ umekuwa na mafanikio makubwa na kupongeza mashirikiano yanayotolewa na Dk. Ru Macdonagh katika kuimarisha mradi huo hapa nchini na kueleza kuwa kuangalia uwezekano wa kuiimarisha hospitali ya Kivunge ni jambo la busara.