Hiki Ndicho Zitto Kabwe Alichowaambia Wapiga Kura Wake Kigoma…!

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ZITTO KABWE

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ZITTO KABWE

HOTUBA YA MH ZITTO KABWE (MBUNGE KIGOMA KASKAZINI) ILIYOTOLEWA LEO TAREHE 15 MACHI 2015

MWANAMAPINDUZI na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara alisema kuwa ili kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na hali fulani ya uendawazimu. Ila tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule ukichaa mzuri wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia kwa dhati pamoja na changamoto nyingi.

Kwa kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka kuboresha maisha ya wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya kuwatumikia kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu. Labda ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa yanayoambatana na ujana yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo ya heshima kubwa ya kuwawakilisha.

Mwaka 2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji wangu mzuri wa kazi na

mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu. Hivyo kwa miaka kumi tumekuwa

bega kwa bega katika safari hii ya pamoja ya kujenga na kuiendeleza jimbo letu, na

leo nimekuja kuwashukuru kwa fursa mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho.

Fursa mliyonipa ni ya kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali

kulitumikia Taifa langu.

Katika miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja na kufanikiwa; na kuna

mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo hatukuweza kuyafanya naomba

radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba kuwapongeza sana kwa kufanikisha.

Kwani kama Mwalimu Nyerere alivyotuambia kuhusu Uhuru na Maendeleo: “Uongozi ni

kuongea na kujadili na wananchi, kuwaelewesha na kuwashawishi. Uongozi ni kufanya

kazi pamoja na wananchi na kuonyesha kwa vitendo mnachotaka kufikia. Uongozi ni

kuwa mmoja wa wananchi na kutambua kuwa mko sawa…. Wananchi hawawezi kuendelezwa

bali wanajiendeleza.” Na ndivyo tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano

wenu tumeweza kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.

Mwaka 2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo hii, ninapoongea nanyi

tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100 kuunganisha Jimbo letu na

majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile tuna mradi mkubwa wa

kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa barabara. Kiujumla kwa

mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la Malagarasi na hivyo kuunganisha

mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo ambalo lilikuwa kilio chetu cha muda

mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu zaidi ni kuwa barabara hizi zinatumika na

wananchi, wafanyabiashara na wakulima ili kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua

masoko.

Tumefanikiwa kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa kuunganisha vijiji zaidi ya

16 hivi sasa. Changamoto kubwa iliyobakia mkoani kwetu ni uzalishaji mdogo wa

umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la kudumu ni kufanikisha mradi wa

Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao utakuwa nafuu na kuwezesha pia

kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na Tabora, na hata kuuza nchi jirani ya

Burundi. Viongozi wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma watakaoingia kwenye uongozi baada

ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015 hawana budi kuweka kipaumbele kikubwa kwa

mradi huu. Bila ya umeme wa uhakika na nafuu hatuwezi kupiga hatua ya kuongeza

thamani ya mazao yetu kwa kujenga viwanda vya usindikaji na kuongeza ajira ya

vijana wetu.

Tumefanikiwa kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji cha Kagunga. Lengo

likiwa ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya Burundi. Kigoma ni mji wa

biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa ya uchumi wa mkoa huu kwa

miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya Biashara ni sehemu ya miradi ya

kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi yake ya kiuchumi katika nchi yetu.

Katika muktadha huo ndio maana tunaendelea na miradi ya Bandari Kibirizi na

Bandari ya Nchi Kavu Katosho. Ndio maana tunaendelea na mradi wa Kituo cha

Usafirishaji Mwandiga (Mwandiga International Transportation Terminal) na eneo

maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote tuliyaanzisha kwa pamoja nanyi ili

kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha ajira kwa watu.

Tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa kuwa na shule katika

kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata hivyo, tuna changamoto

kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika jimbo la Kigoma Kaskazini

zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne wanapata madaraja ya mawili ya chini,

wakati ule daraja la nne na daraja la sifuri. Tumeanzisha mradi wa majaribio ya

kutoa motisha kwa Walimu ili kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha elimu

inaboreshwa. Shirika la Twaweza linaendesha mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na

baada ya mwaka huu tutakuwa tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa

watoto wetu. Bila Elimu bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina maana

yeyote. Serikali imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona namna ya

kuitekeleza katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo, uongozi wa kisiasa

utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna budi kujielekeza vya kutosha

katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za kazi kwa vijana waweze kujiajiri na

kuajiriwa.

Tumefanikiwa kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati zetu chache

zilizokuwepo na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya afya vya

Mahembe na Nyarubanda. Hata hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga kuliko tiba

kwani gharama za afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili hili suala,

ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile ambacho

hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli. Na mniruhusu hapa kunukuu wosia

wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipotuasi kuwa “Maendeleo ni maendeleo ya watu.

Barabara, Majengo, kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na masuala mengi kama haya

si maendeleo, bali ni vitendea kazi tu vya maendeleo” Ndiyo maana kulikuwa na

umuhimu wa kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha maisha ya mwananchi, hususan

kwa upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu wetu ni kuwa katika kipindi hiki cha

miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima.

Tulianza na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo wananchi walijiunga na

NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za afya bure na kujiwekea akiba

kwa ajili ya mafao ya muda mrefu. Mafanikio makubwa yaliyopatikana yamewezesha

wazo hili kusambaa nchi nzima na hivi sasa wakulima wa Korosho, Chai, Pamba,

Tumbaku wanafuata nyayo za Wakulima wa Ushirika wa RUMAKU. Hapa Kigoma wazo hili

sasa linatekelezwa kwa wavuvi wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Ndoto yetu ni

wananchi zaidi ya theluthi moja kwenye nguvu kazi wawe na Hifadhi ya Jamii. Natoa

wito kwa wananchi wengine wenye uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii wajiunge na

vikundi vya ushirika na kuchangia ili kufaidika na mafao ya muda mrefu kama

pensheni lakini pia yale ya muda mfupi kama bima ya afya, mikopo kupitia SACCOS na

mengine yatakayoanzishwa kama bima ya mazao.

Tumefanikiwa kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini. Hivi sasa watu wa

Kigoma tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali. Kujiamini na kushiriki

kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni wajibu wetu kama raia.

Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka na zinaendelea

kutokomezwa. Juhudi zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya

Jamhuri yetu katika kila Nyanja za maisha yetu. Nafurahi kupata fursa ya kushiriki

nanyi katika kujenga heshima hiyo ya Mkoa wetu. Nitaendelea kushiriki katika

kudumisha heshima hiyo.

Nimejifunza mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu. Kama nilivyosema hapo

awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa ya nchi yetu kwa kunipa

jukumu hili nikiwa kijana mdogo. Naamini kuwa ule ukichaa wangu mzuri wa kusimamia

misingi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wangu na kuhakikisha huduma muhimu

zinawafikia nimezipigania. Na katika safari hii nimejenga marafiki wengi sana na

pengine hata maadui ingawa hao ni wachache. Lakini haijalishi kwani mi binafsi

sina uhasama na binadamu mwenzangu.

Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inaendeshwa.

Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni

makosa. Mliniruhusu kufanya makosa na kuyarekebisha makosa hayo kwa hiyo kukomaa

zaidi. Shukrani za dhati ziwaendee wazee wangu ambao mliniongoza mpaka hapa

tulipofika na kunishauri hata kunionya pale palipohitajika. Kwa ujumla nimejifunza

kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndio maana

hamkunisikia tu kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi

yetu na makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima, Wafanyakazi, Wasanii, Wavuvi,

Wana michezo na wana habari.

Katika safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na kuna watu nimewaudhi.

Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale niliowafurahisha ninaomba wasiache

kuniongoza na kunishauri kila wakati. Haikuwa safari rahisi na sikutegemea iwe

rahisi. Kiuhalisia ilikuwa safari ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni

safari yangu kama kiongozi na pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na

kupata mafunzo kuhusu maisha. Ukifika ulikokuwa unakwenda katika safari, unaweza

kutathmini mengi kuhusu safari hiyo, lakini mwisho wa siku unatakiwa ujue kama

safari hii ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati

kabisa ilikuwa ni safari njema.

Ni wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo letu. Kushika kijiti

pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha pale nilipofikia.
Sitakuwa mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba lakini nitaendelea

kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia nyingine.

Sitaacha ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas Sankara unaoleta maendeleo

ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni walewale ambao mwasisi wetu

Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani umaskini, ujinga, maradhi

na sasa tumeongeza ufisadi. Kizazi chetu kina jukumu la kipekee kuendeleza

mapambano haya na nitaendelea kuhakikisha tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa

lenye misingi madhubuti ya uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia

rasilimali za nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.

Asanteni sana Kigoma Kaskazini!