Hemed Morocco amepewa kazi ya kuinoa Simba Sc kwa miezi sita, kimebaini kuwa katika harakati za kurejesha hadhi ya klabu, uongozi wa Simba umemsainisha kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman Morocco ambaye anakuja kuliongezea nguvu na kuliimarisha benchi la ufundi linaloongozwa na Mganda, Jackson Mayanja.
Morocco amefundisha klabu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Coastal Union, JKT Oljoro na Zanzibar Heroes iliyo chini ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga, pia ni Kocha Msaidizi wa Taifa Stars.
Wasifu huu unamfanya kuwa mkongwe na mzoefu katika masuala ya soka, hivyo huenda Simba wakawa wameusha kete yao sehemu sahihi. Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya Simba, zimesema Morocco anakuja kuwa mshauri mkuu wa benchi la ufundi ambako ameanguka saini ya miezi sita.
Morocco amekiri kuwa ni kweli na muda wowote anatarajia kuanza kibarua baada ya kufikia makubaliano mazuri na uongozi wa Simba.
Lakini akashindwa kubainisha kama atabwaga manyanga kuinoa Stars akidai wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujua hatima yake baada ya kupata ulaji mpya.
Katibu Mkuu wa Simba, Enock Kiguha, alikiri kuwa wamemalizana na kocha huyo lakini akadai suala la muda wa mkataba linabaki kuwa siri ya klabu.