Pichani, Generali Ulimwengu akitoa somo.
NIMEPENDEKEZA kwamba, ili kujenga misingi ya diplomasia yenye tija kwa nchi yetu, hatuna budi kuangalia mambo tunayoyafanya na kuachana na yale ambayo hayana manufaa na badala yake yanatubebesha gharama zisizokuwa na sababu.
Nimesema kwamba lazima tuachane na mtindo wa kupeleka misafara mikubwa ya watu ambao hawana kazi ya maana ya kufanya huko waendako bali wanaingizwa katika misafara hiyo ili wapate malipo ya DSA, ambayo nayo ni makubwa kuliko yanayolipwa katika nchi nyingine au katika Umoja wa Mataifa.
Rai yangu hapa ni kwamba hatuna sababu yoyote ya kulipa DSA kubwa kuliko inayolipwa na Umoja wa Mataifa. Hatuna sababu ya kujifananisha na nchi kama Saudia au Oman au Kuwait, nchi zenye ukwasi mkubwa unaoziwezesha kuwalipa watu wake viwango vikubwa. Hizi nchi zinayamudu malipo haya; sisi hatuyamudu.
Nchi yetu inayo matatizo mengi, makubwa na ya msingi. Watu wetu bado ni masikini mno, na kila jitihada inatakiwa kufanywa ili kuwanusuru na umasikini huu ambao hauna sababu ya kuendelea kuwadhalilisha.
Ninapoangalia gharama tunazolipa kwa ajili ya ‘wanadiplomasia’ wetu kusafiri huku na kule ninapata taswira ile ile tuliyonayo katika uhusiano wetu ndani ya nchi. Watawala wanatafuta kila njia wanayoweza kuipata ili kuwakamua wananchi, na wananchi mara nyingi wanajikuta hawana njia ya kuwabana watawala.
Ni jambo la kawaida kwamba siasa za ndani ndizo zinazoelekeza siasa za nje, yaani diplomasia, na kama ndani ya nchi mmezoea kuoneana hata katika siasa ya nje mtaendeleza uonevu huo, au angalau hamtajali iwapo mwenzenu anaonea na kudhulumiwa kwa sababu uonevu na dhuluma ni mambo mliyoyazoea.
Ishara moja inayodhihirisha hili ni kwamba diplomasia yetu hivi sasa haijengi uhusiano wa kupambana dhidi ya uonevu na unyanyasaji. Siasa yetu ya nje hivi sasa ni ya ombaomba, na kila anayetupa ruzuku ni mungu ambaye hatuthubutu kumsema hata kama anawaonea wenzetu.
Tumeona jinsi ambavyo tumekuwa wakimya wakati mabavu yanatumika kuwaumiza wanyonge, na sisi tunaangalia na kuendelea kuwachekea hao wanaofanya unyama huo. Kimsingi hatuna tena misingi ya kidiplomasia tuliyokuwa tumeijenga kwa muda mrefu na ambayo ilikuwa imetujengea heshima. Kwa mfano najiuliza ni nini msimamo wa Tanzania kuhusu ugomvi baina ya Uingereza na Argentina juu ya visiwa vya Malvinas.
Aliwahi kusikika waziri wetu wa diplomasia akijibu swali kuhusu msimamo wa Tanzania miaka kadhaa iliyopita. Swali aliloulizwa lilihusu msimamo wa Tanzania kuhusu kipigo ilichokuwa ikitembeza Israel dhidi ya Lebanon.
Jibu la waziri wetu lilikuwa kwamba msimamo wa Tanzania ni ule ule wa Umoja wa Mataifa kwa sababu sisi ni wanachama wa Umoja huo na msimamo wetu hauna budi kufanana na ule wa Umoja huo. Ajabu!
Kama hiyo ni kweli basi hatuna haja ya kuwa na wizara nzima ya kuendesha diplomasia yetu. Tunachohitaji ni kupokea ‘email’ kutoka New York mara kwa mara kutujulisha msimamo wa Umoja wa Mataifa ili tuutetee kila tuendako.
Ingekuwa msimamo wa nchi yetu ni ule ule wa Umoja wa Mataifa tusingefanya kampeni ya kuifukuza Afrika Kusini kutoka Umoja huo na kuiingiza Jamuhuri ya Watu wa China katika miaka ya 1970. Na kwa mantiki hiyo hiyo Tanganyika ya Julius Nyerere isingetamka kwamba ingejitoa Jumuiya ya Madola iwapo Afrika Kusini ingeendelea kuwa mwanachama katika miaka ya 1960.
Nchi haziendi New York kutafuta misimamo yake. Misimamo hutoka nyumbani na kupelekwa New York ambako hutetewa na kisha kuchakatwa dhidi ya misimamo ya nchi nyingine na hatimaye kupatiwa msimamo wa wakati huo.
Hata pale msimamo unapofikiwa unaweza ukawa ni msimamo wa mpito kwani baadhi ya nchi huendelea kushikilia misimamo yake hadi inapofikia mahali ikakubalika. Hivyo ndivyo tulivyoweza kushinda vita ya kidiplomasia dhidi ya Afrika Kusini, na pia ndivyo tulivyoshinda vita ya kuiingiza Jamuhuri ya Watu wa China ndani ya Umoja wa Mataifa.
Nahisi kwamba ingekuwa leo ndiyo tunajadili kuwafukuza Makaburu na kuiruhusu China wanadiplomasia wetu wa leo wangekuwa wanasikiliza ‘wafadhili’ wanasema nini badala ya mantiki ya haki inaelekeza nini.
Haya ni mambo rahisi ya kueleweka, lakini yanakuwa magumu kuyatekeleza pale wanaotarajiwa kuysimamia wana maslahi mengine kabisa, DSA na safari za anasa. Wala hatuoni haya kwamba wajumbe a nchi nyingine wamekwisha kutambua siri ya ukubwa wa misafara yetu.
Mara kadhaa nimewasikia wajumbe wa nchi nyingine wakitusema. ‘Wa-TZ wengi kweli kweli; kwa nini?’ aliuliza mwanamama kutoka Kenya anayefanya kazi na shirika la kimataifa. ‘DSA’ akamjibu mwenzake kutoka Uganda. Hii si sifa njema; ni sifa inayotufanya tuonekane watu wa hovyo, watu wasiokuwa makini hata kidogo.
Nimekuwa nikirejea kazi za kidiplomasia zilizofanywa zama zilizopita. Misafara iliyofuatana na Nyerere ilikuwa midogo sana, watu sita au saba kutoka diplomasia, walinzi wawili na wasaidizi wa karibu akina ‘Mzee Juma’ wawili, basi.
Siku hizi tumezoea kila aina ya wapambe wamo katika safari ya mkubwa, na wote wanasafiri ‘Business,’ ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari na wapiga picha wa mkubwa. Tunatoa picha ya ukwasi ambao haupo.
Imesemwa mara kwa mara lakini watawala wetu hawajali na wala hawasikii uchungu au woga. Waziri wa Tanzania anasafiri daraja la kwanza akienda Uropa kuombaomba kama kawaida. Ndani ya ndege anayosafiria yumo balozi wa nchi ya ‘wahisani’ ambako waziri wetu anakwenda kuombaomba; yeye ‘mfadhili’ anasafiri daraja la kawaida.
Hawa wawili wanakwenda kuhudhuria kikao hicho hicho cha ombaomba ambacho kimeandaliwa kuisaidia nchi yetu ‘masikini.’ Wanapofika huko, balozi anakaa upande wa nchi yake, upande wa ‘wafadhili,’ na waziri wetu anakaa upande wa ombaomba.
Niliwahi kuandika kwamba hali inapokiuwa hovyo kabisa, na kila kitu kimesambaratika katika hali ya mtu, amekwisha hana mbele wala nyuma, jambo moja tu hubakia likimkinga mtu huyo dhidi ya kuvua nguo na kukimbia uchi mtaani. Jambo hilo ni haya, au soni. Sisi tumekosa soni.
By Generali Ulimwengu
Chanzo: Raia Mwema