Na Augustine Mgendi, Tarime
SERIKALI imesema kuwa haiwezi kumtegemea mwekezaji kwa kila kitu huku baadhi ya mambo yanaweza kufanywa na wanajamii wenyewe katika sehemu huska. Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele katika hafla ya kukabidhi Madawati kwa baadhi ya shule zinazozunguka mgodi wa ABG North Mara, Vifaa vya Shule kwa baadhi ya wanafunzi na Baiskeli ya Magurudumu Matatu kwa watu watatu wasiojiweza.
Alisema kuwa pamoja na misaada inayotolewa na mgodi huo kwa jamii Serikali inashukuru uhusiano mzuri uliopo kati ya mgodi huo (ABG North Mara) na Jamii. Mkuu wa wilaya huyo aliushukuru mgodi huo kwa kutoa msaada kwa walemavu, pamoja na vifaa vya elimu huku akisisitiza kuwa hiyo ni hatua nzuri katika kuiinua jamii.
“Kwanza napenda kutoa shukrani kubwa kwa uhusiano uliopo kati ya mgodi na jamii lakini pia hatuwezi kumtegemea Mwekezaji kwa kila Jambo lazima sisi wenyewe tujitoe katika kufanikisha baadhi ya Mambo yetu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Akimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya Meneja mkuu wa Mgodi wa North Mara, Gary Chapman, alisema Mgodi huo ni miongoni mwa Migodi Afrika ambayo imekuwa ikiwekeza katika Jamii hasa katika suala la Elimu, Afya, Maji na Maendeleo katika Jamii. Alisema Pamoja na kutotimiza mahitaji kwa shule za Sekondary kwa asilimia mia lakini watajitahidi kushirikiana na Jamii jiyo katika kujiletea Maendeleo.
“Mgodi huu ni moja ya Mgodi Afrika ambao unajitolea katika kusaidia Jamii hasa katika elimu, afya, maji na Masuala la Maendeleo, lakini pamoja na kutotimiza Mahitaji ya Jamii kwa asilimia kubwa bado tutaendelea kushirikia na nao,” alisema, Gary Chapman.
Aidha Uongozi wa Mgodi huo umetoa Madawati zaidi ya 1000 kwa shule za Nyangoto na Matare zilizopo katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime Mkoani Mara huku Miradi yote Mitatu ya Elimu, msaada ya Baiskel na Madawati hayo ikigharimu kiasi cha shilingi milioni 188.
Watu waliopewa Baiskeli hizo za Miguu mitatu ni pamoja na Eliza Mwikwabe ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo, Penina Mseti muuza mboga na Nyanya pamoja na Gesongo Chacha ambaye ni fundi wa kuchomelea vyuma.
Awali akisema Risala kwa Mgeni Rasmi Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyangoto, Ghati Keraryo alisema kuwa shule zote mbili za Nyangoto na Matare zina jumla ya Madawati 202 kati ya 654 ambayo yanahitajika. Alisema kwa niaba ya Walimu wa shule hizo wanapenda kutoa shukurani kwa Mgodi wa ABG North Mara kwa kutambua Umuhimu wa Changamoto moja wapo zinazokabili shule hizo ikizingatiwa kwamba shule hizo zipo karibu na Mgodi huo.
Mbali na msaada huo wa madawati kwa shule hizo, msoma risala huyo alisema kuwa bado shule hizo zina upungufu wa Viti 46 na meza 18, huku akiuomba Mgodi huo kuendelea kujenga Shule hizo kama Mkataba ulivyoainisha katika ya Kijiji na Mgodi.