Hatujaweka CCTV Madarasani Kwa ajili ya Kudhibiti Ngono – Prof CBE

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mjema akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu habari za upotoshaji zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu chuo hicho, jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mjema akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu habari za upotoshaji zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu chuo hicho, jijini Dar es Salaam.


Na Aron Msigwa – MAELEZO

MKUU wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Emmanuel Mjema amesema habari zilizoandikwa na vyombo vya habari kuwa uongozi chuoni hapo umeweka kamera (CCTV) madarasani kwa ajili ya kudhibiti ngono madarasani si za kweli na kwamba zililenga kukidhalilisha chuo na kuipotosha jamii kufuatia kuendelea kufanya vizuri katika kulinda maadili na viwango vya taaluma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa chuo hicho alisema habari zilizochapishwa kuhusu kuwekwa kwa mfumo wa kamera za kisasa madarasani na taarifa ya kufukuzwa kwa mwalimu mmoja wa chuo hicho akihusishwa na vitendo vya ngono na wanafunzi, bali wamepotosha kwa kukosa weledi wa kushindwa kupata uhalisia na usahihi wa habari husika kutoka mamlaka za chuo.

Prof. Mjema alisema kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara ni Chuo cha Serikali ambacho kimekua kikitoa Elimu ya Biashara kwa miaka 49 na kuongeza kuwa chuo hicho kinaajiri wakufunzi wake kupitia utaratibu wa serikali wa kutangaza nafasi za kazi kupitia Tume ya Ajira iliyopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma.

Alisema kuwa chuo hicho kina wakufunzi na wataalam wanaoheshimu maadili ya utumishi wa umma na taaluma zao na kuongeza kuwa chuo hicho kina wakufunzi wenye sifa ambao hawahitaji kufuatiliwa na mtu katika kazi zao.

“Nachopenda kusema ni kwamba chuo chetu sasa kinao wataalam na wakufunzi wenye sifa na walioajiriwa kwa kuzingatia kanuni na vigezo vilivyowekwa, taarifa zilizotolewa hazina ukweli wowote na zimelenga kukidhalilisha chuo na kuipotosha jamii”

Alisema kuwa kamera za kisasa zilizofungwa katika vyumba vya madarasa vya chuo hicho zimewekwa kwa lengo la kudhibiti udanganyifu katika mitihani na kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za chuo na kuongeza kuwa juhudi zinafanyika katika mwaka ujao wa fedha kuongeza vifaa hivyo hasa katika maeneo ya kuingilia na yale yanayotumiwa na watu wengi chuoni hapo.

“Napenda kuwafahamisha kuwa kamera za CCTV tulizonazo zimefungwa katika vyumba vya madarasa kulingana na teknolojia iliyopo sasa na ni jambo la kawaida na zimefungwa kwa lengo la kuimarisha ulinzi na si kama ilivyoandikwa kwa kupotoshwa na gazeti hilo na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa zinalenga kudhibiti vitendo vya ngono darasani,” alisema Prof. Mjema.

Aidha kuhusu hali ya ulinzi na usalama chuoni hapo alisema kuwa chuo hicho kimekuwa na utaratibu wa kuweka walinzi getini kwa miaka 49 na kuongeza kuwa hakuna walinzi wapya walioajiriwa kwa ajili ya kukagua mavazi ya wanafunzi hao huku akibainisha kuwa utaratibu uliopo sasa wa kukagua vitambulisho kwa wanafunzi wanaoingia chuoni hapo na wageni wengine wanaoingia ni wa kawaida kwa ajili ya usalama wa chuo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa chuo hicho alisema kuwa chuo hicho kitaanza kutoa masomo ya juu kwa ngazi ya shahada za uzamili kuanzia mwaka ujao wa kitaaluma na kutoa wito kwa wananchi kuichangamkia fursa hiyo.

Pia chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha “Eastern Finland” kitaanza kutoa shahada za umahiri na kufafanua kuwa wataalam wa kuifanya kazi hiyo hapa nchini wapo.

“Tutaanza kutoa mafunzo kwa ngazi ya shahada za uzamili katika mwaka ujao wa kitaaluma, wahadhiri wanaofundisha sasa hapa chuoni wana elimu za juu hivyo kuwezesha mchakato huo kuanza,”

Katika kuboresha kiwango cha elimu chuoni hapo Prof. Mjema ameeleza kuwa chuo tayari kimeingia mkataba na chuo Kikuu cha masuala ya Teknolojia cha Shenyang, kilichopo nchini China ambapo wanafunzi wa vyuo vya CBE nchini wataweza kwenda China kumalizia masomo yao kwa mfumo wa kubadilishana.

“Ni hatua nzuri katika maboresho ya elimu katika chuo chetu kwa kushirikiana na vyuo vya nje hasa Finland na China na sasa baadhi ya wanafunzi wameshaanza kunufaika,” ameeleza Prof. Mjema.