Hatma ya madiwani waliotimuliwa Chadema kesho!

Dk. Willibroad Slaa

Na Janeth Mushi, Arusha

HATMA ya madiwani watano wa Chama cha Damokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaopinga kufukuzwa uanachama inatarajia kujulikana kesho wakati Mahakama itakapotoa uamuzi wa ama kuifuta kesi hiyo au kuendelea kuisikiliza.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Hawa Mguruta anatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi nne zilizotolewa na mawakili wa utetezi, Method Kimomogolo na Albert Msando waliotaka kufutwa kwa kesi hiyo kwa madai ina upungufu kisheria.

Aidha hoja nne za pingamizi zilizowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wanaoiwakilisha CHADEMA, ambayo ni mlalamikiwa wa kwanza na mshtakiwa wa pili, Freeman Mbowe, ni pamoja na mahakama hiyo kukosa uwezo kisheria wa kuchunguza uamuzi wa taasisi huru na binafsi kama Kamati Kuu ya CHADEMA wakidai Mahakama Kuu ndiyo yenye uwezo huo.

Pingamizi jingine ni CHADEMA kukosa uhai kisheria wa kushtakiwa kwa
jina kama walivyofanya walalamikaji ambao wanawakilishwa na wakili
Severin Lawena. Upande huo wa utetezi ulidai kuwa mshtakiwa wa pili (Mbowe) hana mamlaka ya kutekeleza maamuzi yatakayotolewa na mahakama kwa sababu katika kesi hiyo ameshtakiwa kama mtu binafsi badala ya cheo chake cha uenyekiti wa Taifa wa chama.

Kimomogolo alidai kuwa kesi hiyo imepitwa na wakati kwa sababu tayari
walalamikaji hao wamekata rufaa baraza kuu la chama ambacho ndicho
kikao cha kikatiba chenye mamlaka ya kubatilisha maamuzi ya kamati
kuu. Kesi hiyo mefunguliwa na Estomih Mallah, John Bayo, Charles Mpanda, Reuben Ngowi na Rehema Mahamed.