Na Janeth Mushi, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha Septemba 26 mwaka huu inatarajia kutoa uamuzi wa kutupilia mbali ama kuendelea kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa dhidi ya mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.
Jaji Aloyce Mujulizi anayesikiliza kesi hiyo leo mjini hapa amesema uamuzi huo unatolewa baada ya kumaliza kusikiliza kwa faragha suala linalogusa mambo binafsi ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Batilda Buarin.
Akiahirisha kesi hiyo jana, Jaji Mujuluzi alisema kesi hiyo ina madai
yanayomgusa Dk. Burian ambaye hajafungua shauri, hivyo kushauri madai hayo yasikilizwe kwanza faragha, uamuzi ambao uliungwa mkono na wakili anayewatetea walalamikaji wa kesi hiyo.
Usikilizaji wa faragha ulifanyika jana kuanzia saa 2:30 asubuhi na
baada ya hapo, kesi ilianza tena ambapo Jaji alidai kuwa anahitaji kupata muda ili aweze kutoa uamuzi wa shauri hilo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo
dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, ambapo wanaiomba mahakama hiyo ibatilishe matokeo ya uchaguzi huo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Timon Vitalis anayemtetea Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na wakili Method Kimomogolo, anayemtetea Lema kwa
nyakati tofauti mahakamani hapo waliishawishi mahakama kutulipilia
mbali kesi hiyo kwa madai kuwa wadai hawana haki kisheria kufungua
kesi hiyo.
Walidai kuwa anayetakiwa kufungua kesi hiyo kisheria ni Dk. Burian
mwenyewe kama kweli madai ya kutolewa lugha za kashfa, ubaguzi, kudhalilishwa yalifanywa dhidi yake na mlalamikwa wa kwanza. Kwa upande wake, Wakili Alute Munghwai anayewatetea wadai, alisema kesi hiyo ina maslahi ya umma na ndio maana Mwanasheria Mkuu wa Serikali amehusishwa.
Alisema pia serikali ndiyo inayogharimia mchakato mzima wa uchaguzi
kuanzia zoezi la kuandikisha wapiga kura hadi kutangazwa kwa matokeo
na pia imetenga fedha kwa ajili ya kugharimia kesi za uchaguzi tofauti
na inavyofanya kwa kesi binafsi.