Hatimaye Rais wa Zambia, Michael Sata Amefariki Dunia

Aliyekuwa Rais wa Zambia, Michael Chilufya Sata (kulia) akiapishwa.

Aliyekuwa Rais wa Zambia, Michael Chilufya Sata (kulia) akiapishwa.

RAIS wa Zambia, Michael Chilufya Sata amefariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa ya wanafamilia wa Rais huyo, Michael Sata imeviambia vyombo vya habari kuwa rais huyo amefariki dunia katika hospitali ya London alikokuwa akitibiwa ugonjwa ambao haujatajwa hadi sasa. Kifo cha Rais Sata aliyekuwa na umri wa miaka 77 kimetokea ikiwa ni siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy, kilicho dumu madarakani kwa takribani miaka 20.

Michael Sata alizaliwa mwaka 1937 katika Mji wa Mpika, eneo ambalo lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya madhehebu ya Katoliki. Sata aliwahi kufanya kazi kama Ofisa wa Polisi, mfanyakazi wa reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa kikoloni.

Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na kampuni ya teksi. Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa muda mrefu, Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya 1980.

Haraka akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati akiongoza Jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo. Lakini pia alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali- na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la “King Cobra” alikuwa anastahili kuitwa hivyo.

Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa jamii. Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa kisiasa na kudorora kwa uchumi. Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.

Septemba 26, 2014 Satta akiwa New York alishindwa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa viongozi wa dunia katika baraza kuu la umoja wa mataifa ambapo alitakiwa kutoa hotuba kabla ya kulazimika kwenda kulazwa hospitali mjini hapo.

Hakuweza kutoa hotuba hiyo kwa wanachama 193 wa taasisi hiyo ya dunia. Ofisi ya habari katika idara ya polisi mjini New York iliwaambia waandishi wa habari kiongozi huyo alipelekwa hospitali lakini haikutoa maelezo zaidi kuhusu ni hospitali gani wala hali ya Sata ya kiafya.

Ofisi hiyo imethibitisha ripoti kwamba madaktari wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani walimtibu Sata mapema siku hiyo katika hoteli. Rais huyo hajaonekana hadharani kwa takriban miezi mitatu kabla ya kuhudhuria ufunguzi wa bunge la Zambia.

Mwanzoni mwa hotuba yake mjini Lusaka, sata aliwaambia wabunge kwa utani “bado sijafa.” Hata hivyo Wasiwasi kuhusu afya ya Sata iliongozeka nchini Zambia tangu aliposafiri kwenda Israel kwa matibabu mwezi Juni mwaka huu na baadae kujiondoa kwenye macho ya umma.
VYANZO: Mitandao ya Habari