Hatimaye mwalimu kuchekelea

 

 

Na Mwandishi wa Shirika la Daraja

HATIMAYE Shule ya Msingi Kibeto iliyopo Kijiji cha Madindo, Ludewa, Mkoa wa Njombe inatarajiwa kupata walimu baada ya kukaa tangu 2006 ikiwa na ikiwa na mwalimu mmoja.

Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 77, ina vyumba vitatu vya madarasa, ambapo wanafunzi wanasoma kwa kupokezana, huku pia ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati pamoja na ukosefu wa vyoo.

Akizungumza na gazeti hili, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Beda Mtitu, ambaye ni mwalimu pekee anayefundisha shule hiyo, alisema tangu shule hiyo ianzishwe mwaka 2006 anafanyakazi peke yake katika mazingira magumu.

Ofisa Elimu Shule za Msingi wa Wilaya ya Ludewa, Robert Iyela, akizungumza kwa njia ya simu, alisema tatizo lililomfanya ashindwe kupanga walimu katika shule hiyo ni kutokana na kukosekana kwa nyumba za walimu, uhaba wa madarasa na vyoo.

Alisema licha ya wanajamii wa kijiji hicho kuwaeleza juu ya suala hilo, lakini wamekuwa wakivutana juu ya kujenga nyumba za walimu, jambo ambalo linamuwia vigumu kupanga walimu.

“Ni kweli ndugu mwandishi lakini tatizo hilo lipo lakini kwa sasa napanga walimu watakaokuja mwaka huu, tatizo lililopo ni kukosekana kwa nyumba za walimu, maana nashindwa kuwapanga walimu kutokana na kukosekana sehemu ya kuishi, naweza nikawapanga lakini wataishi wapi?” alisema.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo zinaeleza kuwa wanakijiji wameongeza nyumba moja ya walimu, hivyo kufikia idadi ya nyumba mbili, ambayo huenda imechangia ofisa elimu huyo kufikiria kupeleka walimu wengine shuleni hapo.

Taarifa zaidi zilizotufikia zinaarifu kuwa ofisa elimu huyo amelazimika kupanga walimu katika shule hiyo baada ya kuagizwa na afisa elimu mkoa kutokana na habari iliyoandikwa na vyombo vya habari kuhusiana na ukosefu wa walimu shuleni hapo.

Akizungumzia maendeleo ya taaluma shuleni hapo Mtitu alisema, “pamoja na changamoto zilizopo lakini  nimekuwa nikijitahidi kufundisha kadri ya uwezo wangu, kwani mwaka jana nilifaurisha wananfunzi nane kati ya 11 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi”.

Alisema mbinu anayoitumia katika ufundishaji ni kuunganisha baadhi ya madarasa ambayo mitaala yake inafanana kwa kufundisha pamoja ikiwa ni njia moja wapo ya kumaliza mitaala ya kila somo kwa madarasa yote.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ludende, James Luoga, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Madindo, alisema kukosekana kwa walimu wa kutosha shuleni hapo kumechangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu kijijini hapo.