SERIKALI kupitia Wakala wa barabara nchini TANROADS Mkoa wa Rukwa imekamilisha ahadi yake kwa wananchi ya kuwapunguzia changamoto ya usafirishaji wa abiria na mzigo kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Kalambo pamoja na barabara ya Sumbawanga Matai hadi Kasanga port (112km) ambapo Kilomita 71.4 zimeshawekwa lami.
Akizungumza mara baada ya kukagua daraja na barabara hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Rukwa na nchi nyingine za jirani ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.
“Tuliwaahidi wananchi kujenga darala na barabara hii ili wafanyabiashara na wakulima waweze kusafirisha bidhaa na mazao yao kwenda katika masoko kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla,” ameaema Eng. Ngonyani.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Serikali itahakikisha ndani ya kipindi cha miaka mitano inakamilisha ahadi zote walizoahidi kwa wananchi ili wananchi wanufaike na Serikali yao.
“Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ipo kwa ajili ya wananchi wote, na sisi kama wasimamizi tuliopewa dhamana kwenye Wizara tutahakikisha kile tulichokiahidi kwa wananchi tunakitekeleza kwa wakati ili wananchi wanufaike na uchumi wa nchi ukue,” amesisitiza Eng. Ngonyani.
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Rukwa amewataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara na kuacha vitendo vya kung’oa alama za barabarani ambazo zimewekwa ili kuongeza usalama kwa madereva katika matumizi ya barabara hizo.
“Tumeweka alama hizi barabarani kwa ajili ya kuongoza madereva wanaotumia barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea kwa kutokuwepo na alama za tahadhari, hivyo ni wajibu wenu kuzilinda na kuzitunza kwani zipo kwa faida yetu sote,” amesema Eng. Msuka Mkina.
Katika hatua nyingine Waziri Ngonyani amekagua huduma za bandari ya Katanga ambapo amesema Serikali itaendelea kuziboresha bandari zilizopo ukanda wa ziwa Tanganyika ili kuvutia wasafirishaji wa mizigo mikubwa kutumia bandari hizo.
“Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya bandari ya Kalema, Kigoma na Katanga ili ziwe na uwezo wa kupakia na kupakua mizigo mikubwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi,” amesisitiza Eng. Ngonyani.
Naye Msimamizi wa Bandari Mkoa wa kigoma, Bw. Morris Mchindiuza amesema Mamlaka ya bandari TPA imejipanga na imetenga kwenye bajeti yake kiasi cha Sh. bilioni 1 kwa ajili ya upanuzi wa Gati namba moja na hivyo kuchochoa ukuaji wa wa kibiashara na ongezeko la Meli hususani nchi za jirani kama Burundi na DRC Congo.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu, Bandari na Madaraja katika Mkoa wa Rukwa
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.