Hatimaye ‘bifu’ la Mr. II na Ruge lamalizika

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. II na Mkurugenzi wa Clouds Media, Rugemalila Mutahaba wakipeana mikono jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya kupatana na kumaliza tofauti zao zilizotokana na sababu za kimuziki zilizodumu kwa miaka miwili. Huku wapatanisha wa mgogoro huo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi (kushoto) na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu (kulia) wakishuhudia.

Na Mwandishi Wetu

HALI ya uhasama uliodumu takribani miaka miwili kati ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. II na Mkurugenzi wa Clouds Media, Rugemalila Mutahaba imemalizika baada ya wawili hawa kupatana rasmi.

Mbilinyi ‘Mr. II’ ambaye awali alikuwa msanii wa miondoko ya Bongo Fleva pamoja na Mutahaba walipatanishwa jana mjini Dar es Salaam na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi. Katika tukio hilo la upatanishi ambalo pia lilihudhuriwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu pamoja na waandishi wa habari huenda likawa ni matumaini mapya kwenye tasnia ya muziki hasa wa kizazi kipya.

Wawili hao waliingia katika uhasama baada ya Mbilinyi kudai mchakato wa kuandaa Tamasha la kupiga Vita Ugonjwa wa Malaria nchini (Malaria
No More) lilikuwa mikononi mwake lakini baadaye Mutahaba alimzunguka
na kulifanya, hali ambayo ilileta chuki kati yao na hata baadhi ya
wasanii.

Kutokana na uhasama huo, Mbilinyi pamoja na baadhi ya kundi la wasanii wanaomuunga mkono wamekuwa wakishambulia shughuli zote zinazofanywa na Kituo cha Radio Clouds dhidi ya wasanii kwa kusema wamekuwa wakijali zaidi maslahi yao bila kumfikiria msanii.

Hata hivyo, Mutahaba siku zote amekuwa akikanusha kuingilia na kumpokonya Mr. II kazi ya Malaria No More kama alivyokuwa akidai mwenyewe, mgogoro ambao nusura ufikie hatua mbaya kati ya pande zote.

Pande zote zimeweka wazi sasa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa namna yoyote inapotokea ili kukuza tasnia ya muziki nchini, ikiwa ni pamoja na kuweka mbele maslahi ya pande zote kulingana na makubaliano.