HATIMA ya Bunge Maalumu la Katiba imebaki mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, ambalo limemwandikia barua kiongozi huyo wa nchi kutaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu tarehe ya mwisho ya kumaliza vikao vyake. Hiyo ni kutokana na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge hilo kuzua utata wa kisheria na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar. Ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba inaonyesha kuwa limepanga kuhitimisha vikao vyake mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la Rais linaonyesha kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalumu ingeanza Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, siku ambayo mwenyekiti wa Bunge hilo atakabidhi kwa Rais Katiba inayopendekezwa. Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hadi sasa Serikali bado haijatoa tangazo (GN) lingine kuongeza muda hadi mwishoni mwa Oktoba kama alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta wakati akitoa ufafanuzi wa siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti 5 mwaka huu.
Sitta alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi Ijumaa ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na Rais. Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hadi sasa hawajapata maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako waliandika barua ya kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
“Tulimwandikia barua, Katibu Mkuu Kiongozi (Ombeni Sefue) kuomba ufafanuzi wa siku hizo kama ambavyo sisi tungependa iwe, lakini hadi sasa bado hatujajibiwa lakini bado siku zipo nadhani tutajibiwa tu wakati mwafaka,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Sefue alikiri ofisi yake kupokea barua kutoka Bunge Maalumu ikiomba ufafanuzi ambao ungeliwezesha kuongeza siku kwa lengo la kukamilisha kazi ya kujadili na kuandika Katiba inayopendekezwa na kwamba maombi yao bado yanafanyiwa kazi.
“Bado tuna muda wa kutosha tu, ni kweli tulishayapokea maombi ya Bunge Maalumu kuhusu suala hilo na Mheshimiwa Rais akikamilisha kazi yake watajulishwa tu,”alisema Sefue.
Utata wa kisheria
Licha ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina utata wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana ya siku 70 ambazo Bunge lilikaa mara ya kwanza.
Baada ya kusoma hati ya Rais ya kuitishwa kwa Bunge hilo, Februari mwaka huu, Jaji Werema alisema siku 70 zilizotolewa kwa mujibu wa tangazo la Serikali ni za kikalenda na siyo siku za kazi kwa sababu wajumbe wa Bunge Maalumu siyo watumishi wa kuajiriwa.
Maelezo ya Jaji Werema yalitokana na swali lililoulizwa na Mjumbe wa Bunge Maalumu, Ezekiah Oluoch ambaye alitaka ufafanuzi huo kutokana na siku zilizotengwa kuonekana kwamba ni chache na zisingetosha kukamilisha kazi ya kutunga Katiba. Kauli ya Jaji Werema haijawahi kutenguliwa na Mahakama au yeye mwenyewe na kwa msingi huo, kwenda kinyume chake ni kuvunja Sheria ya Kazi na Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya 2005.
Vifungu vya 22 (1) na (2) vya sheria hiyo vinazungumzia ushauri wa kisheria wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu suala lolote analotakiwa kulitolea ufafanuzi, wakati Kifungu cha 23 (1) kinasema ushauri huo unabaki kuwa msimamo wa Serikali katika suala husika, vinginevyo ubatilishwe ama na Mahakama au na AG mwenyewe katika utekelezaji wa wajibu wake. Jana katika maelezo yake, Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue alisema Jaji Werema alikuwa sahihi katika tafsiri aliyoitoa kuhusu siku zilizotolewa na Rais wakati wa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu.
“Jaji Werema yuko sahihi kabisa, kwa hiyo hata Rais atakapokuwa akitoa majibu ya maombi yaliyofikishwa kwake kuhusu nyongeza ya siku atazingatia sheria za nchi,” alisema.
Bunge la Muungano na BLW
Mgogoro mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Kwa kawaida, vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki mbili za vikao vya kamati za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo, basi vitaingiliana na vikao vya Bunge Maalumu ambalo ratiba yake imepangwa kuendelea hadi Oktoba 31, mwaka huu.
Katibu wa Bunge la Muungano, Dk Thomas Kashililah alisema vikao vya Kamati za Bunge hilo vinatarajiwa kuanza Oktoba 13, mwaka huu kutokana na kuwapo kwa miswada mingi ya Serikali inayopaswa kufanyiwa kazi.
“Tuna miswada ya Serikali kama 12 hivi ambayo mingine imekaa muda mrefu, kwa hiyo kamati zetu nyingi zinapaswa kukutana mapema ili kuifanyia kazi vinginevyo tutakwama,” alisema Dk Kashililah ambaye pia ni Naibu Katibu wa Bunge Maalumu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano wa ratiba baina ya taasisi hizo mbili ambazo yeye ni mtendaji wake, Dk Kashililah alisema suala hilo litatafutiwa ufumbuzi kabla ya muda huo kuwadia.
“Nadhani wakati tunafikiria suala la muda wa Bunge la Katiba, hatukufikiria ratiba hizi nyingine, kwa hiyo ni dhahiri kwamba pengine tutalazimika kuangalia jinsi ya kutoka hapo,” alisema.
Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai mwishoni mwa wiki iliyopita alisema kwa jinsi ratiba ya Bunge Maalumu ilivyopangwa lazima itaingilia shughuli za Bunge la Muungano, hivyo uamuzi unapaswa ufanywe ili kuepusha mgongano huo.
“Sisi tumeishaliona hilo kwamba ni changamoto, tulikuwa tukijaribu kujadiliana kuona kama baadhi ya vikao vya kamati vinaweza kuanza mapema hapa Dodoma, lakini uamuzi bado haujafanyika,” alisema Ndugai.
Naye Hamad alikiri kwamba kalenda ya vikao vya Baraza la Wawakilishi inaingiliana na ratiba ya Bunge Maalumu na kwamba wanafikiria jinsi ya kuondoa kasoro hiyo.
“Kuna njia nyingi za kuondoka hapo, pengine tunaweza kumwomba Rais asogeze mbele vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa wiki mbili, maana hiyo inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo, tutalifanyia kazi ili kufahamu jinsi ya kulitatua,”alisema Hamad.
Akizungumzia changamoto hiyo ya mwingiliano wa ratiba za kazi za taasisi hizo, Balozi Sefue alisema jambo hilo ni miongoni mwa yatakayozingatiwa wakati wa kufanya uamuzi.
“Tutakapokuwa tunafanyia kazi suala hilo, tutazingatia hayo yote na tutahakikisha kwamba hakutakuwa na mwingiliano wa aina yoyote,” alisema Sefue.
CHANZO: Mwananchi