Hatari, samaki wenye ‘sumu’ Morogoro
JESHI la Polisi mkoni hapa limewatahadharisha wakazi wa Manispaa ya Morogoro kutonunua samaki, kwa watu wanaotembeza mitaani kutokana na watu wasiofahamika kumwaga vitu vinavyohisiwa kuwa sumu kwenye Mto Ngerengere.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kamanda wapolisi mkoni hapa Adolphina Chialo alisema watu wasiofahamika walimwaga kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu kwenye mto Ngerengere kwa lengo la kuuwa samaki na kwenda kuwauza.
Alisema watu hao wanadaiwa kumwaga sumu hiyo, ambayo bado haijafahamika mara moja kwa lengo la kuuwa samaki na kwenda kuwauza kwa ajili ya kujipatia riziki.
Wakati huo huo watu wanne wamenusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupindiuka katika eneo la Kwambe Dumila Wilayani Kilosa.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Miraji Mbarka (40), Hadija Ally (30) wakazi wa mjini Gairo, Samweli Mlei mkazi wa Chakwale pamoja na mfanyabiashara aliyefahamika kwajina la Mathias Joseph mkazi wa Modeco Mnispaa ya Morogoro.
Alisema ajali jiyo ilitokea Juni 27 mwaka huu saa 7:30 mchana katika barabara kuu ya Morogoro Dodoma , na kulitaja kuwa ni lenye namba za usajili T 489 APU aina ya Toyota Hiace likitokea Morogoro Mjini kuelekea katika Mji mdogo wa Gairo.
Chialo alisema dereva bado hajafahamika na kwamba alikimbia baada ya ajali hiyo, na anatafutwa ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku chanzo kikielezwa kuwa ni mwendo kasi.
Hata hivyo alisema majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.