Hatari; Mvua Kubwa Kunyesha Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi.


NAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza uwezekano wa kunyesha mvua kubwa zinazoweza kuleta maafa katika baadhi ya mikoa ya Ukanda wa Pwani. Kwa mujibu wa taarifa ya tahadhari ya TMA iliyotolewa leo imeeleza mikoa itakayoathirika na mvua hizo ni pamoja na Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba mjini Zanziber.

Taarifa hiyo imesema mvua hizo zinategemewa kunyesha kati ya Machi 05 hadi 07 ya mwaka 2014 na zitakuwa ni mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24, ikiwa ni kiwango cha wastani (65%).

Taarifa imefafanua kuwa hali hiyo inatokana na kuimalika kwa mgandamizo mdogo wa hewa mashariki mwa bahari ya Hindi sambamba na kusogea kwa haraka kwa mfumo wa mvua za msimu (ITCZ) hivyo kuongeza kiwango cha unyevunyevu kutoka baharini kuelekea maeneo tajwa hapo juu.

“…Wakazi na watumiaji wa Bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, wanashauriwa kuchukua tahadhari stahiki. Mvua zinazoendelea na zinazotarajiwa kunyesha zinaashiria kuanza mapema kwa mvua za masika katika baadhi ya maeneo ya pwani ya kasikazini ikiwemo Dar es Salaam,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na ikilazimika itatoa mrejeo kila itakapobidi.