Hatari, Muhimbili yasitisha huduma kwa wagonjwa

Jengo la Wodi ya Wazazi Muhimbili

Na Mwandishi Wetu

HATIMAYE, katika hali isiyokuwa ya kawaida na hatari kwa Watanzania hasa wagonjwa, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hii leo imesitisha huduma zake baada ya madaktari bingwa nao kugoma.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Eligaesha amewaambia waandishi wa habari nchini kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya madaktari bingwa waliokuwa wakitoa huduma hizo nao kugoma na kuandika barua wakieleza kuwa wamezidiwa na kazi, hivyo kusitishwa kwa huduma.

Eligaesha amesema wamefikia uamuzi huo baada ya jana Kamati ya Madaktari Bingwa kuandika barua kwa uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na uongozi wa Hospitali ya Mifupa (MOI) ambapo waliazimia kusitisha huduma katika hospitali hiyo.
Wamesema mgomo huo utaendele mpaka pale Serikali itakapotoa tamko rasmi kuhusiana na muafaka katika madai ya madaktari wanafunzi (intern).

Hata hivyo, mjini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu leo bungeni, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi ameliomba Bunge kusimamisha shughuli zote ili lijadili suala la mgomo wa madaktari. Katika hoja zake Zambi amelitaka bunge kuona suala la mgomo wa madaktari ni la dharura hivyo lijadiliwe ili lipatiwe sulihisho.

Pamoja na hayo akijibu hoja hiyo Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema Bunge kwa sasa haliwezi kujadili suala hilo mpaka kamati iliyoundwa kutatua mgogoro huo itakapomaliza kazi yake.

Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wameungana na Kamati ya Madaktari inayosimamia mgomo na kuitaka Serikali kujibu hoja zao zilizowasilishwa na madaktari wanafunzi ya nyongeza ya mshahara, malipo ya muda wa ziada, malipo ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi na kupandishwa vyeo kwa wakati. Mgomo wa madaktari hapa nchini ulianza Januari 16 mwaka huu ambapo madaktari hao wanaidai Serikali madai yao anuai.