KAMATI ya Maandalizi ya tukio la Okoa Maisha ya waandishi wa habari, imeandaa harambee maalumu ya kuosha magari yaani Media Car wash for health, litakalofanyika Mjini Dodoma, Uwanja wa Jamhuri, siku nzima ya Jumamosi June 25, 2016.
Lengo la harambee hiyo ni kukusanya fedha zitakazotumika kuwakatia Bima ya Afya waandishi wa habari takribani 1000 hapa nchini. Kamati ya Maandalizi ya harambee inajumuisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari chini ya Uenyekiti wa Bw. Benjamin Thompson Kasenyenda, inaomba ushirikiano wakaazi wa Dodoma pamoja na Wabunge. Mtakumbuka kwamba kamati hii ilifanya tukio kama hili viwanja vya Leaders, Jijini Dar es Salaam July 4, 2015, ambapo zaidi ya 30m/-, zilichangishwa.
Fedha hizo zilisaidia gharama za matibabu ya waandishi watatu waliokuwa mahututi wakati huo, mmoja wao akiumwa kansa. Lengo la mwaka huu limebadilika ambapo tumekusudia kuhakikisha kuwa wengi wao wanakatiwa bima ya afya, ili kujikinga na kadhia ya kuchangiwa fedha pale wanapofikwa na maradhi. Aidha, kwenye changizo hili tutakuwa na kadi maamlum za kuomba michango ya mfuko huo, ambazo tutazigawa kwa Wabunge kupitia ofisi ya Bunge. Tutaomba ushirikiano mzuri kutoka kwa Wabunge na wakazi wa Mji wa Dodoma ili kufanikisha zoezi hili.
Pia tumeandika barua kwa Spika tukimwomba awajulishe Wabunge ili wajitokeze kwa wingi kwenye zoezi hili. Waratibu wa Harambee ile ambayo ni Kampuni ya Media Assistant, imefanya utaratibu wa kumleta Miss Tanzania Ms Lilian Kamazima pamoja na wasanii wa Bongo Movies na Bongo Fleva kuja kushiriki zoezi hilo.