RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amemteuwa Bw. Hamphrey Polepole kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa uteuzi wa DC Polepole umeanza tangu Aprili 18, 2016.
Bw. Polepole ambaye ni miongoni mwa makada vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyewahi kuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (mstaafu), Zelothe Steven ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Bw. Polepole pia amekuwa akivuma katika mijadala mbalimbali ya kisiasa na kijamii akijinasibu kutetea maslahi ya Taifa la Tanzania.
Wakati huo huo; Rais Magufuli kesho anatarajiwa kumuapisha Mathias Chikawe kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan. Taarifa ya Ikulu inasema Balozi huyo mteule ataapishwa saa tatu asubuhi na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.