KATIKA kuwapunguzia watanzania mzigo wa gharama za vifurushi vya intaneti kampuni ya mawasiliano ya simu ya Halotel imetangaza kuboresha vifurushi vyake vya intaneti na kuongeza kiwango kulingana na mahitaji ya wateja.
Akizungumzia juu ya maboresho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Lui Van Dai, amebainisha kuwa azimio hilo limekuja baada ya kusikia kilio cha watanzania kuhusu gharama za intaneti kuongezeka lakini vifurushi vikiendelea kushuka kila kukicha.
“Tumesikia kilio cha Watanzania ambao wameendelea kulalamikia gharama za mawasiliano kuendelea kupanda siku hadi siku kitu ambacho kinaathiri matumizi yao. Maboresho haya yanalenga kuwapatia vifurushi zaidi kwa kiasi kidogo cha fedha ambacho kinaendana na mahitaji ya kila mteja.” Alisema Dai.
“Tunatambua teknolojia ya mawasiliano imekua kwa kiasi kikubwa na inatumika katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Sekta hii imekuwa ni kiungo kizuri katika upashanaji wa habari hususani mitandao ya kijamii ambayo ndio njia rahisi na ya haraka kuwafikia watu. Hivyo basi, maboresho haya yanalenga kuendelea kuwapatia Watanzania muda zaidi wa kuendelea kuungana na jamii kwa kufurahia vifurushi vikubwa kwa kiasi kidogo cha fedha.” Aliongezea Mkurugenzi huyo.
Ameendelea kufafanua zaidi kuwa licha ya kufanya maboresho hayo, Halotel imefanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya mawasiliano kwani mbali na kupunguza gharama hizo wanawahakikishia Watanzania kuwa huduma zao ni za uhakika na zinapatikana kila kona ya nchi.
“Hadi sasa tumeweza kuvifikia vijiji zaidi ya 3000 nchi nzima ambapo kitakwimu ni sawa na kusema tumesambaa Tanzania kwa asilimia 95% hadi hivi sasa. Pia tumeunganisha mtandao wetu kwa zaidi ya Kilomita 20,000 za mkongo wa mawasiliano. Hii inafanya huduma zetu kuwa ni za uhakika na kutufanya kinara katika kuyafikia maeneo mengi zaidi kuliko mtandao wowote nchini.” Aliendelea kuelezea zaidi Dai.
“Kwa hali ilivyo ngumu sasa tumeboresha zaidi vifurushi vyetu ambapo kwa Shilingi 499, mteja atapata MB 200 pamoja na dakika za kupiga simu. Kiwango hiko ni kikubwa zaidi cha MB kinachotolewa ukilinganisha ni mitandao mingine kwa zaidi ya 100%. Kwa Shilingi 1000, mteja anaweza kupata MB 450, pamoja na vifurushi vingine vingi. Hivyo nawasihi Watanzania kuendelea kujiunga na Halotel ili waendelee kufurahia huduma zetu kwa gharama nafuu.” Alihitimisha Bw. Dai.
Kampuni ya Halotel licha ya kuwekeza zaidi katika mfumo wa mawasiliano ya simu pia inatoa huduma kwa gharama nafuu zaidi kwa mamilioni ya Watanzania. Dhumuni kuu ni kuwapunguzia gharama na kuwawezesha kuendelea kufurahia huduma za intaneti zenye uhakika zaidi.