KATIKA kufanikisha azma ya kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wananchi wenye vipato tofauti, kampuni ya mawasiliano ya Halotel imeendelea kuunganisha huduma yake ya Halopesa na huduma nyingine zaidi ili kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania.
Katika kulifanikisha hilo Halotel imeingia makubaliano ya mkataba wa utoaji wa huduma na kampuni ya Selcom, ushirikiano utakaowawezesha mamilioni ya wateja wa mtandao huo kutoa na kutuma pesa, kununua vocha za muda wa maongezi na kufanya manunuzi mbalimbali.
Hatua hii itawawezesha watanzania wengi zaidi kufikiwa na huduma za kifedha kwa njia ya mtandao ikiwa ni sehemu ya kufanikisha azma ya serikali ambayo inazitaka taasisi mbalimbali za kifedha kuwafikia wananchi na huduma zao hasa kwa maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel, Bw. Le Van Dai amesema kuwa ni hatua nyingine kubwa katika utoaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi nchini Tanzania. Sasa kupitia huduma ya Halopesa itakuwa imewezesha kupanua wigo kwa wateja wa mtandao huo kuweza, kutoa na kuweka fedha, pamoja na kufanya malipo mbalimbali kwa urahisi zaidi.
“Ushirikiano huu ni wa kipekee katika kurahisisha maisha ya watanzania ambao wamekuwa wakipata tabu kupata huduma za kifedha kutokana na maeneo wanayoishi. Sisi kama Halotel hadi sasa tumewafikia watanzania kwa zaidi ya asilimia 95. Hivyo ni dhahiri kwamba wateja watakaojiunga nasi wataweza kutoa au kuweka fedha huko huko waliko kupitia kwa mawakala wetu ambao wameenea nchi nzima,” alisema Dai.
“Tunatambua changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwasibu Watanzania hasa wa kipato cha chini. Kwani wengi wao walikuwa wanakwama kuweza kupata huduma za kifedha kutokana na miundombinu kutowafikia. Mpaka hivi sasa Halotel ina mawakala zaidi ya 30,000 walioenea nchi nzima. Hii itawawezesha wakazi wa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na mawasiliano kabisa au huduma za kibenki sasa kuweza kupata huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi huko huko walipo,” alihitimisha Mkurugenzi huyo.
Vilevile wateja wa Halopesa wataweza kutoa na kuweka fedha kwenye akaunti zao za Halopesa kupitia mawakala wa Selcom zaidi ya 17,000 wanaopatikana nchi nzima.