MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (35), jana alikosa dhamana na kupelekwa rumande katika Gereza la Segerea hadi leo maombi ya dhamana yake yatakaposikilizwa tena. Mdee pamoja na wenzake wanane, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda washtakiwa hao waliyakana yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Kaluyenda alisema dhamana ipo wazi na kila mmoja asaini bondi ya Sh1 milioni na kuleta wadhamini wawili ambao mmoja kati yao awe anafanya kazi katika taasisi inayotambulika kisheria.
Pia alisema wadhamini hao wawasilishe barua kutoka kwa waajiri wao na kitambulisho cha kazi. Hata hivyo, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama kuwapa nafasi ya kwenda kukagua nyaraka za dhamana zilizowasilishwa na wadhamini wa washtakiwa hao, ombi ambalo lilikubaliwa.
Baada ya kutoa masharti hayo Hakimu Kaluyenda aliahirisha kesi hadi Oktoba 21, mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali, kisha hakimu huyo aliondoka kabla ya mchakato huo wa uhakiki kumalizika.
Mawakili wa Serikali waliporudi jioni, iliwalazimu mawakili wa washtakiwa, Mabere Marando na Peter Kibatala kutoa ombi kwa Hakimu Mfawidhi, Isaya Halfani kuwa washtakiwa hao waachiwe na kwenda kulala nyumbani ili leo wafike mahakamani lakini mawakili wa Serikali walipinga ombi hilo.
Kutokana na pingamizi hilo, Hakimu Halfani aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya dhamana na kuamuru Mdee na wenzake kupelekwa rumande.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Rose Moshi (45), Renina Peter ‘Lufyagila’, Anna Linjewile (48), Mwanne Kassim (32), Sophia Angel (28), Edward Julius (25), Martha Mtiko (27) na Beatu Mmari (35).
Kongola alidai kuwa washtakiwa hao Oktoba 4, 2014, wakiwa Mtaa wa Ufipa, walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi. Alidai kuwa, washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na Kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la pili, siku hiyo ya tukio katika eneo hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kutembea kwenda kwenye Ofisi ya Rais. Alidai kuwa kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 74 na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Lissu akwama
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dodoma imetupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akidai kulipwa Sh79 milioni kama gharama za uendeshaji katika kesi ya msingi. Katika kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2013, Lissu alikuwa akidai gharama za uendeshaji wa kesi iliyokuwa imefunguliwa kupinga ubunge wake ambayo alishinda.
Katika kesi hiyo, Shaaban Seleman na Paschal Halu walimfungulia kesi mbunge huyo wakilalamikia upungufu katika uchaguzi uliompa ushindi mwaka 2010. Jana, Mahakama Kuu ya Dodoma mbele ya Msajili Renatus Rutatinisigwa, ilitupilia mbali maombi ya Lissu huku ikieleza kuwa baadhi ya nyaraka za madai hayo hazikuwa zimejitosheleza.
Kesi ya Mbowe yaahirishwa
Wakati huohuo, kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana iliendelea kupigwa kalenda baada na Mbowe kushindwa kufika mahakamani kutokana na udhuru na hakimu wake kuwa likizo.
Kesi hiyo ya kumshambulia mwangalizi wa uchaguzi mwaka 2010, ilipangwa kuendelea jana, lakini wakili wake, Issa Rajabu alisema Mbowe alikuwa na dharura, lakini pia hata kama angefika, kesi hiyo isingeendelea kwa kuwa Hakimu Denis Mpelembwa anayeisikiliza alikuwa likizo.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Novemba 6, mwaka huu wakati Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai atakapopanda kizimbani kuanza kujitetea. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtimua kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG), Othman Masoud Othman.
CHANZO: Mwananchi